39
‘Karibu..’ Sindi Nalela alitaka kuiondoa ile hali ya kuzubaa
iliyomkuta Patrick Mazimbwe pale mlangoni. Hakujibiwa!
Sindi akautanua mlango kwa mapana kidogo na kujirudisha nyuma
hatua moja akiwa ameuegemea mlango na Patrick akanyanyua mguu kwa kutaka
kukivuka kizingiti cha mlango lakini akajikwaa kwenye lile jenereta lililokuwa
miguuni pake, kujikwaa kule ndiko kulikomrejeshea akili yake sawia.
Akababaika kidogo na kukumbuka kilichomfikisha pale mlangoni.
Soni zikamtembelea na akajikuta akijiinamia na kucheka kidogo kabla ya
kulinyanyua lile jenereta na kuanza kuingia nalo ndani. Hatua mbili tatu za
kumfikisha ndani zilimtosha, akalitua lile jenereta pale sebuleni na kumgeukia
Sindi aliyekuwa anaufunga mlango.
Wakatazamana sasa, kila mmoja akitabasamu na asijue kipi
kitangulie kati ya salamu na utambulisho. Kule kugwayana kukapita sekunde tu na
wote wakajikuta wakigeuza shingo zao kutazama mlangoni ambako Dennis Mazimbwe
alikuwa anaingia.
‘Ooh!...’ Dennis akashtuka kuwakuta watu wawili ambao
hakutarajia wangekutana katika mazingira kama yale na wakati kama ule.
‘unaendeleaje binti?’ akamdaka Sindi kwanza wakati akiufunga
mlango kwa kuusukuma kwa mguu kutokana na kuelemewa na mifuko ya bidhaa
alizokuwa amebeba. Patrick aliyekuwa amerudisha macho yake kwa Sindi alishtuliwa
na kaka yake.
‘Come on Pat!...hebu nisaidie hapa’ Dennis alimnyooshea
Patrick mikono akimuonyesha ile mifuko. Patrick akaiwahi na kuidaka huku Dennis
akimpa maelezo ya wapi pa kuipeleka. Akaondoka na ile mifuko kama mtu mwenye
haraka ya kuwahi kurudi pale sebuleni.
Dennis akamkaribia Sindi na kuondoka naye kuelekea chumbani
alikomfikisha mara ya kwanza. Dakika mbili baadaye akarejea sebuleni na kumkuta
Patrick akiwa ameshaliweka sawa lile jenereta na ni kama vile alikuwa akimsubiri
yeye ili amuage.
‘Kazi imeisha steshonari?’
Dennis akamuuliza Patrick mara tu alipofika pale sebuleni na Patrick
akaitikia kwa kichwa akichungulia kordoni kama mtu aliyetarajia kuona mtut
mwingine akitokjezea uko.
Dennis akalifuata kochi na kujitupa kama mzigo, akilegeza tai
yake na kutanua miguu yake kujipa nafasi ya kulitalawa kochi vizuri.
‘huyu ni nani?’ Patrick akauliza kwa mshawasha anaye
akijiweka kwenye kochi la pili. Dennis akatabasamu kavu, tabasamu lililofikisha
ujumbe uliokusudiwa. Hakutaka kumzungumzia Sindi! Patrick akashusha pumzi na
kiherehere kikzidi kumtekenya kiasi cha kushindwa kujizuia kuhoji tena na tena.
‘Ni mdogo mno kuchukua nafasi ya Daniella…’ Patrick aliongea
kwa kubabaika na Dennis akamtazama kwa jicho la mshangao uliozimwa ghafla na
kicheko kifupi kilichokosa tafsiri rasmi.
‘Sivyo unavyofikiria…’ Dennis akamjibu mdogo wake akishusha
pumzi kwa sauti na kumtazama mdogo wake. Alimtazama tu na ukimya ukapita tena
kati yao.
Patrick akatabasamu na kujiinusha, akijiandaa kuaga na
kuondoka. Hakuwa na mazungumzo mengi na kaka yake. Tofauti yao kiumri na tabia
ya ukimya ya kaka yake vilimfanya mara zote akose namna ya kuzungumza naye
achilia mbali ukaribu wa mtu na mdogo wake.
‘Ngoja niwahi kwangu… naona muda umeenda’ Patrick akazuga
akisugua sugua mikono yake kama mtu aipashaye moto. Dennis akaitikia kwa kichwa
tu huku akimtazama
‘utaniagia kwa binti ndani…’ Patrick akaendeleza mazungumzo
ambayo Dennis aliendelea kuyaitikia kwa kichwa tu pasipo kujibu lolote huku
Patrick akitamani kupaza sauti na kumuita binti yule ili japo amuone tena na
kumuaga.
Akaondoka kwa kaka yake kichwa kikiwa na michirizi ya maswali
iliyomuachia nyufa za kutosha. Binti yule alikuwa nani?... alikuwa pale kama
nani?... Dakika mbili tatu alizomtazama mrembo yule, Patrick Mazimbwe alihisi
akili yake ilikimbilia kusikojulikana. Moyo wake ulikuwa umempenda Sindi
Nalela. Alitaka kumjua, alitaka kumfahamu lakini zaidi alihisi moyo wake
ulitaka kummiliki binti yule lakini tatizo alikuwa ni nani kwa Dennis kaka
yake? Alikosa jibu!
Dennis Mazimbwe alitulia pale kochini kwa dakika nyingi tu,
akionekana kutopea kaika mawazo. Akiwa katika hali ile aligeuza kichwa chake
taratibu na kuitazama meza iliyokuwa na vitabu kadhaa juu yake pamoja na fremu
ya picha yenye ukubwa wa wastani iliyokuwa imeegeshwa hapo. Aliitazama picha
ile kwa kina, uso wake ukionekana kujaa simanzi.
taratibu akayateremsha macho yake toka katika ile picha na
kutazama sakafuni, akayatembeza macho yake sakafuni taratibu na kuyainua juu
sasa akiitazama dari huku kichwa kikiwa kimeegemea kochi. Akashusha pumzi nyingi kwa mkupuo ulionyanyua
mabega yake juu na kuyateremsha chini taratibu.
‘Daniella!...’ akalitamka jina hili kwa hisia zote huku
akifumba macho kama mtu anayesikilizia maumivu.
Alikuwa amemkumbuka mkewe wa ndoa, alikuwa amemkumbuka mno
Daniella Carter. alikuwa amewakumbuka watoto wake mapacha, Ilishapita mwaka
mzima tangu utokee mfarakano mkubwa kati yake na mkewe, mfarakano ambao mpaka
dakika ile ulikuwa kama uliotokea jana yake. Ulimuumiza moyo mno na kitu pekee
alichokuwa akikisubiri ni huruma ya Daniella kwake.
Maisha yake yalikuwa yamejaa vurugu za kutosha. Pamoja na
watu wengi kumuona kama mwanaume msomi, mtulivu, mwenye furaha na mafanikio ya
kutosha wengi hawakuwa wakijua maisha halisi ya Dennis Mazimbwe! Laiti tu
wangejua theluthi ya jitimai aliyokuwa nayo Dennis pengine wengi wangekiri si
kila mara pesa huleta furaha!
8888888888888888888888
Nyanza Mugilagila alikuwa amemaliza kufanya hesabu zake za
biashara. Kiasi cha pesa alichokuwa nacho kitandani kilimfanya atabasamu peke
yake. Biashara ilikuwa imemuendea vile alivyokuwa anataka na kwa kiasi kikubwa
alikuwa na furaha moyoni mwake. Wakati akimalizia kuzihifadhi zile pesa katika
sanduku lake, akaiona biblia yake ndani ya sanduku na kuitoa. Picha ya Sindi
iliyokuwa katikati ya biblia hiyo ndio hasa iliyomfanya aichomoe biblia toka
sandukuni.
Akaketi kwa kuegemea ukuta, huku akiitazama ile picha ya
Sindi aliyoishika kwa mikono miwili. Ugumu wa kumpata Sindi ulikuwa wazi mbele yake
japo hakutaka kukiri hilo lakini moyoni pia hakukata tama. Alisali kila
alipolala na kila alipoamka akimlilia Mungu amrudishe Sindi mikononi mwake.
Aliitazama picha ile kwa dakika kadhaa kisha taratibu
akairejesha kwenye biblia na kuitupia sandukuni tena. Alisikitika peke yake, Pamoja
na kuzunguka huku na kule, pamoja na kukutana na wanawake wa kila aina katika
ile biashara ya mitumba bado Nyanza hakuwa amekongwa moyo na mwanamke yoyote
yule zaidi ya Sindi Nalela!
88888888888888888888
Saa sita mchana katika jengo la ofisi za Jerry Agapella
kulikuwa na pilikapilika kubwa. Wafanyakazi walikuwa wakipitapita huku na kule
huku wakipata vitafunwa na kubadilishana mawazo. Ndio kwanza walikuwa
wamemaliza kumkaribisha Jerry Agapella ofisini kwa mara ya kwanza tangu atoweke
katika mazingira ya kutatanisha.
Mkurugenzi alikuwa amerejea kazini rasmi na siku hii alikuwa
ofisini kwake katika kiti cha kazi, akifunua faili hili na kufunika lile,
akipokea simu hii na kukata ile. Aliteleza na kiti toka sehemu moja kwenye
nyingine huku simu ikiwa sikioni na mara kadhaa akilazimika kuibana kwa bega
ili mikono iweze kushika hiki na kile kwa wakati mmoja. Alikuwa na kazi
kpitiliza!
Wakati akitekeleza majukumu yake, mlango wa ofisi yake
ukafunguliwa taratibu na maua yakatangulia mbele na kumshtua Jerry.
‘Hellow!’ sauti ya kike ikaita na muitaji akisikilizia
muitiko wa salamu yake kabla ya kujitokeza
Jerry akatabasamu na hatimaye akacheka kabisa! alishamtambua muitaji
kwa kuitazama miguu tu!
‘hata ungekuwa nje ningekutambua tu Pam…’ akategua
kitendawili na kufanya Pamella ajitokeze mzima mzima huku naye akicheka.
Jerry akanyanyuka na kumlaki Pamella. Wakakumbatiana kwa
bashasha kwanza wakitaniana na kucheka.
Jerry akayapokea yale maua na kuyaweka juu ya meza kisha akamgeukia Pamella
na kuendelea kuzungumza naye.
‘Wait kwanza..’ Pamella akamkatisha akimtazama Jerry usoni
‘nini?’ Jerry akauliza kwa wasiwasi na shauku
‘Umekula?’ Pamella akauliza
‘No…’ jerry akajibu akitikisa kichwa na Pamella akamshika
mkono tayari kumuongoza nje ya ofisi
‘Tunaenda wapi?’ Jerry akauliza kwanza
‘niachie mimi…’ Pamella akajibu, akilifuata koti la Jerry
lililokuwa limeegeshwa kwenye kiti chake cha kazi na kuja kumvalisha Jerry.
‘I just miss my best friend…’ Pamella alimnong’oneza Jerry
wakati akimvisha lile koti na kufanya Jerry aitikie kwa kichwa akikubaliana na
ile kauli. Wakatoka wakicheka mule ofisini na kuingia mapokezi ambako vicheko
vyao vilikata ghafla.
Clarita Gabson alikuwa mapokezi akiwa na maua yake pia. Ndio
kwanza alikuwa anamalizana na sekretari wa Jerry. Pamella Okello sasa
akamshikilia Jerry vizuri kwa mbwembwe zote akitaka Clarita amuone kwa marefu
na mapana.
Jerry alisimama kama sanamu, mkono wa kulia ukiwa mfukoni na
mkono huo huo ukiwa umeng’ang’aniwa na Pamella. Mkono wa kushoto ulikimbilia
shingoni ghafla kabla ya kuteremka na kuingia mfukoni pia. akatabasamu wakati
akimtazama Clarita ambaye anaye tabasamu bovu liliupamba uso wake kwa lazima.
‘Congrats!’ Clarita akamudu kutamka wakati akimfuata Jerry na
kutaka kumpatia yale maua. Mkono wa kulia uliokuwa umeng’ang’aniwa na Pamella
ulishindwa kutoka kwa vile Pamella aliudidimiza usiinuke na wakati huo huo
alishindwa kuyapokea yale maua kwa mkono wa kushoto. Usingekuwa ustaarabu!
Pamella akayawahi na kuyapokea kwa mtindo wa kuyanyakua.
‘Mmmh…mazuri…’ akayanusa na kuyasifia kisha kuyatupia kwenye
moja ya viti vilivyokuwa mapokezi hapo. Clarita akaduwaa!
‘Lets go!...’ Pamella akamuamrisha Jerry ambaye alimtazama
Clarita kwa tabasamu na kumshukuru kwa kumuinamia kidogo huku ule mkono wa
kushoto ukitoka mfukoni na kushika kifua ili kufikisha hiyo heshima.
Wakaondoka!
Clarita akawatazama kwa mshangao, kuanzia walipopiga hatua ya
kwanza mpaka walipotokomea mbele ya upeo wake
‘Shit!’ akalaani akihema kwa ghadhabu na Sekretari akicheka kichinichini. Akayanyakua maua yake na kuinua
kichwa chake juu, pasipo kuaga akatoka kwa hatua ndefundefu na kuishia.
Sekretari aliyekuwa na baadhi ya mabinti pale mapokezi wakaangua kicheko kirefu
kwa tukio lile.
‘aisee kuna siku zitapigwa hapa mpaka mshangae…’ binti mmoja
alivunja kicheko
‘Hands down kwa Pamella…the girl knows how to handle
bitches!’ Sekretari akadakia
‘saaana!... ulikuwepo siku ya sherehe ya Mzee Agapella…
Pamella mwehu aisee… aombe Mungu asitokee wa kumpindua tu…’ binti mwingine
aliyekuwa kwenye mashine ya fotokopi alionya
‘Hakuna!... Pamella ana pesa…ni mzuri… amesoma halafu mzee
wake anajulikana… Jerry atataka nini kwa mwanamke mwingine mpaka amuache
Pamella?.... akitokea wa kuuteka moyo wa Jerry akamuacha Pamella Okello I swear
nitatembea uchi mwenge mpaka posta…’ Sekretari alijiapiza kabisa na kufanya
wenzake wacheke.
8888888888888888888
Siku mbili tatu baada ya Sindi Nalela kufika nyumbani kwa
Dennis Mazimbwe. Nanny aliyekuwa mtumishi wa Dennis alijitahidi kumzoesha
mazingira ya nyumba ile huku akimsaidia kutibu majeraha madogo madogo aliyokuwa
nayo. Nanny alicheka peke yake namna Sindi alvyokuwa akijifunza kutumia baadhi
ya vifaa vya umeme vya mule ndani.
Alicheka zaidi alipomuwashia Sindi mashine ya kusafishia
carpet iliyomfanya Sindi aruke kwa hofu. Alijikuta tu akimfurahia binti huyu
mno na ndani ya siku hizi mbili aligundua kitu kikubwa ambacho alisita
kumuuliza lakini pia alitaka sana kukiongea na Dennis kwanza. Alihisi Sindi
alikuwa na mimba changa!
Jioni hii baada ya kazi zake, Nanny alimuaga Sindi na
kuondoka zake na hivyo kumuacha Sindi peke yake. uenyeji alioanza kuupata
angalau ulimuondolea hali ya kujikunyata. Aliweza kuwasha luninga na kuangalia
kupoteza muda au hata kuingia jikoni na kupika hiki au kile.
Muda huu wa saa mbili usiku, Sindi alikuwa amejikunyata
katika sofa akiwa anatazama luninga huku akimenya chungwa juu ya sahani
aliyokuwa ameipakata. Ghafla akasikia mngurumo wa gari ana akahisi mwenyeji
wake Dennis alikuwa amerejea toka kazini. Akajiinusha kidogo na kwenda
kuchungulia dirishani.
Akaguna kwanza! halikuwa gari la bosi wake, akatanua pazia
zaidi na kuchungulia vema lile gari lililoingia na kuegeshwa karibu kabisa na
ngazi za kulifikia lango la kuingilia ndani. Mlango wa dereva ukafunguliwa na
kijana jamali mtanasati akateremka na kujinyoosha kidogo, akirekebisha suruali
yake kiunoni na kufunga mlango.
Sindi akafumba macho kwa sekunde mbili nzima! akayafumbua na
kukodoa tena pale dirishani safari hii akiyatoa macho yake kana kwamba alitaka
yaone kwa umbali ambao hakupata kuuona tangu azaliwe. Bado alichoona mwanzo
ndicho hicho hicho alichokiona muda ule. Almanusura apige yowe lakini sauti
ilikwamia kooni na kumletea ukavu wa sauti.
Alimeza mate kwa juhudi kubwa akizidi kutumbua macho na sasa
mikono ikimchezacheza kwa hamaniko.
Kijana aliyekuwa akimtazama alisimama pembeni ya gari lile
akionekana kuongea na simu taratibu na hapo hapo akipiga hatua akizifuata zile
ngazi kwa madaha.
‘…Niko hapa kwako tayari…Mzee amesema niipitie
niichukue…sawa…’ alisikika akiongea na sauti ile ile, sauti ya mtu yule yule.
Sindi alihisi pumzi zikikaribia kukata. Akaachia pazia na
kurudi kinyumenyume huku akitetemeka. Alikuwa amemuona Jerry Kristus Agapella!
Mlango aliokuwa akiutazama ukagongwa!
ITAENDELEA....
No comments:
Post a Comment