....Baada ya kumalizana na SIRI YANGU..., nimekuja na kitu waraka wa mwisho, hadithi niliyoitunga mwaka 2009 ikiwa maalumu na dedication mama yangu mdogo Mary Samwel.
Mungu azidi kukupa maisha marefu nizidi kufaidi upendo yako!
Kwako SAKINA
Nakuandikia waraka huu hali nikijua wazi kuwa utakuwa waraka wangu wa mwisho kwako na kwa walimwengu. Nauita waraka wa mwisho kwa vile nimedhamiria kuukimbia ulimwengu uliojaa kila aina ya lila na fila na kwenda kule kusikorudika.
Sitajali walimwengu watanihukumu vipi kwa uamuzi wangu huu kwavile yaliyonikuta yanatosha na aibu niliyoipata pia inatosha acha nikapumzike na masahibu ya dunia.
Sakina, Dunia uwanja wa fujo nikiwa na maana kila mmoja huja na mirindimo yake, Dunia mti mkavu kiumbe usiuelemee lakini zaidi dunia tambara bovu lisolositiri makovu! na haya nimeyashuhudia mimi mwenyewe ndani ya miaka yangu arobaini na mbili niliyovuta pumzi ya bure ya mwenyezi mungu.
Nikisema nimlaumu Karima kwa kumleta kiumbe huyu aliye chanzo cha yote haya yaliyonikumba nitakuwa nakufuru lakini pia nikisema niulaumu ulimwengu kwa kutonipa tahadhari naona kama nitakuwa najikosha kwa vile nilipokanywa sikusikia la mwadhini wala mteka maji msikitini. Wembe nilioulilia sasa umenikata!
Sakina, nimekutendea mengi ya kufurahisha na kuhuzunisha. Nimekutendea yale ambayo kwa hakika kwa binadamu mwingine kamwe asingeliweza kunistahi na kunisamehe lakini wewe sakina uliyafumbia macho na kunipa nafasi kadhaa za kujirekebisha.
Aibu yangu ilikuwa yako vilevile. Sakina nasita hata kukuita mpenzi kwa sababu ya yale ambayo yametokea kati yetu lakini kwa jinsi ninavyojutia sina maneno ya kutosha kuuelezea uchungu wa toba nilio nao. Nakutaka radhi kabla sijaueleza ulimwengu yaliyonikuta!
Sakina, naandika waraka huu hali matone ya machozi yakizidi kuulowanisha waraka huu, najuta, najuta na narudia kusema najuta nikiwa na maana kuwa najuta kuliko neno majuto linavyomaanisha.
wahenga walisema asiyefunzwa na mama hufunzwa na ulimwengu na leo hii nakiri ulimwengu umenishikisha adabu!
Sijui nianzie wapi kusimulia haya yaliyonikuta, niko njia panda nisijue basi la kupanda. Pengine nianze na siku hii iliyozaa mambo yote haya, siku ambayo nitailaumu mpaka naingia kaburini!
ITAENDELEA...
No comments:
Post a Comment