“ unasemaje Jonas! Ulinibaka ….sikufanya vile kwa hiari yangu yaani pamoja na kuistiri ile aibu leo unaniambiaje?” nilipayuka kwa ghadhabu hali naye akiwa na hasira zake.Ukweli alinitibua hasa!
“mimi ni mume wa mtu Karen!” alinipandishia
“leo ndio mume wa mtu ila siku ile ulikuwa mume wa mbuzi si ndio?” nilimuuliza kwa kejeli.
“kama hutaki kuitoa usinihusishe kwa lolote Karen!”
“sitakuhusisha wewe ila mkeo na viongozi wenzio”
“Shut up! Unadhani ni sifa kuutangaza upuuzi kama huu Karen?”
“ndio unagundua saa hizi kuwa ni upuuzi! Mimba sitoi na kuilea utailea…toka nje upesi shetani mkubwa wewe!” nilimfukuza kwa hasira. Aliuendea mlango na kuufungua kisha akatoka na kuubamiza kwa nguvu. Niliketi chini na kuangua kilio kama mfiwa. Niliomboleza kwa masaa kadhaa pasipo kunyamaza.
Sikujua ningeieleza nini jamii juu ya ujauzito ule. Ningewaeleza nini wazazi wangu na marafiki zangu achilia mbali ndugu na jamaa. Nisingeweza kukiua kiumbe hiki kisicho na hatia. Nililia mpaka usingizi ukanipitia.
Sikuwa na amani moyoni na hasa nilipomtazama Iloma. Nilijitahidi kumkwepa na kukaa mwenyewe nikitafakari hatma yangu. Nyakati zingine niliupitisha usiku huku nikisononeka na kulia, huu ulikuwa ni mtihani mwingine mkubwa kwangu. Siku chache baadae nikiwa katikati ya kazi zangu ofisini. Jonas aliingia ghafla ofisini kwangu. Zilikatika dakika kadhaa tukitazama pasipo kuongea.
“ unataka nini ?” nilimuhoji na kuvunja ukimya
“ Nisamehe Karen! Sikustahili kukujibu vile hata kidogo, nakubali kuilea mimba hiyo kwa moyo mmoja …niliongea yale kwa hasira tu”
“Tafadhali toka ofisini kwangu! Sina haja na msaada wako Jonas, sina shida na wewe…toka nje…tokaaa na tokomee” nilizungumza kwa sauti kiasi Jonas alihisi kama angeendelea kukaa pale si ajabu mambo yangeharibika.
Alitoka nje huku akionekana kusononeka. Nilirudi kuketi mezani pangu huku tayari machozi yakiwa njiani.
Alfajiri ya siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni jumapili, niliamka nikiwa sina amani moyoni. Furaha ilikuwa imekimbilia kusikoeleweka. Nilijiandaa kinyonge na kuelekea kanisani. Kila aliyekuwa ananifahamu alinitazama kwa mshangao kidogo.
Uso ulionekana kujaa majonzi ambayo nilishindwa kabisa kuyaficha moyoni mwangu, macho yalikuwa yamejaa mithili ya mtu aliyekesha akitwanga gunia la vitunguu.
Niliingia kanisani na kuketi mbele kabisa wakati mzee wa kanisa alipomkaribisha jonas atoe taarifa ya kamati ya vijana kwa ufupi.
Alinitupia jicho la wizi na kuchapua hatua za haraka haraka kuelekea mbele. Sikummaliza kabisa! Nilihisi hasira hasa nilipokumbuka majibu yake siku ile..
“ bwana yesu asifiwe!” alitamka kwa sauti ndogo iliyokosa uchangamfu
“ Ameeeeeen!” kanisa liliitikia kwa sauti kubwa na furaha kama ilivyokuwa kawaida pale Jonas aliposimama kuongea kila mmoja alimfurahia si tu kwa namna alivyoongea kwa kuvutia bali pia ule muonekano wake wa mtu wa mungu!
“…Kwa baraka zake mwenyezi mungu leo hii tena tumekusanyika hapa katika ibada hii ya kumshukuru mungu. Hatuna budi kumshukuru mungu kwa upendo wake wa ajabu kwetu wanaadamu, Kwa ufupi kamati ya vijana imefanikiwa kukamilisha miradi ifuatayo” alifungua faili lake na kabla ya kutamka chochote alinitupia tena jicho la wizi. Kisha akaendelea
“tumekuwa tukitoa mafunzo ya robo…samahani mafunzo ya kiroho kwa ajili ya vijana wenzetu waliokatika ndoa na hata kwa wale wanaotarajia kufunga ndoa katika juma hili. Kwa hakika tumefanikiwa kwa asilimia sitini…aah! Samahani kwa asilimia tisini kuimarisha roho ya kanisa. Bwana yesu asifiwe sana! Pili ni kwamba mradi wa ukuzaji…samahani usambazaji neno..” alijichanganya kiasi cha kuwafanya waumini watazamane kwa mshangao, haikuwa kawaida kwa Jonas kukosea kosea vile taarifa za kanisa na namna alivyokuwa akiongea kwa sauti ndogo ya kusitasita ndio kabisa kanisa zima ilionekana kumsikiliza kwa mshangao wa waziwazi.
Wakati akiendelea kusoma taarifa hiyo kwa kujikanganya alinishuhudia nikinyanyuka toka pale kitini na kupiga hatua za taratibu kuelekea nje. Asilimia kubwa ya waumini waligeuza shingo zao na kunitazama. Nadhani wengi walitarajia kuniona nikipiga kinanda kanisani na kuimba mara baada ya taarifa ile kama siku zote nifanyavyo.
Nilikuwa mwimbaji mzuri kanisani na wengi walivutiwa na namna nilivyokuwa nikipiga kinanda kanisani na kuimba peke yangu lakini siku hiyo mambo yalikuwa tofauti. sikutaka kabisa kuusikia unafiki wa Jonas mbele ya halaiki ya watu waliofika kuabudu na kumsikiliza yeye kama mtu wa mungu na nilijua fika kuwa ningejichanganya kama Jonas na hivyo kuongeza maswali vichwani mwa watu..
Niliondoka kabisa kanisani na kurudi nyumbani. Niliingia ndani na kujitupa kochini kama gunia la viazi. Pasipo kujielewa nilizama mawazoni na kwa hasira nilizokuwa nazo machozi yaliupamba uso wangu pasi kujitambua akilini.
Wakati wote huo sikuwa nimetazama upande wa pili wa sebule hii ambako mama alikuwa ameketi akinitazama. Nilishtuliwa na sauti ya mama iliyonitoa kabisa mawazoni
“ na sasa unajichongea kaburi Karen, alikupa mapenzi gani mwanangu mpaka ushindwe kumsahau kabisa akilini mwako?...tazama! umekonda Karen uso umechujuka kwa mawazo na umeshindwa kusali sababu ya Kelvin, Kelvin ni nani hata akuharibu hivi mwanangu kwanini hutaki kuukubali ukweli kuwa amekuacha na hutampata tena?” mama alinifokea bila kujali kuwa hatukuwa tumeonana kwa takribani mwezi mzima na wala hatukuwa tumesalimiana.
ITAENDELEA.....
No comments:
Post a Comment