Friday, September 6, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (37)

37

Wale vijana aliokuja nao kusomba vyombo ndio waliomtoa katika lindi la simanzi. Akajikuta tu akiwalipa pesa walizokubaliana pasipo kuhamisha hata kijiko. Wakaondoka wakimuacha na wapangaji wawili watatu waliokuwepo muda huo. Kila mmoja akisema lake lakini hakuna kati yao aliyemuona Sindi wakati akiondoka!


Jerry alihisi kama yu ndotoni, Ni usiku uliopita tu alikuwa na Sindi, alikula chakula chake, akaoga maji yake na akaisikia sauti yake. Muda ule aliokuwa ameketi pale hakukuwa na chochote cha Sindi achilia mbali lile tegemeo kuwa angelirejea pale. Aliumia kupitiliza! Alichokifanya Sindi kilikuwa zaidi ya adhabu.

Nusu saa baadaye Jerry Agapella alijikusanya na kuita taksi, Aliingia na kutoka mule ndani mwake na asijue alilotaka kufanya kwa wakati ule. Akatoka mpaka nje na kuuliza uliza kwa baadhi ya watu waliokuwa na biashara zao maeneo yake. Hakuna hata mmoja aliyekiri kumuona Sindi asubuhi ya siku ile.

Pengine angepata hata uelekeo wa alikoelekea, ama pengine angepata hata muda alioonekana akiondoka, labda angejua pa kuanzia. Hakuambulia taarifa yoyote ya maana. Taksi ilipokuja akapanda nyuma na kukilaza kichwa chake kwenye kiti, kiitazama sehemu ya juu ya gari kana kwamba ingempatia majibu ya sakata lililomkuta!

Mpaka saa moja kabla ya kufika pale alishajipanga kwa mengi, nyumba yake aliyokuwa anaishi ndio nyumba aliyotaka Sindi akaishi, sio kuishi tu alitaka kubadilisha hati ya umiliki iwe na jina la Sindi. Alitaka amueleze ukweli kuhusu Pamella lakini pia ukweli kuwa alikuwa anampenda na angemuoa yeye na si Pamella. Alishapanga kumrudisha Sindi shule kama si chuoni. Yote hayo aliyapanga usiku uliopita, akayapanga asubuhi ya siku hiyo na asijue mwenzake alikuwa na mipango yake pia.

Wakati ile taksi ikiacha barabara ya mtaa na kuingia barabara ya lami ilipita kituo cha daladala kilichokuwa cha kwanza baada ya kona ya kuingilia barabarani. Taksi ile ilipita taratibu kutokana na msongamano wa daladala zilizokuwa zikiingia kituoni hapo na kutoka.

Dirisha la kiti cha nyuma alichoketi Jerry lilikuwa wazi kabisa na hivyo, Sindi aliyekuwa ameketi kituoni hapo akiyatazama magari yaliyokuwa yakipita hapo alimuona vema Jerry Agapella ambaye akili yake kwa wakati ule ilikuwa maili nyingi toka pale alipokuwa. Aliitazama ile taksi kwa jicho la huzuni  mpaka ilipofika mbali na upeo wa macho yake, akainamisha uso wake chini akisikilizia maumivu ya moyo.

sauti mbili zilipiganandani ya kichwa chake. Moja ilimtaka aikimbilie ile taksi na kumsikiliza Jerry lakini sauti nyingine ilimsihi kuendelea na maamuzi yake na kumkimbia mtu aliyemuona wa hatari kwa maisha yake. Alitulia vile akiitazama ardhi kwa jicho pembe na asiitambue akilini. Ule ushungi aliokuwa amejitanda kwa wakati ule ulikuwa mzito kuliko gunia la kilo mia. Alitaka sana kurudi nyumbani kwao lakini pia hakujua mapokezi yake yangekuwaje, aliogopa mno kumkaribia baba yake tena akiwa na ujauzito wa mtu asiyemfahamu.

Alipowaza kuutoa ule ujauzito, akili ilimkumbusha bajeti aliyokuwa nayo mkononi, akakumbuka pia kuwa alishajiondoa mikononi mwa Jerry, ni wapi angejiuguzia?. tangu alipotoka nyumbani kwa Jerry alikuwa ameketi pale kituoni kwa masaa matatu, akiwaza na kuwazua, akitafakari cha kufanya na asikione mbaya zaidi mwili ulihisi uchovu na maumivu ya hapa na pale huku njaa nayo ikianza kumkung’uta.

Akagutuka ghafla na kuangaza huku na kule, siku ilishafikia katikati na hakuwa amefanya uamuzi wa maana. Haraka akaamua kutafuta chumba cha wageni maeneo ya ubungo ili alale hapo na kisha asubuhi tayari angekuwa na uamuzi wa mwisho. Akainama kidogo na kuokota sanduku lake la nguo. Akavuka barabara kuzifuata taksi zilizokuwa upande wa pili akiamini zingemfikisha salama alipotaka.

Alipojiinua na kuanza kupiga hatua kuikaribia barabara, alisikia watu wakimpigia kelele ambazo hakuzielewa kwanza mpaka pale alipogeuza kichwa upande wa kulia na kushuhudia gari dogo likiimkaribia na kumchota. Hakukumbuka kilichoendelea!
88888888888888888888888888

Jenifa na Fiona waliongozana kutoka jikoni, Jenifa akiwa na bakuli lililojaa popcorns huku Fiona akiwa na glasi mbili pamoja na chupa kubwa ya soda. Walikuwa katika maongezi waliyotoka nayo huko jikoni. Jenifa alitua lile bakuli juu ya meza ndogo pale sebuleni na kuivutia karibu na sofa. Akaketi na kuikamata rimoti ya luninga akipunguza sauti ya muziki uliokuwa ukisikika toka katika lininga.

Fiona alizitua zile glasi kando ya Bakuli na kuanza kazi ya kuifungua ile chupa
‘Pamella?’ aliuliza akikazana kuzunguza mfuniko wa chupa ya soda kubwa aina ya cocacola
‘Yeah…nimewasikia kabisa…I was like what?... Pamella na tabia zake zile akiingia humu si atatupelekesha mno’ Jenifa aliongea akidokoa popcorns kidogo na kuanza kuzitafuna wakati akimtazama mama yake wa kambo akimimina soda kwenye zile glasi

‘Ina maana kuna vitu vinaendelea na sisis hatujui kitu kabisa!’ Fiona alishangaa
‘Ndio hivyo…baba na Jerry wanafanya yao kimya kimya…nashangaa hawataki kutushirikisha…’ Jenifa alilalamika akichukua glasi na kupiga mafunda kadhaa huku mama yake akizoa fungu la popcorns na kuzibugia kwa mkupuo. Akatafuna kwanza na kuzipunguza mdomoni kisha kama mtu aliyesubiri kwa hamu kuzimeza na kuongea, akalalamika

‘Jana nimeenda hospitali mwenzangu…. si Jerry akanikatalia kumuona baba yako?... yaani sikuamini kabisa…na daktari naye akamuunga mkono yaani nilifukuzwa kama gaidi wakati Kristus ni mume wangu’ akalalamika akitafuna mabaki ya popcorns na kusukumia na soda

‘Kwanini?... alikuzuia kwa misingi ipi sasa?’jenifa akauliza naye akiketi vizuri
‘Ndio nilichouliza na jibu sikupewa…. this is not fair Jenifa… nimewapokea kama wanangu… mmeishi hapa bila manyanyaso yoyote kwanini kaka yako ananijengea chuki kwa baba yako?’ Fiona alionyesha uso wa huzuni iliyojaa unafiki ndani yake

‘Mmmh!... Jerry akuzuie kumuona baba?...ili iweje kwanza?’ Jenifa bado alikuwa na mashaka
‘Ndio mimi nimejiuliza sana…yaani jana Mungu tu anajua nilivyoondolewa kwa aibu pale wodini…’ Fiona aliongeza chumvi
‘Ngoja jioni leo nitamfuata kwake…nitaongea…labda kuna kitu mama… ila kwa sasa hebu usimuwazie Jerry…. tangu arudi naona muda mwingi hayuko sawa… just mvumilie tu’ alirai Jenifa akitabasamu kumfariji mama yake wa kambo. Simu iliyokuwa juu ya meza sehemu ya kulia chakula ikaita. Ilikuwa simu ya Jenifa na akalazimika kusimama na kwenda kuipokea. na kutokomea zake ghorofani huku akiongea na simu.

Fiona Agapella akachungulia kama Jenifa alishapotelea kule juu, kisha taratibu akatabasamu kifedhuli na kuchukua simu yake iliyokuwa kwenye sifa la pili pale sebuleni. Akabonyeza namba na kuzipiga huku akisubiria simu yake ipokelewe kwa tabasamu. Sekunde mbili tatu simu ile ikapokelewa na Fiona akatazama tena kule ghorofani kuhakikisha hakukuwa na mtu.

‘… fanya unalojua just make sure Agapella hatoki hapo uko hospitali akiwa hai that is all… ndio nimetoa amri… inaonekana ameshajua kitu kwanini anizuie nisimuone… akuanzaye mmalize tu before it is too late…. nimeshasema fanya uwezalo asikanyage hapa ndani akiwa hai…. pesa zipo usijali…’akakata simu ile na kucheka taratibu, kicheko kile kikipandisha sauti mpaka kuwa kicheko kikubwa cha furaha. Alianza kuhisi ushindi ukirejea mikononi mwake.
888888888888888888888888888888

Meddy alikuwa na hekaheka kubwa nyumbani kwa Jerry. Alikuwa akijaribu kuongea hili na lile jioni hii ya saa moja akijaribu kumuweka sawa rafiki yake. Pombe zilizokuwa mbele ya Jerry zilimtisha na kwa kiasi Fulani  aliona zilikaribia kumtia wehu rafiki yake. aliongea kwa hisia, akimsihi, akimbembeleza na kumpa moyo Jerry japo hata yeye mwenyewe alihisi aliyoyaongea hayakuwa na maana yoyote kwa Jerry hasa kwa wakati kama ule.

‘Kunywa hakutabadili ukweli kuwa Sindi amekimbia…cha msingi na kutulia tujue nini cha kufanya Jerry… hebu ona… ona ulivyo devastated best… be a man na uliface hili jambo kiume…’ Meddy aliongea akikusanya chupa za pombe ziliozkuwa mbele ya Jerry na kuzihamishia mbali na pale. Jerry alikuwa ameketi kwa kujiinamia akiwa amepakata kichwa chake mikononi mwake.

‘najua unampenda Sindi…najua alichofanya kimekuumiza na siwezi kukisia hata robo ya hali unayojisikia…but come on Jerry…you are a man!’ Meddy aliongea akiwa sasa amejishika kiuno mbele ya Jerry ambaye aliinua uso wake uliojaa machozi na kumtazama Meddy kama mtoto aliyehitaji uwepo wa mama yake kwa muda ule.
Machozi yalikuwa yakimtiririka na ni dhahiri hakuweza kuyazuia pamoja na kujikaza kiume. koo lake lilididimia ndani kwa nguvu kila alipojizuia kulia hali magego yake yakisigana kupambana na kwikwi alizotaka zibakie ndani kwa ndani. Alilia kiume!

Meddy akahisi naye uchungu ukimtembelea! alitaka kumsaidia rafiki yake lakini hakujua aanzie wapi na afanye nini.
‘just like that?.... Sindi ameondoka?... sijui yuko wapi… sijui ana hali gani… sijui anafanya nini..sijui amekula..sijui amelala wapi….Meddy sijui Sindi yu salama au lah… what should I do now… ana kiumbe changu tumboni Meddy… she is innocent… oh lord!’ Alishindwa kuongea na akajiinamia tena, safari hii Meddy akishuhudia mabega ya rafiki yake yakichezacheza na akajua Jerry alikuwa analia. Akashusha pumzi kwa nguvu na kupitisha kidole cha shahada na kidole gumba machoni pake na kuvikutanisha puani.

Ukimya ukapita kati yao mpaka pale Jerry alivuta kamasi nyepesi na kuinua uso wake, akijaribu kutulia na kujikaza. Meddy akatembea mpaka pale alipoketi Jerry na kuketi kando yake. Maneno ya faraja yalishamuishia, alimkodolea macho rafiki yake na asipate neno hata moja la kumfariji. Walipotazamana wakajitahidi kutabasamu…

‘Jerry!’ akamuita kwa upole akimgusa begani
‘Pole..’ Meddy akampa ple rafiki yake akiwa bado amemgusa begani na Jery akatabasamu tena katikati ya ile huzuni
‘it is gonna be okay… you remember that time nilipoachwa na yule mmasai?...’ alimkumbusha Jerry tukio moja la nyuma lililomgusa yeye na Jerry akatabasamu kiasi cha kuonyesha meno huku akitikisa kichwa na kufuta machozi

‘Uliniambia if she was meant to be with me…she will come back….but time is the best healer… with time everything is gonna be okay… now it is your turn kusikia maneno yako mwenyewe toka kwangu…’ Meddy aliongea kwa upole na taratibu huku Jerry akisikiliza na kutazama chini kama mtu anayewaza.

Akabweua kidogo na kutikisa kichwa tena, tukio lile bado liligoma kuaminika kichwani mwake. akashusha pumzi na kulaza kichwa sofani, akiibebesha mikono yake juu ya kichwa kama mateka.

‘Naenda kijitonyama mara moja… kuna inshu nafuatilia usiku huu …nitakupigia baadaye kidogo…promise me hutagusa zile chupa pale’ Meddy alimsemesha Jerry ambaye aligeuza kichwa kitu na kumtazama rafiki yake.

‘Nahitaji kumuona Mzee kabla sijalala… nipitishe hospitali mara moja then utanipitia unirudishe…I cant drive aisee…’ Jerry aliongea kwa unyonge akijiinua toka sofani
‘Poa…  twende’ Meddy alijibu akimtazama rafiki yake alivyonyanyuka na kuelekea ndani huku akimuacha yeye anasikitika peke yake pale sebuleni.

Waliondoka pale na kueekea hospitali alikolazwa Mzee Agapella. Meddy alimshusha getini na kuendelea na safari yake. Jerry Agapella akaingia mapokezi, akisalimiana na nesi aliyekuwa mapokezi, akaongea naye mawili matatu kisha akakwea ngazi kuelekea juu zilipo wodi.

Ndani ya hospitali hiyo hiyo chumba cha tatu toka alicholazwa Mzee Agapella. Msichana aliyekuwa amepotewa na fahamu alikuwa kitandani akiendelea na matibabu. Dennis Mazimbwe akiwa kando ya kitanda pamoja na daktari wa zamu. Dennis alikuwa akimsikiliza yule daktari kwa umakini mkubwa na moyo wake sasa ulipata ahueni kusikia hakuwa ameumia sana.

Tangu alipomgonga mchana ule mpaka alipomfikisha hapo hospitali, binti yule hakuwa na fahamu kabisa. na wala hakujua hata jina lake. Alimtazama vile alivyokuwa amelala kiutulivu na kumhurumia. Alikuwa binti mzuri sana na mdogo kiumri. Kwa dakika kadhaa alikuwa akimshukuru Mungu mno kwa kumuokoa binti yule. Wakati alipokuwa anakaza mwendo barabarani akili yake ilikuwa kwa Rebecca, mke wa mzee Okello.

Ugomvi kati yao ulikuwa mkali mno kiasi cha Rebecca kutopokea simu wala kujibu ujumbe toka kwake. Aliumia sana kutuhumiwa kuwa na uhusiano na Fiona wakati hilo halikuwepo na kamwe lisingekuwepo. Akili yake ilikuwa ikiwaza mengi na wala hakumuona binti huyu aliyekuwa akivuka barabara.

Dennis Mazimbwe alimalizana na daktari akatoka katika kile chumba na kuanza kuondoka. Akiwa anaziteremsha ngazi akakutana na Jerry ambaye naye alikuwa akipandisha ngazi.
‘Are you okay Jerry?’ Dennis alimuhoji Jerry kwa udadisi. Ni dhahiri aliiona tofauti kubwa usoni mwa Jerry
‘nina headache kali tu… sijameza dawa but I’ll be okay unajua tena…mizunguko mingi sana’ alijitetea Jerry

‘ooh…pole sana… umekuja kumuona mzee?’ akauliza Dennis ambaye taarifa za Mzee Agapella kutotaka kuonana na watu zilishamfikia
‘yeah!...’ akajibu Jerry akipepesa macho kama mtu aliyetaka kukatisha maongezi yale haraka iwezekanavyo na Dennis alimuelewa

‘Pole sana Kijana…. he will get well soon… usiwaze sana… pole sana’ alimpiga piga Jerry begani akimfariji na Jerry akatabasamu tu.

Wakaagana na Jerry akaandisha ngazi kuelekea wodini kwa baba yake huku Dennis akitoka eneo la hospitali.

….. NINI KITATOKEA?.... USIKOSE KUJA HAPAHAPA!!

1 comment:

  1. tengeneza tamthilia ya kwenye luninga itakuwa hot sana

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger