Friday, July 19, 2013

SINDI.....NA LAURA PETTIE (28)

28


Alikimenya kiazi cha kwanza na kukitupia kwenye sufuria dogo lililokuwa na maji. alikuwa ameketi kitandani, miguu ikiwa sakafuni na katikati yake kukiwa na beseni dogo lililosheheni viazi mviringo.

Akaokota kiazi cha pili na kuanza kukimenya taratibu, akasita kwanza na kuibua uso wake kuutazama mlango wakati mlango wa chumba kile ukifunguliwa na mfunguaji kujitoma ndani. Alikuwa Jerry!


Sindi Nalela akaurudisha uso wake chini na kuendele kukimenya kiazi kilichokuwa mkononi mwake kana kwamba hakuona mtu yoyote pale mlangoni. Jerry akashuha pumzi na kuchapua hatua za kivivu akimkaribia Sindi na kutua mfuko mdogo aliokuwa nao pembeni mwa Sindi.

‘Habari za hapa?’ Jerry akajaribu kusabahi akitegemea kutoitikiwa na hakuitikiwa kweli. Mawazo uumba!
Sindi alikaa kimya akiendelea na kazi yake, asijali kule kusimama kwa Jerry mbele yake wala kile kimfuko kilichowekwa kando yake. Hasira mwenzake kiburi!

Jerry akajisemesha semesha akilalamikia joto mara usafiri, pengine tu kuleta hali ya mazungumzo lakini ikawa kama mtu anayezungumza na kivuli chake mwenyewe. Akanyamaza!
Akatoka pale mbele ya Sindi na kuifuata kona moja ya kitanda iliyokuwa nyuma ya Sindi na kuvua shati alilokuwa amevaa. Akaketi kitandani na kuvua na viatu huku mara kadhaa akimtazama Sindi kwa kituo na asimmalize.

Akasimama na kuufuata mlango, akitundua taulo lake na kulifunga kiunoni kisha akavua ile suruali yake.
‘Ndoo ya kuogea iko wapi?’ akamuuliza Sindi ambaye hakujishughulisha hata kumtazama sembuse kumjibu. Jerry akashusha pumzi na kuangaza angaza hakuiona hiyo ndoo aliyohitaji. Akafungua mlango na kutoka huku nyuma Sindi akiinua uso sasa na kuutazama mlango ule kana kwamba ndio uliomkosea.

kiazi kilichokuwa mkononi kilikuwa kimememenywa nusu, akachomeka kisu kwenye kiazi akianza tena kumenya kisha akasita. Asimenye wala kutoa kile kisu. alitulia vile akitazama sakafuni kama mtu aliyekuwa anawaza. Ghafla tu akatupa kile kiazi ndani lile beseni dogo pamoja na kisu.

 Mguu wake wa kushoto ukilisukuma mbele lile beseni lililokuwa chini katikati ya miguu yake. Akainama kidogo na kunawa mikono kwenye sufuria lililokuwa na viazi vilivyomenywa.

Akanyanyuka na kutoka mule chumbani, dakika kadhaa Jerry akaingia na kukuta patupu. Akavitazama vile vitu alivyokuja navyo kwenye mfuko, vilikuwa vile vile. Akasikitika na kuketi kitandani. Hakuwa mtu aliyependa magomvi maishani mwake. Ile hali ya Sindi kununa ilimtesa kuliko hata ugomvi wenyewe uliosababisha yote yale.

Akiwa anawaza hili na lile, Sindi akafungua mlango na kuingia ndani akiwa na nguo zilizoonekana zimetoka kuanuliwa. Akampita Jerry na kulifuata sanduku ambalo alizibwaga zile nguo juu ya sanduku.

‘Sindi!’ Jerry akageuka mzima mzima na kumkabili Sindi ambaye hakuitika
‘Mwenye nyumba anadai pesa ya ulinzi..’ Sindi akageuka na kumjibu kwa hasira
‘Kwa sasa hivi sina mama…na..nisikilize kwanza’ Jerry akajikuta akijibu bila kuwaza mara mbili na wakati huo akitaka kumgusa Sindi na kujikuta akisukumwa na ule mkono wake kukwatuliwa.

Sindi alitaka tena kumpita ili atoke nje lakini Jerry akamuwahi kwa kusimama na kumzuia kwa kumvuta na kumbana ukutani.
‘niachie bwana!’ Sindi alisema kwa hasira
‘tatizo nini Sindi…’ Jerry akauliza akizidi kumbana Sindi pale ukutani
. Sin di akafurukuta kidogo na kutulia baada ya kugundua asingeweza  kujinasua pale alipobanwa. Akainamisha kichwa chini na kutazama  pembeni.

‘Nisamehe kwa yote Sindi…. natamani nikueleze hali ilivyo angalau ujue sijakusaliti mke wangu’ Jerry akabembeleza
‘Usiniite mkeo…sitaki usikii’ Sindi akafoka zaidi akisindikiza na msonyo wa kero
‘Wewe ni mke wangu Sindi…’ alibembeleza Jerry, akimtazama Sindi usoni, uzuri wake ulikuwa umeongezeka maradufu. Hata wakati ule aliokuwa na hasira, Jerry aliiona sura nzuri ya kuvutia, kushawishi na kuhamasisha.

‘…Niachie!’ Sindi akainua uso na kumuamrisha Jerry lakini macho yake makubwa ya mviringo yalikanusha ile amri. Jerry akatabasamu kama mtu mzima anayemtazama mtoto mkaidi anayeona ana uwezo wa kupambana naye. Taratibu akamuachia Sindi ambaye alitoka pale ukutani na kwenda kuketi kitandani.

‘Hela ya Ulinzi in ahitajika…’ akarudia tena taarifa yake na kumfanya Jerry naye akaketi kando yake
‘Shing’ ngapi?’ akahoji
‘Elfu sita mia tano’ akajibu akiwa na ile ile hali ya kununa
‘Kwa sasa hivi sina mama…ngoja kesho nikitoka kazini nitakuwa nimeshapata’ Jerry akazungumza taratibu akimtazama Sindi usoni huku moyoni akijua alikuwa anadanganya.

‘Kuzunguka na wanawake uko unajua sana…ila kutafuta elfu sita mia tano mpaka ukazengee kibaruani….huoni aibu Jerry?....hivi ikitokea dharura humu ndani utafanya nini?.... kodi iliyopita nimelipa, umeme nimelipa, hela za taka nimetoa, haya mchango wa jumuiya nimetoa kwa biashara changa tu ambayo hata faida sijaifaidi…wewe kia siku kibaruani cha maana nini ulicholeta hapa zaidi ya simu ambayo umehongwa uko na wanwake wako kisha unakuja kunidanganyia hapa….aibu tupu’ Sindi akasonya na kutikisa kichwa kwa huzuni

‘Sasa unanisimanga kwa kutotoa hela au nini?’ Jerry akahoji kwa jazba kidogo
‘Nakwambia ukweli….wewe ndio mwanaume humu ndani sio mimi…aliyenitoa kijijini kunileta hapa nani kama sio wewe?’ sindi alizidi kuja juu

‘Basi yaishe…naona kukosa kwangu pesa masimango yanaanza’ Jerry alitaka kuuzima ugomvi
‘Masimango ukiyasikia utayajua?....’ akasonya ‘…yaani najuta kuliko majuto yenyewe…  sijui akili ilihamia wapi nikadanganyika hivi… bora hata bikira yangu ningempa Nyanza angenithamini kuliko hivi nilivyojichanganya…’ Sindi akazidi kufoka zaidi

‘Sindi!...Sindi!...’ Jerry akageuka mbogo
‘kwani uongo?’ Sindi naye akapandisha
‘Naona kelele haziishi humu ndani….natoka zangu’ akanyanyuka na kulifuata sanduku ili avae. Sindi naye akanyanyuka na kuvifuata viatu vya Jerry akatoka navyo hadi mlangoni na kuvirusha nje kama takataka

‘Fanya haraka…. nishakutupia matairi yako nje….fanya uondoke nibaki na amani yangu’ Sindi akajibu na kurejea kuketi kitandani. Jerry hata ile tshirt iliyokuwa mikononi mwake aliiona kama kiroba cha simenti ghafla. Akaishia kuishikilia mkononi akimtazama Sindi na asiamini kama ni Sindi aliyekuwa anamjua. Akatikisa kichwa kulia na kushoto kwa sekunde kadhaa kabla ya kutupa ile Tshirt juu ya sanduku na kumfuata Sindi pale kitandani.

‘Hivi ni wewe Sindi Nalela?!’ akauliza akishangaa pia
‘Hapana huyu kivuli chake….fanya hima uondoke’ akamhimiza huku yeye Sindi akinyanyuka na kutoka nje. Jerry akashusha pumzi asielewe hata moja!
888888888888888888888

Meza ndogo iliyopambwa na vyakula vya kuvutia ilikuwa imebarikiwa watu wawili tu. Ukimya uliotawala kati yao ulimaanisha mmoja wapo hakuwa katika hali ya kukifurahia kile chakula cha usiku. Patrick Mazimbwe alitafuna chakula chake taratibu ahuku akimtazama Pamella kwa udadisi.

Mkono uliokuwa na kijiko ulikichota chakula na kukipindua pindua pasipo kukitia mdomoni hata kidogo. kile kilichokuwa mdomoni kilimungunywa na kuzungushwa mdomoni pasipo kumezwa. akili yake haikuwa pale wala hisia zake hazikuwa na yule aliyekuwa naye.
‘heey’ Patrick alimzindua Pamella kwa kugonga gonga meza upande ule wa Pamella.
‘What is wrong honey?’ Patrick akamuuliza Pamella ambaye alivuta tishu na kutema kile chakula alichokuwa akikimung’unya mdomoni. akasogeza kiti nyuma na kunyanyuka

‘Asante Nimeshiba!’ akatoka mezni  na kumuacha Patrick amezubaa na chakula che kwenye kijiko. Naye hamu ya kula ikamuisha. akanyanyuka na kumfuata Pamela ambaye alikuwa anaelekea cumbani.

akatabgulia kuingia Pamella kisha Patrick akafuatia nyuma
‘Whay have I done Pam?’ Patrick akahoji kwa sauti ya kujali.
Pamella akageuka na kulaza shingo yake upande
‘Nothing Pat!...i need to be alone…please leave me alone’ Pamella akaongea kwa huzuni akizidi kumchanganya Patrick

‘ni kuhusu pesa za mini super market?’ uso wa Patrick ulijaa wasiwasi, mashaka na huzuni kwa wakati mmoja. Pamella hakujibu, alikuwa akimtazama Patrick katika namna ya kumtaka amuelewe kuwa alihitaji kuwa mwenyewe kwa wakati ule.
‘Okay babe…chukua cheki hii kesho uka…’ alizungumza akivuta kutabu cha hawala kilichokuwa juu ya meza moja iliyokuwa chumbani kwa Pamella na Pamella akamuwahi na kumkatiza

‘It is not about money Patrick…leave me alone!’ akaongea kwa sauti iliyoashiria alitaka kulia lakini alikuwa akijikaza. Haikuwa sauti ya amri lakini ilimshurutisha Patrick kurudisha chini kile kitabu cha hawala  na kumtazama Pamella kwa huzuni.

‘ukihitaji chochote…please let me know babe’ akamnasihi huku akimfuata na kumkumbatia. akambusu kwa upendo na Patrick akaondoka akimuacha Pamella mwenyewe. Ni kama alisubiri kwa hamu Patrick aondoke ili ajipe nafasi ya kuomboleza. aliketi kitandani na kujiinamia akionekana wazi alikuwa akitokwa na machozi. Ghafla tu akasimama na kukifuata kioo kikubwa kilichokuwa ukutani. akajitazama usoni akijaribu kutabasamu katikati ya huzuni ile. Jerry Agapela alikuwa amegeuka mwiba wenye ncha kali moyoni mwake! Pengine alijua Jerry angeendelea kumlilia na kumbembeleza miaka yote. ukweli kwamba ipo siku angechoka na kutazama pembeni haukuwahi kupita akilini mwake. Mabadiliko ya Jerry yalikuwa kama kutandikwa fimbo ya utosi!
8888888888888888888888

Ndani ya chumba kimoja kilichosheheni makorokoro mithili ya stoo. Vijana wawili walikuwa wameketi mkekani wakiushambulia ugai kwa samaki wadogo wadogo wa kukaanga almaarufu kama dagaa mchele. Maongezi yao yalionekana kujaa vicheko na raha tele huku ugali ulisogea kwa kasi kubwa.
‘Pale Mwenge pazuri mno kwa biashara hasa nguo za kike….nimepapenda sana’ Nyanza alimeza funda la ugali na kuzungumza huku lafudhi yake ya kisukuma ikisikika kwa mbali.

‘Kuna wateja nawafuata kabisa majumbani…biashara ya nguo inalipa sana…kuna kiwanja geza ulole ukoooo nje ya mji nimenunua kwa biashara hii…’ Sakala alimjibu naye akikwanyua samaki wale na kuwatia mdomoni.
‘….ukishazoea mji tu basi hakuna kitakachokushinda binamu’ akaendelea kumtia moyo Nyanza ambaye sasa aligeukia sufuria la ugali na kunawa yale maji yaliyotumika kulowekea sufuria. Akanyanyua jagi la maji na kujimiminia katika bilauri ya chuma. Akapiga funda kadhaa na kunyanyuka, mwenyeji wake naye akivuta lile sufuria na kunawa.

Wakasafisha liel eneo walilotumia kulia na Sakala akamuonyesha nyanza godoro la kulalia, yeye akimuaga kuwa anenda kwa mpenzi wake anayeishi mtaa wa pili. Sakala akaondoka na Nyanza akabaki peke yake. Akatoa biblia yake na kussoma kabla ya kusali. Taratibu katika ile biblia akaitazama picha ya Sindi Nalela nay eye wakiwa wamesimama kwenye mti. Picha pekee aliyopata kupiga na Sindi.

Aliitazama Picha ile kwa muda kabla ya kuifungia katika biblia na kuiweka chini ya mto. Akatulia akiwa amelala chali na kuitazama dari kichwani mwake sauti ya Sindi, vicheko vya Sindi, matani ya Sindi na taswira ya Sindi vilishidana kupishana na kumfanya atabasamu.
‘Sijaona kama wewe Sindi….uko uliko jitunze mke wangu…jitunze niwe wa kwanza kwako…niwe wako milele zote’ akatamka kwa matumaini makubwa lile tabasamu likizidi kuchanua.
8888888888888888888888888

Mlinzi wa kwanza anachungulia kwenye kitundu cha kuangalia nje. Anashtuka na kutoa macho. kidogo azimie palepale, anajikaza kisabuni na kurudi kinyumenyume. mwenzake aliyesehemu yao ya kupumzikia anamshangaa na kumhoji
‘Oyaaa vipi?’ anamuuliza kwa sauti ya chini kidogo na anapoona mwenzake anazidi kurudi kinyume nyume. anachukua silaha na kumfuata mwenzake

‘Kuna nini?’ anauliza na mwenzake anamuonyesha kule alikochungulia
‘Kuna nini kwani?’ bado anauliza na asipate hata ujasiri wa kwenda alikotoka mwenzake.

Kengele inalia tena na  wote wanatazamana. ujasiri kati yao unatetereka kidogo kama binadamu. Yule mlinzi wa pili anaamua kujitosa kwenda kuona alichoona mwenzake.
‘Ooh mama!’ anapiga yowe akirudi kinyume nyume na kuanguka, bado anasota kwa matako na mikono kurudi nyuma kumbe ya kheri na mwenzake.

Sasa nyuso za hofu zinafanana na kengele inapolia tena. Yule mlinzi wa pili anapiga magoti na kukemea alichoona
‘Baba wewe ni ngao…wewe mkuu wa wakuu wewe ni muweza…eketeza roho ya pepo…katakata roho ya kuzimu…teketeza…’ anakatishwa na mwenzake
‘inakuwaje sasa?’ mwenzake anauliza na anamharibia sala mwenzake. Shetani anacheka nusu kufa!

Jerry Agapella anaisikia ile sala na kujikuta akicheka kule nje
‘Oyaa swedi fungua bwana’ anamuita mlinzi mmoja kwa jina la sasa wanapigwa na bumbuwazi kabisa. macho yakitoka mithili ya mtu anayemeza tango pori.
Kwao Jerry ni marehemu, ukichanganya na vile alivyokuwa amevaa. Akili zao zilihama. Ilikuwa heri kukutana na mwizi aliyehai kuliko kukutana mtu  aliye mzimu!

Baada ya hekaheka ndogo ndogo, wakafungua mlango na Jerry akaingia kwake. Akaingia mpaka ndani. Alizunguka ndani mwake akitazama vitu vyake namna vilivyokuwa vimejaa vumbi. alitabasamu kwa huzuni akikumbuka mara mwisho alipokuwa akitoka pale kwa ajili ya safari yake. Alitabasamu kwa huzuni.

Akaketi kwenye kiti kimojawapo katika meza ya kulia chakula na kutulia hapo. Akaitazama simu yake ya mkononi aliyopenda kuitumia nyumbani hapo. ilikuwa palepale alipoiacha na kama ndani mwake kulikaguliwa basi simu ile haikuguswa kwa kutoonwa au kupuuzwa vile tu ilikuwa mahali ambako palijaa vitabu kibao

Akaichukua simu ile na kuitazama kwa sekunde kadhaa. Machozi yakimlengalenga mwanaume huyu. kama mtu aliyejikaza kisabuni alibonyeza namba zilizoonekana kukaririwa kichwani. Akaipiga ile namba na kuiweka simu sikioni huku tabasamu la huzuni likiupamba uso wake. Aliisikilizia namba ile ikiita

‘Hallow…’ sauti nzito, sauti aliyoitambua mara moja, sauti aliyoimiss kwa muda mrefu, sauti ya baba yake Mzee Agapella ilipokea
‘Hallow…’ iliita tena na Jerry hakuweza hata kuipokea machozi yalimtiririka pamoja na kujikaza kiume
‘Jerry…’ baba yake aliita naye sauti yake ikionekana kutetemeka
‘Naam baba’ akamudu kuitika na wote wawili wakawa wakitirirkwa na machozi pasipo kuongea lolote tena. kila mmoja alibanwa na kwikwi kooni.


………... LETS GOOO…….

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger