32
Alikirudisha kile kifaa cha kupimia ujauzito katika kile
kibahasha kidogo cheupe na kukiweka pembeni yake. Kichwa kilikuwa na matundu
ghafla. Ufahamu ulimtoka na kukimbilia kusikojulikana. Akashusha pumzi ndefu,
akihisi pia tumbo likimcheza. Akanyanyuka na na asijue kilichomnyanyua.
Akalikodolea macho kochi lililokuwa mbele yake pasipo kuelewa kwanini
alilitumbulia macho.
Pumzi nyingine ndefu ikamshuka, alihisi kuchoka maradufu,
alihisi vichomi vikimvamia ghafla na
kutoweka. Mwili ukamsisimka!
Katika safari yake ya mapenzi hakuwahi kukumbana na kadhia
kama hii. Mbija fupi ikamtoka na akili yake ikimtuma amtafute Sindi popote
alipo aje kumtoa katika suluba ile ya wasiwasi. akaufuata mlango lakini akili
nyingine ikamzuia kuugusa ule mlango na akajikuta akigeuka na kukitazama
kitanda, pale ilipokuwepo ile bahasha yenye kifaa.
Sekunde mbili alizosimama hapo, zikampa uamuzi aliouona wa
busara zaidi. akarejea na kukichukua kile kifaa kisha akakitia kwenye wa shati
alilokuwa amelitundika mlangoni. Akarejea kitandani na kujilaza chali akimngoja
mhusika!
Kule kwa Jamilla Sindi alikuwa alikuwa amejilaza kitandani
naye mawazo yakionekana kumjia na kutoweka pamoja na stori za kuchekesha
alizokuwa akipewa na Jamilla. akili yake ilikosa utulivu kwa kiasi Fulani na
chanzo kikiwa siri yake.
Wakati wakiongea hili na lile mlango ukafunguliwa na mpangaji
mmoja akatumbukiza kichwa tu
‘Mkubwa wa jiko kidogo?’ akasema akipenyeza mkono ili
amiminiwe chumvi mkononi
Jamilla akaachana na upishi na kuifuata chumvi kwenye
kikabati kidogo humo chumbani
‘we umelala hapo mumeo uko ndani anajua uko hapa?’ yule
mpangaji akauliza na kufanya Sindi na Jamilla wageuze shingo zao na kumtazama
kwa mshangao
‘Mume wa nani?’ Jamilla akauliza
‘Nani?’ Sindi naye ukaunga na swali
‘Jerry!...mbona kaja saa nyiiingi katupita hapo nje kitambo
tu’ yule mpangaji sasa akaingiza kiwiliwili chote ndani.
‘Khe makubwa!’ Sindi akanyanyuka na kuteremsha miguu chini
akizitafuta ndala zake kwa miguu yake huku akiikusanya khanga yake na kuikaza vema kiunoni. Sindi akatoka na
kuwaacha yule mpangaji na Jamilla
‘Utamkatia safari ya talaka mwenzio….unamvundika humu kwako
kule kwake mumewe anapiga mihayo tu’ yule mpangaji akasema akitania huku
akikinga mkono na Jamilla kummiminia chumvi kiganjani. Jamilla akabinua midomo
yake na kuguna.
‘Sasa hivi utasikia ngumi zao…’ akajibu Jamilla na kufanya
yule mpangaji acheke kishambenga.
Sindi aliingia chumbani kwake na kumkuta Jerry ameketi
kitandani. uso uliojaa wasiwasi ulimfanya Jerry amtazame kiudadisi zaidi.
‘Umekuja muda mrefu?’ akauliza Sindi akionyesha kukosa amani
na macho yake yakiangalia kitandani pale alipoiacha ile bahasha. Hakuiona!
‘Ulikuwa wapi?’ Jerry akauliza kwa upole tu akijiinusha na
kuketi kitako
‘Kwa jamilla hapo….nilijua huji’ akajitetea na macho yake
yakiangaza chini kama mtu anayetafuta kitu na Jerry akajua alichokuwa
akikitafuta.
‘Una njaa?’ Sindi akamuuliza akisimama na kusugua sugua
mikono yake kwenye mapaja yake.
‘Sijala mama’ Jerry akajibu huku akiitazama miko ya Sindi
iliyokuwa inahangaika kwenye yale mapaja. Aliuona wasiwasi wake dhahiri pamoja
na kujitahidi kuwa sawa mbele ya Jerry.
‘Ngoja nikuombee mboga kwa Jamilla…maana sikununua kitu leo’
Sindi akasema akigeuka
‘Kuna samaki nimeleta wako hapo kwenye mfuko’ Jerry
akamuonyesha mfuko alioutua kwenye kochi mara tu alipofika.
Sindi alipoutanua ule mfuko akaona sendozi na khanga.
Tabasamu pana likaupamba uso wake. Akageuka na kumtazama Jerry kwa furaha. Lile
tabasamu, ule uso wa furaha ndio hasa Jerry alitaka kuuona kila siku kila
mahali. Akafarijika kumuona Sindi akiviweka vile viatu chini na kujaribisha.
Vikamtosha.
‘Asante’ Sindi akajibu akavivua na kuvikamata mkononi na
kisha kupiga goti la heshima kwa Jerry. Avirudisha viatu kwenye mfuko na kutoa
khanga iliyokuwa kwenye nailoni lake. Akaikunjua kwa upana akiitazama kwa
furaha
‘Imeandikwaje?’ Jerry akamuuliza na Sindi akaiinua juu zaidi
ile khanga na kuisoma kwa sauti kidogo.
‘Nikikosa nirekebishe’ Sindi akasoma haya maneno na kumgeukia
Jerry na lile tabasamu la kukata na shoka. Akamfuata Jerry kitandani na
kumtazama tu huku tabasamu likishindwa kukatika.
‘nimekusamehe’ Sindi akatamka kwa sauti ndogo na Jerry
akamkumbatia.
Kuna amani ilipita kati yao kwa wakati ule, amani ambayo
ambayo Jerry alitamanni idumu maisha yao yote. Sindi akatoka mule chumbani na
kwenda chumbani kwa Jamila. Akamkuta anapakua
‘Sijadondosha bahasha yoyote nyeupe wakati natoka?’ Sindi
akauliza wasiwasi ukimfanya akunje uso kidogo. Jamilla akatikisa kichwa kukataa
na akiangaza pia huku na kule kuona kama angeiona.
Sindi akarudi kwake, akamuwekea Jerry maji ya kuoga.
Alipotoka kwenda bafuni Sindi akaanza upya kuisaka ile bahasha kwa kasi ya
ajabu. alikung’uta mpaka shuka na
kulitandika upya. akasimama akihema kwa nguvu akijaribu kufikiria pengine
alikuwa ameiweka mahali alipopasahau.
Akainama na kuchungulia uvunguni, wakati huo Jerry naye
akaingia chumbani na Sindi akanyanyuka haraka na kujibaraguza kumalizia
kutandika kitanda
‘Unatafuta nini?’ Jerry akamuuliza na Sindi akakataa kuwa
hakuna anachotafuta. Almanusura Jerry acheke kwa sauti namna Sindi alivyozuga
kuwa hakukuwa na kitu anachotafuta.
Wakati wa kula Sindi
akaonekana kuzama mbali kimawazo na mara kadhaa Jerry alimshtua na kumuuliza
kama kulikuwa na tatizo. Sindi akakataa katakata. Wakati wa kulala Jerr
akatangulia kulala akimuacha Sindi anaenda kuoga nay eye akalala akijifanya yu
usingizini wakati Sindi akirudi toka bafuni.
Sindi akamchunguza kama ameshalala aliporidhika akaanza upya
kuangaza na kupekua kwa tahadhari huku na kule. Alichokitafuta hakukipata. Akasimama
kinyonge katika kati ya chumba hiki akiwaza na kuwazua Jerry alimtazama na
kutabasamu kwa vile alijua ni nini kilikuwa kinamsumbua na kumhangaisha vile.
888888888888888888888
Asubuhi ya jumapili, jua lilishakuwa na makali ya kutosha
kukausha hata nguo. Nyumbani kwa Mzee Agapela kulikuwa na pilika pilika nyingi
za hapa na pale. Kulikuwa na sherehe ndogo ya kuzaliwa ka Mzee Agapela na pia
alitaka sherehe hiyo iwe ya kumshukuru Mungu kwa kumrejesha kijana wake
nyumbani.
Mzee Agapela mwenyewe alikuwa ofisini kwake ndani ya nyumba
yake akizungumza na Mwanasheria wake Dennis Mazimbwe. Walikuwa wakiongea mengi
kuhusu kampuni ya Mzee Agapela na masuala mengine ya kisheria. Mazungumzo
yalipoanza kumhusisha Jerry, Mzee Agapela akataka kuyakata mazungumzo.
‘sitakaa nikuelewe Kristus!... kwanini will ina jina la
Fiona….yaani asilimia 80 ya mali zina jina la Fiona…kwanini?...huoni
unachofanya ni kucheza pata potea…na mbali na hayo siogopi kumtuhumu kuhusika
na kupotea kwa Jerry na…’ Dennis akakatizwa
‘Enough Dennis!’ Mzee Agapela akakemea kwa jazba kidogo
akifumba macho na kusikilizia hali ya mapigo yake ya moyo kwenda kasi.
Akajitahidi kujituliza!
‘….unachofanya ni hatari Krist…’ Dennis akashindwa kuvumilia
‘She is my wife…’ Mzee Agapela akapangua hoja
‘and what about Jenifa….Jerry?’ Dennis hakuelewa
‘najua uliandika will hii ukiwa na hasira baada ya lile tukio
la Jerry na Fiona….but…eeh…huwezi…I mean…’ Dennis alishindwa hata kuweka sawa
sentensi zake
‘Nakulipa ufanye ninavyotaka…. nitakapohitaji ushauri
nitakueleza kwa sasa the meeting is over’ Mzee Agapela akahitimisha mazungumzo
na Dennis akajikuta akilazimika kukubaliana na mteja wake. Wakaagana na Dennis
akatoka mule ofisini na kuelekea sebuleni.
Wakati akiikaribia sebule akasikia akiitwa nyuma na
alipogeuka alimuona Fiona akija kwa mwendo wa maringo huku akitabasamu.
‘Habari za asubuhi?’ Dennis akamsabahi na Fiona akamrembulia
macho tu huku akiimung’unya midomo yake
‘Utakuja kwenye party usiku?’ Fiona akauliza akiitupilia
mbali ile salamu na wakati huo akikitumia kidole cha shahada kuchora chora
kwenye kifua cha Dennis ambaye aliukamata mkono wa Fiona na kuuondoa kwenye
mwili wake
‘Sijajua bado…’ akajibu Dennis akitaka kugeuka na kuondoka
‘Wait’ Fiona akamzuia kwa kuushika mkono wa kushoto wa Dennis
kwa kutumia mkono wake wa kushoto. aliukamata barabara kama mtu alitaka apewe
usikivu kwa lazima. Dennis akauangalia ule mkono wa Fiona kuanzia pale
alipomshika mpaka usoni pake. Akamtlizia macho!
‘I need to talk to you’ Fiona akasogeza uso wake mpaka na uso
wa Dennis na kuyatamka maneno haya kwa sauti ya kutafuna maneno lakini
iliyofika vema masikioni mwa Dennis.
‘Excuse me ma’am’ Dennis akaukwatua tena mkono wa Fiona na
kugeuka. Akachapua hatua za haraka akimuacha Fiona anamtazama kwa ghadhabu
iliyofichwa na tabasamu la kulazimisha.
Dennis alipoishia Fiona alielekea kule ofisini kwa mumewe
Mzee Agapela. Alipoingia tu mumewe aliyekuwa ameshika kitu mkononi alivuta droo
na kukiweka haraka. ingawa alifanya haraka sana lakini tayari Fiona alishaliona
tukio lile.
‘Happy birthday my babe’ akamfuata mumewe na kumkumbatia kwa
nyuma pale kwenye kiti aichokuwa amekaa.
‘thanks honey’ Mzee Agapela alijibu akitabasamu huku akigeuza
kiti upande na kumvuatia Fiona mbele yake.
‘A shopping will do you good…’ akamwambia mkewe na kumfanya
amkumbatie tena kwa furaha na kumbusu kwa fujo. Kule kukumbatiana kulileta
picha tofauti. Fiona alibinua macho yake kuonyesha kile alichoambiwa wala
hakikumgusa. Mzee Agapela naye alionyesha
kile alichosema wala hakikutoka moyoni. Lakini walipoachiana kila mmoja
alikuwa na tabasamu lake usoni. Unafiki ulishafikia ngazi ya digrii!
Baada ya kuchangamshana kwa hiki na kile walitoka mule
ofisini lakini dakika mbili baadaye Fiona alifungua mlango wa ofisi kwa
tahadhari ya kutotaka upige kelele kisha akajitoma ndani na kuufunga tena kwa
tahadhari. Akatembea kwa kunyata akipiga hatua kubwa kubwa mpaka ilipo ile meza
ya kazi ya Mzee Agapela. Akaifungua droo aliyohisi mumewe alitumbukiza kile
alichokuwa amekishika wakati ule alipoingia.
Alipoivuta droo kwa urefu wa kukaribia kuing’oa yote, akaiona
fremu ya picha iliyokuwa imelazwa kwa kuficha picha iliyokuwepo. Akatabasamu na
kuitoa taratibu pengine akijua ni yake. Alikosea!
Moyo ulimdunda mara mbili ya kawaida, mikono ikamtetemeka
alipoigeuza na kuiona sura ya Sophia Agapela. Marehemu rafiki yake aliyemuua
kwa mikono yake, marehemu mke wa Agapela. Alihisi koo likimkauka ghafla kiasi
cha mate kupita kwa taabu. Akaikodolea macho ile picha na asiamini kama ndio
iliyokuwa mikononi mwa mumewe. Alimuua Sophia na kumtoa machoni pa Kristus
lakini kumbe hakuwa amemtoa moyoni mwa mwanaume huyu. Alihamanika!
8888888888888888888888
Sherehe ya Mzee Agapela ilileta mihangaiko mpaka kwa familia
zilizoalikwa kwenye sherehe hiyo. Pamella na mama yake walikuwa katika moja ya
maduka ya nguo mjini wakichagua hiki na kile. Walikuwa wakitembea taratibu
Pamella akiwa na nguo walizochagua, akiwa amezining’iniza kwenye kiwiko cha
mkono huku wakitembea na mama yake sehemu iliyokuwa na nguo nyingi
zilizotundikwa.
‘Nataka kumjua anayetoka na binti yangu….kwanini
unanificha?... I’m your mother…’
‘Najua mama wakati ukifika nitasema…’ Pamella akagoma
kumtajia mama yake jina la mwanaume aliyenaye katika mahusiano. Mama yake
akamtazama kwa jicho la kumrai awe wazi na Pamella akaona aweke wazi.
‘Patrick Mazimbwe’ akatamka kwa aibu kidogo
‘Mazimbwe?... ana undugu na yule lawyer Dennis Mazimbwe?’ Mama
yake Pamella aliuliza kwa shauku akiacha kutembea na kusimama mbele ya Pamella.
‘Yees mom… Patrick Mazimbwe ni mdogo wa mwisho wa Dennis
Mazimbwe’ Pamella alijibu swali la mama yake huku akigeukia nguo aliyokuwa
anataka kuichukua. Akaitoa na kuiweka kwenye kiwiko na kumgeukia mama yake
ambaye bado alikuwa akimtazama kwa mshangao wa wazi kabisa.
‘Mama nini?’ akamzindua mama yake ambaye alitikisa kichwa
katika namna ya kujitoa katika ule mshangao lakini furaha yote ikiwa imetoweka
usoni mwake
‘Mama!... hutaki niwe na mtu au ni nini?’ Pamella akamuuliza
mama yake ambaye uso wake ulishahamanika zaidi
‘No!...no darling…tunahitaji muda tuongelee hili suala…’so
you have been dating Mazimbwe and…’ akakosa maneno na kumfanya Pamella
amshangae zaidi
‘Kuna nini mama?’ Pamella akaona aulize kwa marefu na mapana
na mama yake akashusha pumzi na kutikisa kichwa. Jasho likionekana kumvaa
lakini akajitutumua kujiweka sawa kidogo na wakaendelea kutembea.
Mwisho wa lile eneo lililotundikwa nguo kulikuwa na kioo
kikubwa kilionyesha nje vizuri kabisa. Pamella alifika pale mwisho na kusimama
akitazama nje huku akigeuka na kumtazama mama yake alikuwa akipekua mkoba wake
kama mtu anayetafuta kitu.
Pamella akiwa amesimama pale kwenye kioo akawaona watu wawili
wakiwa wamesimama nje ya duka wakitazama upande uliokuwa na nguo za kiume.
Kwanza aliwatazama na kuwapuuza tu huku akigeuka na kumtazama mama yake ambaye
bado alikuwa akitafuta hicho alichokuwa anatafuta.
Ghafla akili yake ikagonga ubongo wake na kuushughulisha,
akayarudisha macho yake haraka kwenye kioo, upande ule waliosimama wale watu
wawili wakiongea na kunyooshea midoli iliyovishwa nguo za kiume iliyokuwa kwa
ndani.
Akakunja uso na kukaza macho yake, kati ya wale wanaume
wawili aliokuwa anawatazama mmoja alikuwa ameshapata kumuona mahali. Ule urefu,
kile kicheko na ile sura havikuwa ngeni kwake.
‘Oh my God…Nyanza!’ akapiga ukelele na kumshtua mama yake na
baadhi ya wateja waliokuwa mle ndani. Akageuka na kumfuata mama yake kwa kasi
akambwagia zile nguo alizokuwa amezishika na kutoka nje kwa kasi.
Alipamiana na watu kadhaa, na kukimbia kuelekea nje ya duka
lile. Akaangaza na asione mtu tena zaidi ya wapiti njia wengine. Akakimbia
mpaka kwenye kona ya mwisho wa duka lakini watu walikuwa wanapitapita kiasi cha
kutoona dalili za uwepo wao. alichokiona Pamella hakikuwa kivuli.
Alikuwa amemuona Nyanza mwenyewe akiwa na Sakala na wakati
Pamella akikimbia kuelekea ule upande aliohisi wameelekea Nyanza na
Sakala walikuwa wamesimama kwenye kibanda cha magazeti
pembeni wakisoma magazeti huku wateja wengine wakiwa wamewaziba. Pamella
akabaki amesimama pale nje uso ukiwa umetahayari!
Kule ndani mama Pamella alikuwa na simu sikioni, kwenye kona
ya duka
‘Dennis huu sio wakati wa kufanya utani unanielewa…..?’ Mama
Pamella aliongea kwa jazba
‘Patrick hatoki na Pamella…nina uhakika asilimia zote….
msichana aliyetambulishwa kwangu sio Pamella… nashangaa hiki unachoongea…. niko
katikati ya majukumu muda huu…’ Dennis Mazimbwe aliongea kwa sauti ya ukali
kidogo
‘I don’t have to remind you Pamella is your blood daughter
and Patrick is your brother….’ aliyatamka maneno haya akiuma meno na kufumba
macho kuonyesha ni kiasi gani aliumia kuyatamka na kukata simu. Jasho lilikuwa
linamtoka!
…… TWENDE TU UTAYAJUA YOTE…..
tobaaa kumbe pamela yule c babaake!!!
ReplyDelete