Monday, May 23, 2011

SIRI YANGU 6.....Na Laura Pettie

..... “ wewe unashtuka hivi Karen unadhani mimi nilishtuka kiasi gani?”
“ No! unajua… sasa…kwani rafiki yako huyo anamfahamu huyo mwanamke?” nilimtupia swali huku maneno yakigongana gongana na kama Iloma angekuwa makini angehisi kitu katika kauli yangu.
“ anasema hamfahamu lakini kama atakwenda naye tena hapo hotelini basi atammaki sura vizuri”
“ lakini usipende kusikiliza maneno ya watu Iloma”
“ hawezi kunidanganya, jonas amebadilika mno tabia sijui nimfanyeje jamani”
nilishusha pumzi na kutafuta haraka cha kusema nikakosa!
“ naomba leo uje uongee naye mbele yangu nyumbani wewe anakuheshimu na nadhani itasaidia kidogo” iloma alitamka taratibu bila kujua kuwa alikuwa ananiweka katika mtihani mkubwa mno.
“ lakini Iloma kwanini usilipeleke swali hili kwa mshenga wenu?”
“ nitakwenda kama ushauri wako kwake hautasaidia Karen”
nikakwama kabisa. Nilitumbua macho tu nikiwa sinahata la kusema. Nikarejea kitini pangu na kujitupa kwa nguvu.
“ nitajaribu!” nilimpa jibu fupi na tabasamu likachanua usoni pake.
“ nadhani leo baada ya kazi twende wote nyumbani kwangu”
“ hapana shaka!” alisimama na kuja kunikumbatia pale nilipokuwa nimeketi kisha akatoka na kwenda kuendelea na kazi zake.

Alizidi kunichanganya mno. Sikujua ningeongea nini na jonas na wala sikujua usiku wa siku hiyo ningeongea nini mama juu ya inshu ile ya mimi kulala nje bila taarifa.

Niliinamisha kichwa changu mezani na kutafakari moja baada ya jingine pasipo hata kufikia muafaka wa kile nilichokuwa ninawaza. Wakati wa chakula cha mchana nilijiweka ‘busy’ sana ili kukwepa kuwa karibu na Iloma na hivyo sikutoka ofisini. Wakati nikiendelea na kazi simu yangu ya mkononi iliita na mpigaji alikuwa Jonas.

Mapigo ya moyo yalibadili kasi kiasi nikahisi joto la ghafla likiuvaa mwili wangu. Simu iliendelea kuita kwa muda na hatimaye ikakatika yenyewe. Dakika tatu mbele jonas alipiga tena safari hii niliikata na kuzima simu kabisa bila kujali watu wengine muhimu ambao wangenitafuta kwa shida za maana.


Jioni ya siku hiyo tuliondoka wote na Iloma na kuelekea kwake. Siku hiyo iloma alikuja na gari lake ambalo hakuwa akilitumia kwa muda mrefu baada ya kupata ajali. Tuliwahi kufika kwake mapema tu na kwa hakika nilianza kustaajabia mazingira ya nyumba hii ya rafiki yangu Iloma. Ilikuwa imepita muda mrefu tangu nimtembelee kwake kwa mara ya mwisho alipojifungua mtoto wake Kim.

Mara baada ya kukaribishwa ndani nilikumbana na harufu moja mbaya niliyoshindwa kuitabiria ni harufu ya nini. Sebule yake yenye makochi mazito ya kisasa yalikuwa shangala baghala huku baadhi yakionekana kuwa na alama za mikojo ya mtoto! Vitabu na magazeti vilisambaa kila kona na kufuta kabisa mandhari tulivu ya nyumba hii.

Nepi kadhaa zenye kinyesi zilikuwa zimetelekezwa chini na kim mwenyewe alikuwa ameketishwa kwenye kapeti akiwa amevalishwa fulana bila hata nguo ya ndani. Uso mng’aavu wa kim wenye kulandana vema na baba ulikuwa umetapakaa uji uliokauka na kwa hakika fulana aliyokuwa amevaa ilitia kinyaa! Bakuli lenye uji wa mtoto lilikuwa limetelekezwa chini karibu na mlango huku inzi wakilizengea.

Nilichagua sofa moja na kuketi wakati Iloma alijitoma ndani na kuniacha nikikagua mazingira ya jumba lile ambalo kwa hakika lilitakiwa kuwa katika usafi wa hali ya juu. Nilihofia kumpakata hata Kim kwa kuhofia kuchafuliwa na haja kwa vile hakuvalishwa chochote na hivyo kuishia kumpungia mikono na kumsemesha kwa hili na lile.

Dakika chache baadae Iloma alirejea ukumbini akiwa amevalia fulana moja nyeupe na kujifunga khanga kiunoni.

Nilimshangaa zaidi! fulana hiyo sikuelewa kama ilikuwa chafu au rangi yake ndio ilikuwa imefubaa hali kadhalika khanga aliyokuwa ameivaa haikumstahili mwanamke kama yeye tena mke wa mwanaume mtanashati kama Jonas! Hapo ndipo nipoanza kuhisi sababu za Jonas kusaka mwanamke mwingine.
“ Lawama! Wee’ lawama!” alimuita mtumishi wake wa ndani. Pengine nikitegemea kutokea kwa msichana mwenye umri wa kati ikawa sivyo. Msichana mdogo mwenye umri kati ya miaka kumi ama kumi na mbili alikuja mbio pale sebuleni na kusimama mbele yetu. Akapiga goti na kunisalimu. Nikaitikia hali nikimtumbulia macho si tu ya mshangao wa namna alivyokuwa mchafu toka utosini mpaka nyayoni bali pia kwa ule udogo wake! Lawama alimchukua mtoto na kutokomea nae jikoni, nikamgeukia Iloma
“ anaweza nini huyu Iloma?” nilimuuliza kwa hamaki
“ ni bora huyu kuliko kuleta wasichana waliopevuka humu ndani” alinijibu kwa kujiamini kabisa
“ hofu ya nini! humuamini Jonas kiasi cha kuhatarisha maisha ya mtoto wako kwa kuajiri mtoto kama huyu asiye jua hata kuoga!!!” nilishindwa kumuelewa
“ Karen! Mwanaume si mtu wa kumuamini asilimia mia moja! Ni bora kitoto hicho kisichojua kuoga angalau utaishi kwa amani, nashukuru anajua vikazi vidogo vidogo!”
“ sikubaliani nawe Iloma!” nilizidi kuhamaki
“ hutakubaliana nami kwa vile hujui hali halisi.” Alinipa jibu lililonifunga mdomo
ukimya ukapita kati yetu na Lawama akarejea pale ukumbini akiwa na chano chenye glasi ya juisi. Alipoitua ile juisi mezani niliitazama vema ile glasi na kushuhudia madoa ya uchafu yakiwa yameipamba glasi ile hali chano ile iliyobeba glasi ikiwa na nyufa. Sikujisikia kunywa tena ile juisi lakini pia sikutaka kumuonyesha wazi Iloma kuwa glasi yake ilikuwa na kasoro. Nikaamua kuinywa hali nikimuomba mungu aniepushe na maradhi ya tumbo!

Wakati tukiongea hili na lile, honi ilisikika nje na nikajua kuwa Jonas alikuwa amewasili. Punde aliingia ndani na kutukuta pale sofani. Akajenga tabasamu kama ilivyo ada yake na kuja kunisalimu. Hatukutazamana hata machoni kwani nilikiondosha haraka kiganja cha mkono wangu na kujifanya kutafuta kitu katika pochi yangu. Iloma ambaye hakujishughulisha hata kumpokea mumewe aliyeishia chumbani alipaza sauti na kumuita lawama. Mtoto yule akaja tena mbio na kupiga goti mbele yake.

“ una masikio magumu sana Lawama! Nikueleze mara ngapi kuwa baba akija umpokee hiyo briefcase yake na kim ameshaoga?” akamuhoji
“ bado mama!” akajibu haraka lawama hali akijivuta nyuma pengine kujiweka mbali na dhoruba ya kofi kama lingemkumba
“… unataka sasa nitumie fimbo kukukumbusha kila kitu eeeh! Haya upesi potea” akamfukuza Lawama.
Jonas aliporejea sebuleni aliketi sofani na kwa sekunde kadhaa alionekana kuanza kukerwa na harufu ile iliyokuwa kero kwangu pia.
“Mama Kim kuna nini kimeoza humu ndani?” Jonas alimuuliza mkewe
“ Labda ni hizo nepi za mtoto hapo chini” alimuonesha mumewe beseni dogo lililokuwa na nepi chafu kwenye kona ya kuelekea kordoni.
“ sasa huoni kuwa ni kero kwa hii harufu, hebu ziondoe upesi” Jonas alimkaripia Iloma ambaye wala hakujishughulisha kuzitoa zaidi ya kumuita Lawama kwa sauti na alipokuja alimuagiza kutoa zile nepi hali zingine alizichukua chini kando ya sofa. Licha ya nepi zile kuondoshwa lakini bado harufu iliendelea kutawala.
Jioni ya siku hiyo tuliongea mengi na Jonas. Nilijitutumua kumuhoji Jonas sababu za yeye kumfanyia yote yale mkewe ambaye naye alikuwa kando yangu akisapoti maneno yangu.
Jonas hakuongea kitu zaidi ya kunitazama kwa chati na kutikisa kichwa kuonyesha kunielewa pale nilipompa ushauri wa kuwa wazi kwa mkewe na kujaribu kurekebishana pale anapoona tofauti!
Alimtaka radhi mkewe na nikajiona kama mtu aliyetua mzigo mzito baada ya kuongea hayo.

ITAENDELEA....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger