52
Fiona Agapella akaweka ndita kadhaa usoni na akili yake
ikilikumbuka tukio moja lililotokea hivi karibuni, ingawa hakulipa uzito tukio
hilo kwa wakati ule lakini kwa sekunde hizi mbili tatu tukio lile lilikuja na
uzito wa tani za kutosha kutikisi mbuyu.!
Akaikumbuka barabara siku hiyo aliyomtembelea Iloma kazini
kwake, na wakati wakiongea hili na lile akaingia kijana aliyekuwa amevalia
t-shirt yenye maandishi ya kampuni moja ya usafirishaji vifurushi. Akamuulizia
Iloma na alipoelekezwa alipo akamkabindhi kifurushi kilichokuwa kimefungwa
kiustadi. Iloma akasaini na kukipokea.
Alionekana kukifurahia kifurushi kile lakini hakuonyesha
shauku ya kutaka kukifungua pale muda ule na Fiona hakuwa na wazo la kutaka
kujua ni kitu gani na kilitoka wapi, ila kwa muda huu akili ya Fiona ilijaa shauku
ya kukiona tena kile kifurushi. Akanyanyuka kwa mwendo wa haraka na kuanza
kupekua huku na kule. Alihama droo moja hadi nyingine, kisha akaingia kabatini
ambako pia aliambulia patupu.
Akasimama akiwa amejishika kiuno, akili yake ikiendelea
kumshawishi azidi kukitafuta hicho alichokuwa anakitafuta. Akaiongoza miguu
yake mpaka kwenye kordo moja chumbani hapo kulikokuwa na boksi kubwa lililobeba
sanduku moja juu yake. Akalishusha sanduku lile na kulifungua lile boksi.
Shabash! alichokuwa anakitafuta kilikuwa ndani ya lile boksi.
Akakitoa na kurudi nacho kitandani, akiharakisha kukifungua
kwa shauku ya kutosha. Akaachama mdomo na kutoa macho. kulikuwa na hereni
zilizofanana na mkufu vyote kwa pamoja vikiwa rangi ya fedha na kunakshiwa kwa
kito cha almasi. Fiona akaweweseka sasa akitoka tena mbio na kulifuata sanduku
lake dogo na kulifungua. Akatoa mkebe mwingine uliofanana vile vile na ule
aliokuwa ameutoa katika boksi na vidani vilivyokuwa ndani vilikuwa vya
kufanana.
Akahisi kitu kama kichomi kikimgonga moyoni, hakikuwa kiyu
cha kawaida vitu kufanana namna hii. Akapata akili ya kurudisha kila kitu
mahala pake na kisha kusimama mbele ya ile dressing table akijitazama na akili
yake isitambue kwanini alisimama pale akijitazama. Hata ile dhamira yake ya kusafisha
kucha ilipotelea mbali na kumuacha akiwa haelewi ni kipi alipaswa kufanya muda
ule.
Akiwa amezama mawazoni, mlango ukafunguliwa na Iloma akaingia
akitabasamu
‘Nilijua umeshatoka’ akamsemesha Fiona akikifuata kitanda na
kuutua mkoba wake. Pengine alitarajia Fiona angelijibu chochote kuendeleza
mazungumzo lakini haikuwa hivyo. Fiona alikuw anamtazama tu kana kwamba alikuwa akigeuka kuwa kiumbe
cha ajabu taratibu.
Iloma akakunja uso kidogo na kumtazama Fiona kwa mshangao
‘Fifi!...’ akamuita kwa upole akianza kumsogelea. Fiona
hakujibu kitu ni kama vile akili yake haikuwa pale muda ule
‘nin kimetokea?’ Iloma akauliza tena akiwa ameshamkaribia
rafiki yake na kuendelea kumdadisi. Kama mtu aliyerudiwa na akili alishusha
pumzi na kumtazama Iloma usoni
‘Unawasiliana na Kristus?’ akamuuliza Iloma ambaye alitanua
macho yake kwanza na kurudisha kichwa nyuma huku kuguna katika namna na
kushangaa kidogo
‘Kristus?’ iloma akauliza akiwa bado anashangaa
‘Agapella!’ Fiona akarahisisha swali lake akiwa bado
amemkazia macho Iloma
‘No!... sijaongea naye tangu siku ile uliponituma’ Iloma
akajibu naye akimtazama Fiona kwa udadisi
‘Una uhakika?’ Fiona akawa kama haamini ile kauli ya Iloma
‘Sasa nikufiche ili iweje au itanisaidia nini mimi… wait!...’
iloma akageuka kwanza akimpa kisogo Fiona na kufumb amacho kwa nguvu mno kana
kwamba alitaka kujiweka sawa kabla ya kumgeukia tena Fiona.
Alipogeuka akamtazama Fiona na kumrushia swali kali sana
‘unadhani nawasiliana na Agapella kisirisiri?’ Iloma akagonga
mfupa wa swali na kumnyong’onyeza Fiona
‘Simaanishi hivyo’ Fiona akababaika kwa vile nia yake ilikuwa
imewekwa wazi ghafla na yule yule aliyetaka kumtuhumu
‘Sasa una maana gani kuniuliza kama nawasiliana na
Agapella?... Fifi kama umefikia hatua ya kuniwazia hivyo ni bora urudi kwa
mumeo kabla hatujakorofishana vibaya’ Iloma akaja juu kidogo
‘Sijakutuhumu Iloma… nimeuliza tu’ Fiona akajitetea akimpita
Iloma na kwenda kusimama nyuma ya Iloma naye iloma akapiga hatua moja mbele na
kumgeukia Fiona wakawa wamebadilishana nafasi za kusimama
‘hakuna swali lisilo na sababu Fiona…. ndio maana tangu
mwanzo nilikataa kujihusisha na huu usuluhishi’ Iloma akajitetea
‘What about vidani ulivyonavyo kuwa sawa na nilivyonavyo?’
Fiona akaona aweke wasiwasi wake kweupe.
Iloma akamtazama Fiona kwa sekunde kadhaa pasipo kuwa na
jibu. Akili yake ilichemka maradufu na kumtafutia jibu la kujitetea. Akalipata!
‘Una nguo ngapi zinazofanana na zangu?... au ni wewe tu
unayestahili kuwa vidani?... what if nimemwambia mpenzi wangu aninunulie vidani
vilivyonivutia toka kwako… hilo ni kosa?’ Iloma akauliza akianza kuona ujinga
wa mazungumzo yale na hatari iliyo mbele yake.
Fiona akakubali kushindwa
‘Okay!... samahani kwa kukufikiria vibaya’ akajibu akiifuata
pochi yake na kutoka. Iloma akashusha pumzi kama mtu apigaye mluzi na kukifuata
kitanda kwa unyonge. akaketi hapo akipepesa macho kama mtu aliyenusurika
kufumaniwa katika hatari. Akahema kwa nguvu, mabega ayakipanda na kushuka.
Mpaka dakikaile tayari alishakutana kimwili na Kristus Agapella na akakiri moyo
ulishafunguka kwa mzee huyu!
Fiona alichomtendea Marehemu Sophia mama wa Jerry na Jenifa,
mke mkubwa wa Mzee Agapella ndio kilichokuwa njiani kumkuta yeye mwenyewe
kupitia rafiki yake kipenzi Iloma! Je ataujua ukweli na akijua atafanya nini?
888888888888888888888
Dennis Mazimbwe ana mkewe Daniella walitoka ofisini na kuanza
kuifuata kordo iliyokuwa inaelekea mapokezi. Dennis alikuwa ametangulia hivyo
ilikuwa rahisi kwake kumuona Rebecca Okello aliyekuwa mapokezi pale mbele ya
meza ya sekretari. Meza ya sekretari alikuwa upanze wa kushoto mara tu
umalizapo kordo na kuingia mapokezi na vile Dennis alitangulia hamaniko
alilolionyesha usoni lilimfahamisha Rebecca moja kwa moja kuwa hali haikuwa
shwari.
Akazunguka ule upande wa sekretari ghafla na kuingia miguuni
pa sekretari akiusahau mfuko mdogo aliokuwa ameuweka miguuni pake wakati akiongea
na sekretari yule ambaye alikuwa bado hajaelewa kilichokuwa kinaendelea.
Dennis akafika mapokezi pale na mkewe Daniella akawa wa
kwanza kuongea na yule sekretari akimtania
na kumuuliza hiki na kile. Daniella alisimama pale alipokuwa amesimama Rebecca
hivyo mfuko ule aliouacha Rebecca pale chini ulikuwa kando yake.
Rebecca kule chini akahisi ule mfuko ungeleta balaa
akanyoosha mkono na kutambaza taratibu sakafuni akiufuata ule mfuko ili aufiche
kule chini alikokuwa amejificha na bahati mbaya mkono wake hakufikia kile
kimfuko zaidi ya kuishia kukanyagwa na Daniella aliyekuwa anasogea mbele ili achukue kikaratasi
kilichoonekana kumvutia pale mezani.
Daniella alihisi kukanyaga kitu. Akatazama kule chini na
kuuona ule mfuko na asijue kulikuwa na mtu kule chini akiugulia maumivu ya
kukanyagwa na ko ko ko yake.
‘Naona kuna mteka amesahau mfuko wake hapa chini’ Daniella
alisema akitaka kuinama ili auokote. Rebecca akapiga ishara ya msalaba huku
akipuliza vidole vyake na Dennis akamuwahi mkewe na kuuokota ule mfuko kwa vile
alijua kuinama kule kungemfanya amuone Rebecca.
Akafanya jitihada zote za kumuondoa Daniella pale na kwenda
naye nje. Rebecca aliposikia mlango umefungwa akajitoa kule chini na wakati
akimalizia kutoka akajigonga kichwani kwenye ile meza ya sekretari.
Akalaani, akapuliza vidole na kusugua alipojigonga na
Sekretari yule akajizuia kucheka akinyanyuka na kumuomba asubiri akamtafutia
barafu akande vidole. Kule nje Daniella na Dennis waliingia garini na Dennis
akadai amesahau funguo za gari ofisini. Akamuomba Daniella amsubiri nay eye
akatoka mbio na kurudi ofisini, pale mapokezi.
Alimkuta Rebecca akifungwa na sekretari kitambaa kilichokuwa
na barafu. Dennis hakujali pengine kwa kutojua ni nini kilikuwa kimemkuta
Rebecca. Aliukwanyua mkono wa kushoto wa Rebecca ile sehemu karibu na kwapa na
kumburuza kama mtoto. Akafungua mlango wa ofisi na kumtupia ndani Rebecca kabla
ya yeye kuingia na kufunga mlango.
‘nitaongea hili kwa mara ya kwanza na ya mwisho Becca’ Dennis
alifoka sasa
‘…. usikanyage ofisini kwangu bila kunipigia simu Rebecca’
akaotoa onyo
‘umeanza kuniwekea masharti Dennis?!’ Rebecca hakuamini kauli
ile kauli
‘kuna wakati utumie
akili kufikiri… Daniella ni mke wangu na anafika hapa wakati wowote… wakati huu
si sawa na wakati alipokuwa hayupo… huelewi nini?’ Dennis aliongea kwa haraka
na msisitizo kuonyesha kukerwa na Rebecca
‘Kwanini yeye usimzuie kufika hapa kama unavyonizuia?’
Rebecca naye akauliza na kumfanya Dennis atamani kumnasa kibao ili angalau aone
hatari anayoiona yeye kwa kufika kwake pale bila taarifa.
‘… hebu kuwa busara Becca... Daniella amekusheshimu sana kwa
kujua kinachoendelea bila kumfikishia mumeo… angalau mpe heshima yake kama mke
wangu wa ndoa… sipendi upumbavu’ Dennis sasa aliangalia nyuma kwa wasiwasi
akirudi nyuma kukishia kitasa tayari kwa kutoka. Alihisi Daniella angemfuata
nyuma
‘Lakini ulisema utamtaliki hivi karibuni…’ Rebecca alikuwa
bado na hali ya kutoamini Dennis alikuwa anamgombeza vile kama mtoto
‘ni mpaka hapo hiyo karibuni itakapofika kwa sasa usikanyage
ofisini kwangu bila taarifa vinginevyo utanipoteza’ akatishia Dennis na kushika
kitasa cha mlango
Sekretari alikuwa akisikiliza mazungumzo yao mlangoni na alipoona
kitasa kinacheza akageuza miguu haraka kurudi mapokezi lakini hakupiga hatua
nyingi Dennis alishatoka na akamshangaa kumuona sekretari wake pale kordoni.
Yule dada akavunga kuulizia hiki na kile lakini Dennis hakumsikiliza akampita
na kuishia zake.
Binti akabaki kordoni akitazama ule mlango wa ofisi ya
Dennis, pengine alitarajia Rebecca angetoka, kinyume chake akasikia kitu
kikipasuliwa kwa nguvu zote. Akaharakia kwenda kule ofisini kwa Dennis, fremu
yenye picha ya Daniella iliyokuwa mezani pa Dennis ilikuwa imesambaa kila kona.
Wanawake hawa wawili wakatazamana tu mmoja akiwa na mshangao na mwingine akiwa
na hamaniko!
88888888888888888888
Sindi Nalela alikuwa akibubujikwa na machozi wakati Tima
alipokuwa anangoja jibu la swali lake kwa mara ya pili tangu aliulize.
‘Upo tayari?’ akarudia tena lile swali kwa mara ya tatu na
Sindi akaitikia kwa haraka kama mtu aliyekata shauri ya liwalo na liwe.
‘Nimeshakwambia inataka uvumilivu na narudia tena kama kweli
unataka huyu mtoto azaliwe itakupasa kuvumilia yote kwa kipindi cha miezi
mitano iliyobaki… uko unakoenda hakuna raha wala starehe yoyote… na sitaki
kukuficha kuwa kuna maisha ya unafuu… ni vile tu unahitaji kumuokoa huyo mtoto…
ila kama huwezi ni bora ukubali tu kuiondoa hiyo mimba na maisha yaendelee’
Tima aliongea taratibu, akitaka Sindi amuelewe na akiweke akilini kile
alichokuwa akiambiwa kwa wakati ule
Sindi aliitikia tu na mara kadhaa akigeuza uso wake na
kumtazama Nadina aliyekuwa ameketi kando yake akijaribu kumfariji na kumpa
nguvu.
‘Nani atakuwa anaenda kumuona sasa?’ Nadina akamuuliza Tima
‘nitaenda usiwe na hofu… mradi tu Sindi aniahidi atavumilia
na kamwe hatachukua uamuzi kinyume na huu tuliokubaliana’ Tima akatoa maelezo
ambayo kwa kiasi Fulani yalimpa Nadina matumaini ingawa moyo wake ulijaa
mashaka mengi mno. Kuna maswali alijiuliza pasipo kupata majibu lakini hakutaka
kuyauliza kwa uwazi akichelea kuonekana mjuaji.
Jioni ilipoingia, Sehemu kubwa ya jengo la danguro ilikuwa
kimya. Vijakazi vilikuwa vikitumikia mabwana ndani ya vile vyumba. pur
ukushani chache zilikuwa kule kwenye casino ambako kwa siku
kama hii ya mwisho wa wiki kulikuwa kunajaa watu wenye fedha zao. Sindi na
Nadina walitazamana kwa sekunde kadhaa na kukumbatiana, kila mmoja akilia. kuna
kitu mioyoni mwao kiliwaumiza ni kama vile ilikuwa mara ya mwisho kwao kuonana
na kamwe wasionana tena baa da siku ile.
Wakalia kwa uchungu, kwa muda mfupi waliokaa pamoja walikuwa
kama ndugu, walipita dhoruba pamoja na walipofarijika walicheka pamoja lakini
sasa iliwapasa kutengana na mmoja wao alikuwa akielekea kusikojulikana.
Waliumia!
Nadina akavua rozari yake na kumvalisha Sindi
‘utakapohisi upweke itazame rozari hii… itakufariji’ akaongea
akiushika ule msalaba wa rozari na kumtazama Sindi usoni.
‘Sijui ninakokwenda…’ Sindi alisema kwa kwikwi na kuongea kwa
mara ya kwanza jioni ile. Alikuwa kimya kwa muda mrefu sana akionekana mwenye
mawazo na mara kadhaa akilia kimya kimya.
‘imetosha sasa… twende sindi’ Tima aliwaachanisha na kumshika
mkono sindi akimuongoza sehemu iliyokuwa na nyasi nyingi. Sindi alitembea
kichwa kikiwa kinatazama nyuma kule alikosimama Nadina ambaye naye alitembea
kumfuata Sindi huku akilia, akamfuata mpaka alipopotelea kwenye zile nyasi na
kusikia geti dogo likifunguliwa. akafumba macho na kuruhusu machozi zaidi
akalia, akalia peke yake, kwa dakika alizosimama pale alihisi
dunia ilikuwa imemgeuzia mgongo tena kwa mara nyingine. Mtu aliyemuona kama
ndugu alikuwa ameondoka maishani mwake na hakuwa na hakika ya kumuona tena.
Sindi na Tima walipotoka nje ya geti lile dogo lililokuwa
limejengwa nyuma ya nyumba ile kwenye eneo ambalo hakuna mtu aliyepata kuwaza
kuwa kulikuwa na geti walitokezea kwenye pori.
Jua lilikuwa linaelekea ukingoni na kufanya rangi za kuvutia
kwenye angala wadidu. Vivuli vyao vilikuwa virefu wakati jua lilipokuwa
likizama taratibu. umbali mfupi toka pale walipotokea. Walikutana na vijana
wawili ambao walionekana kuwa pale wakiwasubiri wao.
‘Utaondoka na watu hawa… umesikia?’ Tima alimpa sindi maelezo
akimkabidhi mkoba mdogo aliokuwa nao. Sindi akaachia mdomo wazi. Aliwatazama
vijana wake kwa awamu, kwa uso uliojaa wasiwasi na hofu kubwa. Moyo ulimuenda
mbio mno.
Ilikuwa ni afadhali kuongozana na Tima mpaka mwisho kuliko
kuongozana na wanaume pekee asiojua ni watu wa aina gani na bora angejua
alikokuwa akielekea. Sindi aliogopa, aliogopa mno!
‘ Usihofu… sawa?... utafika salama… na nitakuja kesho kutwa
kukuona… be strong…sawa?’ Tima akazungumza naye akimshika mabega na kumtikisa
kumtoa katika ile hali ya taharuki iliyomkuta ghafla.
‘Kambaulaya binti mwenyewe ndio huyu… naomba mfanye kama
tulivyoongea’ Timakaongea na wale vijana
‘usijali dada… hamna shida’ kijana mmoja aliyeonekana kuwa na sura ngumu
na misuli ya kutisha alimvuta Tima pembeni na kuzungumza naye kwa muda. Tima
akatoa kitu kama karatasi na kumpatia kwa haraka sana yule kijana ambaye naye
alikipokea kwa haraka na kukihifadhi mfukoni.
Sindi aliyaona yote haya na hofu ilimzidi lakini hakuwa na
jinsi. Wakati huu giza lilishaanza kuingia na Tima aliporejea kwake
alimkumbatia kwa nguvu na kumnpng’oneza
‘Be strong!’ kisha akamuachia na kuanza kuondoka pasipo
kugeuka nyuma wala kumpungia mkono. Wale vijana wakaanza mwendo na Sindi
akajikuta akiaza kuchapua hatua kuwafuata nyuma. Moyo wake ulikuwa mzito sana
hasa alipowatazama wanaume hawa ambao kimuonekano tu ilitosha kumfahamisha kuwa
hawakuwa watu wema lakini kwa muda ule angefanyaje? akaishika rozari ile
kifuani akiwa amekumbatia vifurushi vyake na kuendelea kuwafuata watu hawa
waliogeuka mara kadhaa na kumtazama kwa macho yao makali.
888888888888888888888888
Ufukwe wa bahari ya hindi ulikuwa ukileta upepo mwanana eneo
zima la hotel ya Sunrise muda huu wa saa tatu usiku. Meddy aliyekuwa ametoka
eneo la bahari na kuja kuketi kwenye kiti chake alimtazama Jerry na kusikitika
kwa kutikisa kichwa, Jerry alionekana kuzama mbali kimawazo wakati akiyatazama
mawimbi ya bahari yaliyopambana na upepo na kuleta mvumo wa kuvutia ufukweni
hapo.
‘Jerry!’ Meddy akamshtua Jerry kwa kumuita
taratibu Jerry akaondoa macho yake toka kule baharini na
kumtazama Meddy. Walikuwa wameketi
kwenye vile vitanda vya kupumzikia beach. Jerry alikuwa amelala chali mikono
yake ikiwa imekutana nyuma ya kisogo. meddy alikuwa ameketi akimtazama Jerry na
wakati huo akijifuta maji mwilini.
‘unawaza nini?’ Meddy akamuuliza
‘Mtoto wangu..’ akajibu Jerry akirudisha macho kule baharini
‘Mtoto?’ Meddy hakumuelewa haraka
‘…sidhani kama ni rahisi kuondoa mawazo kuwa kuna mtoto wangu
kwenye tumbo la mwanamke ninayempenda sana…na sijui mtoto huyo yu hai au mfu…
sijui mwanamke huyo anaishi maisha gani… unadhani amani ya moyo itatoka wapi?’
Jerry akaongea kwa uchungu
‘Come on Jerry!... kwanini unazungusha mambo namna hii?’
Meddy aliongea kwa jazba kidogo
‘Kivipi?’ Jerry naye aliuliza akimtazmaa tena Meddy
‘Sio wewe uliyeapa kuwa hutoleta tena inshu za Sindi katika
maisha yenu na Pamella?.... kama hutaweza kuhimili haya mambo ni bora umwambie
pamella ukweli… I cant stand kuona Pamella anaingia mahali ambako ataishi
maisha ya kuumizwa kila siku sababu tu akili yako iko kwa mtu mwingine’ Meddy
aliongea kwa hasira
‘… Pamella anaingiaje hapa?’ Jerry naye akaja juu akinyanyuka
na kuketi akitazamana na Meddy
‘Pamella ni rafiki yangu… maumivu yake yote hunishirikisha…
siwezi kusubiri awe anakuja kunililia kila siku kwa sababu ambazo ningeweza
kuzizuia… be a man Jerry!... damn! be a
real man… face her na umwambie ukweli au meza kila kitu na uanze maisha upya’
Meddy alimgombeza mwenzake na asijue hali aliyokuwa nayo Jerry ilikuwa ni
mtihani tosha
‘… kirahisi hivyo?... kama ungewahi hata kumpa mimba msichana
na akaitoa angalau ukausikia uchungu ninaousikia hapa labda ungeongea kitu
kingine… sio rahisi kama unavyodhani..angalau ningekuwa na uhakika mimba yangu
ameitoa… sijui binti wa watu yuko wapi?... sijui anaishi maisha gani… sijui
mimba niliyompa inamtesa kiasi gani…unaniambia be a man?... how? niipuuuze hii
inshu nzima na kufanya kama vile sindi hakuwahi kutokea maishani mwangu?...
sina roho mbaya kiasi hicho… na infact nampenda Sindi… nampenda sana…I’m a man
enough to confess this ….now be a man enough to let Pamella know this’
akanyanyuka na kuondoka pale alipokuwa ameketi. akatembea kuelekea baharini
akimuacha Meddy amenywea, akimuhurumia mwenzake na akishindwa kujua alipaswa
kufanya nini sasa. akamshuhudia kwa mbali rafiki yake akifuta machozi.
Akakiri Jerry alikuwa na maumivu ambayo hakuna mwingine
aliyeyaona isipokuwa yeye. ilikuwa imesalia wiki moja na siku kadhaa ndoa yake
na pamella ifungwe, wakati watu wote wakiwa katika shamra shamra za kuandaa
harusi ni Jerry tu hakuwa na amani ya moyo.
88888888888888888888
Ofisi ya Adella ilikuwa na dirisha lililoelekea kule casino.
Mara kadhaa alisimama katika dirisha hilo na kuangalia yale yaliyokuwa
yakiendelea ndani ya casino yake. Mlango wa ofisi yake ukafunguliwa na Tima
akaingia akitabasamu.
‘Done!’ akatamka kwa furaha na Adella akaachia kicheko na
kukimbilia kwenye friji ndogo iliyokuwa hapo. Akatoa mvinyo na kuzifuata glasi
mbili zilizokuwa kwenye kabati jembamba lililokuwa kwenye kona.
akampatia Tima glasi moja na kummiminia ule mvinyo
‘cheeeers!’ wakasema kwa pamoja na kucheka
‘Wamemchukua kama ng’ombe anayekwenda machinjioni’ Tima
akatamka akisogea kule dirishani
‘Wala hakuwa na wasiwasi?’ Adella akauliza kwa furaha
‘aliokuwa nao ila imani yake kwangu nadhani ilimfanya
asiogope kufuatana nao’ Tima akasema akitabasamu
‘uliwaambia wahakikishe hakuna kinachopatikana?’ Adella
akauliza kwa furaha akirejea kuketi kwenye kiti chake cha kazi
‘Wale vijana si umewatafuta mwenyewe… kazi yao zi unaijua na
pesa juu nimeongeza yaani wahakikishe watakapomzika wanapanda mti kabisaa!’
Tima akamfurahisha bosi wake aliyekuwa naandika cheki ya pesa muda ule
‘chukua hii… shopping ya maana inakuhusu… now sina mtu wa
kuniweka roho juu… yule binti alikuwa msumbufu mno…na angezidi kukaa hapa si
ajabu kuna mambo yangeharibika vibaya mno… aisee! umetumia usanii wa hali ya
juu kuwatenganisha mbwa wale…’ Adella aliongea kwa furaha akimkabidhi cheki ile
Tima ambaye aliipokea na kuibusu kwa furaha kubwa.
Mirindimo ya wimbo wa Nadina ulisikika na wakajikuta wakikata
kicheko chao na kumsikiliza Nadina. Adella alisimama na kulifuata dirisha. Kwa
pamoja wakawa wanamtazama Nadina pale kwenye jukwaa la Casino
Ukumbi ulikuwa umezizima kwa ile mirindimo ya taratibu,
lakini mzizimo ule uliletwa na muimbaji mwenyewe. Alikuwa anatokwa na machozi
na kuimba kwa hisia mno. Ni kama vile alitaka aliyekuwa anamuimbia amsikie.
Sauti yake kali ilipaa hewani na kutetemesha nyoyo za watu pale alipokifikia
kibwagizo ambacho wengi walimsaidia kukiimba
‘….Nenda nenda nenda na wala usiangalie nyuma…na wala
usinitafute tena na wala usinikumbuke… nimekubali kwa moyo mmoja tuuu… kuwa
sitokuwa nawe …mileleee… nenda nenda nenda na wala usiangalie nyuma…’
akakirudia kiitikio kile safari hii sauti ikififia na kwikwi za kilio
zikimzidia mwisho akaacha kuimba na kuinamia kipaza sauti huku akilia. watu
wakabaki wanamshangaa.
ITAENDELEA
NIACHIE MAONI YAKO!
No comments:
Post a Comment