51
Maneno yaliyokimbizana toka kichwani mwake yaliishia
kusikojulikana, kinywa kilibaki wazi wakati macho yakiongezeka ukubwa kwa kadiri
alivyoyatumbua, ile mikono aliyoifumbata kifuani ilitetemeka kiasi cha
kuonekana dhahiri ikitingishika, Kwa wakati ule kichwa chake hakikufanya kazi
sawa sawa, hakuna alililofikiri kwa muda ule, fuvu lilibaki tupu tu kama mtungi
uliotoboka. Wahaka juu ya wahaka!
Patrick akasimama, naye akitanua macho na kuvuta pumzi kwa
nguvu kidogo, kujipa nafasi ya kuzuia yale machozi yaliyomtoka kwa uchungu…
akayafuta kwa mkono ule ule uliokuwa na bastola, akitumia ile sehemu ya mkono
wa sweta alilokuwa amevaa.
Zile hatua chache alizopiga zilimrejeshea Pamella akili yake
na akagundua maisha yake yalikuwa hatarini. Hakujipa nafasi nyingine ya
kufikiri, aliugeukia mlango na kuhangaika na kitasa, akijaribu kulilenga tundu
la ufunguo pasipo hata kukitazama kile kitasa alichokuwa anahangaika nacho.
Hakufikia hata theluthi ya lengo lake, Patrick alishamfikia
na kumuondoa pale mlangoni kwa mtindo wa kumvuta na kumsukumia mbali
‘Mama yangu…Mungu wangu!’ yowe la hofu likamtoka, wakati
akipepesuka na kuangukia kando ya meza iliyokuwa katikati ya sebule yake. Hofu
ya kifo aliyokuwa nayo ikamrejea maradufu ya mwanzo wakati akimtazama Patrick
aliyekuwa amesimama pale mlangoni akimtazama pamoja na ile bastola mkononi. Kwa
sekunde zile hakuwa Patrick mchumba wake wa zamani… si tu kwa ile sura ya
kikatili aliyokuwa nayo muda ule bali kwa kule kumshikia bastola, kwa Pamela
kulimaanisha kifo!
‘Patrick Please…Patrick nisikilize’ aliita sasa machozi
yakizivamia mboni za macho yake na taratibu akisota kurudi nyuma, aliyekuwa
anamlilia akamuacha asote mpaka afike aendako na akagotea kwenye sofa na
kutulia hapo akijikunyata na kutetemeka zaidi. Zilikuwa zimekatika dakika
kadhaa na Patrick alikuwa hajaongea chochote. Hili lilimuwewesesha kupitiliza!
‘… haikuwa nadhiri
yangu Patrick’ akarai, akijaribu kukisia sababu ya ujio wa mtu huyu
‘Patrick nakuomba’ akarai tena na sijue ombi lake lilimaanisha
nini. Aliyekuwa anamrai alikuwa ameinamisha kichwa chini tu pasipo kumsemesha
wala kumfuata pale alipokuwa akitetemeka.
Ukimya ukapita kati yao hadi pale Patrick alipoamua kwa
hiyari yake kuuvunja ule ukimya kwa swali lililotua kichwani mwa Pamella kama
kipande cha tofali.
‘Unaolewa na Jerry.. si ndio?’ Patrick akauliza akinyoosha
shingo yake na kuikakamaza kana kwamba swali lile aliliuliza akitarajia jibu
tofauti. Pamella hakujibu alimtazama Patrick kwa huruma, uso ulishalowana
machozi yaliyochanganyikana na jasho… kwa dakika zile tu alishachakaa. Hofu
kitu kingine!
‘Nimekuuliza swali!’ Patrick akasisitiza kujibiwa na Pamella
hakujua ajibu nini kunusuru maisha yake. Alitaka kukataa lakini akili yake
ilimuonya kuwa Patrick alikuwa anaujua ukweli wote sasa… alitaka pia kukubali lakini
akili yake ikamuonya pia kuwa angesambaratishwa palepale. Akabaki njia panda na
asijue ni kiasi gani alizidi kuipandisha hasira ya Patrick Mazimbwe.
‘…Pamoja na yote niliyokufanyia Pamella… Pamoja na yote Pam…
hivi hiki ndio umeamua kunilipa?... kuniacha kwa staili hii… namna hii… come on
Pam… niambie ulihitaji nini ambacho sikuweza kukupatia?... I worked hard kama
mtumwa nikidhi mahitaji yako…starehe zako… na kila kitu… ni hiki ndicho
ninachostahili in return?’ Patrick aliongea kwa hasira akitembea toka pale
mlangoni na kumkaribia Pamella na kisha kurudi mlangoni.
‘Patrick sivyo unavyowaza… sivyo Pat… sivyo dear’ akajitetea
Pamella akiinua mikono juu katika namna ya kuomba huruma ya Patrick.
‘usiniite dear Pam…usicheze na akili yangu…’ akakemea Patrick
‘Namaanisha ninachoongea…’ Pamella akapata nguvu ya kujibu
sasa baada ya Patrick kuweka nyuma ile bastola aliyokuwa nayo mkononi
‘kipi?...kuwa unampenda Jerry kuliko mimi…si ndio?’ Patrick
akauliza kwa sauti ya juu ya kupayuka
‘No… ni chaguo la wazazi wangu Pat… why would I break up
namna ile bila sababu…why?... sikuwa na jinsi’ akajitetea Pam machozi
yakimtiririka na taratibu akijiinusha na kupiga magoti mbele ya Patrick… mikono
yake ilinesa nesa hewani wakati akitafuta cha kujazia sentensi za utetezi wake
na asikipate
‘So unaolewa na Jerry?’ swali likarudi palepale
‘Patrick I love you…I swear…I love you’ Pamella akaropoka
akidhani pengine angeliweza kuibadili hali ile na ghafla tu akasikia risasi
ikipiga hewani na kumfanya aangushe yowe lingine kali a kujikunyata.
Alitetemeka kuliko mwanzo, akalia kuliko mwanzo
‘Uongo mwingine ukiongezeka… watakuta maiti mbili hapa…
tukukose wote’ Patrick akaonya na sasa akimvunja nguvu zote Pamella aliyekuwa
analia bila mpangilio. Akikiona kifo mbele yake. Patrick akaokota chupa ya
pombe na kupiga funda kadhaa.
Ule mlio wa risasi ulisikika mpaka kwa mlinzi pale nje,
alitoka mbio mpaka dirishani na kujaribu kuchungulia ndani. Lakini vioo vya
madirisha havikumruhusu kuona ndani ispokuwa aliisikia sauti ya Patrick na
vilio vya Pamella.
‘Hofu aliyokuwa nayo ilimfanya atoke kuomba msaada kwa
walinzi wenzake. Dakika kumi tu zilitosha kukusanya watu kadhaa nje ya nyumba
ya Pamella.
‘Usiniue Pat… nakuahidi it is me and you mpaka mwisho hata kama
nitaolewa na Jerry kwa shinikizo la wazazi… moyo wangu uko kwako Pat’ Pamella
alilia na akamlilia Patrick mno.
Majibiszano yao yakakatizwa na sauti za watu kule nje…
Patrick akatanua pazia dirishani na kuona kijiumati kidogo cha watu. Akaiweka
bastola yake kwenye midomo yake akimpa Pamella ishara ya kunyamaza kimya.
Akatulia na kusikilizia zile kelele nje
‘Utafungua mlango na kutoa kichwa tu na uwaambie hakuna
tatizo… kinyume na hapo nitaachia risasi ya kisogo’ Patrick akaongea kwa sauti
ya amri akimuamrisha Pamela asimame pia.
Kwa woga akasimama na kujifuta machozi, akampita kwa hofu
Patrick na kufungua mlango. Akasita kwanza na kuusikilizia mdomo wa bastola
uliokuwa kisogoni mwake. Dakika zile alijihisi kufungiwa kipande cha bomu
kisogoni, alihisi baridi mpaka kwenye mifupa!
Akafungua mlango nusu, akimeza mate kwa juhudi kubwa mno,
akajilazimisha kutabasamu na kuongea mawili matatu aliyoona yangeridhisha nyoyo
wale watu pale nje. Mazungumzoa yakachukua sekunde za kutosha kumfanya Patrick
aikandamize ile bastola kisogoni. Pamella akafumba macho na kuuma meno,
alikaribia kuachia yowe kubwa lakini onyo alilopewa lilimkumbusha utamu wa
uhai. Akagugumia chini kwa chini.
Baada ya watu wale kujiridhisha wakaondoka ingawa mlinzi wake
alibaki amesimama akishangaa pengine akili yake ikijiuliza mara mbilimbili kile
alichokisikia. Mlango ukafungwa na Pamella akageuka na kusimama wima kama
mlingoti, kisogo kikielekea mlangoni sasa.
Ile harufu ya pombe kali ikamfikia vema na wakati Patrick
alipomkaribia zaidi na kuitumia bastola yake kuupapasa uso wake, Pamella
alipeleka uso pembeni. Ikawa kama amempa ruhusa na kuibusu shingo yake hali
mkono ule usio na bastola ukivifuata vifungo vya vya blauzi ya Pamella.
Akafurukuta akitaka kumzuia na mdomo wa bastola ukahamia
chini ya kidevu. nguvu zikamuishia, akaweweseka na machozi yakashika kasi sasa
wakati Patrick alipoitatua ile blauzi ya Pamella kwa nguvu zote na
kuvisambaratishia mbali vifungo vya blauzi ile.
Alijua kitakachofuata, alijua kama angepambana kuna hatari kubwa
ingempata, akajaribu kutulia kwanza wakati Patrick alipokuwa amesimama mbele
yake akimtazama tu.
‘Nakupenda Pamella… usiniache’ Patrick akasema kinyonge
akimtazama Pamella usoni. Akajitutumua kutabasamu macho yake yakiitazama kwa
kuibia bastola ile aliyoshika Patrick.
‘Niahidi hutaniacha’ akaomba Patrick akimsogelea tena Pamella
na safari hii akiirudisha nyuma ile bastola aliyokuwa nayo
‘…siwezi kukuua Pam… nitaanzia wapi… nitaanzia wapi Pamella’
akaongea kwa sauti ya kilevi akiuondoa mkono uliokuwa na bastola kule nyuma na
kumshika Pamella aliyeshtuka kidogo na kumkodolea macho mwenzake akiwa badi na
ile hofu.
Wakatazamana, wakatazamana tena na tena na taratibu Patrick
akamfuata Pamella kwa ukaribu zaidi, akambusu, akampapasa wakati Pamella
akishindwa kutoa ushirikiano wowote ule kwa sekunde chache za mwanzo kisha naye
taratibu akajikuta akiinua mikono na kutoa ushirikino. hakujua tu kuwa hili
alilokubali kulifanya sasa lingeiwinda furaha yake baadaye! kwa wahati huu
hakuwaza, hakujua wala kufikiria!
88888888888888888888888888
Adella alitembea kwa kasi wakati alipoufungua mlango wa ofisi
yake na kukifuata kiti chake cha kazi huku nyuma Tima naye akiingia na
kuubamiza mlango,
‘Kwanini?... ili iweje?...’ Tima aliuliza kwa ghadhabu wakati
Adella akishika afaili moja na kuliacha kisha kushika lingine na kulibamiza
mezani kwa hasira
‘Kwasababu ni ofisi yangu na Sindi ni mjakazi wangu… tangu
lini unanipangia cha kufanya Tima… tangu lini? Adella akauliza kwa hasira akiwa
amesimama kando ya meza yake
‘Tangu sasa Adella… this is too much… mimba yake ni kubwa
sasa…mtoto ameshajiumba… unataka kuitoa mimba ya miezi minne kwa roho gani
uliyonayo… kwanini wako hukumtoa akiwa tumboni’ Tima naye akahoji kwa hasira
akiweka mbali heshima ya mtu na bosi wake.
‘Wow! this is serious… isn’t it?’ Adella alikunja uso wakati
akiuliza hili swali
‘na zaidi… kama unadhani binti yule nakuletea hasara niko
radhi nishike nafasi yake mpaka atakapojifungua… niko tayari kutumika tena kama
ninavyokutumia ili niokoe maisha huyu kiumbe… kama ni pesa ndio inayokupa roho
hii ya kinyama acha nika hudumie wateja wako kwa ajili ya Sindi’ Tima akongea
kwa kujiamini
‘…huyu binti anakuhusu nini Tima?’
‘Hanihusu kitu na kumsaidia mtu si mpaka akuhusu… nimepitia
magumu mengi lakini haijaniondolea utu wangu… never… never’ Tima alizidi kuwa
mkali
‘Unapambana na mimi sio?’ Adella alikuwa bado hajaamini kama
Tima alikuwa ameamua kulishupalia suala lile kwa nguvu zote
‘Sina cha kupoteza… kufa?.. nani ambaye hatakufa?...
uniue?... tangu nilipopoteza mtoto wangu nilipotea naye…nilikufa naye… sina cha
kupoteza Adella.. sina’ Tima alikuwa amesimama imara mno na Adella akamtazama
na asiamini. Alikuwa amemtumikia kwa miaka mingi mno na pamoja na yote mabaya
aliyomfanyia. Tima ndiyo alikuwa kama nguzo yake kwa nyakati kadhaa ingawa bado
alikuwa mtumishi wake
‘unahitaji kupumzika Tima… niache peke yangu kwanza’ Adella
akajibu na Tima akaondoka taratibu na kumuacha mwenyewe. Machozi yakalenga
Adella, kwikwi moja kali ikamkaba kooni na akajikuta akiuma midomo yake na
kubana pumzi kwa ndani kisha akshusha pumzi moja ya nguvu. Akakaza roho
akaufuata mlango na kutoka!
Kule chumbani kwa Nadina na Sindi kulikuwa na maongezi kati
yao. Sindi alikuwa analia wakati akisimulia alikoyapata yale madawa. Alikuwa
amemuibia yule muhindi anayemchezea nachi. Alitaka kufa taratibu, alitaka kufa
bila maumivu, hakukuwa na dawa yoyote ya kumfanya ajiue kama alivyotaka, njia
pekee na rahisi aliiona ni ile.
Sindi aliongea mengi na kwa mara ya kwanza Nadina alibaki
mdomo wazi wakati akimsikiliza Sindi huku naye akitiririkwa na machozi. Sindi
alikuwa kimya siku zote lakini hakuacha kukumbuka kwao, kumkumbuka mama yake na
familia yake hususani mdogo wake Peter.
Sindi hakuacha kuumia
kwa yale maisha aliyokuwa anaishi, hakuacha kuumia alipomkumbuka Jerry na
ulaghai aliomfanyia, akaumia zaidi kuwa alikuwa na mimba ambayo aliamini
alipewa na mtu ambaye hakuwahi kumpenda bali alikuwa akimtumia. Aliamini Jerry
hakuwa na mapenzi na yeye na pengine alishasahau kama aliwahi kuwa na msichana
kama yeye.
‘lakini bado unampenda Jerry’ Nadina akamuuliza kwa upole na
Sindi akajilazimisha kutabasamu na kuitikia kwa kichwa
‘Sana…sana tu!’ akajibu akilishika tumbo lake. kuna mtu mmoja
tu hakugonga kichwani mwake. Nyanzambe Mugilagila!
Wakati wakiongea na kufarijiana, mlango ukafunguliwa na
Adella akaingia na kusimama karibu na mlango
‘Uwe tayari kesho jioni… kuna mtu atashughulikia suala lako…
kama unataka kulia na kuomboleza… it is okay… baada ya wiki utarejea kazini…
abortion njema’ akatamka kwa tabasamu kana kwamba alichokuwa anaongea kilikuwa
kitu cha maana na faraja. Akatoka na kuwaacha mabinti hawa wamepigwa na butwaa
kisha ghafla wakaangua kilio na kukumbatiana.
Kule kuponea chupuchupu kukiona kifo kulimfanya Sindi aione
thamani ya mtoto wake na dhambi yake ya kutaka kumuondoa lakini hili la mtu
mwingine kumuondolea mwanaye tumboni kwa nguvu na shurti lilikuwa zaidi ya
maumivu. Aliutamani muujiza! kwa mara ya kwanza alishuka sakafuni na kupiga
magoti akiinua mikono juu… Akamuita Mungu kwa sauti, akilia na akageuka kulia
na kushoto akiitazama dari na kusihi Mungu amsikie japo katika hili tu.
8888888888888888888
Kulikucha! siku nyingine ya juma, siku mpya. Sebuleni kwa
Okello, sehemu ya kunywea chai wanawake wawili walikuwa mezani wakistaftahika.
Wakiongea na kucheka kuonyesha namna asubuhi ile ilivyokuwa njema kwao
‘… lakini hivi Dennis Mazimbwe alishatalikiana na mkewe?’
Annie, dada yake Rebecca akauliza wakati akitua kikombe cha chai kwenye kisosi
chake
‘Waaapi!... Daniella amerudi mwaya… tena kwa kashda na
tashtiti’ Rebecca akajibu akivuta midomo yake
‘usiniambie!...’ Annie alisukuma kikombe cha chai mbele
kidogo
‘karudi… kajaa tele… na wiki aliyokuja… tuligongana
supermarket… akaninyeshea mvua ya kejeli almanusura nimtie kofi’ Rebecca
akaongea kwa hisia hasa
‘Hahahahaa umtie kofi mwenye mali… sijaona mzungu mvumilivu
kama huyu… na yooote yale bado karejea tu?... na Dennis anasemaje?’ Annie
akauliza akilaza shingo upande
‘Analo la kusema?... nimemuweka hapa’ vidole vinne toka kile
cha mwisho vya mkono wa kulia vikagonga kiganja cha mkono wa kushoto.
kumaanisha alipomuweka Dennis
‘Hafurukuti!’ akatamba Rebecca
‘Mmmmh… mwanasheria na mvi zake!’ Annie akashadadia na
Rebecca akacheka
‘Yote kwa yote… huyu Mzee uliyemkubalia ndoa bila mapenzi
toka moyoni akijua hii misele yako
tutachonga majeneza mangapi na ya futi
ngapi?’ Annie akaisema hofu yake
‘Atajulia wapi?... akili yake inawaza aninunulie gari gani…
anipeleke wapi basi… ipo siku nitadai talaka yangu na nitaolewa na Dennis’
Rebecca akaonyesha dhamira yake
‘Na huyu Mzee akuache uende tu… na Dennis akupokee tu wakati
Daniella yupo?’ Annie busara zilimuongoza kuliko mdogo wake
‘hawezi kunifanya kitu bwana… nasubiri kusikia wanatalikiana
lini ili nijue naanzia wapi… siwezi ishi maisha ya kujifanyisha ninampenda mtu
wakati nimependaye yupo hai tena karibu tu… it is time niishi maisha halisi’
Rebecca akaongea kwa kujiamini
‘Hayaa!... hakikisha kabla hujaomba talaka lile duka la jumla
na lile duka la vifaa nya ujenzi unaandika jina la langu kabisa… hatutaki
kugombea mirathi sie’ Annie akamfanya Rebecca acheke sana na wakati huo mlango
ukafunguliwa na Pamella akaingia akiwa na mifuko ya shopping
‘Yaani umemrithi mama yako mpaka tabia za kipuuzi..’ Annie
akamdaka Pamella aliyeanza kucheka kabla ya salamu
‘Shopping asubuhi asubuhi…’ Annie akajiinusha kumlaki
Pamella. Akamsaidia baadhi ya mifuko na kuiweka mezani. Pamella akamuinamia
mama yake na kumbusu shavuni kama salamu kisha
akaketi. Kulia kwake akiwa mama mkubwa na kushoto kwake akiwepo mama
yake.
‘ gauni la kitchen party lipo tayari… naaa…’ akakatizwa na
mama yake mkubwa
‘ya magauni na magagulo weka kando kwanza… mwanangu itabidi tuongee
kidogo kuhusu uko unakotaka kwenda’ Annie akaanza
‘Aunt sidhani kama kuna jipya ambalo silijui… namjua Jerry
ndani nje’ Pamella akataka kukwepa yale maongezi
‘Wapo waliowajua juu chini na ndoa zikawa chaaali!... mtoto
mbishi wewe… hebu sikiza uko… usije ukatupa shida anayoileta mama’ako sasa
hivi’ Annie akananga na Rebecca akaguna kuonyeshwa kutopendezwa na lile jiwe
alilorushiwa
‘Unaguna nini?... una kipya kipi cha kumfunda mwanao
ukajivunia kuwa mama… kakufuma na mwanaume mwingine kesho na keshokutwa mambo
yakienda mrama tutasikia na yeye kafumwa na mwanaume mwingine… upuuuzi mtupu…
weka masikio yako hapa… ujue ndoa sio kwenda kubadili mikao kitandani tu… sio
kwenda kuamrisha watumishi ndani… sio kujivika mivyuma kidoleni mpaka mifupa
inapata kutu… ni zaidi ya hayo na mumeo huyu… alivyo vile… ukileta ubishororo
utageuka pazia la stoo ndani.. halifungiliwi wala halisogezwi… mwanaume
anatunzwaa mwanangu’ Annie akaongea kwa kunesa nesa na Pamella akazungusha
macho yake kuonyesha nusu aliyakubali na nusu aliyakataa
‘Siendi kuwa housegirl ma’ mkubwa!... na anajua nimetoka
familia gani mimi’ Pamella akajitetea
‘Haya!... mwanaume wa kiafrika huyu… kijana kabisaa …umletee
madoido ya kizungu… sawaaa… usijekuitisha tu kikao cha dharura kuomba silaha za
maangamizi … nitakusuta na tarumbeta za bendi ya magereza’ Annie akawachekesha
mtu na mama yake na maongezi mengine yakichukua nafasi. Pamella alidhani
alikuwa amemjua Jerry vya kutosha bila kujua moyo wa mtu ni kiza kinene!
Rebecca akasimama na kuwaambia alikuwa najiandaa kutoka!
88888888888888888888888
Dennis Mazimbwe alikuwa ofisini kwake pamoja na mzee Kristus
Agapella. Walikuwa katikati ya maongezi yao ya kikazi na Mzee Agapella alikuwa
anahitaji kubadili wosia wake tena. Alitaka kuliondoa jina la Fiona katika
wosia ule na Dennis alikuwa anamshangaa.
‘ni maamuzi tu… huu utakuwa usia wa mwisho na sitaubadli
tena’ Mzee Agapella akaweka msimamo wake ambao bado ulikuwa umemfanya Dennis
amtumbulie macho Mteja wake na asiamini.
‘… wewe huyu huyu ndio unabadili usia?... unamuondoa
Fiona?... hivi ni nini kimekuonyesha nilichokuwa nakiona?’ Dennis akauliza
akitabasamu
‘wanawake watu wa ajabu sana Dennis…’ Agapella akatikisa
kichwa
‘Fiona ni zaidi ya ajabu… yuko wapi kwanza?’ Dennis akauliza
‘Nilidhani unajua alipo… niliambiwa mko karibu sana’ akapiga
kijembe akikumbuka maneno ya Mzee Okello aliyewahi kumwambia amchunge sana
Dennis anaweza kuwa anatembea na mkewe
Dennis akacheka kwa sauti, akacheka sana kisha akamtazama
Mzee Agapella
‘Fiona atakuwa mwanamke wa mwisho kuhatarisha maisha yangu
sababu yake… huwa anakuja hapa kushawishi hiki na kile… ila ni muda sasa
sijamuona… lakini sio kuwa na ukaribu… mimi na yeye hatuivi pamoja…’ Dennis
akajitetea akianza kukusanya makabrasha yake kama mtu anayetaka kujiandaa
kutoka
‘Sijui alipo… sijapokea simu yake hata moja… moyo wangu
umekuwa na wingu zito juu yake.. nahisi nahitaji kukaa mbali naye kwa muda’
Agapella akaongea kwa masikitiko na wakati huo simu yake ikiita. Akaipokea na
kuongea na mpigaji ambaye alikuwa Mzee Okello.
‘Okay, bwana sasa andaa kila kitu kuhusu wosia… nitakuja
kesho jioni tuzungumze zaidi na kuhitimisha kila kitu… Mr. Okello yuko hapo
kwenye maegesho… tunaelekea kwenye ule mkutano wa wawekezaji...’ akaongea
Agapella akinyanyuka na kuweka sawa suruali yake kiunoni
‘Oh! kumbe ni leo… sawa basi… nadhani kabla ya wiki hii
kuisha kila kitu kitakuwa kwenye mstari’ Dennis akaitikia na wakapeana mikono
na Mzee Agapella akatoka. Dennis akabaki mwenyewe ofisini, dakika mbili tatu
mlango ukafunguliwa na Daniella akaingia
‘That is my wife!’ Dennis akamlaki akisimama na kumbusu mkewe
midomoni kabla ya kumuachia kiti chake na
yeye kujiegemeza kwenye meza
Wakatazamana tu huku Daniella akitabasamu kama mtu aliyetaka
kusema kitu cha furaha
‘haya niambie…’ Dennis akamuhimiza
‘Nascom wamekubali kufanya kazi na mimi’ akaitoa hiyo taarifa
iliyomfanya Dennis ataoe macho kwanza
‘Wow!...’ akabweua kwa furaha akimvuta mkewe na kumkumbatia
kwa nguvu akamuachia kidogo na kumbusu mkewe kimahaba
‘…I’m proud of you babe’ Dennis akampamba Daniella na kumbusu
tena pajini
‘But… umeahidi kuvunja uhusiano wako na Rebecca… na iwe hiyo
Dennis… iwe hivyo darling… just you and me and our kids…’ Daniella akamdekea
mumewe ambaye alitingisha kichwa kukubalinaa naye.
‘Nakupeleka lunch leo… kila kitu juu yangu’ Daniella
akamwambia mumewe naye akainua mikono juu kama mateka. Akitoka pale kwenye meza
na kulifuata koti lake.
‘Natumaini itakuwa mwanasheria wa Nascom bi. Daniella Mazimbwe…’ Dennis akatania na
kumfanya Daniella acheke kwa nguvu
‘… nadhani walitarajia kukutana na muafrika
mwenzao...nilipotokezea mbele yao it was like… Huh?! are you bi. Mazimbwe?’
Daniella akaongea akicheka
Furaja ilikuwa imerejea maishani mwao, ndoa ilianza tena
kuimarika .
Wakati wanandoa hawa wakiongea hili na lile Rebecca Okello
alikuwa akiegesha gari lake mbele ya
jengo lile la ofisi ya Dennis. Alikuwa pale kumchukua Dennis kwa ajili ya
chakula cha mchana kama alivyozoea kuja kumchukua kila alipojisikia.
888888888888888888888888
Fiona Agapela alikuwa akijipamba mbele ya dressing table.
alihangaika na wanja, akauweka shika chini na kushika lipstick akauweka chini
na kuokopa sponji ya kusawazishia poda… akaipitisha usoni mpaka aliporidhika na
ule mwonekano.
Wakati alipojitazama tena akagundua kucha zake za mkononi
zilikuwa zimebabuka rangi na hazikuvutia. akavuta droo ya dressing table na
kutafuta pamba. Akapekua pekua mpaka alipoiona pamba lakini pia akavutika kuona
kimkebe kizuri cha kuvutia kilichokuwa mule ndani ya droo.
Akataka kukipuuuzia lakini akajikuta tu akikichukua huku
akitabasamu na kukifungua. Akakumbana na mkufu mzuri wenye kidani cha almasi.
Kwanza aliduwaa nao mkononi kabla ya kukurupuka kuugeuza geuza kama mtu
anayeuchunguza. Akatoka mbio mpaka kwenye sanduku lake. Akalifungua na kutoa
mkebe mkubwa uliohifadhiwa chini ya sanduku na kuufungua. Akamwagia kitandani
vitu vyote vilivyokuwa ndani humo.
akachakura kwa kupangua hiki na kile na hatimaye akaupata
mkufu wake uliofanana vile vile na huu alioutoa kwenye dressing table ya rafiki
yake iloma. akalinganisha, mikufu ilifanana kila kitu mpaka mkebe wa kutunzia.
Akazubaa kwanza akili yake ikirudi nyuma miaka kadhaa… Mzee Agapella
alipomletea zawadi ya mkufu huu siku ya kuzaliwa kwake.
Fiona akakunja uso, akili ilimletea maswali na majibu
yasiyooana hata chembe. Rafiki yake alikuwa si mtu wa kuvaa vidani vya gharama
kama hivi. hisia zilizomjia ghafla kichwani zilimfanya atunduwae, jazba nazo
zikipanda sekunde hata sekunde
‘Iloma?!’ akajiuliza, akajiuliza kwa sauti kubwa akishangaa
pia
ITAENDELA….
Mimba ya Sindi itakuwaje?... Dennis kule ofisini itakuwaje…
Iloma na Fiona itakuwaje?
Usikose kurudi hapa hapa!...Tuko katikati ya starehe karibu tukielekea ukingoni
tatizo unachelewa sana laura kurudi huku kwenye hadithi majani tunakaa week mbili hadi tatu jamani
ReplyDelete