49
Gari aina ya Acadia iliserereka barabarani ikiwa katika
mwendo wa kasi kiasi, dereva aliyekuwa ameukamata usukani kwa mikono yote
miwili alikuwa akibubujikwa na machozi kiasi cha kushindwa kuona mbele vizuri.
Akauondoa mkono wa kushoto toka kwenye usukani na kuutumia kupangusa machozi
yaliyoonekana kuuelemea uso wake.
Akaurudisha mkono kwenye usukani na kukata kona, akiiacha
barabara ya lami na kukamata njia yenye changarawe, akaongeza mwendo kidogo,
sasa akiuma midomo yake na kuimeza kwa ndani katika namna ya kujaribu kujiweka
sawa, alibana pumzi kidogo na kufanya mishipa ya shingo imsimame kabla ya
kuiachia pumzi sambamba na ile midomo yake. Taratibu ule mwendo kasi ukapungua
kadiri alivyokuwa akiikaribia nyumba ya ghorofa moja iliyokuwa mita kadhaa mbele yake.
Akapunguza mwendo na kusimama upande wa pili wa nyumba ile,
akzima gari na kushusha kioo cha dirisha lake taratibu, akaitazama, akaingalia
na kuikodolea macho ile nyumba iliyokuwa
inavutia machoni si tu kwa ujenzi wake bali pia mng’ao wa taa nyingi zilizokuwa
zimewashwa usiku huu wa saa tano kasoro.
Daniella mke wa Dennis Mazimbwe akakilaza kichwa chake kwenye
kiti wakati akiyahamisha macho yake toka kule kwenye ile nyumba na kutazama
mbele. Akili yake ilikuwa katika ushindani na dhamira yake moyoni. Alitaka
kuteremka toka mule garini na kuingia ndani ya nyumba ile ya Mzee Okello.
Alitaka kuonana na Rebecca pamoja na mumewe, alitaka kuyasema yote ya moyoni
mwake mbele ya Okello. Alitaka Rebecca aonje hata theluthi ya uchungu
anaousikia kuona ndoa yake ikiparaganyika sababu yake.
Dhamira yake ilibeba kisasi cha ajabu, kilichovaa joho la
hasira na kofia ya chuki lakini akili yake haikubweteka na kukubaliana na
dhamira yake. Aliona kama alikuwa anaelekea kuleta athari zaidi kubwa kuliko
zilizopata kujitokeza. Akatulia vile akitazama mbele kama mtu aliyepotewa na
akili.
‘…huwezi kulia tu maisha yako yote sababu ya Dennis…anapaswa
kuamua kuwa na wewe au huyo mwanamke… Daniella you deserve the best… kwanini
umpiganie mwanaume?...why?... yeye ndiye anapaswa kukupigania usiondoke kama
kweli anakupenda… niahidi hutalia tena sababu ya Dennis na kama itatokea
fungasha vifurushi vyako na uanze maisha yako… mtaliki!’ maneno ya mama yake
wakati akizungumza naye yalipita kichwani mwake kama kipande cha sinema. uso
wake ulitulia na hata machozi yalishakoma kutoka.
Daniella akashusha pumzi ndefu, akipunguza ukubwa wa macho
yake na ndita mbili zikikunjika usoni pake. Pumzi ile ikamrejesha pale
alipokuwa. Akazikusanya nywele zake za rangi la samawati na kuzirudisha nyuma,
akizifunga kwa chupio yaliyokuwa amebandika kichwani pake.
Kama mtu aliyepata wazo jipya, akawasha gari lake na
kuliondoa eneo lile taratibu. Akili yake ilifanya uamuzi pale pale na alipotoka
pale alielekea lodge moja ya kisasa na kuamua kuutumia uisku ule peke yake,
akiutafakari uamuzi wake nap engine akijipa mikakati ya kuutekeleza. Wakati
akifanya uamuzi wa kulala nje, mumewe alikuwa katika hekaheka ya kumtafuta
mpaka pale alipopata uhakika kuwa Daniella alikuwa salama ndipo naye alipouweka
ubavu kitandani, ikiwa ni usiku wa saa nane na vichapo kadhaa.
888888888888888888888
Wakati watu wengine wakiusaka usingizi kwa bidii zote,
Patrick Mazimbwe alikuwa chumbani kwake akipiga funda kadhaa za pombe. Uso wake
ulikuwa mtulivu mno na wala hakuonekana kuwa na maumivu yoyote wakati ule.
Alikuwa ameketi kwenye sofa lililokuwa chumbani kwake na kunyoosha miguu juu ya
stuli aliyoiweka mbele yake. Pembeni kwa mbele aliweka laptop iliyokuwa
ikionyesha picha zake na Pamella, zikipishana sekunde hata sekunde. Alizitazama
taratibu huku chupa ya pombe kali ikipanda kuelekea mdomoni na kushuka taratibu
kisha kutua juu ya paja lake la kushoto bila kuachiwa.
Alitabasamu, tabasamu lililokosa tafsiri rasmi, akaikodolea
macho picha ya Pamella Okello iliyojitokeza kwa mara nyingine, akaitazama
ilivyotulia pale na kisha kupotea kabla ya kujitokeza nyingine iliyowaonyesha
yeye na Pamella wakiwa ufukweni. Picha ile ilidumu kwa sekunde moja tu na
Patrick akajikuta akiifunga laptop yake pasipo hata kuizima.
Akatulia tu, akatulia sasa akiwaza mawazo yaliyokuja katika
mpangilio mbovu. kichwa kikamzunguka, kwa wakati ule hakuona thamani hata ya
pumzi aliyokuwa anaivuta. Kwa wakati ule ndio aligundua ni kiasi gani alikuwa
namapenda Pamella Okello kuliko Clarita Gabson. kwa wakati ule ndio aligundua
ni kiasi gani furaha yake ilikuwa imajengwa juu ya msingi wa uwepo wa Pamella.
Kama kuna mtu angelimweleza kuwa mapenzi yanaua wiki chache zilizopita si ajabu
angelimcheka kupitiliza, lakini sasa hali aliyokuwa akiisikia na kuihisi
ilitosha kumhakikishia kuwa mapenzi yanaua!
Akabugia pombe yake kwa fujo mno, nyingine ikishindwa kuingia
mdomoni na kuchuruzika pembeni, Alipoitua ile chupa alikuwa akihema mithili ya
mwanariadha aliyemaliza mzunguko wa mbio za kuruka viunzi. Akaangaza angaza
mule chumbani kana kwamba alitarajia kuona taswira yoyote ya kumpa ahueni,
hakuona chochote, hakuona lolote, hakuona yoyote! Akafumba macho na kusikilizia
maumivu ya moyo! kuachwa ukusikie tu na kukusoma karatasini!
88888888888888888888
Wingu lililokuwa limetanda usiku uliopita, lilileta mvua ya
asubuhi na mapema. Mvua ya rasharasha iliyonyesha bila kukatika tangu alfajiri.
Baridi ndogo iliyohitaji japo koti la kuzugia iliongeza utamu wa mvua ile ya
asubuhi. Dennis aliingia ofisini kwake, koti yake likionekana kuwa na matone
machache ya mvua iliyomnyeshea wakati akitoka kwenye maegesho na kulifuata
jengo la ofisi.
Alivua koti lake na kulitundika sehemu yake, akaifuata meza
yake ya kazi na kuitua briefcase yake juu ya meza. Macho yake akatua
kwenye karatasi chache zilizokuwa
zimeunganishwa pamoja. Akakunja uso wakati akiziokota na kuzisogeza usoni, zile
ndita zikawa tatu sasa.
Mkono wa huohuo uliokuwa na zile karatasi, ukaziminyia kidogo
na kuifuata simu ya mezani. Akabonyeza namba mbili tatu na kusikilizia
‘Huu ni upuuzi gani hapa mezani?’ akahoji akiwa ametoa macho,
jazba zilikuwa zinapanda kwa kasi ya ajabu. Hakungoja hata yule aliyempigia
amjibu. Akakata simu na kuurejesha mkonga sehemu yake, kisha akachanua tena
zile karatasi na kuzisoma kwa mara ya pili kana kwamba akili yake ilikuwa
imesahau yote aliyoyasoma mara ya kwanza
Sekretari wake akafungua mlango na ukingia kwa kasi kidogo,
uso ukiwa na wasiwasi
‘hizi barua za wiki iliyopita zinaletwa kusainiwa leo kwa
misingi ipi?’ Dennis akauliza kwa sauti kali kidogo
‘Zilisahaulika kwenye faili la barua zinazoingia…samahani kwa
hilo’ Skretari akajitetea na asijue moto aliouwasha
‘Ulisahau?... unalipwa mshahara hapa kusahau vitu?... hujui
majukumu yako?... ujinga gani huu sasa?... hebu nenda kaandike barua zenye
tarehe ya leo na uwatumie fax ya kuwaomba radhi kwa kuchelewesha majibu..
uzembe wa aina hii siutaki ofisini hapa na kama unadhani akili yako haina uwezo
wa kutunza kumbukumbu kaa pembeni…kuna watu wanahitaji kufanya kazi ufanisi sio
kuleta excuse za kijinga jinga kama hizi’ Dennis akagomba kwa ghadhabu na kumtupia
sekretari wake zile karatasi.
Binti wa watu akaziokota kiunyonge na kutoka mule ofisini
akiwa na maswali mengi kichwani. Ni mwaka wa tano sasa tangu aanze kufanya kazi
na Dennis Mazimbwe. haikuwahi kutokea kugombezwa namna hii, kwa staili hii kwa kosa
kama hili kwani ni mara nyingi walikuwa wakisahau vitu na kuvirekebisha
kirafiki tu bila kukaripiana kama watoto.
Dennis akajihisi ahueni baada ya kutolea hasira zake kwa
sekretari wake. Akaketi kitini na kuanza kushika hiki na kile lakini dakika moja
tu ilipokatika kijana mmoja akaingia ofisini kwake akiwa na faili mkononi.
‘Mr. Mazimbwe… kuna appointment mbili leo jioni sasa tunata…’
kijana wa watu hakumalizia hata kauli yake kwani Dennis alimkata jicho kali na
kumjibu katikati ya maelezo yake
‘hivi ni kwanini hamuwezi kufinalize kitu bila kuleta miguu
yenu humu ndani… sidhani kama mtindo huo ndio nitakuona mchapakazi Edgar!...
please show yourself out!’ Dennis akamalizia kwa kuinamia laptop yake na
kuendelea na alichokuwa anafanya. Yule kijana akawayawaya kidogo akionekana
kupigwa na butwaa kwa lile jibu. Taratibu akaondoka zake.
Nafuu nyingine
ikamtembelea Dennis, asijue ni kiasi gani nafuu aliyokuwa anaitafuta
ilikuwa imewaumiza wengine wasiohusika na vurugu zake kichwani. robo saa tu
zikapita, Simu yake ikaita, akaipokea na sekunde kumi na tano tu baadaye
Rebecca Okello akaingia mule ofisini.
Alikuwa amevalia gauni lake jeusi ilililonakshiwa kwa
kitambaa cha kitende kiunoni kilichochanuka kama mwamvuli. Lilikuwa gauni
lililombana kiasi na kuonyesha umbile lake tulivu la kiutu uzima. Lilikuwa
limeishia chini kidogo tu ya magoti. kiatu chake kirefu kiasi kililandana rangi
na kile kitambaa cha kitange kiunoni na sehemu ya kola.
kichwani alikuwa na afro dogo, tulivu, lililozungushiwa utepe
mwembamba wa kitenge. Alionekana kama mwanamke wa kisasa aiwakilishaye afrika.
Weupe wake wa asili uliokoza na kurutubishwa na vipodozi, uliirudisha nyuma
miaka ya Rebecca. Alikuwa mrembo! mrembo hasa!... Pochi yake aliibana kwapani
mkono wa kushoto wakati akiingia kwa kuusukuma mlango kwa mkono wa kulia
uliokuwa pia na funguo za gari.
Akaingia mwanamke, akiichafua pia ile ofisi kwa manukato
yaliyosisimua pua yoyote ya mwanaume rijali aliyejua thamani ya manukato.
Dennis akainua uso na kumtazama Rebecca alivyoufunga mlango na kuchapua hatua
kadhaa kumfuata. Akatembea mpaka pembeni ya kiti cha Dennis na kujiegemeza
kwenye ukingo wa meza mbele ya Dennis.
Wakatazama tu! Dennis akiwa ameketi kwa mtindo wa kulaza
kichwa kwenye kiti chake huku akijizungusha taratibu kulia na kushoto
‘Why are you doing this to me Dennis?’ Pamella akauliza kwa
sauti ya kubembeleza. midomo yake minene iliyonakshiwa kwa rangi yam domo
ikimwemweseka na kuzidi kuvutia pale meno yake meupe yaliyopoonekana
Dennis akajiinua kidogo na kushusha pumzi kwa nguvu.
Ilihitajika nguvu ya ziada kumshinda shetani!
‘Becca!..’ Dennis akaita kwa sauti ya chini kisha akasita
kwanza
‘… Daniella is back’ akajieleza na kujieleza uko kukamkera
kweli Rebecca aliyejikuta akitazama kando
‘nisikilize mama… nisikilize basi’ akabembeleza Dennis
akiugusa mkono wa Rebecca ambaye taratibu aligeuza kichwa na kumtazama Dennis
ambaye alijiinua na kusimama wima, Akamzidi Rebecca urefu na aikawa zamu yake
kumtazama Rebecca toka juu
‘…kuna wakati nahisi tunakoelekea kila kitu kitakuwa wazi… I
won’t be safe’ akatoa hofu yake uso wake pia ukionyesha ile hofu waziwazi
‘Kwanini?... kwanini usiwe safe?’ Rebecca alijaaliwa uzuri wa
kubabaisha ila si ubongo wa kufikiri kwa kina. Mungu hakupi vyote!
‘wewe ni mke wa mtu Becca… Okello mumeo ni mtu
tunayefahamiana… what if akijua kinachoendelea?... what if akijua Pamella si
binti yake…ni binti yangu… hawezi kuniacha salama’ akajaribu kumuelewesha
lakini Rebecca ahakuonyesha kushrushwa na hilo
‘La Pamella haliwezi kujulikana labda mimi na wewe mmoja wetu
atoe siri… kitu ambacho hakiwezekani… kuhusu mimi na wewe… mi sioni cha
kumfanya akudhuru… mapenzi yakiisha
yameisha na nina uhuru wa kuwa na mwingine’ Rebecca akajieleza na
kumfanya Dennis azidi kuuona umbumbu wa mwanamke huyu aliyeiteka nafsi yake kwa
miaka mingi. Utu uzima ulikuwa umemfika Rebecca, lakini tabia na uwezo wake wa
kufikiri ulikuwa wa Rebecca yule yule aliyemuona kwa mara ya kwanza katika
harusi ya Okello na Rebecca.
‘… hata tukimuweka pamella kando… mimi ni mwanaume…I know how
it feels mke wako, mwanamke unayempenda unapohisi tu kuwa anaguswa na mwanaume
mwingine achilia mbali kuachwa na kwenda kwa mwingine… naweza kuua Rebecca..
naweza kufanya jambo la kijinga sana… kwa vile najua inavyouma’ Dennis akaongea
kwa upole akimtazama Rebecca usoni.
‘Kwa hiyo ina maana Daniella akiamua kuwa na mtu mwingine
utaumia pia?’ Rebeca akamtega
‘Sana!... sana tu… sitaki kukuficha Rebecca… sisis ni watu
wazima sasa… mapenzi ya kitoto hakuna tena… nakupenda Becca but that doesn’t
mean simpendi Daniella… I love her, she is my wife… amepita mengi sana sababu
yangu…’ Dennis akaongea akiutazama uso wa Rebecca uliokuwa umesinyaa na kujaa
hali ya kutotaka kusikia yale aliyokuwa akiyasema Dennis
‘So unamoenda zaidi yangu si ndio?’ Rebecca akauliza akiukwatua
mkono wake toka mkononi mwa Dennis
‘Siwezi sema juu ya hili Rebecca…it wont be fair na sitaki
kudanganya’ Dennis sasa akamsogelea zaidi Rebecca na kutaka kumtomasa lakini
akazuiwa
‘I swear Dennis… nimeolewa na Okello nikakuta watoto wengine
kwake… nikamzalia okello mtoto mmoja tu wa kike na akwa wa kike pekee kwa
Okello na bahati mbaya si wake ni wa kwako… hivyo nina mtoto mmoja tu maishani
mwangu niliyezaa na wewe.. Dennis ukiniacha nakuhakikishia utakuja kunizika…
sitanii…ukiniacha ni umeniua… sijali kitu…’ Rebecca akatoa onyo
‘Usiseme hivyo Babe… no! sina hata wazo la kukuacha Rebecca..
sina kabisaaa… it is me and you mpaka mwisho…ondoa hayo mawazo ya kujiua sijui
kufa…please!’ akamsogelea zaidi na kumkumbatia Rebecca kuongezea nguvu yale
maneno yake lakini uso wake ulionekana kuelemewa na maneno yake mwenyewe. Kauli
za Rebecca kujiua kwa ajili yake zilishajirudia sana kiasi alihofu zingetimia
endapo angejaribu kufanya alichotaka kufanya. Kumuacha Rebecca moja kwa moja!
Wakaachiana na Rebecca Okello akatabasamu, nuru na amani ya
moyo vikionekana moyoni mwake.
‘You are my life Dennis… I wish tuwataliki wenzi wetu na
tuoane sisi… nimechoka kuibia ibia mapenzi Dennis… ila kama huwezi kumtaliki
Daniella angalau na mimi nijali kama unavyomjali yeye… usiniache Dennis…
nitakufa!’ akarudia tena ile kauli na kumkera Dennis sasa
‘Rebecca!’ akamuita kwa msisitizo, akimshika mabega yote
mawili
‘…naomba usirudie hii kauli ya kufa kwa ajili yangu… sikuachi
sawa?... sikuachi Rebecca…’ Akajikuta akiahidi tena na tena pasipo kuwa na
uhakika na kile anachoahidi.
Wakatazamana na kukumbatiana tena kwa mahaba mazito.
‘Baba Pamella!’ Rebecca akamuita Dennis, akamtania kwa
kumuita vile wakiwa vile vile walivyokumbatiana na Dennis akacheka akimuachia
Rebecca na kumbusu pajini kwa upendo.
8888888888888888888888
Jerry na Pamella walikuwa mbele ya mtaalamu wa kuandaa
harusi. Ofisi ya mtaalamu huyo ilikuwa kubwa iliyosheheni mambo mengi ya fani
yake. Mwanadada huyu alikuwa ameketi kwenye kiti cha peke yake akiwatazama Jerry
na Pamella waliokuwa wamebanana katikati kwenye sofa moja la kutosha watu
wawili.
Kwa haraka tu, Pamella Okello alionekana kuwa na furaha zaidi
ya Jerry Agapella.
‘nataka rangi wa pinki iliyopauka na nyeupe na kahawia
hivi…yaani kitu mchanganyiko Fulani
mzuriii… eti honey we unaonaje?’ Pamella akamuuliza Jerry ambaye alionekana
kutokuwepo katika yale mazungumzo
‘Jerry!’ Pamell akamsukuma kidogo na kumshtua Jerry
‘Oh.. what…nini?’ akauliza akijitutumua kutabasamu. Pamella
akaeleza tena mawazo yake na Jerry akaitikia tu bila kupinga
‘Babe… kila kitu unasema sawa sawa… huna chochote cha
kuongeza jamani?’ Pamella akalalamika
‘nakuamini babe…’ Jerry akajibu na kumbusu midomoni Pamella.
Yule mtaalamu wa kupanga harusi akatabasamu tu na kuwatazama wapendanao hao ila
hata yeye alihisi bwana harusi hakuwa na ile hali ya kufurahia mipango ya
harusi yake. Akamezea!
‘sasa mimi nitakupa sample ya namna tunavyopamba… mfano kuna
viti na meza aina tofauti tofauti na kuna mpangilio wa matukio katika harusi…
it is just we make your event very unique in a way hata wewe unabaki na
kumbukumbu safi kabisa’ Mtaalamu akasafishia njia kazi yake na Pamella
akaitikia ilhali Jerry alipepesa macho tu.
Wakajadiliana hapo na kufikia muafaka wa kurudi tena siku
mbili mbele. Wakatoka hapo kwa mtaalamu na kutoka nje ambako mvua sasa
ilishaacha kunyesha ila manyunyu yalibaki yakidondoka taratibu. Pamella
akasimama kado ya gari lake na kumtazama Jerry aliyekuwa naongea na simu. yale
manyunyu yalimfanya akunje uso na kuukinga kwa kiganja cha mkono.
‘Hey…bye babe!’ Pamella akamuita Jerry aliyekuwa bado
akiongea na simu na kumpungia mkono. Alihisi angezidi kulowana kwa kumngoja
Jerry ambaye wala hakuysjali sana yale manyunyu. Jerry naye akampungia mara
tatu na kuendelea na simu yake
Pamella akaondoa gari na kuishia zake, Jerry akmaalizia
mazungumzo na kulifuata gari lake. Akawasha na kuliondoa akielekea nyumbani
kwao.
Alimkuta baba yake jikoni akikaanga mayai.
‘Wasaidizi wako wapi?’ Jerry akashangaa
‘sio kila wakati unahistaji kuzungukwa na watu… wakati
mwingine kuwa mwenyewe kunakupa nguvu ya kuufurahia uhai ulio nao’ baba yake
akamjibu akigeuza yai lake lililokuwa limeungua vibaya mno.
Akazima jiko na kulipakua yai lake kwenye sahani.
‘leta uma na kisu tushambulie hiki kitu’ akamuagiza mwanae
yeye akitangulia kuelekea sehemu ya kulia chakula
Jerry akacheka kwanza wakati akilifuata kabati, pale mezani
Jerry alimpa baba yake uma na kisu, yeye akijimiminia maji tu na kuketi kiti
kilicho mbele ya baba yake
‘Huli?’ baba yake akamuuliza akianza kukata lile yai
‘Nope!... lilivyoungua hivyo?... no! enjoy tu’ Jerry akacheka
kwa sauti akimtazama baba yake aliyekuwa amekunja uso baada ya kutupia kipande
cha yai mdomoni.
alipoanza kutema vitu alivyohisi visingemezeka, Jerry
akazidisha kucheka zaidi. Mzee Agapella akaisogeza sahani pembeni na kuvuta
karatasi ya kufutia mdomo. Akajifuta na kuiweka ndani ya ule msosi.
Sasa akamgeukia kijana wake huku naye akijimiminia maji.
‘You don’t look excited wakati ni harusi yako Jerry’ baba
yake naye akatoa wasiwasi wake
‘niko sawa baba… ni vile mambo mengi sana… kuna harusi, kuna
kazi ofisini na mambo mengine binafsi… ila niko sawa’ Jerry akajitetea
‘Umepewa likizo ya mwezi mzima…na nimekaimu nafasi yako
ofisini mpaka urejee… nini kinakupa hofu Jerry?... unaoa binti mzuri, rafiki
yako wa siku nyingi, mwanamke anayetoka katika familia kubwa inayofahamika na
zaidi una support toka kila mahali…. nini kinafanya uwe mnyonge mnyonge hivi?’
‘Niko sawa kabisa… labda ni hofu tu ya kuwaza ndoa itakuwaje…
nimeona mengi baba toka ndoa yako na mama hadi nah ii ya Fiona ambayo sijui
ndio imeshavunjika au lah… naona kama ndio mwanzo wa maisha mengine kabisa’
Jerry akajitetea akitafuta sababu ilhali akijua wazi kilichokuwa
kinamnyong’onyesha si kile alichokiongea.
Mzee Kristus Agapella akamtazama kijana wake kwa umakini
mkubwa. Aliiona hofu ya mwanawe na akahisi hali ya kujilaumu pia kwa kumletea
ile hofu aliyotaja. Akajitutumua kutabasamu
‘Jerry!’ akamuita kwa upole akimsogezea uso mbele kuleta
umakini
‘ndoa haina kanuni kama hesabu!... kitakachoijenga ndoa hii
ukute ndio kinachoivuruga ndoa ile… ndoa ni wewe na mwenza wako!... ni maisha
ya kila siku kati yako na mwenza wako… Kilichonitokea mimi si lazima kikutokee
wewe labda tu ufuate nyayo nilizofuata mimi… I made a mistake Jerry… na majuto
ya kosa nililofanya kwa Sophia nitaingia nayo kaburini!... najua siwezi
kubadili kitu lakini nimechagua kuishi maisha ya kujisamehe nikiamini mimi ni
binadamu nakosea na kupotoka’ Mzee akaongea kwa hisia zaidi
‘I married Sophia for love… nikamuona Fiona kwa tamaa… sijui
hata akili ilikuwa wapi.. sijui hata ilikuwaje lakini maisha niliyoishi na
Sophia ndio maisha ninayoyaita ya furaha… muoe mwanamke unayempenda kwa
dhati…ambaye unadhani hutaona udhaifu wake kwa mapana kuliko ubora wake… you will
be happy son!... ndoa sio harusi siku zote zipo nyakati za msiba pia… zipo
nyakati za kushikamana na kutengana… zipo nyakati za kulia pamoja na kulia peke
yako lakini mwisho wa siku ni upendo wa dhati ndio uwaleta tena pamoja na
kudumisha ndoa… anayekuvumilia ndiye anayekupenda!’ Mzee akatulia kidogo
kupisha mate yapite kooni
‘… tunatoka nje…sawa! tunacheza rough nje…hiki sio kitu cha
kufichana Jerry lakini mwanaume anayemuheshimu mke wake hatokaa afanye rough
hizi kwa uwazi wa kumfanya mkewe ajue! Never! ever!’ akatikisa kichwa kwa
msisitizo
‘and you let mom know uko na Fiona!’ Jerry akaongea kwa sauti
ya kumsuta
‘Yes!... na ndipo majuto yalipo na ndipo maswali yalipo…
sijui ilikuwaje… sijui Jerry…’ Agapella akawa mkweli kwa kijana wake
‘and I hope Pamella ndiye mwanamke uliyetayari kumvumilia na
kuona mapungufu yake kwa mbali sana… niko sahihi?’ baba yake akamuuliza na
Jerry akatabasamu tu. Swali hili hakulijibu mdomoni bali alilijibu moyoni kwa
kutamka kimoyomoyo ‘hapana!’
8888888888888888888888888888
Nadina alitembea kwa madaha kwenye kordo ya kuelekea kwenye
vyumba vyao vya kulala. alipoukaribia mlango wa chumba chake alivua kiatu
kimoja na kuchechemea kidogo kabla ya kuvua cha pili na kuvishika mkononi.
Akaufikia mlango na kuufungua, akiusukumia mbele na kutanguliza kichwa
akitabasamu.
Akaguna na kurudisha nyuma kichwa chake, akautanua mlango kwa
mapana ya kutosha na kuingia shingo ikimnyoosha na kukitanguliza tena kichwa
kuchungulia huku na kule. Akamuona Sindi Nalela ameketi kitandani kwa mtindo wa
kujikunyata kama mtu asikiaye baridi.
‘Sindi..Sindi…’ Nadina akaita kwa hofu akivitupa vile viatu
mkononi na kumharakia Sindi pale kitandani. Akaketi na kumtikisa Sindi
aliyekuwa anatetemeka na kupepesa macho kama mtu alijawa na hofu kupitiliza,
ama aliyeona kitu cha kushtukiza.
‘Sindi… nini kimetokea?’ akamuuliza akizidi kujisogeza karibu
yake na kumtikisa. kule kumkaribia kukamfanya Nadina aone damu puani mwa Sindi
na damu ile ikamsisimua na kumfanya atanue macho yake zaidi kana kwamba alitaka
kuihakiki ile damu kwa kutumia macho.
Moyo ulipiga kwa kasi ya ajabu mno, mikono ikamtetemeka
wakati ile damu ilipokuwa inazidi kutokeza puani na kuchuruzika kuelekea kwenye
midomo ya Sindi. Nadina akachanganyikiwa zaidi Sindi alipoanza kulegea na
akionekana wazi kuishiwa nguvu
‘Jerry…’ Sindi akatamka kwa sauti hafifu macho yakimlegea
zaidi na ile damu kuongeza kuongezeka taratibu. Nadina akanyanyuka na kutafuta
kanga, akaitumia kufuta ile damu na hapo hapo akipata akili ya kumlaza chali
kitandani kabla ya kutoka kuomba msaada.
hakujua wala kukisia Sindi alikuwa amekutwa na masaibu gani.
‘jerry…’ akaita tena na umakini wa Nadina ukaongezeka baada
ya kulisikia jina hili kwa mara ya pili
‘Jerry ni nani?...Sindi…Sindi…Jerry amekufanyaje?’ Nadina
alihaha kutaka kujua zaidi wakati Sindi akielekea kupoteza nguvu zaidi
‘namtaka Jerry..’ akasema tena kwa shida safari hii machozi
yakitiririka pembezoni mwa macho yake na ile damu ikiongezeka
‘Mungu wangu…Jerry ni nani?... Sindi jamani… Sindi…Sindi’
Nadina sasa alikaribia kuwehuka, akauliza kwa kupayuka, akauliza kwa hamaki,
akauliza akitetemeka. Sindi akamtazama tu akimwemwesa midomo yake. Ni kama vile
alitaka kusema neno kamili lakini sauti yake ilikwamia kooni. Alikuwa amelegea
kupitiliza na damu haikuacha kumtoka puani. Sindi akatabasamu, tabasamu
lililoashiria maumivu yaliyogusika kwa mikono ya binadamu.
Nadina akasimama ghafla na kumtazama Sindi kwa macho ya
mshtuko. alitetemeka mpaka utumbo. alimtazama Sindi vile alivyokuwa amelegea na
zile damu na lile tabasamu. Kwa mikono iliyotetemeka akamuinamia tena huku
akilengwa na machozi na kuitazama blauzi ile aliyoivaa Sindi. akaitazama kwa
umakini na kukitumia kidole chake cha shahada kusugua unga mweupe ulionekana
kwa mbali juu ya ile blauzi.
Akalisugua lile eneo na kukipeleka kile kidole puani. Akahisi
kuishiwa nguvu, akahisi kuhamanika, kutetereka machozi yakamtiririka. Alihisi
kumpoteza Sindi, alihisi kulikuwa na zaidi ya maumivu katika maisha ya Sindi.
Sindi amekuwaje?... nini kimempata?... Siri ya Dennis na
Rebecca ipo salama?... Daniella ameamua nini?... Jerry ana lipi linalomsibu
asifurahie harusi yake ijayo… Majibu yote yapo hapa hapa!!
ITAENDELEA…..
I appreciate your project!
ReplyDeletenamba 50 naisubiria kwa hamu sana
ReplyDeleteiam speechless laura nasubiria sehemu ya 50 tuu
ReplyDelete