...Niliingia ndani nikiwa na mambo mengi kichwani lakini zaidi nilisumbuliwa na kitu moyoni mwangu. Kitu kipya kabisa ambacho hata mimi mwenyewe sikukielewa vema. Zilikuwa ni hisia ambazo nilihisi ni mpya kabisa katika mfumo wa mishipa ya fahamu zangu. Niliishia chumbani ambako baada ya kujitupa kitandani nilipitiwa na usingizi mzito. Nilikuja kushtuliwa na mama yangu aliyekuja kuniamsha kwa ajili ya kupata mlo wa usiku
“ kulala gani huku Karen!” mama alinilalamikia
“ nimechoka mama na hata chakula sijisikii kula kabisa”
“ acha upuuzi Karen! Ina maana bado Kelvin amejaa akili mwako!...sasa sikiliza binti mapenzi yanasumbua mno na kama utayapa nafasi yakuendeshe basi jua utakuwa mtu wa kuishi kwa maji na mkate”
“ ni bora na hivyo mama mimi sijisikii kula hata huo mkate, unadhani hiki alichonifanyia Kelvin ni kitu cha kusahaulika kwa miezi miwili tu, itachukua miaka mama”
alinitazama kwa muda kisha akasogea na kuketi kitandani pangu. Alinikumbatia kisha taratibu akaniachia na kutabasamu. Ilikuwa kawaida yake na nilizidi kumpenda kwa tabia yake hii. Alionekana wazi kutafuta maneno ambayo yangenifanya nimuelewe vema
“ Karen binti yangu! Maisha yamejaa uchaguzi na unayo haki ya kuchagua maisha unayotaka wewe. Kelvin ni nani hata ayatawale maisha yako….ni nani hata atoweke na furaha yako kwanini hutaki kumwambia mungu asante kwa kumuondoa Kelvin maishani mwako kwa vile hujui amekuepusha na nini na amekuandalia nini hapo mbele Karen”
“ nilimpenda Kelvin mama…nilimpenda sana” nilinung’unika kwa huzuni
“ I know baby! Najua hilo lakini yote ni maisha. Wengine wanafiwa na waume zao wiki tu baada ya kuoana Karen na bado wanaishi na wengine wameolewa tena wamezaa na pengine kusahau yaliyopita” nilimtazama mama kwa muda kisha nikamkumbatia tena Si kwamba nilifarijika na maneno yake bali nilitaka tu afarijike na hali yangu. Usiku huo ulipita nikiwa na mawazo mengi mno. Sikuweza hata kupitisha kijiko kimoja cha chakula na cha maana kilichoingia tumboni ni juisi tu ya passion.
Asubuhi ya jumatatu niliamkia kazini kama kawaida. Bosi wetu Mr.Tummy aliniita ofisini kwake mara tu nilipoingia ofisini. Nilipitia mafaili kadhaa na kuangalia ratiba ya siku hiyo kisha nikaelekea ofisini kwa Mr. Tummy. Niligonga kisha nikakinyonga kitasa na kuusukuma mlango kwenda mbele. Niliingia ndani na kumkuta Mr. Tummy ameketi kitini pake akijizungusha kwa madaha hali akizungumza na simu yake ya mkononi. Alinipa ishara ya kuketi katika kiti kilichokuwa mbele ya meza yake. Nikaketi kwa adabu na kumsubiri amalize kuongea katika simu yake. Dakika mbili baadae aliiweka simu yake mezani na kuachia tabasamu
“ shikamoo Mr. Tummy” nilimsabahi kwa heshima kwa vile alikaribiana kiumri na baba yangu Mzazi.
“ marhabaa Karen habari za weekend, habari za mapumziko, habari za kujirusha eeh!” alinisemesha huku akitafuta tafuta kitu katika faili lililokuwa mbele yake. Niliachia kicheko kwa vile ambavyo alikuwa akinihoji kana kwamba alikuwa kijana wa rika langu.
“ nadhani mambo safi! au siyo?” alinitupia jicho la pembeni huku akitabasamu.
“ bila shaka ndio bosi” nilimjibu nikilikatiza tabasamu langu
“ sasa binti kuna kazi moja ya kufunga yale mahesabu ya mapato ya kampuni. Ingawa ni mapema kidogo lakini ni bora yakiandaliwa mapema ili tujue ni kiasi gani kitakwenda benki na kiasi gani kitatumika kununulia gari la kampuni” alinipa maelezo
“ sawa bosi nitakamilisha kazi hiyo mara moja… kuna lingine?”
“ aaah! Hapana binti waweza kwenda kuanza kazi mara moja” aliniruhusu kuondoka nami kwa adabu nilikiachia kiti na kurudi ofisini kwangu. Nilipita mapokezi alikokuwa Iloma na kumsabahi lakini hata hivyo hakuonesha uchangamfu hata kidogo. Nilihisi Iloma alikuwa na matatizo makubwa katika ndoa yake. Nilimkaribia zaidi na kumuuliza
“ Iloma ni nini kinakusumbua siku hizi!” nilitaka kujua zaidi kwa vile kama ni suala lake na mumewe bado sikuona tatizo na hilo lingekuwa kwa watu wengi.
Jonas alikuwa akifahamika kama mfanyabiashara maarufu mwenye pesa na utu kati ya watu. Mwanaume mwenye kujihesimu na kamwe hakuwahi kupatwa na kashfa yoyote ya ajabu na kama haitoshi Jonas alikuwa na uongozi ndani ya kanisa tulilokuwa tukisali na mara zote alionekana kama mfano kwa vijana wenzake wenye ndoa changa. Sikutaka kulipa uzito suala la Iloma kuwa mnyonge sababu ya mumewe Jonas. Iloma aliacha kazi aliyokuwa akiifanya mbele ya kompyuta na kunitazama.
“ Karen tutaongea wakati wa lunch maana sasa nafikiria mengi mno” aliniambia kwa sauti hafifu iliyoonesha hasira za ndani kwa ndani, macho yake makubwa ya mviringo yalikuwa yakipepeseka huku na kule katika hali ya kushindana na hisia fulani. Sikutaka kumdadisi zaidi nikarejea ofisini kwangu na kuanza kuchapa kazi. Mara kadhaa Jonas alifika pale ofisini kwetu kikazi na nilikuwa nimemzoea kwa kiasi Fulani.
Alikuwa mpole na muungwana sana na sasa alikuwa amemtibua Iloma kwa lipi? Wakati nikiendelea na kazi zangu mida ya saa sita na robo alifika mayasa mhudumu wetu pale ofisini, aliingia ofisini kwangu na kujisimamisha mbele yangu akiwa na bahasha mkononi
“ haya mama vipi tena?” nilimuuliza nikijiandaa kucheka kwa vile siku zote mayasa alikuwa mwanamke mwenye maneno mengi yaliyojaa utani. Alijizungusha na kunesanesa kwa madaha kisha akaanza kuniimbia.
“ mesenja kaleta balaa nyumbani kwa meneja bila kufahamuuuu” aliniimbia kibwagizo hicho na kunifanya niangue kicheko. Akanikabidhi bahasha ile iliyokuwa mkononi mwake na kuniambia kwa sauti ya kunong’ ona “ ukila na kipofu usimshike mkono Karen na utamu wa nanasi ulile kwa nafasi!”
sikumuelewa anamaanisha nini. Niliitua mezani ile bahasha iliyokuwa haina hata anuani wala muhuri wa huko itokako zaidi ya jina langu tena moja tu. Nikamtazama Mayasa kwa kituo wakati akigeuka na kuanza kupiga hatua za maringo kuelekea mlangoni, nikakumbuka kumuuliza kitu
“ mayasa!” nilimuita haraka kabla hajakifikia kitasa akageuka na kunitazama
“ nani amekupa barua hii?” nilimuuliza
“utamjua tu ukiifungua lakini mwenzio nimeshakamata elfu kumi kwa kuileta tu hapa hivyo usifikiri aliyenituma kibarua hicho ni sakala kama mimi” alinijibu na kutokomea kabisa. Nikabaki nimeduwaa nikiikodolea macho ile bahasha. Sikutaka kuwazia kuwa pengine imetoka kwa Kelvin kwa vile binadamu huyu alikuwa nchini Botswana alikokwenda mara baada ya kufunga ndoa na isitoshe aliponipigia simu nilimjibu vibaya mno na kumtaka asinitafute kwa vyovyote vile naye akanijibu kwa hasira kuwa hatojisumbua kwa lolote juu yangu. Ingawa niliumia kwa jibu hilo lakini sikuhitaji kumnyenyekea tena Kelvin!
Niliacha kazi zangu zote na kuyahamishia mawazo yangu katika ile bahasha. Taratibu niliifungua na kutoa karatasi iliyokuwemo ndani mwake. Ilikuwa ni barua fupi tu iliyoandikwa hivi
‘ tafadhali tuonane mara baada ya saa za kazi. Nitakupitia hapo jioni na teksi ya Dulla na tafadhali uwe peke yako na fanya maarifa Iloma asijue kuwa nimekupitia mimi. Nina maongezi muhimu sana na wewe
Mr. Jonas’
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment