36
Jenifa Agapella na Clarita Gabson marafiki wa tangu utoto
walikuwa nyumbani kwa Mzee Agapella wakipeana michapo mbalimbali huku wakiandaa
chakula chepesi cha kupata jioni ya siku hiyo. Clarita alikuwa na kikopo chake
cha ice cream, akiikwangua hiyo ice cream kwa kijiko na kuila taratibu kana
kwamba hakutaka iishe haraka, wakati huo akiwa amesimama kwa kuigemea friji
kubwa iliyokuwa jikoni hapo.
Jenifa alikuwa akiandaa mayai na mikate iliyokuwa juu ya meza
ya kupikia huku mara kadhaa akiiacha kazi yake na kumgeukia Clarita kupiga soga
kwanza.
‘Yaani sijawahi kujua hata anachompendea Pamella… hasikii
haoni Clari’ Jenifa alizungumza akirejea tena kukoroga mayai aliyoyavunjia
katika bakuli
‘That witch!.. nxa!... yaani simpendi Pamella jamani
angelijua hili hata kukaribiana na mimi asingethubutu… halafu ulimuona
alivyokuwa anamemganda Jerry kwenye Party…’
‘hana aibu yule… nilimchukia zaidi kipindi mama anaumwa…
Clarita!...hata kumshika mama mkono alikuwa anaona kinyaa’ Jenifa akageuka tena
soga zikipamba moto
‘usiniambie!’ Clarita akashangaa
‘I wish ungekuwepo…. anakuja na Jerry mpaka wodini kisha
anasimama mlangoni kule wakati mama yuko huku…’ akasema Jenifa akimuonyesha
umbali wa mlango na kitanda cha mama yake ulivyokuwa.
‘hata Salamu?..’ Clarita akauliza akiacha kujiegemeza na
kusimama wima, akimkodolea macho Jenifa
‘Nini salamu?... hata pole tu ya mbali walaa’ Jenifa
akaongezea chumvi sasa akijisahaulisha zile nyakati chache ambazo Pamella
alijitutumua kumkaribia mama yake na kumpa pole, achilia mbali kutoa pesa
kuwasaidia hapa na pale. Yote hayo alijisahaulisha kwa wakati ule.
‘Sasa na yote hayo…Jerry anampendea nini?’ Clarita akahoji
akipiga hatua kumfuata Jenifa pale alipokuwa amesimama. Wakawa mkabala na
kumpunguzia Jenifa kazi ya kugeuka
‘sijawahi kujua haki ya mama…sijui!.... wengine washirikina
tu… nasikia hata mama yake alitumiaga mzizi kumkamata yule Mzee… ndio maana
hafurukuti kila analosema yule mama yule Mzee anatii tu…’ Jenifa akaongea
kiushabiki sasa akisahau baba yake naye alikuwa ameshikiwa akili na mwanamke
mwingine wakati wakimuuguza mama yao.
Clarita akatikisa kichwa tu akiwa bado na mshangao usoni.
Wakati wakitaka kuzungumza zaidi wakasikia mlango ukifunguliwa na watu wawili
wakiingia na kuongea kwa sauti ya juu kidogo. Wakatega masikio wakitazamana!
‘Meddy siwezi ni ngumu kuliko unavyofikiria… na siwezi kumuoa
Pamella kama wanavyotaka wao wakati kuna mtu mwingine niliyemharibia muelekeo
wa maisha tayari’ Jerry alijitetea mbele ya Meddy akionekana wazi kuchanganywa
na kauli ya baba yake iliyomtaka ajiandae kumuoa Pamella.
‘Umeshazungumza na Pamella kuhusu hili suala?’ Meddy akauliza
taratibu akimhurumia rafiki yake
‘Lipi?’ Jerry naye akauliza asimuelewe Meddy
‘hili la kumuoa yeye…anajua kuwa wazazi wenu wana mipango
gani?’ Meddy akajieleza akiweka mikono yake kwenye mifuko ya suruali na
kumtazama Jerry kwa umakini.
‘Sijui…I just don’t know what is going on…. awe anajua au
hajui… sijali kuhusu hilo Meddy… akili yangu sasa inawaza cha kufanya juu ya
Sindi basi’ Jerry akajibu akishusha pumzi kwa mdomo na kutikisa kichwa chake
huku na kule.
Kule jikoni Jenifa na Clarita walitazamana kwa mara nyingine,
nyuso zao zikiwa na matuta kadhaa. Hawakuyaelewa yale mazungumzo. Wakajisogeza
karibu na mlango wa kutokea jikoni hapo kuelekea sebuleni walikokuwa akina
Jerry.
‘Okay may be… umatafute kwanza Pamella umwambie ukweli kuhusu
Sindi na hali yake… ama kusanya nguvu umwambie kweli Sindi kuhusu wewe… just
come out Jerry.. the truth will set you free…’ Meddy alitoa ushauri na Jerry
akamgeukia na kumtazama kana kwamba alichoongea kilikuwa ni kitu kipya kusikika
duniani.
‘What!...ni come out?...how?...naanzaje?... nianze tu kuwa
Sindi you know mimi ni hivi na hivi… just like that!... na utegemee atakuamini
tena maishani mwako… No!.. No Meddy…No!’ Jerry akaweweseka akionekana kuzidi
kuchanganyikiwa maradufu. Meddy akamhurumia zaidi, alihisi ni kwa kiasi gani
hali ilikuwa tata kwa rafiki yake.
Jerry akakurupuka na kupandisha ngazi haraka akifuata hicho
alichokuja kukifuata. Dakika mbili baadaye waliondoka pale na kuelekea kwa
Meddy huku nyuma Jenifa na Clarita wakibaki wameachama midomo!
‘Sindi?...Sindi ni nani tena?’ Clarita akauliza yeye ndio
akionekana kuguswa mno nay ale mazungumzo. Jenifa alikuwa bado amekunja uso
kama mtu aliyekuwa anajikumbusha kitu kichwani kisha ghafla uso ukamchanuka na
akajikuta akiachama tena mdomo na kutanua macho hali akimtazama Clarita.
‘Whaat!’ Clarita akahoji kwa shauku naye akimtazama Jenifa
kwa msisitizo
‘Aaaww!...hili jina nilishalisikia tena kwenye mazungumzo ya
Jerry na Pamella… it was like Pamella alikuwa anamlalamikia Jerry kuhusu huyo
Sindi’ Jenifa akategua kitendawili na asijue alimchanganya Clarita kiasi gani
‘But who is she?...huyo Sindi ni nani?’ Clarita akauliza kwa
jazba kidogo na Jenifa akabetua bega lake la kulia kujibu lile swali kuwa
hakumjua huyo Sindi. Uso wa Clarita ukajaa huzuni ghafla. Mapambano ya
kumgombea Jerry hayakuwa yake na Pamella tu, kulikuwa na mwanamke zaidi ambaye
alionekana kuwa na nguvu kuliko wao wawili. Alihisi mkuki moyoni kiasi cha
kutolipa uzito suala la Pamella kuolewa na Jerry!
8888888888888888888888888888
‘ Mom I’ll be okay!...usijali… nilishaahidi mwezi huu ukiisha
narudi nyumbani’ Pamella aliongea na mama yake wakati akimsindikiza mlangoni.
‘Baba yako anaongea hili kila siku…. please honey na iwe kama
ulivyoahidi…you don’t want to break your dad’s heart….right?’ Rebecca, Mama
Pamella aliongea na binti yake pale mlangoni hali akimtazama kwa upendo
bintiye.
Pamella akatabasamu na kumkumbatia mama yake. kisha
wakafungua mlango na mama aktoka nje akipunga mkono. Pamella akasimama pale
mlangoni mpaka mama yake alipotoa gari lake nje ya geti na mlinzi kufunga geti.
Pamella akarudi ndani kwake na kusimama pale sebuleni akiitazama sebule yake
asijue aanzie wapi.
Akayatazama majarida
yaliyokuwa yametapakaa kwenye kochi, akavitazama vinywaji vilivyokuwa juu ya
meza, akazitazama nguo zilizokuwa kwenye kochi lingine zikingoja kukunjwa,
akashusha pumzi na kutikisa kichwa, akionekana kuchoka na kutotamani kugusa
chochote kwa wakati ule.
Akajishika kiuno kwanza, akizitazama zile nguo kwenye kochi,
akafanya maamuzi!
Akaenda ndani na kurudi na tenga dogo la plastiki la kuwekea
nguo, akazikusanya na kuzitumbukiza katika tenga kisha akalifunika.
Alipolinyanyua na kutaka kuelekea nalo ndani. Akasikia mlio wa hodi. Uso wake
ukakimbilia kwenye saa iliyokuwa ukutani na kuguna!
