Tuesday, July 23, 2013

SINDI.....na LAURA PETTIE (29)

29


Jerry Agapela alishindwa kuendelea kuzisikiliza kwikwi za baba yake, aliiteremsha simu chini na kuitua mezani, akiiacha hapo na kufuta machozi kwanza. Taratibu akijaribu  kuhema na kujituliza nafsi.


Mzee Kristus Agapela naye aliikata ile simu yake na kuidumbukiza kwenye koti lake alilokuwa amevaa, mkono wake wakushoto ukifuta machozi yaliyokuwa ayanamporomoka.  kijana wake, mtoto wake aliyemfanya akakosa usingizi kipindi chote alichotoweka alikuwa amempigia simu, alikuwa ameisikia sauti yake. Alijihisi yu ndotoni.

Jenifa Agapela aliyekuwa anatazama luninga, aliondoa macho yake na kutazama ngazi zilizokuwa azikielekea juu, alimuona baba yake akishuka kwa mkongojo wake haraka haraka kuja pale sebuleni. Ile haraka aliyokuwa nayo ilimfanya, afinye uso kidogo na kumtazama baba yake katika namna ya kutoielewa haraka ile ililetwa na nini.

Mzee Agapela alipoikanyaga ngazi ya mwisho aliangaza huku na kule kama mtu anayetafuta kitu.
‘Funguo?’ Jenifa akauliza akihisi ndicho kitu alichokuwa akikitafuta baba yake
‘Yeah…ziko wapi?’ Mzee Agapela akahoji na Jenifa akamuonyesha kwa kidole mahali zilipokuwa funguo hizo. Akazifuata na bila kuaga alikokuwa akielekea akatoka na kuubamiza mlango.

Jenifa akaguna na kuendelea kutazama luninga, lakini kabla hajaiweka akili yake sawa, Fiona akatoka jikoni akiwa na amevaa apron na gloves maalumu za kushikia vitu vya moto. Aliingia pale sebuleni huku akizivua zile gloves mikononi na kumtazama Jenifa kiudadisi.

‘Baba yako alikuwa anaulizia nini?’ akamuuliza Jenifa
‘Funguo za gari’ Jenifa akajibu pasipo kumtazama Fiona ambaye udadisi ulizidi kumjaa
‘Mh! kwani ametoka?’ akahoji tena sasa akimalizia kuvua zile gloves na kuzitupia juu ya meza iliyokuwa katikati ya sebule ile maridadi. Jenifa akaitikia kwa kichwa akijaribu kuiweka akili yake luningani.
Fiona akaitazama saa ya ukutani, muda ule haukuwa muda wa Agapela kutoka kwenda popote pasipo kuongozana naye wala kumuaga. Akaguna kwa sauti na kumtazama Jenifa kana kwamba alikuwa na majibu ya maswali yaliyokuwa ayakikimbizana kichwani mwake.
‘Atakuwa ameenda wapi saa hizi?’ akamuuliza Jenifa ambaye aligeuza kichwa kivivu na kumtazama Fiona usoni bila kumjibu. Kumtazama kule kulimpatia majibu Fiona kuwa alikuwa anaiendekeza hofu.

‘Lazima niwe na wasiwasi…hajaaga anaenda wapi… na hali ya baba yako unaijua… sitaki tena presha za polisi hapa kama alizoleta Jerry’ Fiona akaongea mithili ya mtu anayejali zaidi usalama wa mumewe huku moyoni akiwa na yake.

‘Mom!..relax!...baba ni mtu mzima asingeondoka hapa kimya kimya kama uko aendako anahisi kuna hatari…. sema kama unahisi may be…ana totoz na nini na nini…mzee bado handsome ohooo….’ Jenifa akamtania Fiona aliyeziokota zile gloves aizotupia juu ya meza na kumrushia Jenifa pale kochini huku wakicheka.

‘kichwa chako…kaangalie chakula jikoni…naenda chumbani mara moja..’ Fiona akazigeukia ngazi na kuelekea chumbani huku Jenifa akizima luninga na kunyanyuka kuelekea jikoni
888888888888888888888888888

Mzee Agapela akiwa na mlinzi wake yule aliyekuwa akimfuatilia Jerry, waliingia kwa Jerry dakika arobaini na tano tangu wazungumze katika simu. Mlinzi yule alisimama mlangoni huku Mzee Agapela akipiga hatua na kusimama katikati ya sebule ya Jerry akiangaza huku na kule. Uso wake ulijaa wasiwasi, ulijaa mashaka na shauku ya kumuona mtoto wake. mara kadhaa aligeuka kumtazama mlinzi wake kwa macho ya hofu.

Mzee Agapela pamoja na kuhakikishiwa na walinzi kuwa Jerry alikuwa ndani bado akili yake ilikuwa ikipambana na mawazo yake yaliyopingana na moyo wake. Akataka kupiga hatua moja kwenda mbele lakini akasita baada ya kusikia hatua za mtu zikitkea kwenye kordo. Akatumbua macho kwa bidii na sasa mkongojo wake ukitetemeshwa na mkono uliokuwa ukitikisika.

Jerry akatokea pale sebuleni akiwa na taulo mkononi, akikausha kichwa chake na uso wake. Wakaimama kama masanamu kwa sekunde tatu, wakitazamana tu pasipo kuongea wala kukaribiana.
‘Jerry!’ baba yake akaita akitaka kupiga hatua kumfuata lakini miguu ikipata uzito ghafla
‘Jerry…’ Mzee alitetemeka machozi yakimlenga lenga. Jerry hakuitika wala hakumfuata mzee wake. aliendelea kuganda pale pale akimtazama baba yake kama kiumbe cha ajabu.

Hakutegemea baba yake angepata akili ya kumfuata pale nyumbani lakini alijua alifanya vile kwa kuwa simu aliyotumia kumpigia ilitumika nyumbani kwake siku zote.
Wakati wakitazamana na kila mmoja akiwa ametahayari Mzee Agapela, akalegea, ule mkongojo ukitoka mkononi mwake na mwili wake wake kudondoka chini kama kifurushi.

Taharuki ikaanzia hapo! Jerry alitupa kile kitaulo alichokuwa ameshika na kumkimbilia baba yake, yule mlinzi aliacha kusimama kama sanamu kule nyuma na kumuwahi bosi wake. Wakamuita, wakamtikisa, wakajaribu kumnyanyua na kumtoa nje. MzeeAgapela alikuwa amepoteza fahamu!

Safari ya kumkimbiza hospitali ilianza na kila mtu akiwa na taharuki. Mapokezi hospitali Mzee alipokelewa na kukimbizwa chumba cha dharura. huku nje wakiwaacha Jerry na mlinzi wamesimama wakisubiri. Yule mlinzi alisogea pembeni na kumpigia simu Jenifa kumtaarifu kuwa Mzee wake alikuwa hospitali.

Baada ya nusu saa, Daktari alitoka na kumuita Jerry.
‘Ni mshtuko tu…lakini anahitaji kupumzika kwanza’ dokta yule aliongea na Jerry huku akimpa moyo na kumuondolea hofu
‘Naweza kumuona?’ Jerry akaomba nafasi ya kumuona baba yake
‘Yeah!...unaweza yupo wodini kule juu…ila sidhani kama naweza kuzungumza…labda kumuona tu na si kuzungumza naye’ Dokta alimkubalia na Jerry akaitikia akikubaliana na masharti ya daktari. Wakaongoza na kwenda wodini. Wakati wakiiacha mapokezi Jenifa na Fiona nao waliingia kwa kasi na kukimbilia kaunta ya mapokezi.

Wakati Fiona akizungumza na nesi wa pale kaunta, Jenifa alimuona mlinzi baba yake na kumfuata mbio.
‘Nini kimetokea?’ Jenifa aliuliza kwa wasiwasi lakini mlinzi hakumjibu zaidi ya kushusha pumzi na kuonekana kusita kusema alichotaka kusema
‘Jeni!’ Fiona alimuita Jenifa ambaye aliachana na mlinzi na kumfuata mama yake wa kambo.

‘Wamesema yuko wapi?’ Jenifa akauliza wasiwasi ukionekana kumtawala kuliko mama yake
‘Wodi namba 14 kule juu..’ Fiona akajibu huku akianza kupiga hatua na Jenifa akimfuata. Wakaitafuta lifti kwa kasi. Lifti ilionyesha ilikuwa juu sana. Jenifa akaona inamchelewesha, akaachana na lifti na kuzifuata ngazi. Kitendo kile kilimfanya Fiona naye amfuate Jenifa kule kwenye ngazi.

Walikwea ngazi haraka haraka na wakati huo, Jerry akiwa amesimama pembeni ya kitanda cha baba yake, akimtazama vile alivyokuwa usingizini. Daktari aliyekuwa kando yake. Alimgusa begani akimpa ishara ya kumuacha  mgonjwa apumzike. Walipoanza kupiga hatua mlango ukafunguliwa na Fiona akawa wa kwanza kuingia.

Kwanza alitunduwaa! akili zilimpaa, alimkodolea macho Jerry Agapela kwa juhudi zote nab ado asimini aliyekuwa amesimama mbele yake alikuwa Jerry. Mishipa yake ya fahamu ikapoteza nguvu ndani ya sekunde hizo chache alimtazama Jerry, akadindoka na kuzirai.

Kimuhemuhe kingine! Daktari akatoka kuita nesi na wakati huo huo Jenifa aliyekuwa ameganda mlangoni akimtazama kaka yake, alilengwa na machozi. hakuweza kumsaidia Fiona wala hakuweza kumsogelea Jerry aliyemkumbilia Fiona na kumtikisa tikisa.
Daktari na manesi wawili wakaja na kitanda cha kusukuma, Fiona akawekwa kitandani na kukimbizwa wodini nyingine.

Jerry na Jenifa wakapata wasaa wa kusimama pamoja katika ukimya. Jenifa akamfuata kaka yake na kujitupa kifuani pake. Akalia! akalia kwa uchungu  na kumfanya Jerry naye ahisi uchungu.

‘I missed you Jerry…’ Jenifa aliongea akibubujikwa na machozi na akizidi kumkumbatia kaka yake. Hawakuweza kuongea kitu, walikuwa na mengi ya kuzungumza lakini kwa wakati ule na mahali pale wasiongeweza kuongea kitu.

Wakarudi wodini kwa baba yao na kusimama pembeni ya kitanda cha baba yao wakimtazama, namna alivyokuwa ametulia usingizini. Jerry akamvutia mdogo wake kando yake na kumkumbatia huku akimbusu utosini. Mpaka muda huu usiku ulishakuwa mzito vya kutosha!
8888888888888888888888888

Mvua za rasharasha zilizoanza ghafla alfajiri ya siku hii ziligeuka mvua kamili ilipotimia saa moja asubuhi. Anga lilikuwa hafifu mno, huku mvua nayo ikigoma kukatika. Sindi alikuwa kitandani, ingawa hali ya hewa ilimruhusu kuuchapa usingizi kwa kadiri alivyotaka lakini hali haikuwa hivyo.

Alijipindua huku na kupindukia kule, akautazama mto wa kulalia anaotumia Jerry, akauupapasa na kuuvutia kifuani. Akalala chali na kuubeba kifuani kwa sekunde kadhaa kabla ya kunyanyuka na kuketi kitako akiuweka kando ule mto. Alijinyoosha na kupiga mihayo miwili mitatu kisha akateremka kitandani na kuufuata mlango.

Alitundua shati moja la Jerry na kulitazama kwa upendo mno, wakati akilipeleka puani na kulinusa. Harufu ya jasho la Jerry ilipita puni mwake na kumuingia hadi moyoni. Akaliondoa puani na kurudi nalo kitandani. Akaketi miguu ikiwa imening’inia chini na kulipakata lile shati huku akiwa anatazama ukutani kama mtu anayewaza.

Tabasamu likamtoka, tabasamu zuri la upendo. Akapandisha mabega yake juu wakati akivuta pumzi na kuishusha sambamba na mabega yake.
‘Jerry!’ akalitamka jina la Jerry kwa sauti ya chini kisha akalitazama tena lle shati la Jerry.

Alikuwa amemkumbuka mno, akajinyanyua na kuanza kutandika kitanda.  akasita kidogo alipoinama kunyoosha shuka. mlango ulikuwa unagongwa. Akanyanyuka na kwenda kuufungua. akihangaika na makomeo na funguo. Mlango ulipofunguliwa Jerry aliyekuwa anamuwaza dakika chache zilizopita alikuwa mlangoni.

Akatoka pale mlangoni na kurejea kitandani. Jerry akaingia na kufunga mlango huku akitabasamu kimya kimya. Akamfuata Sindi pale alipokuwa ameketi, akaketi pembeni yake.
‘Babe..’ akamuita Sindi ambaye alikuwa amegeuzia kichwa dirishani
‘bado umenuna?’ Jerry akauliza tena na Sindi akajifanya hakusikia lile swali

Jerry akainama na kuanza kuvua viatu vyake
‘Na kwanini usivulie hivyo viatu uko nje?’ Sindi akamgeukia na kuanza kelele zake
‘Samahani…’ Jerry akajibu akagusa moyo wake kwa kiganja chake. Akanyanyuka na kutoka nje kuvua viatu kisha akarudi ndani.

Sindi alikuwa akimtazama tu na Jerry naye auso ulikuwa na tabasamu lililokuja na kufichika
‘Hela umepata?’ Sindi akauliza tena kwa sauti ya shari
‘Ndio mama…’ akajibu akilala upande na kutoa noti noti zilizojikunja toka mfuko wa nyuma wa suruali. akazinyoosha kiganjani. Zilikuwa elfu kumi na tano
‘Hizi hapa na hela ya matumizi’ akamkabidhi Sindi ambaye alizipokea na kuzirushia kitandani.

Akanyanyuka na kutoka nje, huku nyuma Jerry akacheka peke yake na kutikisa kichwa. alianza kuamini alichoambiwa na Meddy asubuhi hiyo alipompigia simu na kuongea naye kuhusu matukio ya jana usiku likiwemo la Sindi kuwa mgomvi.
‘Ushampachika huyo…. hivyo vihasira hasira….ni mtu anajiumba uko ndani….’ alitakumbuka maneno ya Meddy na akajikuta akicheka zaidi  kichini chini

Wakati akikitazama kitanda akaliona shati yake chafu pale kitandani, akalitazama tu na kujikuta akitabasamu tena. Sindi akaingia na kusimama katibu na ndoo zenye maji ya kupikia. Akitafuta sufuria la kubandikia maji.

‘Baada ya chai nitatoka kidogo mama…naenda mahali kucheki dili’ Jerry akamsemesha Sindi ambaye aligeuka taratibu na kumtazama Jerry kama kituko Fulani
‘hata sasa hivi toka tu…. kwani huwa unaaga unaenda wapi…toka tu hata muda huu…usinipigie kelele’ Sindi akajibu kwa ghadhabu kidogo
‘Inamaana nikitoka huwa unapata amani sana Sindi?’ Jerry akauliza uso ukibadilika na lile tabaamu likitoweka

‘Sana tu…huwa natamani usije kabisa… na hata ukienda usirudi’ Sindi akajibu akisonya na kutoka na lile sufuria la maji. Jerry akakunja uso na kuduwaa kidogo. Akili yake ilishindwa kuamini kama ni kweli Sindi alikuwa na mimba au ile ndio ilikuwa tabia halisi ya Sindi Nalela. Akaaamua kuondoka!
8888888888888888888888888

Fiona Agapela alikuwa kama mwehu ndani ya nyumba, Jenifa alikuwa akijitahidi kumtuliza lakini hali ilikuwa si njema kwake.
‘Mom what is wrong?’ Jenifa alimuuliza kwa mashaka wakati Fiona akitembea tembea mule ndani kama mwehu. Mlango wa sebuleni ukifunguliwa na Jerry Agapela akaingia akiwa smart kuliko alivyomuona jana yake. Nywele zake zilikuwa zimenyolewa, ndevu zilizojazana ovyo zlikuwa zimenyolewa kiustadi na muonekano halisi wa Jerry Agapela ndani na mavazi ya gharama ulimrejeshea uhai wake. Fiona aliganda kama sanamu wakati Jerry akifunga mlango na Jenifa kumlaki kwa furaha.


almkumbatia mdogo wake huku akimtazama Fiona ambaye naye alimkazia macho. Chuki baina yao ilionekana waziwazi…

......NAISHIA HAPA KWANZA....

2 comments:

  1. hahahaaaaa!!!! laura kumbe utabiri nauweza nilikwambia sindi kijusi kishazama kwa stomach!!! fiona safari hii lazma apate uchizi, hela zimeliwa na jerry hajafa

    ReplyDelete
  2. HAHAHAHAHAAAA.... wait and see dear lol!.... FIONA kizunguzungu kitupu

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger