35
Fiona Agapella alimeza mate kwa juhudi zote wakati akijaribu
kujiweka sawa kumpokea Mzee Okello. Macho yake yalicheza kulia na kushoto katika
namna ya kutafuta utulivu wa nafsi. Akameza tena mate kwa juhudi kiasi cha
kufanya koo lake lididimie ndani kwa nguvu kidogo. Alihamanika!
Mzee Okello akamfikia Fiona na kuachia tabasamu lilienda
sambamba na salamu ya mkono. Fiona akaupokea mkono wa Mzee Okello akijitahidi
kutotetemeka kabisa lakini hofu na wahaka aliokuwa nao vilijionyesha usoni pake
na kupotea.
‘Umekuja kumuona Mr. Dennis?…vipi yupo?’ Mzee Okello
akamuuliza Fiona maswali mawili mazito ambayo kwa wakati ule jibu la haraka
halikuibuka kichwani mwa Fiona.
‘Nilikuwa natokea uko juu… Nikaona nipite kumtaarifu hali ya
Kristus’ Fiona akajibu akionyesha ngazi zilizokuwa zikielekea juu na Mzee
Okello akakunja uso kama mtu aliyekosa kuelewa alichoambiwa. Uko juu
alikoonyesha Fiona kulikuwa na ujenzi mdogo unaoendelea na hakuna mantiki ya
Fiona kutokea uko juu na hapo hapo akili yake ikachukuliwa na suala la hali ya
Kristus.
‘Kwani Mzee anaumwa?’ akauliza kwa sauti iliyowafikia vema
Rebecca na Dennis ambao kwa wakati huo walikuwa wakihangaika kuvaa na kujiweka
sawa.
‘Alipata matatizo ya kiafya asubuhi ya leo…mmmh…uko hospitali
na mmm…he’ll be okay’ Fiona alibabaika waziwazi kiasi cha kumfanya Mzee Okello
amtazame kwa mshangao wa chinichini.
‘Okay!...i see yuko hospitali gani?’ Mzee Okello akauliza na
swali likawa gumu kwa Fiona kwa vile hakujua Jerry alimpeleka hospitali gani
baba yake. Akababaika tena na Mzee Okello akaona anambana kwa maswali ambayo
alikuwa anashindwa kuyajibu kwa uhuru.
‘So yupo…?’ Mzee Okello akauliza akiunyooshea mlango wa ofisi
ya Dennis.
‘sidhani maana naona mlango umefungwa’ Fiona akajibu
akijaribu kukishika kitasa na kukinyonga. Mlango ukafunguka!
Butwaa la ghafla likamvaa Fiona na akajiona mjinga zaidi
mbele ya Mzee Okello ambaye sasa alishindwa kabisa kumuelewa Fiona. Akatabasamu
na kumuonyesha ishara ya kutangulia kuingia. Fiona akaingia kizobazoba akiwa
bado hajaelewa ni nini kilikuwa kinamtokea. Butwaa la pili likampiga alipomuona
Dennis akiwa mbele ya laptop yake akiendelea na kazi na sasa aliinua uso wake
na kuwatazama wageni wake kwa tabasamu.
‘Oh! karibuni…’ akainuka na kutangulia kushikana mikono na
Mzee Okello huku Fiona akionekana kuangaza angaza na kuihoji akili yake kama
ilikuwa sawa. alikuwa amemuona Dennis na Rebecca. aliwaona kwa macho yake, imekuwaje?
alikuwa anaota?
‘Ms. Agapella!’ Dennis akamshtua Fiona aliyekuwa kama mtu
aliyepotelea mawazoni ghafla. Fiona akazinduka na kumpa mkono Dennis hali
akijaribu kutabasamu. Dennis akaongea mawili matatu na Mzee Okello kuhusu
masuala ya kisheria huku Mzee okello akiomba muda na siku ya kuonana naye kwa
shida zake.
‘Nimeona gari la mkeo wakati naingia getini…nadhani atakuwa
around’ Fiona akaingilia maongezi akimtazama Dennis usoni na kutaka kuona
mshtuko atakaoupata. Alitaka kujihakikishia kuwa alichokiona hakikuwa
mazingaombwe. Dennis akashtuka sambamba na Mzee Okello mwenyewe. Fioba akahisi
ushindi!
‘Mke wangu?’ Mzee Okello akamuuliza Fiona akiwa amekunja uso
kiudadisi
‘Yeah…nilidhani labda amekuja kumuona Mr. Dennis… au may be
alikuwa na shughuli zingine’ Fiona akaongea huku akimdadisi Dennis ambaye
alimkunjia uso ghafla na kisha kumgeukia Mzee Okello
‘Hajafika hapa…’ akakanusha na ghafla akashtuka ‘ oh…au
atakuwa duka la vipodozi uko nyuma’ akajitahidi kurudisha hali sawa lakini
Fiona alimkaba
‘uko nyuma si wana parking yao…’ akamhoji Dennis
‘Kama kumejaa watu huwa wanaegesha magari yao huku mbele…’
Dennis akajibu na akiona wazi nia ya Fiona kukazania maelezo yale
‘Ooh!...i see hebu ngoja nimpigie nimuulize yuko
wapi…ningependa kujumuika naye ….you know us women…tukifanya shopping pamoja
…it is all about kipi bora kipi original…’ Fiona aliiinamia pochi yake na
kuanza kutafuta simu wakati Mzee Okello akishindwa kuyaelewa mazungumzo ya hawa
watu wawili.
‘Zunguka tu hapo nyuma…unaweza kumkuta’ Dennis akashauri
akihofia simu kuita na kusikika wakati Rebecca akiwa anamalizia kupitia dirisha
la chumba cha stoo ndogo iliyokuwa ofisini umo. Fiona akatabasamu na kupuuza
ushauri wa Dennis. Akazitafuta namba za simu za Rebecca na kuzipiga. Simu
iliita na ikapokelewa
‘Yes!’ Rebecca akapokea
‘Uko wapi?’ Fiona akauliza na Rebecca akajibu haraka tu
‘Niko duka la vipodozi huku nyuma… kuna nini?’ Rebecca
akauliza wakati huo akitembea toka kule nyuma alikokuwa huku akijiweka sawa.
‘Okay!...fine…’ Fiona akakata simu na kuduwaa
‘Go join her… mkateketeze pesa zetu… women and shopping
huwezi kuwatenganishaMzee okello akamsemesha Fiona na Dennis akiunga mkono na
kuwatania wanawake. Fiona akaaga na kuondoka.
Wanaume wakabaki na maongezi yao kisha Mzee Okello akaaga
pia.
Huku nyuma Dennis akashusha pumzi na kwenda stoo ambako
mafaili yaliyokuwa yameliziba dirisha yalikuwa yametapakaa ovyo sakafuni.
Akaanza upya kuyapanga huku akitikisa kichwa. Skafu ndogo iliyokuwa mikononi
mwa Rebecca ilikuwa imebaki sakafuni. akaiokota na kuinusa huku akitabasamu na
kushusha pumzi nyingine ndefu.
‘Rebecca!...i love you’ akatamka polepole akifumba macho na
kuipeleka ile skafu puani. Alihisi mapenzi yake kwa mwanamke huyu yalikuwa
yanaelekea kumuingiza hatarini.
88888888888888888888888
Muziki wa taarabu ulikuwa unasikika toka chumba kimoja wapo
katika nyumba aliyopanga Sindi Nalela. Alikuwa Mzee Yusuph na kundi lake la
Jahazi na huyo aliyekuwa akiusikiliza huo wimbo hakuuacha upite hivi hivi,
aliimba sambamba naye kwa madoido yote wakati akiunga mboga yake jikoni.
Alikuwa Jamila!
Mpangaji aliyekuwa anapita kordoni alipita kwanza kisha
taratibu akarudi kinyume na kusimama mlangoni kwa Jamila ambaye alipomuona huyu
mpangaji alilala ubavu na kuifikia redio iliyokuwa pembeni tu na kupunguza
sauti.
‘Subalkheir Chemwali’ alimsabahi Jamila
‘Alkheir mgonjwa vipi?’ Jamilaa akauliza akifunika sufuria na
kumgeukia mpangaji huyu ambaye alijikaribisha mpaka kitandani.
‘Mahututi garagara mauti….tunamsalia mtume tu!’ akajibu
mpangaji akiutandua ushungi wake na kuubwagia mapajani
‘Kwani haongei kabisa?’ Jamilla akauliza akitoa macho
‘kakata na kauli nakwambia…ingekuwa vijijini kule tungesema
keshakufa…wamemvisha mijimashine puani nasikia ndio anapumulia’ mpangaji yule
mwanamke mwenye umri wa makamo akaelezea hali ya mgonjwa wake lakini ghafla
kama mtu aliyekumbuka kitu akatoa macho pah!
‘Daada! kama duniani wawili wawili basi huyu niliyemuona ni
pacha utozi kwa unyayo’ akajitanua kishambenga akianza stori yake
‘Nani huyo?’ Jamilla anaye shingo ikamsimama
‘Yaani nimemuona mtu kama Jerry…yaani Jerry mtupu…’
‘Umemuona wapi?’ Jamilla akasotesha matako kidogo akisogea
mbele kana kwamba hakuwa anamsikia vizuri yule
mpangaji
‘Uko hospitali dada….yaani Jerry kabisaa ila sio kwa mavazi
haya anayovaa wala si kwa huu umaskini ninaomuona nao….alikuwa na msichana kama
wanafanana hivi…yaani jamani huyo kama akimuona Jerry atamkimbia wallah…ni
mzimu wake kwa kule kufanana’ Mpangaji akajieleza mwenyewe na Jamilla akacheka
kwanza.
‘Basi uliyoona wewe kuna siku nami niliyaona shosti… Kidogo
nigongwe na gari kwa kushangaa mpaka nikahisi naingiwa na wehu….ila ndio hivyo
mkewe anakataa kuwa si yeye…labda wanafanana…nikaguna tu nikanyamaza ila kama
na wewe umeona basi shoga itakuwa ni mapacha hawajuani au ndio mtu mmoja
anatucheza shere’ Jamilla akaongea akinesanesa na akitoka pale kigodani na
kukaa chini kabisa
‘Kheee! makubwa dada!...mmmh ndio ukute ni mashushushu hawa
watu….sie tunadhani ni wenzetu kumbe wapo kazini ohooo….kuna mama f’lani
alikuwa anapenda kukaa posta pale karibu na ilipokuwa shule ya sekondari
Forodhani…alikuwa kibonge flani kama mwehu hivi… tukijua mwehu tu siku alikuja
kuzolewa pale na mapolisi wana mibunduki mirefu unaambiwa aligeuka mzima
ghafla….’ Mpangaji stori ilipamba moto
‘Usinambie wewe…’ jamilla alishika tama
‘Ndio tukaja kujua kumbe alikuwa shushushu toka Malawi… mpaka
leo yaani hawa vichaa nikiwaona huwa siamini wote wana matatizo ya akili….sasa
ndio huyu mwenzetu ukute labda kaolewa na usalama wa taifa hajijui au anajua
ila ndio yuko kazini’ Yule mpangaji akafanya Jamilla akanyanyuke ghafla
‘Hebu ngoja…’ akatoka na dakika moja tu akarudi na Sindi
akiwa kamshika mkono. Wakamuweka chini. Wakimweleza yote waliyoyajua na Sindi
akabaki mdomo wazi
‘Jerry???’ akauliza akiwa ahamini
‘humjui hata dada wa kufikia upo tu hivi leo akisema
amemaliza kazi yake na akaondoka asikuage utaanzaje kumtafuta?’ Yule mpangaji
akamuuliza swali la msingi sana
‘anatoka anarudi usiku anaenda wapi?....kazini kwake
hupajui…eti anajenga nyumba…anajenga wapi?.... usala wa taifa huyu wenyewe
tunaita mashushushu dada….uko kijijini ukute alikuja kupeleleza tu’ Jamilla
akaongea kwa hisia hasa
‘Kijijini alikuja ameumia sana…ilikuwa tusingemuokota
angekufa kwa kweli’ Sindi alijibu woga ukionekana kumtawala isivyo kawaida.
‘Wana mbinu hawa Sindi…. wapelelezi! wanaweza hata kuzaa na
wewe akaishi na wewe akimaliza kazi anasepa zake… hapo ulipo una mimba tayari
utazaa hapo na ataishia na mtoto siku moja unabaki kinywa wazi…’ Yule mpangaji
alipigilia msumari wa hofu moyoni mwa Sindi ambaye sasa alikuwa ameshikilia
kifua chake akisikiliza huku na huku.
‘Kama bado hata miezi miwili bado kaitoe shosti…. unamwambia
imetoka bahati mbaya kisha unasepa zako…bora kuondoka bila kitu kuliko uachwe
na mzigo wa kulea mtoto usiyejua asili yake… fanya ya kufanya urudi kijijini
kwenu ukatulie na Nyanza wako… atakusamehe tu…. mwenyewe nimeogopa hapa mpaka
basi’ Jamilla alitoa ushauri, akaongea kwa marefu na mapana akimuacha Sindi
njia panda!
88888888888888888888888
Saa moja jioni, Mzee Agapella alikuwa wodini, hali ikiwa
imetengamaa kiasi Fulani, Jerry alikuwa amesimama kando yake akimtazama baba
yake kwa huzuni iliyochanganyikana na hali ya kukataa kile alichokuwa ameambiwa
na baba yake.
‘I can’t marry Pamella…baba please!... na sidhani kama ni
mahali sahihi kuongelea hili’ Jerry aliongea kwa kurai
‘Najua…lakini nahisi nahitaji kuona harusi yako…nahitaji
kuona naondoka nikiwa nimekuacha kwenye familia…’ Mzee agapella akaongea kwa
huruma
‘Baba huendi popote…. unaumwa na unatibiwa na utapona… stop
this naondoka…naondoka…we still need you…I’ll marry for love na sio sababu
nyingine’ Jerry alijitetea, akitaka baba yake amuelewe
‘What is wrong with Pamella?... amekuwa rafiki yako miaka…
unamjua na tunaijua familia yake…baba yake amekubali kila kitu…’ Mzee akajaribu
kushwishi zaidi
‘Baba!...how could you do that?....unafinalize makubaliano ya
ndoa bila kunishirikisha?...’ Jerry alihisi kubanwa
‘It is for the best son!’ Mzee Agapela akajiinusha kidogo kwa taabu akisaidiwa na kijana wake.
Wakati Jerry akitaka kumpinga zaidi mlango wa chumba alicholazwa ukafunguliwa
na Mzee Okello akaingia. Jerry akalazimika kukata malumbano na kutoka.
Wazee hawa wakasabahiana, wakazungumza hiki na kile na mwisho
Mzee Okello akazungumza kitu kilichomuacha Mzee Agapella mdomo wazi.
‘…kuwa makini na Dennis’
‘Dennis Mazimbwe’ Mzee Agapela akauliza na Mzee Okello
akaitikia kwa kichwa akionyesha wazi hakuwa anatania
‘Kwanini?...ni mwanasheria wangu’ Mzee Agapela alihisi ubaridi Fulani mwilini
‘Kuna kitu kinaendelea kati yake na mkeo Fiona…just chunguza
tu….nahisi kuna kitu kati yao…maka si mahusiano basi ni dirty deals..si
unazijua’ Mzee Okello alaiongea taratibu akitaka mzee mwenzake amuelewe na
hakumuelewa!
‘Dennis!!....What I know hawa watu wawili hawaelewani
kabisa!...what is going on?’ Mzee Agapella akaonyesha kushtuka sana kiasi cha
kuhema kwa nguvu kila sekunde.
‘Relax!.... ufanye uchunguzi….wanawake si viumbe vya
kuwaamini… Fiona anaweza kuwa anakusaliti…chunguza tu!’
Mzee Agapela akahisi kule kuhema kunamletea maumivu yale ya
kichomi cha moyo. Akahema tena kwa nguvu na kumtia hofu Mzee Okello ambaye
alimuuuliza kulikoni. Hali ikazidi kuwa mbaya na Mzee Okello akatoka kumuita
daktari haraka.
……KARIBU TENA….TUBURUDIKE HAPAHAPA!
mh! kizungumkuti! kweli babu jinga inama ufikiri.mali yako inaliwa
ReplyDelete