Alilitua tenga chini na kuufuata mlango. Akaufungua na
Patrick Mazimbwe akaingia ndani.
‘wow! hujagongana na mama hapo kwenye kona?’ Pamella
akamuuliza akifunga mlango na kumgeukia mpenzi wake
‘Nimemuona anapiga kona pale kwenye baa kuingia barabara
kubwa’ Patrick akajibu akilegeza tai yake na kujitupa kwenye lile kochi
lililokuwa na nguo.
‘na ungemkuta hapa ingekuwaje?’ Pamella akauliza akilifuata
lile tenga na kuliinua tena, akalipachika kiunoni upande wa kushoto
‘Si ndio angenifahamu sasa au?....’ Patrick akajibu
akitabasamu na Pamella akamtazama tu bila hata kuliunga mkono lile tabasamu
akageuka na kuyanza kuelekea ndani kisha kama mtu aliyekumbuka kitu akamgeukia
Patrick
‘you can’t be serious!’akatamka akiwa na uso ulionuna na
kuishia ndani akimuacha Patrick anatabasamu peke yake na kunyanyuka kulifuata
lile kochi lililokuwa na magazeti. Akayasogeza na kuanza kuyapitia juu juu
Pamella akarejea na kuketi kando ya Patrick ambaye
aliyakusanya magazeti yake aliyoyarudika mapajani na kuyabwaga kwenye meza
iliyokuwa mbele yake kando ya vinywaji.
‘Sijakuona tangu juzi…’ Patrick akaanza kuzungumza mkono wake
wa kulia ukiligusa paja la Pamella lililokuwa wazi kutokana na kuvalia
kikaptura kifupi
‘Mama anakaba sana siku hizi…she wants to be kila nilipo
yaani natamani likizo iishe haraka nirejee kazini…’ Pamella akajibu mkono wake
wa kuume ukikuna kichwa chake na kutibua tibua nywele zake
‘Lazima atamani kuwa nawe muda mwingi..wewe ni binti pakee na
zaidi amekuwa mbali nawe miaka sasa…mingapi sijui?’ Patrick akauliza
‘Sita…au saba’ akajibu Pamella akitabasamu
‘Hivi kwanini lakini?...’ Patrick akachimba
‘ni long story Babe….tuyaache hayo…tuongelee yetu sasa… mi
nataka kukutana na Dennis kaka yako’ Pamella akapeleka ombi lililotua kama
konzi kichwani mwa Patrick
‘Why?’ akajikuta akiuliza haraka uso pia ukibadilika
‘Why?... Patrick!....mimi kufahamiana na kaka yako mkubwa ni
dhambi kiasi cha kuuliza kwanini?’ Pamella akahoji akionyesha kutofurahia namna
ombi lake lilivopokelewa
‘No..i mean…namaanisha pengine una kitu cha kuongea naye…he
is a lawyer bwana… may be una shida binafsi’ Patrick akajitetea haraka licha ya
moyo wake na akili yake kujua wazi ni nini Pamella alimaanisha
‘No!,,,sio mambo ya kikazi… nataka nimjue tu nay eye ajue
mimi na wewe tu wapenzi…that is all babe…tunahitaji kupiga hatua moja ya
uhusiano wetu….mimi mama anajua kila kitu kuhusu sisi…it is time na kwako mmoja
ajue kinachoendelea….la bda uniambie huna future na mimi’ Pamella akaongea
taratibu akimtazama Patrick usoni na ule uzuri wake ukizidi kung’aa lakini pia
ukishindwa kuutuliza moyo wa Patrick ambaye ombi hili lilikuwa gumu kupitiliza.
Alishamtambulisha Clarita kwa Dennis, angeanza vipi kumtambulisha Pamella pia.
Dennis alikuwa kaka yake mkubwa, aliyemlea kama mwanaye baada
ya wazazi wao kufariki kwa ajali wakati Patrick alipokuwa na miaka miwili.
alikuwa mtoto wa mwisho aliyezaliwa uzeeni uko ambaye hakutarajiwa kabisa.
Dennis ndiye aliyebeba jukumu la kumtunza wakati huo akiwa ndio ameanza
kujitegemea.
Dada yao aliyemfuatia Dennis aliolewa na bahati mbaya
alifariki wakati akijifungua hivyo Katika kukua kwake Dennis alikuwa kama baba
yake na kaka yake. Asingeweza kumfanyia upuuzi wa kumletea wanawake tofauti
tofauti. hivyo ombi la Pamella lilikuwa kitanzi shingoni!
Pamella akamtazama Patrick alivyokuwa amezubaa na ghafla tu
Pamella akasimama na kumwambia alikuwa jikoni kwa ajili ya kuandaa chakula chao
cha usiku. Patrick akabaki peke yake. Akionekana kukosa raha na kutopea katika
mawazo! Mchezo aliokuwa anaufanya ulianza kumchezea mwenyewe bila kujua Pamella
Okello ni mtoto halali wa Dennis kaka yake!
88888888888888888888888888888
Usiku huu pia haukuwa mzuri wa Sindi Nalela. Pale kitandani
alipoketi alijikunyata na kuukumbatia mto kwa juhudi zote. Akiitafuta faraja na
asiione. Moyo ulimuuma mno. alijizuia kutolia lakini maumivu na majuto
yaliyokuwa yakimtembelea yalimsukuma kumeza mate kwa juhudi zote na kuyazuia
machozi.
akatoka kitandani na kulifuata sanduku lake, akalifungua na
kulichambua upoande mmoja kisha akatoa kibahasha ambacho alikimimina kitandani
na noti kadhaa zikadondokea kitandani. alihesabu zile pesa na kuridhika
zilikuwa sawa na zilimtosha kuondoka pale kurejea kwao. Akazirudisha mahala
pake na kuketi kitandani pale kama bwege!
Dakika moja tu ilimkumbusha Mungu alipo, akaifuata biblia
yake na kupiga magoti ukingoni mwa kitanda kisha akaiweka biblia mbele yake
kifua chake, mikono yake ikikutana na kufumbatana mbele ya uso wake huku viwiko
vya mikono vikiwa vimegota kitandani. Akasali!
‘Mungu wangu….nimekosa…nimekosa mimi…
Mungu…nitazame…nakuhitaji wakati huu…nakuhitaji Jehova…nimepotea… nimepotea
Yesu… nishike mkono..nionyeshe nini nifanye…nionyeshe mwanga wa amani ulipo…’
akasita kidogo na machozi yakamteremka wakati kwikwi za kilio zikimkaba kwa
muda, akapumua na kujitahidi kuendelea
‘Nimetenda dhambi kubwa… nimekukosea Mungu wangu…lakini
nakuja mbele zako… eeh Mungu wangu…’ akshindwa kuendelea kusali na akajikuta
akiketi kitako chini na kulia kwa kuomboleza. Akalia kwa uchungu sana. Alikuwa
ametoroka nyumbani kukimbia ndoa, alikuwa amemuacha mwanaume aliyempenda
Nyanza, na sasa alikuwa mjamzito pasipo ndoa wala muelekeo. Alikuwa
amejivurugia maisha ndani ya muda mfupi tu bila kutarajia. Hakukuwa na cha
maana alichofanya!
Alilia zaidi, alipokumbuka usia wa mama yake, alipokumbuka
kauli za baba yake, alipokumbuka aibu aliyoitia familia yake na sasa alikuwa
anarudi kuwaongezea aibu ya kuwa na mimba ya mtu asiyemjua vizuri. Aliumia,
aliumia sana sana sana. Alitamani kuamka toka katika ile ndoto na kujikuta
kijijini kwao akiisha maisha aliyokuwa naishi, akijiiba kukutana na Nyanza wake
na kurejea kwao. Pengine angeolewa tu na hatimaye angeachika na kumrudia Nyanza
lakini sio hivi alivyofanya!
Sindi alilia mno lakini maji yalishamwagika!
8888888888888888888888888888888
Kulipokucha, Asubuhi ya siku iliyofuata Dennis Mazimbwe
alikuwa ofisini kwake. asubuhi hii haikuwa njema kwake hata kidogo hasa baada
ya kupata ugeni huu uliokuwa mbele yake.
‘You know what Fiona!... get out of my office Now!’ Dennis
aliongea kwa msisistizo sentensi ya mwisho akitamka neno moja moja kama mwalimu
anayesoma imla kisha neno la mwisho akalipaza na kulipayuka kwa ghadhabu wakati
Fiona akitabasamu pale alipokuwa ameketi.
‘Dennis!...’ Fiona akamuita akitabasamu huku akinyanyuka
‘shida yangu n indigo sana..sana sana….kuona WILL ya
Agapella…just to know who is written there…and I’m done na milioni 15 ni zako
ndani ya wiki hii…ugumu uko wapi hapo?’ Fiona akauliza akiwa tayari amemfikia
Dennis pale alipokuwa amesimama kando ya kiti chake cha kazi. Walisimama
mkabala na Fiona akaminua kichwa na kumtazama Dennis usoni huku akimung’unya
midomo yake na kumrembulia macho Dennis.
‘Nimesema hapana!.... tafadhali Ms. Agapella naomba uondoke….
ninaiheshimu taaluma yangu kuliko unavyofikiria….please show yourself out’
Dennis akapangua mikono ya Fiona na wakati akiishika ili kuiondoa mlango
ukafunguliwa na Rebecca akaingia ghafla na kuganda mlangoni akiwashangaa namna
walivyokuwa wamekaribiana na vile Dennis alivyokuwa ameishika mikono ya Fiona.
Dennis akaiachia mikono ya Fiona ghafla na Fiona akatabasamu
akijinyanyua kidogo na kumbusu Dennis shavuni. kisha kwa mwendo wa maringo
akaifuata pochi yake na kuelekea mlangoni alikokuwa amesimama Rebecca, mke wa
Mzee okello.
‘He is all yours now’
akamtamkia Rebecca kwa sauti ya chini lakini iliyomfikia vyema na kutoka
zake akitabasamu.
‘Dennis! how could you?’ Rebecca akapayuka akiwa amehamanika
mno na Dennis akajikuta akitoka mbio kumuwahi Rebecca ambaye alikuwa anageuka
ili aondoke. Denis akamkimbilia na kumkamatia kordoni.
‘Niachie!...Dennis!...Dennis!’ Rebecca alikuwa analia sasa
akiipangua mikono ya Dennis iliyokuwa imekazana kumzuia asiondoke. Dennis
akamshinda nguvu na kumbana ukutani huku akiomba amsikilize.
‘Sitaki…sitaki….niachie’ Rebecca akafurukuta na kufanikiwa
kujitoa mikononi mwa Dennis kisha akatoka mbio na kuishia zake nje. Pasipo
kujua pale kwenye parking Fiona alikuwa kwenye gari akimtazama alivyotoka kwa
kuchanganyikiwa na kuanza kulia kwenye gari. Hata alipopita na gari lake mbele
yake hakuliona gari la Fiona. Mwanamke huyu akacheka kicheko kirefu cha ushindi
huku akitikisa kichwa. Alichotaka kujua sasa kilikuwa wazi mbele yake!
Kule ndani Dennis alikuwa na hali mbaya mno, alikazana kupiga
simu ya Rebecca ambayo iliita pasipo kupokelewa na mwisho ilisikika ikimtaarifa
namba hiyo ilikuwa haipatikani.
‘Shit!’ akaibamiza simu yake chini huku akihema kwa ghadhabu
kwelikweli.
8888888888888888888888
Fiona Agapella baada ya kuvuruga ofisini kwa Dennis
akanyoosha njia mpaka hospitali alikokuwa amelazwa mumewe. Aliegesha gari lake na kutoka kwa mwendo wa madaha na
furaha. Akapita mapokezi na kupandisha ngazi kuelekea wodini. Alipoufungua
mlango na kuingia Jerry aliyekuwa ameketi kwenye kiti akijisomea gazeti
alinyanyuka haraka huku akimtazama baba yake kama alimuona Fiona.
Alimuwahi na kumkamata mkono akimvutia nje haraka sana.
Wakasukumana mpaka nje na kusimama nje ya wodi
‘Nini?....unanizuia kumuona mume wangu?’ Fiona aling’aka
‘Mumeo?....una uhakika Mzee Agapella ni mumeo?....’ Jerry
naye alimjia juu
‘Oh! Son naona unakuwa kwa kasi kubwa sana mpaka unasahau
nani ni nani katika familia’ Fiona akaongea kwa kebehi lakini akijitahidi
kutabasamu
‘familia?....hivi nawe unajihesabu katika familia ya
Agapella?.... kwa kitu gani?...kwa lipi?...’ Jerry naye alirudisha kebehi
akitabasamu. Kwa mtu aliyembali angehisi walikuwa na mazungumzo mazuri ya
kufarijiana!
‘Jerry! siko hapa kugombana na mtu…nahitaji kumuona mume
wangu’ Fiona akataka kumpita Jerry lakini akazuiliwa
‘Hataki kukuona!....that is all’ Jerry akamjibu akigeuka
kumtazama daktari aliyekuwa nakuja upande wao. daktari alipowafikia akawasabahi
kwa awamu na kumuuliza Jerry hali yam zee.
‘hajaamka bado…’ Jerry akajibu na yule daktari akamgeukia
Fiona
‘Mama itabidi uongozane na mimi ofisini…tunahitaji
kuzungumza’ yule daktari akatamka taratibu mbele ya Fiona ambaye uso wake
ulishaa hasira
‘hata hapa liseme tu’ akajibu akimtupia macho Jerry na Jerry
akaitikia akimaanisha kutoa ile ruhusa
‘Mr. Agapella ameomba usimuone mpaka atakapotoka hospitali…
na sisi tunaheshimu matakwa ya wagonjwa wetu endapo tu yanaonekana kuwa ya
msingi… hatutahitaji kutumia nguvu kukuondoa eneo hili… kuwa muungwana tu na
ujaribu kukaa mbali na Mr. Agapella kwa kipindi hiki’ Dokta aliongea kwa hatua,
uso ukionyesha hali zote za kujiamini na kusisitiza anachoongea.
‘Nini?... siwaelewi’ akang’aka
‘Ndio taratibu zetu…just make sure hujivunjii heshima kwa
kuondolewa na walinzi wetu…sidhani kama italeta picha nzuri kwa familia ya
Agapella…. asante!’ dokta akainama kidogo na kuingia chumba alichokuwa amelazwa
Mzee agapella, akiwaacha mtu na mama yake wa kambo wakitazamana.
‘…. Ulidhani nikirudi nitakukimbia maisha?... I’m back to
protect my family!’ Jerry alimuinamia Fiona na kumpasulia kipande cha ukweli
ambao ulimfanya Fiona atunduwae. Baridi ikimtembelea mpaka kwenye mifupa.
Akimtazama Jerry vile alivyokuwa anaishia kordoni nay eye kubaki akiwa
ameachama mdomo wake kwa bumbuwazi. hakutarajia kusikia kauli ile toka kwa
Jerry. moyo ulimuenda kasi zaidi alipowaza pengine Jerry aikuwa anajua kila
kitu kuhusu kutekwa kwake. Alichachatika!
888888888888888888888888
Saa tatu usiku Jerry aliingia kwa Sindi Nalela na kumkuta
amelala kwa kujikunyata kitandani. Aliingia na mbwembwe za hapa na pale lakini
Sindi alikuwa amepooza mno. Ule ukali na kiburi cha hapa na pale havikuwepo
siku hii na Jerry alionekana wazi kuvimiss ghafla.
Alimuandalia chakuka akiwa kimya na mwenye uso uliosawajika
kiasi cha kumtisha Jerry mwenyewe. Baada ya kula. Jerry alipelekewa maji ya
kuoga bafuni na alipotoka tu. Sindi aliivamia suruali ya Jerry na kuitafuta
wallet. akaipata na kuifuangua kwa pupa. Noti kadhaa za elfu kumi zilizofikia
laki mbili na kitu zikamtunduwaza Sindi. Huku akitetemeka akakichomoa
kitambulisho cha kura cha Jerry na kukilaza usawa wa macho yake
‘Jerry Kristus Agapella’ alilisoma lile jina akitetemeka
vibaya mno kisha taratibu akakirudisha na mwili ukihisi kuishiwa nguvu pia.
Akajitutumua kurejesha kila kitu sehemu yake na sasa alitamani kupiga mayowe
kwa nguvu zote. Alikuwa amedanganywa, alikuwa ameingizwa mjini. Jerry John
hakuwa Jerry John, alikuwa Jerry Kristus Agapella. Maneno ya akina Jamilla sasa
yalimuingia kuliko mwanzo na akayaamini kupita imani yenyewe ilivyo.
Wakati akiwa na lile hamaniko lililomkaba vyema, Jerry akaingia
pale chumbani na kujifuta maji. kisha akavaa bukta yake na kumfuata Sindi pale
alipokuwa ameketi. alimtazama kwa mshangao namna alivyokuwa anatetemeka pasipo
kuongea wala kupepesa macho.
‘Sindi!...una nini leo?...nini mama?’ akamuuliza kwa upole na
Sindi akasimama ghafla na kuanza kurudi kinyume nyume akimtolea macho Jerry na
machozi yakimporomoka.
‘Jerry wewe ni nani?’ akauliza kwa sauti iliyofifishwa na
kilio kilichokuwa kimekaba, midomo ikimtetemeka na machozi yakiteremka kwa kasi
‘Mimi ni nani?....una maana gani Sindi’ Moyo wa Jerry uliruka
almanusura uchomoke kifuani.
‘Wewe ni naniiii?.... wewe sio Jerry John….wewe ni
nani?....unataka nini kwangu?’ Sindi alikuwa ameshaufikia mlango na kusimama
hapo akilia kiasi cha kujiinamia.
Jerry alipooza ghafla, nguvu zilimuishia haraka sana na
maneno yakampotea kichwani. Akili ilikimbilia kusikojulikana. Swali la Sindi
lilikuwa kama shambulizi la kushtukiza, na kule kubabaika kukamfanya Sindi
ajumlishe na kutoa, akagawanya na alipozidisha dio akapata jibu kuwa Jerry
alikuwa mpelelezi kweli kama alivyoambiwa na akina Jamila.
Jerry alipogutuka na kutaka kuanza kumfuata Sindi, Sindi
alikurupuka na kufungua mlango akikimbilia chumbani kwa Jamilla. Jerry akahisi
mambo yameharibika. Akataka kumfuata Sindi na kumweleza ukweli wote bila kuacha
neno lakini pia akili yake ilikuwa imevurugika mno na Sindi alikuwa amehamanika
mno. Wasingesikilizana wala kuelewana.
Akaitafuta simu haraka sana na kumpigia Meddy, akishindwa
kujieleza kiufasaha japo Meddy alimuelewa.
‘Usimtafute usiku huu utamfanya azidi kuchanganyikiwa….
hatakuelewa kabisa….jaribu kulala kesho asubuhi tafuta nyumba sehemu nyingine
haraka sana…unanielewa?.... tafuta nyumba umhamishe hapo kwanza…kisha ndio sasa
nitakuja tuongee naye na tumuweke sawa…muda huu hataweza kukuelewa’ Meddy
alitoa ushauri wake naye moyo ukimuenda mbio kana kwamba sakata lile lilikuwa
limemkuta yeye.
Jerry akakubali kwa shingo upande. usiku ule ulikuwa usiku
mrefu mno kwa Jerry. hakulala kabisa na asubuhi alitoa elfu hamsini na kuziacha
kitandani akiacha ujumbe kuwa zilikuwa pesa za matumizi na angerejea baadaye
kidogo na kuzungumza naye.
Aliporejea saa sita mchana akiwa na gari la kuhamisha vitu
Jerry hakumkuta Sindi Nalela wala nguo zake. Alipomfuata Jamilla naye akashtuka
kujua Sindi alikuwa ameondoka bila kumuaga hata yeye rafiki yake. Jerry
akachanganyikiwa vibaya mno. akaingia chumbani na kupekua kama mwehu kuangalia
vitu vya Sindi na asione hata kimoja. Sindi alikuwa ameondoka zake na nguo zake
na vitu vyake tu na kuacha kila kitu alichopewa na Jerry.
Juu ya mto wa kulalia Jerry aliona karatasi iliyokunjwa
vizuri ikiwa imelazwa hapo. akaifuata na kuifungua, akishuhudia zile elfu
hamsini zikidondoka chini na wala sijali kuziokota
‘Jerry Kristus Agapella… nimeondoka! tafadhali usinitafute
kwa vile sirudi nyumbani… hii mimba ni zawadi ya ujinga wangu nitaamua kuitoa
au kuitunza. Nashukuru kwa kuniharibia maisha, nashukuru kwa kunihadaa,
nashukuru kwa yote Jerry, Mungu akubariki.
panapo majaaliwa kila kheri.
Sindi Nalela
Yalikuwa maandishi machache, yaliyoandikwa kwa mlalo wa
kuvutia, mwandiko wa kike, mwandiko wa mwanamke aliyempenda sana. Jerry
aliiachia ile barua ipeperushwe na upepo uliokuwa ukivuma toka dirishani wakati
yeye akiwa amesimama kama nguzo akiwa bado haamini alichosoma!
Katika wakati huu, katika kipindi hiki, katika siku hii,
Jerry alikitamani kifo ghafla!... upweke ulimvaa na maisha yalikosa thamani
ndani ya sekunde chache tu alizojua asingemuona tena Sindi.
…… NIPE MAONI YAKO….
No comments:
Post a Comment