Thursday, May 26, 2011

SIRI YANGU 11....Na Laura Pettie

Sikukumbuka kitu mpaka nilipokuja kuzinduka nikiwa hospitali. Nilipofumbua macho nilishuhudia kitanda changu kikiwa kimezungukwa na watu kadhaa. Nilimtambua mama aliyekuwa analia muda wote, nilimtambua dada yangu Debby ambaye naye alikuwa analia, nikamtambua Kelvin aliyekuwa karibu yangu kabisa.

Nilifumba macho tena kuvuta kumbukumbu zangu. ‘jonas amefariki usiku huu kwa ajali ya gari kinondoni’ maneno hayo yalipita ubongoni mwangu na ghafla nilipiga yowe
“ mamaaaa! Mama jonas, jonas jonas mama?... mama jonas yuko wapi?” nililia wa sauti ijapokuwa walijitahidi kunituliza lakini asikudanganye mtu kilio cha kufiwa hakituliziki. Nililia sana mpaka nilijihisi kuchoka na sauti kunikauka.

Kelvin akaniambia nililetwa pale jana usiku na hivyo nilikuwa nimepoteza fahamu kwa muda mrefu. Sikuwa nasikia la mnadi dini wala mteka maji msikitini. Yote yalikuwa kama ndoto ama habari Fulani ya kufikirika isiyo na ukweli hata chembe.
Jioni ya siku hiyo nilitoka hospitali na kwenda kwa jonas.

Nilipouona umati wa watu pale nyumbani ndipo nilipoamini kuwa Jonas alikuwa ameniacha. Ndani vilio vilikuwa vikali mno kukawa hakuna wa kumbembeleza mwenzake. Nilipoingia ndani Iloma aliyekuwa amevikwa nguo nyeupe aliponiona alipiga mayowe na kutaka kunyanyuka ili anifuate. Nilimsogelea na tukakumbatiana kwa nguvu.

Iloma alikuwa analia jamani. Alikuwa analia mno na kwa uchungu hasa! Hivyo ndivyo Jonas alivyoniacha, hivyo ndivyo jonas alivyonipigia simu saa moja kwa kifo chake. Alikuwa ameondoka bila kusubiri kauli yangu. Ningejua ningemwambia yote akiwa hai! Leo amekufa, jonas amelala na sitamuona tena na ina maana yale niliyotaka kumwambia sitamwambia tena!. Inaniuma sana na itaniuma mpaka kesho.

Ajali mbaya ya gari iliyotokea baada ya tairi la gari lake kupata pancha na kuyumba na hatimaye kugonga msingi wa nyumba ndio iliyomuua Jonas. Alizikwa makaburi ya kinondoni na kumuacha mjane iloma akiwa na mzigo wa kumlea mtoto wao wa pekee kim.

Miaka imekatika kama maji katika mkondo wake. Kidonda alichoniachia Jonas hakiponi bali kinazidi kuleta maumivu ambayo hayasimuliki mdomoni wala hayaandikiki kitabuni. Nimekwisha jifungua mtoto wa kiume aitwaye Junior Jon. Mtoto huyu mzuri wa kiume ananiliza kila uchao.

Nimekonda kama uchelewa kwa mawazo na sononeko la moyo. Vikao vya familia vimeshakaa mara kadhaa kujadili suala la kumtambulisha baba wa mtoto lakini nimeendelea kukataa kumtaja kwa kisingizo kuwa yuko nje ya nchi.najua uongo haukidhi haja ya milele na ndio maana nahisi mzigo wa siri hii ukiwa mzito moyoni mwangu hasa ninapomtazama Junior.

“ sasa mwanangu vipi kuhusu huyu mkwe, maana mimba tumekusaidia kulea na mtoto amezaliwa na anakuwa lakini baba yake hatukijui hata kivuli chake” baba alinieleza usiku mmoja mara baada ya chakula

“ atakuja tu baba” nilimjibu nikitegemea angekubaliana nami
“atakuja …atakuja….lini? anaogopa nini kujitokeza hadharani ana uso wa nyani?”
“ hapana baba!”

“ sasa! Kinachomshinda kuja nini ama kinachomshinda kutuma hata mshenga nini?”
“ mpe nafasi ajiandae jamani. Kuja atakuja tu” nililalamika kiasi kwamba baba alishindwa hata la kuendelea kusema

“ sawa mama, sisi tutangoja lakini mwambie afanye hima maana Junior huyu anahitaji kulelewa na wazazi wote wawili!”
“ sawa baba” sikungoja swali, maoni wala hoja ya nyongeza. Nikajiondokea zangu na kwenda kulala
Natamani kuueleza ulimwengu ukweli lakini sijui nianzie wapi jamani. Iloma ambaye tumekuwa naye bega kwa bega tangu afiwe na mumewe sidhani kama atanielewa siku nikiiweka hadharani siri hii na sielewi ataniweka katika kundi la watu wa namna gani wanafiki ama mahayawani! ingawa sasa Iloma ameolewa tena na yupo kwa mumewe mpya Roho inanisuta, roho inaniuma mno kwa vile Junior sasa ananiuliza mama baba yangu yuko wapi!

Nashindwa niseme nini. Maneno ya Jonas yanazunguka kichwani pangu kila uchao. Namkumbuka mno hasa masaa machache kabla kifo chake alipofika ofisini kwangu, aliponipigia simu na kuisikia sauti yake kwa mara ya mwisho. Nakiri nilimpenda na hata sasa nampenda ingawa hayupo nami.

Nawauliza walimwengu! Nisaidieni kupata jibu! Niitunze siri hii mpaka lini? Mwanangu nitakuja kumjibu nini kuhusu baba yake? Je nikiiweka hadharani siri hii jamii itanichukulia vipi, Iloma atanifikiriaje mimi, wazazi wangu watanionaje nanyi walimwengu mtanihukumu vipi?
Ama siri hii ibaki kuwa siri yangu!!!?


Email: queenlauryn5@yahoo.com
Inbox me in facebook: laura Pettie

Wenye majibu mnisaidie, nakaribisha maoni, ushauri n.k, hadithi imeishia hapa, kaeni mkao wa kula na kitu kingine toka kwa yule yule mwandishi wako Laura Pettie!

1 comment:

  1. awwwwww nimejikuta nalia i thought ulikuwa umetunga kumbe ni story ya kweli hmmm let me add u on facebook

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger