Monday, May 30, 2011

WARAKA WA MWISHO...2 Na Laura Pettie

Ilikuwa jumapili, jumapili tulivu, jumapili iliyobeba mvua za rasharasha zilizokuja na kutoweka na kuondoa vumbi na hali joto iliyokuwa imelikamata jiji kwa miezi kadhaa.

Kama kawaida ndani ya siku hii waumini mbalimbali wa madhehebu ya kikristo walijumuika na wenzao katika kumwabudu mungu makanisani.

Nami nilikuwa mmoja wao nikiwa na mchumba wangu Sakina Mtanga mwanamke niliyempenda na nitakayempenda kwa dhati mpaka kufa. Mara baada ya misa tulitoka kanisani na kuingia garini tayari kwa kuelekea nyumbani ambako kwa siku hiyo niliamua kupumzika na mchumba wangu huyu kwa minajili ya kupanga hili na lile kuhusiana na ndoa yetu ambayo haikuwa mbali


Wakati nikielekea gari langu nililokuwa nimepaki umbali mfupi toka lilipo geti la kuingilia kanisani nilisikia sauti ya sakina ikiliita jina langu kwa sauti. Nikageuka nyuma na kuangaza angaza katika namna ya kumtafuta ili nipate kujua mahali alipokuwepo.

Nikamuona Sakina akiwa amesimama pembezoni mwa mti kubwa uliokuwa karibu na lango la kuingilia kanisani akiwa pamoja na kijana mmoja ambaye hakuwa mgeni sana machoni pangu ila kwa wakati ule sikumtambua haraka.

Nilichapua hatua za haraka haraka na kuwaelekea kule alikosimama Sakina na kijana yule huku akili akijaribu kupambanua haraka haraka ni wapi hasa nilipata kukutana na yule kijana aliyekuwa amesimama na mchumba wangu Sakina.

Nilipowakaribia nilitumbua macho yangu kwa mshangao hali kiganja changu cha mkono wa kuume kikimbilia kinywani na kuzuia ukelele wa mshangao uliotaka kunitoka ghafla bila ridhaa yangu.

“ Bonny!” niliita kwa sauti hali nikimtazama kijana huyo pasipo kuamini macho yangu. Bonny naye akiwa katika hali ya kustaajabu aliachia kicheko kifupi kisha kwa haraka akaja kunikumbatia kwa furaha. watu wachache waliokuwa wamesimama karibu nasi waligeuka na kututazama kwa mshangao.

Tulikumbatiana kwa sekunde kadhaa kabla ya kuachiana na kuendelelea kutazamana kwa mshangao wa kutoamini kabisa.

“ siamini macho yangu Jimmy, unajua nilipomuona Sakina nikahisi na wewe utakuwa hapahapa” Bonny aliongea kwa furaha
“ kwanini?” nilimuuliza kimtego hali nikijua vema jibu ambalo ningelipata toka kwa Bonny
“ Mlikuwa hamuachani toka Makongo sekondari!” alijibu haraka haraka na wote kwa pamoja tukaangua kicheko cha furaha.
“ uko wapi siku hizi maana toka tuachane makongo mabest wote sina mawasiliano nao”
“ ndio nimerudi toka Japan, sasa hivi niko Kizito construction company”.Bonny aliongea kwa bashasha hali akishindwa kabisa kuizuia furaha isijianike usoni pake.

“Jamani twendeni basi nyumbani mkaulizane vizuri” Sakina aliingilia kati maongezi yetu na sote kwa pamoja tukakubaliana naye.

Tuliongozana kuelekea garini. Dakika kumi na tano baadaye tulikuwa sinza kwa Remmy nilikokuwa naishi na mchumba wangu Sakina.


ITAENDELEA...

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger