Thursday, January 30, 2014

SINDI....na LAURA PETTIE (55)

55

Aliendelea kuketi pale chini akititirikwa na machozi, Alimtazama Tima pale alipokuwa amelala chali akimtazama. ilikuwa kama vile Tima alikuwa amemkodolea macho nap engine muda mfupi tu baadaye angelinyanyuka na kuanguka kile ckiheko chake kirefu. Pengine angelimzomea Nadina kidogo na kumwambie alitaka tu kumshtua. Akasubiri hilo litokee na halikutokea. Tima alilala vile vile akimtazama vile vile pasipo kujitikisa wala kupepesa macho. Ukweli ukaanza kumuingia Nadina kuwa Tima alikuwa marehemu!



Alipojitahidi kuishinda ile jitimai iliyomvamia ghafla usiku huu alishindwa na akajikuta akiangua kilio upya baada ya kuitazama ile rozari iliyokuwa mikononi mwake. Akalia kwa sauti ya kwikwi, akalia mno kiasi cha kamasi nyepesi kumtoka. Alitaka kutoka pale lakini uzito aliokuwa akiuhisi mwilini ulimdidimiza pale. 

Simu ya Tima iliyokuwa pembeni ya mwili yake ikatoa mwangaza na mlio ulioashiria kuita kwa simu. Nadina akaitazama tu kwa sekunde kadhaa kabla ya kurejewa na hali fulani ya kugutuka. Akajiinua kwa taabu kidogo na kuifuata ile simu akiwa na woga. kioo cha simu kilionyesha jina la Adella. Akahisi baridi mpaka kwenye mifupa! Alisisimka na kwa mara ya kwanza aliuona mwili wa Tima kama maiti na roho ya hofu ikamtawala kupita mwanzo. 

Akarudi kinyumenyume na kusimama tena kwa sekunde kadhaa akiitazama ile simu ilivyokuwa inaita, sauti ya mlio wa simu ukichanganyana na wimbo Nakei Nairobi wa mbilia bel uliokuwa hewani. Kelele zile angalau zilimrejeshea robo ya akili yake na akahisi angekutwa pale na maiti ya Tima. Akaitazama ile barua aliyoandikiwa na Tima ikiwa pale chini, akaitazama tu asijue aiokote au lah.

Tima alikuwa amemtaka aondoke pale haraka sana na alikuwa amempa njia ya kuondokea lakini bado alikuwa ameshapoteza muda wa kutosha akiwa analia na kuweweseka peke yake pale ndani. halikuwa jambo rahisi kwake.

Mlio wa simu ulipolatika, angalau Nadina alishusha pumzi na kwa haraka akaiokota ile barua na kuikunja vizuri kisha kuiifadhi kwenye brezia yake. Akalifuata kabati na kusimama tena kwa sekunde kadhaa akizitumbulia macho zile pesa zilizokuwa karibu na ufunguo.

Lahaula! hazikuwa pesa kidogo kama alivyodhania. Zilikuwa nyingi mno mbele ya macho yake. Hakuwahi kushika kiasi kama kile cha pesa tangu kuzaliwa kwake na sasa pesa nyingi zilikuwa mbele ya macho yake lakini katika hali iliyomnyima furaha kuzifurahia.

Nadina akaangaza huku na kule akitafuta cha kuwekea, akaiona bahasha kubwa eneo la chini ya kabati, haraka akaiokota na kuitumia kuhifadhia zile pesa. Akaibana kwapani, akikwapua na zile funguo. Akageuka tena ule upende wa kitanda na kumtazama Tima. Alitaka tena kuketi chini na kuanza kulia lakini moyo ulishapata wasiwasi wa kukutwa pale, akili ilishamrejea sasa na alijua ameshapoteza muda wa kutosha.
ile rozari ilikuwa bado i mkononi. Akaitoa bahasha kwapani na kuibana mapajani wakati akiivaa ile rozari na kujaribu kuifunga vyema sehemu alipokatikia

Akairudisha bahasha kwapani na kuanza kurudi kinyume nyume akiuelekea mlango. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio sana. Akaufukia mlango na kuugeukia akaufungua lakini ghafla akaufunga mlango na kusimama akimtazama tena Tima. Machozi yalimlengalenga tena. akapiga ishara ya msalaba na kumuaga Tima. Pamoja na taharuki yote angalau alikumbuka uwepo wa Mungu.

Akaugeukia tena mlango na kusimama akiwaza alilokuwa anawaza. Alipepesa macho kama mtu aliyepotewa na wazo na alijaribu kulikumbuka kisha ghafla akaufungua mlango, akiuchomoa ufunguo uliokuwa mlangoni hapo na kutoka nao. Akaufunga mlango kwa ufunguo kule nje ya chumba na kuusokomezea kwa ndani. 

Akatoka kwa mwendo wa haraka uliojaa hatua za woga. Akaimaliza kordo salama na kuziteremsha ngazi zilizokuwa zinaelekea kwenye Casino, akalifikia lango la Casino na kulifungua. Akajitoma kwenye casino na kupita kwa haraka akielekea nje. Akaangalia huku na kule akiwaza aufuate mlango wa kutokea moja kwa moja au aende kwanza chumbani kwake kuchukua hata nguo zake chache.

Akakata shauri kuchukua nguo zake mbili tatu, akatembea kwa mwendo wa haraka na ile bahasha kwapani, akijaribu kuonekana sawa kwa wale aliopishana nao wachache wakigeuka kumtazama pengine kwa ule mwendo wa haraka ama tu kwa namna lile vazi lake fupi lilivyokuwa limeshikamana na mwili wake wa kuvutia.

Hakulifikia lile jengo la makazi yao. Akamuona Adella kwa mbali akiongea na baadhi ya watu karibu na eneo lile. Akarudi kinyumenyume na kushtukia akimgonga msichana mwenzake.

‘Nadina! vipi?’ mwenzake akamshangaa namna alivyoshtuka na kumtolea macho huku akimeza mate kwa juhudi kubwa kiasi cha kuzamisha koo lake kwa ndani. 
‘Kwanza umemuona Tima?... Madame Adella anamtafuta’ yule binti akamzungumzisha Nadina ambaye ndio kwanza alimkodolea macho na majibu yakionekana kukimbilia kusikojulikana. 

Yule msichana akamtazama Nadina katika namna ya kumshangaa na kutomuelewa. Akaamua kuguna, akibetua mabega juu na kuyashusha kisha akendelea na safari yake. Nadina naye akatazmaa kule aliko Adella hukua akianza kuondoka. Alanusura apamie nguzo ya nyumba. akasimama kwanza akiwa hajui achukue uelekeo upi ulio salama ili kulifikia lile geti. 

Akazunguka nyuma ya Jengo lile la makazi yao na kuona mashuka yakiwa yameanikwa hapo na baadhi ya nguo zikiwemo khanga. akaifuata moja kwa kasi na kuianua, haraka akaifunga kwa kuviringisha juu ya ile bahaha yenye pesa. Alihisi bahasha ile ingechanikia njiani. akaanua nyingine na kujitanda, kwa mwendo wa kunyata huku akitazama sehemu zenye mwanga kama zilikuwa na usalama akapita kwa haraka mno  na kutimua mbio akilifuata lile geti. 
 Kulikuwa na nyasi ndefu za kuogopesha hasa kwa usiku kama huu lakini kwa wakati ule alitaka mno kuiokoa nafsi yake. Akazipangua nyasi kwa tahadhari na kulifikia geti. Akaligusa kufuli huku mikono ikimtetemeka na mara kadhaa akitazmaa nyuma kuona kama kulikuwa na usalama wa kutosha.

Alijaribu kufungua lakini ufunguo ulimgomea kwanza, akahangaika nao mikono ikizidi kutetemeka na ghafla akasikia watu wakizungumza umbali mfupi tu toka pale alipokuwa. Almanusura aanguke chini kama mzigo. Akajikaza kwa nguvu zote na kuchuchumaa akisikilizia yale maongezi.

Akagundua walikuwa makahaba wenzake wakianua zile nguo zilizokuwa zimeanikwa. Hakuna aliyeshtukia kuwa kulikuwa na upungufu wa nguo kwa wakati ule. Akawasubiri mpaka walipoondoka nay eye akaligeukia kufuli na kulitazama kwa macho ya hasira yaliyochanganyikana na hofu.

Akatulia kwanza kwa kushusha pumzi na kuchomoa ufunguo. Akagundua alikuwa amechomeka ufunguo mdogo ambao ambao hakujua hata ni wa nini kwa dakika zile. Akachomeka ufungu wa pili na ukakubali, akauzungusha na kufuli likafyatuka. Moyo ukatulia lakini kiherehere kikashika kasi na sasa ndio akajua ule mdogo ulikuwa wa kufungulia kitasa kilichokuwa hapo mlangoni. kaufungua na kulivuta geti. Likafunguka!

Akajitosa nje akikumbana na upepo, giza la kuogopesha na kijimsitu mbele yake. Miguu ilihisi kumfa ganzi. Kama si kukimbia eneo lile si ajabu angelirudi ndani haraka sana lakini hakuwa na chaguo lingine isipokuwa kujitosa msituni kule na kuelekea popote kwa nguvu zote. Akalikumbuka geti, akalifunga na kusimama tena akiutazama msitu uliokuwa mbele yake.

‘Mungu wangu!’  akatamka maneno haya mawili kwa sauti ya chini, pua  zikimcheza kwa woga! Akakaza roho na kupiga hatua moja, akapiga nyingine taratibu akachanganya mwendo, lile furushi la lenye bahasha ya hela likiwa kifuani. Baridi ilimkung’uta kisawasawa. Akageuka nyuma na kulitazama lile jengo alilotoka, akalitazama katika namna ya kutamani kulirejea na kujihifadhi kwa hii baridi iliyomkata maini lakini ilimpasa kusonga mbele bila kujali kama atakayoyakuta uko mbele yangekuwa na nafuu kuliko hapa alipotoka.

Taratibu akauzana mchaka mchaka akikazana kutazama mbele kwa bidii, huku moyo ukimuenda mbio. Nadina akazama vichakani, porini, gizani akiiacha nuru mbali na upeo wa macho yake, ni mwanga wa mbala mwezi tu ndio uliomtofautishia vitu kwa maumbo ya vivuli kabla ya kuvifikia
8888888888888888888888

Ikawa Asubuhi ikawa jioni na hatimaye usiku na kukakucha!
Nadina aligutuka toka usingizini akiwa chini ya mti aliamua kupumzika. Alimka ghafla na kukipapasa kile kifurushi chake. Kilikwepo! 
Akashusha pumzi na kutulia, akiyapoteza maruweruwe ya usingizi na kuangaza huku na kule. njaa ilikuwa inamuuma kupitiliza na pale alipokuwa hapakuwa na dalili hata ya maji ya kunywa sembuse kitu cha kutafuna. Akashusha pumzi na kutulia hapo akiwaza uelekeo wa kushika maana sasa angalau angejua uelekeo aendao.


Ile rozari iliyokuwa inaning’inia kifuani pake ilimpa tabasamu la faraja, angalau aliamini ilikuwa inamlinda. Tabasamu lile likafifia tena wakati alipotulia na akili yake kumrejeshea kumbukumbu za kuwa alikuwa mwenyewe sasa. Wawili aliowaona kama ndugu hawakuwepo tena duniani.

Akamuwaza Sindi.
‘Sindi!’ akaliita jina lake taratibu, akikumbuka mara ya kwanza walipoletwa pamja katika ile jehanamu ya duaniani, akakumbuka alipomsaidia kutoroka, akakumbuka kipigo walichopokea pamoja, akakumbuka mengi ya kuchekesha waliyopita pamoja, akakumbuka yote kiatokwa na machozi na hatimaye akaikumbuka sura ya Sindi dakika chake kabla ya kuagana naye. Akaumia, akaumia mno, akaumia sana. Nadina akajiinamia na kulia, akaomboleza wakati akikumbuka Tima alipowaweka chini kwa pamoja na kuongea nao kuhusu kutoroka. faraja aliyowapa kipindi chote hiki, akakumbuka walivyochanganyikiwa kwa hali ya Sindi kutumia madawa. Akakumbuka mengi sana na yakamliza zaidi pale chini ya mti alikokuwa ameketi akipigwa na miale ya jua la asubuhi, akiumwa na njaa na kujaa uchovu kupitiliza

Kilometa kadhaa toka pale alipokuwa Nadina, kulikuwa na hekaheka ya vitanda na mikeka. Watu walikuwa wamesimama makundi  makundi wakiongea hiki na kile. Walioshika tama, walioshika viuno, walioketi chini wakilia, na waliopata japo nguvu ya kubembeleza wenzao wote walikuwa eneo hili la danguro la Madame Adella. 

Taarifa za kifo cha Tima zilishasambaa haraka sana asubuhi ile baada ya mlango kuvunjwa na yeye kukutwa akiwa ameshafariki. Kwa kuogopa polisi kufika pale haraka walimpakia garini na kumkimbiza hospitali iliyo karibu wakati wakijua ameshakufa. Ilikuwa imepita robo saa tu tangu mwili wa Tima uondolewe pale lakini bado ile taharuki ya mtu kufia ndani tena kwa kujiua ilikuwa bado inazunguka hewani.

Adella alikuwa ofisini kwake akiwa amesimama na mikono yake ikiwa juu ya meza. Alikuwa ametulia vile kwa dakika za kutosha. Alipoinua uso, macho yalikuwa makavu mno, hakukuwa hata na dalili za panic usoni mwake. mlango ukafunguliwa na binti mmoja akaingia na kusimama pale pale karibu na mlango

‘…hayupo!’ akatamka yule binti na Adella akamtolea macho
‘hayupo?’ akarudia jibu la yule binti kwa mtindo wa swali lililotoka kwa sauti ya kukemea kiasi cha kumfanya yule binti akaribie kuruka kurudi nyuma. Alimshtua.
‘Mwambie Guzo nampa masaa mawili awe anajua huyu Malaya yuko wapi’ akatoa amri na yule binti akameza mate kwa juhudi zote akibabaika kidogo.

‘Nini?’ Adella akampatupia swali akiwa na hali ya kushangaa pia kwani alijua kulikuwa na la ziada toka kwa yule binti aliyekuwa amefumbata mikono kifuani
‘…Guzo hayupo tangu siku ile aliyoondoka Sindi’ yule binti akajibu na Adella akaduwaa. Akataka kuunganisha matukio ambayo haykuungana hata kwa bahati mbaya. 
‘Hakurejea?’ akauliza tena safari hii akitoka pale alipokuwa na kumkaribia huyu binti wa watu aliyeitikia kwa kichwa tu

‘Na mwenzake?’ akahoji akijua wazi lile neno mwenzake lingeeleweka vema kwa yule msichana kwani Guzo alikuwa na mwenzake aliyependa kuongozana naye. Walikuwa vijana na Adella na kila mtu alijua mishe zao Ilikuwa za hatari lakini makazi yao yalikuwa pale ingawa pia waliondoka kikazi na kuwa nje ya mji kwa kipindi walichojua wenyewe.

Adella akahisi akili ikichoka kufanya kazi ghafla. ni kweli baada ya kuongea nao siku ile na kuwatuma ile kazi Guzo na mwenzake hawakurejea, alitarajia wangelifuata pesa zao siku ile lakini hawakutokea akajipa moyo wangezifuata tu lakini sasa alianza kupata wasiwasi. Simu zao zilikuwa hazipatikani, na pale ndani hakuwepo sambamba na kutokuja kuchukua pesa zao ndio kabisa Adella alihisi mkanganyiko wa kutosha!!

‘Niite mlinzi wa Casino’ akaagiza na yule binti akatoka kwa haraka na kumuacha adella akiwa na hali Fulani iliyoashiria kupigwa bumbuwazi sasa.
akarejea kwenye kiti chake na kuketi akiwa tazama huku na kule na asitambue vile alivyokuwa anavitazama. Akili ilienda kasi mno.

Kifo cha Tima alikiweka kando kwanza, akamuwaza Nadina, pesa aliyomlipia kama mjakazi wake ilimuuma sana. Alikuwa hajaingiza pesa ya kutosha kuridhika na nafsi yake kuwa potelea mbali. Wakati akiweweseka pale kitini mlango ukafunguliwa na mlinzi akaingia na kusimama kinidhamu mbele ya bosi wake.

‘ Nadina ametoroka!’ akatamka kwa sauti ya kati tu  na mlinzi akakodoa macho kwani alimjua Nadina na ndiye aliyeshuhudia siku ile wakipokea kipigo na Sindi.
‘Chukua wenzio wawili muingia huko porini nyuma ndani ya masaa mawili nataka awe mbele yangu akiwa hai’ akatoa amri na yule mlinzi akaitikia na kutoka akimuach aadella peke yake.

Hakugeuka kutazama kule alikotaka kutazama mlango ukafunguliwa na Meddy akaingia kwa kasi kiasi cha kumshangaza mno Adella.

‘Nini kimetokea?’ akauliza akiwa amehamanika mno
‘Juu ya nini?’ Adella akauliza kana kwamba hakukuwa na lolote la ajabu lililotokea kwenye danguro lake asubuhi hiyo

‘Kuhusu Tima!?’ Meddy alimeza mate akingoja jibu kwa hamu na Adella akabeua, akatabasamu na kutoa kicheko cha chini chenye wingu la dharau na kebehi. taratibu kwa maringo ya kike akamtazama Meddy akimrembulia macho yake makubwa na kufunua kinywa chake.

‘Amejiua!’ akajibu neno moja na kulikaribisha tabasamu tena usoni pake. Meddy hakumuelewa. akavta kiti klichokuwa mbele yake na kuketi sasa akimtazama Adella alivyokuwa ananesanesa kwenye kiti chake

‘Amejiua?... halafu unatabasamu kana kwamba ni kitu chema?’ Meddy akamshangaa
‘Ulitaka nifanyeje? nilie?... kwa sababu zipi za msingi?.... kwangu mimi amepata pumziko alilotaka kupata vinginevyo angesema linalomtatiza tukamasaidia’ Adella akaongea bila wasiwasi

‘Come on Ade!... kuwa binadamu bwana… kifo ni kitu kingine’ Meddy akajaribu kumsahihisha na akawa amekosea mno
‘… sasa ulitaka nifanye nini…. nilie?... kama hakuna kilichopungua kwenye Casino yangu  nilie kwa sababu mtu akifa unapaswa kulia?....No!... kama una lingine la kujadili liweke mezani ila kama unazungumzia kufa kwa Tima… pesa niliyomnunulia ilisharudi na chenji ikabaki na faida ikapatikana… may she rest in peace. Amen!... nina kazi za kufanya Meddy..excuse me!’ Adella akatabasamu tena akimuacha  Meddy hoi maraduru

‘…Nadina ameenda wapi?’ Meddy sasa akakunja uso wakati akiuliza hili swali na Adella akalikata lile tabasamu a kusogeza uso wake mbele ya Meddy
‘Malaya unayemuulizia ndio ninamsaka muda huu… ana majibu mengi ya maswali yangu… lets hope for the best wamlete akiwa hai uko alikokimbilia….i swear somebody is gonna pay kwa kila linaloendelea humu ndani’ akamaliza kujibu akiyakata maini ya Meddy kuliko alivyodhania.

‘amekukosea nini?....’ Meddy akababaika akauliza swali lile kwa sauti ya kuhamanika
‘…. this time sitaki kumrudisha mavumbini kama nilivyofanya kwa Sindi… Atahitajika kuwa mfano kwa wenzake. Adellaakanyanyuka na kuufuata mlango. Akaufungua na kumuita Meddy ambaye alibaki kuduwaa.

Meddy akageuka na kumtazama Adella
‘Sindi amekuwaje?’ akauliza sasa masikio yake yakiogopa kupokea majibu
‘Amekufa!...’ Adella akajibu tena kama vile kile alichoongea kilikuwa kitu cha kawaida mno.
‘Nini?...amekufaje?...Sindi amekufaje?’ akababaika
‘Mr. amekufaje amekuwaje please leave my office…. kama unadhani una cha kushtaki…au kupigania…wahi kituo cha polisi…make sure you are smart enough kabla hujamake your first move… nisingependa kukuona ukipanda kizimbani kwa kesi ya mauaji… you know what I mean!... now with due respect get out!’ Adella akaamrisha akitabasamu

Meddy akasimama akiyumba na kupiga hatua kuufuata mlango. akasimama kwenye kizingiti cha mlango akimtazama Adella ambaye alijivuta kwa juu kidogo na kumbusu shavuni kisha kuufunga mlango.

Meddy akaendelea kusimama pale kizingitini akiwa bado hajaamini alichosikia. Ilikuwa kama vile masikio yalijaa mivumo ya ajabu iliyomvuruga kichwani. Mwili uliloa jasho, koo likamkauka na kwa sekunde kadhaa kauli za Adella zilipita akilini mwake na kuitibua mifumo ya fahamu zake. Alifadhaika!
8888888888888888888888888888

Wakat asubuhi hii ikiwa ya huzuni kwa watu wengine, kwa familia ya Okello hali ilikuwa tofauti. Meza ilijaa watu wenye furaha wakipata staftaha. Kulikuwa na vyakula vya kupendeza machoni na mdomoni. Annie dada wa Rebecca, Pamella na Rebecca pamoja Santina na wanafamilia wengine walikuwa mezani. 

Maongezi na vicheko vilikuwa vimepamba moto  pale mezani. Santina akajiinamia na kutoa simu iliyokuwa kwenye mfuko wa suruali yake aina ya Jeans. Namba za mpigaji alizifahamu. akanyanyuka na watu wakamtamzama

‘Sorry napokea simu…’ akaaga na watu wakaendelea na maongezi pmoja na kula, akatembea kuifuata kordo huku akitazama nyuma na akiikata ile simu baada ya kupokea. Akatembea haraka zaidi na kukata kulia akikaza mwendo kuufikia mwisho wa kordo uliokuwa na mlango. Akagonga mara moja na kufungua mlango. Akajitosa na kuufunga.

Akasimama akishusha pumzi na kumtazama Mzee okello aliyekuwa amesimama na kujiegemeza kwenye meza yake ya kazi. Hiki chumba kilikuwa ofisi yake ya nyumbani.
‘Unataka nini?’ Santina akauliza kwa sauti ua kukereka kidogo
‘Nikuulize wewe umekuja kufanya nini kinyume na makubaliano yetu’ Okello akauliza akiweka nyuma glasi ya mvinyo aliyokuw anayo mkononi. Akapishanisha mikono yake na kuifumbata juu kidogo ya kitambi chake. Ukubwa wa macho yake ulipungua wakati akimtazama Santina

Alikuwa binti mrefu mwenye umri sawa na binti yake Pamella.  Hakuwa mwembamba, mwili wake ulisheheni nyama za kutosha. Kichwani alikuwa na rasta za asili alizozisokota na kuzifunga nyuma katika mtindo wa kifagio. Alikuwa na rangi ya kuvutia ya maji ya kunde na hata pale alipokuwa amesimama. Okello alimeza mate na kufaidi kumtazama Santina Mkandawile, ile suruali ilikuwa umebana katika namna ya kuvutia mno na kuliweka umbile lake la kibantu haswaa kuonekana wazi.

‘Pamella ni rafiki yangu… hukutaka nihudhurie harusi yake kwa misingi ipi?’ Santina akauliza akipiga hatua pia kumkaribia Okello.
‘Lakini sivyo tulivyokubaliana’ Okello akapinga
‘Kwa hiyo unataka nikae miaka kwa miaka uko ulikoniweka kwa kisingizio cha kusoma… kwa miaka mingapi nitapaswa kudanganya na kujificha?’ Santina akawa mkali kidogo

Okello akatazama pembeni na kushusha pumzi
‘Nakosa amani nikikuona’ akakiri mzee wa watu
‘Kwa sababu zipi?... wewe ni wa kwanza kuzaa nje ya ndoa yako?... wakat unajenga mahusiano na mimi hukujua ni mwanamke na nina uwezo wa kushika mimba?’ Santina akizid kuwa mkali
‘sio hivyo’ Okello akapinga
‘Kumbe ni vipi?’ Santina akakunja uso

‘Usijisahaulishe kuwa Pamella ni rafiki yako, na wewe ni kama dada yako na zaidi ya yote nimekulea kama mtoto wangu baada ya wazazi wako kufa…okay baba yako alikuwa my bestfriend….come on Santina tunaleta picha gani’ Okello akaongea kwa kukatakata sentensi zake

‘Kwa hiyo?’ Santina akauliza kwa kujiamini, yoye hayo aliyoyaongea Okello yalikuwa marudio kwake na kama ni aibu aliitenda. angeificha mpaka lini.
‘Umemuacha na nani?’ Okelo hakujibu swali ya Santina akauliza la kwake
‘Na rafiki yangu… please! usiniite tena private namna hii kwa mazungumzo kama haya… sitaki kujenga wasiwasi wowote kwa muda huu….’ akatulia kidogo na kuingiza mkono kweye mfuko wa kushoto wa jeans yake. akatoa picha na kumpatia Okello.

Okello akaipokea na kuitazama. Ilikuwa picha ya mtoto wake aliyezaa na Santina! Calist!
‘ kwa kipindi hiki mimi ni binti yako na wewe ni baba yangu…. hakuna la ziada’ Santina akatamka taratibu na kugeuka kuufuata mlango

Okello akamuita kwanza akitaka kutoa dukuduku lake pia. Santina alipogeuka Okello akaliweka wazi
‘It is not about Calist…’ akajitutumua
‘Mmh! kumbe?’ Santina akahoji akiwa vile vile amegeuza shingo tu

‘Ni kuhusu Meddy!’ Okello akajibu na kumfanya Santina ageuke sasa mzima mzima
‘Amekuwaje?’ Santina akauliza akimtazama Okello kijeuri
‘Usinifanyie hivyo Santina… unajua nakupenda sana ila nisingependa kuona ule ukaribu wako na Meddy unarejea’ akabembeleza mzee wa watu akimfuata Santina ambaye alitamtazama Okello bila kituo

‘…unanichagulia marafiki?’ Santina akahoji kwa jeuri akipindisha midomo yake
‘Hapana mpenzi wangu… hapana… ila nataka ujue naumia sana na ndio maana nafanya juu chini ukae mbali na Meddy… uwe na maisha mazuri unayotaka… umlee calist wetu’ Mzee akaongea taratibu akimshikashika Santina ambaye alimtazama tu huyu mzee aliye sawa kiumri na marehemu baba yake.

Akamung’unya midomo yake na kumrembulia macho Okello
‘Nitaangalia cha kufanya usiumie…’ akajitoa mikononi mwa Okello na kuufuata mlango. Mwili wake ukitikisika na kumnyong’onyeza mno Mzee wa watu.

Santina akatoka mule ofisini akitabasamu na kumuacha Okello akiitazama picha ya mwanawe. Santina akakifuata chumba chake cha kulala na kuingia humo. Simu yake ilikuwa inaita. Akaipokea kwa furaha na kuongea na huyo rafiki yake aliyemuachia mtoto.
‘Nipe niongee naye…’ akaomba kumsikia mtoto wake na alipomaliza kutaniana naye hapa na pale akarudi kwenye mazungumzoa na rafiki yake
‘hali iko shwari tu… ila kila mtu ananishangaa nilivyonenepa zaidi; Santina akaongea akicheka
‘Lakini ndio wakati muafaka umtafute huyo Meddy umwambie ukweli kuwa una mtoto wake… angalau ajue mapema ana mtoto somewhere jamani’ yule rafiki yake akamshauri
‘mmmmh! mapema mno mpenzi… Okello bado anahudumia mtoto akijua ni wake unaweza kumwambia Meddy halafu akatibua kila kitu tukarudi bongo kuhenya na maisha… ngoja kwanza niwekeze vya kutosha…but yeeeyi I just wanna meet my man Meddy… ile one night stand bado iko akilini’ Santina akaongea akicheka na kujipindua pindua pale kitandani kwa raha zote.
888888888888888888888888888888888

Jioni hii Meddy anaitumia peke yake ufukweni wa bahari, akionekana kutopea mawazoni. Alitaka sana kumshirikisha Jerry Agapella kuhusu ile habari ya kifo cha Sindi lakini moyo ulikuwa mzito mno. Angeanzia wapi? Siku mbili nyuma Jerry alikuwa amebadilika mno, alikuwa ameacha kusononeka na kuzubaa na ile hali ya kuchangamkia harusi yake ilikuwa imeanza kumpata.

Alihisi kumletea zile habari za Sindi kungetibua kila kitu na si ajabu angaahirisha hata kufunga ndoa yenyewe. Aaliogopa pia kuwa chanzo cha kuvunjika kwa mipango ya harusi na kumuumiza Pamella Okello rafiki yake.

Alitaka kumuona Nadina, alihisi popote pale atakapokuwa amekimbilia Adella atampata, alijua kwa mazingira yalipo danguro lile biti yule asingejua uelekeo wa kukimbilia bila kushikwa. Akawaza maumivu atakayokuwa anayapata baada ya kushikwa. Akafumba macho na kusigina magego yake kwa nguvu.

Alitaka kunyanyuka pale na kufanya jambo lolote ambalo lingemuokoa Nadina toka mikononi mwa Adella lakini alishapewa onyo na alimjua Adella vizuri sana. Hakuwa mwanamke wa kuchezea kizembezembe. Akaiwaza ile kauli ya kifo cha Sindi. akahisi mwili ukimtetemeka. 

Huyo aliyekuwa akimuwaza alikuwa amesimama nje ya kibanda cha mzungu akikoka moto jioni hiyo tayari kwa kupika. Angalau alitabasamu wakati akichochea moto ule katikati ya mafiga huku akimtupia mzungu yule mzee akicheza na mbwa wake mita chache pembeni yake. Akatabasamu zaidi alipohisi mihangaiko ya mtu ndani ya tumbo lake.

yeye alitabasamu lakini Nadina alikuwa akikimbia kwa nguvu zote, akianguka na kuinuka, akijikwaruza na kujichoma. Pengine kama si kule kukimbizwa na watu alowaona wakimfuatilia asingekuwa akikimbia hivi.

Akakimbia kwa kadri alivyoweza  mpaka pale alitokezea kwenye korongo refu lililokuwa maji chini, maji ya bahari. Hakujua chochote kuhusu kuogelea. Alijua kujitosa pale kulimaanisha kufa. Angelitokaje baada ya kujitosa ilhali hakujua kuogelea. Alitweta kwa nguvu wakati akitokwa na machozi huku akilitazma korongo lile

Wale wanaume watatu walishafikia lile eneo nao wakitweta kwa nguvu na kumtazama huyu binti.
‘Jisalimishe binti’ akaamriwa na mmoja wa wale wanaume huku wakimkaribia taratibu. Nadina akalitazama korongo na kugeka kuwatazama hawa watu watatu.
Afe tu! ama akubali kurudi mikononi mwa Adella! 

Akijirusha inamaana alikuwa ameamua kujiua, alielewa ilikuwa dhambi kubwa kwa Mungu, lakini pia aliliogopa korongo lile. Akawaza namna atakavyosimama mbele ya Adella tena mtetezi wake Tima akiwa hayupo. Nadina akasimama kama bwege kwa sekunde kadhaa akikosa uamuzi.

ITAENDELEA….

2 comments:

  1. laura bhana umenikatishia utamu!!!!

    ReplyDelete
  2. daaaah!aghhhhhhhhhh!maskini mzee okello watoto wote wa kusingiziwa,nadina akikamatwa sisomi tena peti bse mateso atakayokutana nayo ctaki kushuhudia.

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger