38
Jua la saa nne asubuhi lilishachomoza kwa makali ya kiasi
chake. Utulivu mkubwa ulikuwa umetanda eneo kubwa la jumba la Mzee Okello…
sauti chache zilizosikika zilikuwa za watumishi waliokuwa wakifyeka nje na
kupunguza michongoma iliyoizunguka nyumba hiyo. Kwa mbali zilisikika ngurumo za
magari toka barabara kuu ya lami iliyokuwa mita kadhaa toka lilipo jumba hilo.
Rebecca Okello, mke wa Mzee Okello, mwanamama mwenye umri wa
makamo tu, mwenye uzuri wa asili na umbile la kuvutia alikuwa amesimama
dirishani akiwa na kikombe cha kahawa mkononi hali mkono mwingine ukiwa
umekishikilia kisosi kilichoambatana na kikombe cha kahawa, aliinywa taratibu
kahawa yake huku akitazama nje kupitia dirishani pale na akili yake ikionekana
kuchotwa na mawazo yaliyoitesa nafsi yake mno. Uso wake ulikosa nuru!
Ni kama vile Kahawa ile ilishindwa kupita kooni kama
alivyotarajia, aliimeza kwa mafunda ya kuhesabu kwa taabu na akajikuta
akishusha pumzi na kugeuka kukitua kile kikombe juu ya kabati lililokuwa na
sinia lililobeba jagi la kahawa na sukari. Alikitua kisosi kisha akakiweka
kikombe juu yake. Akageukia kule dirishani safari hii akifumbata mikono yake
pamoja chini ya kifua chake. Alitulia vile akiwaza, akiumizwa na aliyokuwa
akiwaza na wala asitambue kuwa mumewe Mzee Okello alikuwa amesimama mlangoni
kitambo tu akimtazama!
‘Becca!..’ Mzee Okello akamuita mkewe ambaye wala hakumsikia,
akapiga hatua kumfuata na ahatimaye akamshtua kwa kumgusa begani. Rebecca
akageuka na kumtazama mumewe usoni, akijilazimisha kutabasamu na akijilazimisha
kuvunga kwa kutaka kukichukua tena kile kikombe cha kahawa lakini mumewe
akamzuia na kumshika mkono.
Akamuondoa pale dirishani na kumleta mpaka kitandani, akaketi
na kumuomba mkewe aketi kando yake. Sekunde tatu za mwanzo alimtazama mkewe kwa
upendo hasa!
‘Becca!..’ akamuita kwa sauti ya upole sana na mkewe
akamtazama kwa uso ule ule uliokosa nuru huku akiyateremsha macho yak echini
kama mtu aonaye soni
‘kama kuna kitu kitapunguza siku zangu za kuishi basi ni
kukuona ukiwa huzuni Rebecca… tangu juzi unalia kimya kimya… kuna tatizo gani
mke wangu’ Mzee Okello aliongea taratibu akimtazama mkewe ambaye uso wake
ulizidi kusawajika na matuta kadhaa yakajipanga usoni pa mkewe, alionekana wazi
kushindana na hali Fulani ya uchungu ambao Mzee Okello alitakamani kuujua na
hatimaye kuuondoa. Mkewe hakujibu!
‘Nafanya kila ninaloweza kukupa furaha Rebecca…. kila
ninaloweza mama… lakini…’ akakosa la kuongeza na kubaki mdomo wazi baada ya
mkewe kuangua kilio cha chinichini. Mzee Okello akashusha pumzi sasa na
kumkaribia mewe zaidi. akamvutia ubavuni pake na kumkumbatia. Rebecca akalia
kwa muda kisha taratibu akajiondoa mikononi mwa mumewe na kujiinamia tena.
‘nimekuumiza wapi mama?... umesikia nini?’ Mzee Okello
aliuliza naye akionekana kukosa raha sasa
‘Una mwanamke mwingine…’ Rebecca akajibu akiwa bado
amejiinamia na akijua wazi alikuwa akidanganya. Kilichokuwa kikiitesa nafsi
yake ni tukio la kumkuta Fiona akimbusu Dennis Mazimbwe. Aliumizwa kupitiliza
na mpaka dakika ile hakuwa amepata suluhu na Dennis. Mzee Okello akakunja uso
na kumtazama mkewe kiudadisi.
‘Becca!’ akamuita kwa mshangao kidogo na kubweua huku
tabasamu likija taratibu usoni pake
‘Mwanamke?... niache mwanamke bora duniani ndani mwangu
niende nje kutafuta nini?... nani amekwambia ujinga huo?... ‘ Mzee Okello aliongea
na mkewe akiupeleka mkono wake usoni pa Rebecca na kumfuta vijimachozi
vilivyokuwa vimebakia mashavuni.
‘Siwezi… siwezi kufanya ujinga huo…never!... Never Rebecca…
njoo mama’ akamsogelea mkewe na kumuweka tena kifuani pake kwa mapenzi yote na
asijue kilichokuwa moyoni mwa mkewe. Dakika mbili baadaye kitita cha pesa
kilikuwa mezani na Mzee Okello alimtaka mkewe akanunue alichohitaji, akamtaka
atulize nafsi kwani hakukuwa na mwanamke wa kumzidi yeye maishani mwake Mzee
Okello. Alipotoka na kuishia Rebecca akaketi kitandani na kuangua kilio upya,
akiomboleza kwa uchungu zaidi huku mikono yake ikiwa kifuani., aliyafumba macho
yake na machozi yakamtiririka kwa kasi huku midomo ikimchezacheza. Alilia
haswa!
Ooh Dennis…Dennis why?’ alisema akiwa amejiinamia na
kuendelea kulia
888888888888888888
Patrick Mazimbwe aliegesha gari lake nyumbani kwa kaka yake
Dennis muda huo wa saa nne asubuhi na kuremka kwa kasi kidogo, akishindwa hata
kufunga mlango wa gari lake. Alikimbia kidogo kuwahi mlangoni na kubonyeza kengele
mara kadhaa akiashiria haraka aliyokuwa nayo. mlango ukafunguliwa na bibi wa
makamo aliyempokea kwa tabasamu na kumbatio la furaha
‘Nanny!..’ Patrick alimlaki bibi yule
‘Patty…ooh mwanangu… haya vipi?’ alilakiwa Patrick kwa furaha
kubwa na Patrick akamkumbatia na kumbusu pajini bibi yule huku naye akionekana
kufurahi kumuona
‘Jenereta lipo?...’ akamuuliza kwa haraka yule bibi na
kumkatishia furaha yake
‘Huulizi hali zetu kwanza…wakimbilia kuuliza Jenereta…kwani
ndio lililokufungulia mlango?.... Patrick!!…’ yule bibi alisema kwa ukali
kidogo akifunga mlango na kumvutia Patrick ndani zaidi akimpeleka sehemu ya
kulia chakula
‘No!...unajua nina haraka sana… steshonari kubwa kule juu
umeme umekatika na jenereta imegoma kuwaka…kuna kazi Fulani… ooh Dennis!’
Patrick alikatisha maelezo yake mara tu alipomuona Dennis akitokea kwenye kordo
akiwa na nguo za kulalia. Hakutarajia kumuona Dennis pale muda kama ule siku
kama ile.
Dennis alifikicha macho yake kuashiria ndio kwanza alikuwa
anatoka usingizini. Akawakaribia na kumsugua sugua begani yule bibi huku
akimbusu utosini na kuachana naye kisha akamgusa begani Patrick na kuachana
naye, akaifuata meza na kujimiminia chai ya moto. Pasipo kuweka sukari akapiga
funda moja la kugugumia na kutua kikombe.
Wakati wote huu Yule bibi na Patrick wakimtazama kwa
mshangao. Akawageukia na kujaribu kutabasamu.
‘Hujaenda kazini?’ yule bibi ambaye ni mtumishi wa miaka
mingi wa Dennis alimuuliza Dennis akionekana wazi kushangaa kumuona Dennis pale
‘nitaingia mchana nadhani… huh!...mbona uko hapa muda huu?’
Dennis alijibu na kumgeukia Patrick
‘Nimefuata Jenereta mara moja…’ Patrick alijibu kwa adabu na
Dennis pasipo kujibu kitu aliwapita tena na kuelekea chumbani kwake akiwa na
kile kikombe cha chai. Lakini kabla hajaufikia mlango wa chumba chake alisita
na kuwageukia Patrick na yule bibi, akawakuta bado wanamtazama. Akatabasamu na
kugeuka mzima mzima sasa akiwatazama vizuri na kama mtu aliyekumbuka jambo
alitembea tena kurejea pale walipokuwa.
‘unamfahamu Pamella Okello?’ akamtandika Patrick swali moja
jepesi tu lakini lililomfikia Patrick kama konde la uzani wa dunia. Patrick
akatoa macho na kumtazama yule bibi kana kwamba alihitaji amsaidie kujibu. Yule
bibi akamonga Patrick konzi la kisogo
‘jibu!’ bibi akamuamrisha kama mtoto
‘yeah!...namjua…amekuwaje kwani?’ Patrick akauliza uso wake
ukipoteza hali ya kujiamini na Dennis akibinua midomo yake na kutikisa kichwa
juu chini mara kadhaa
‘Mna ukaribu wowote au urafiki..’ Dennis akauliza tena
akiguguna ndani kwa ndani na kutikisa kichwa
kulia na kushoto harakaharaka akimaanisha kama kuna chochote zaidi ya hivyo
alivyovitaja.
‘hapana..no!,,,,najua tu ni binti wa Okello…nothing
more…nothing serious… kwani kunaa…’
akakataa haraka haraka lakini pia akataka kudadisi zaidi ila Dennis hakumpa
nafasi hiyo, aligeuka na kuanza kuufuata tena mlango wa chumba chake na kuishia
chumbani.
Patrick akatoa macho na kushusha pumzi ndefu mithili ya
mluzi.
‘unamjua si ndio….umemdanganya kaka yako!’ Bibi akamsuta
‘I swear Nanny… mambo yanakoelekea sasa mmmh…’ akaguna tu na
kufanya yule bibi acheke wakati Patrick akionekana kutafakari ghafla
‘Clarita hajambo?’ Bibi akauliza na Patrick akagutuka na
kukumbuka kilichomleta
‘Jenereta liko wapi?... nataka kulichukua sasa
hivi…nitalileta jioni…’ alisisitiza shida yake na bibi akamvutia jikoni
kumuonyesha lilikokuwa hilo jenereta. Akalichukua na kulipeleka kwenye gari.
Baada ya kuliingiza kwenye buti ya gari. Alisimama kwenye mlango wa gari na
kumtazama yule bibi.
‘Nikija saa moja nitakukuta?’ akamuuliza
‘Saa moja kamili ukija na dakika tano hunikuti… ila nadhani
Deni atakuwepo sidhani kama ataenda kazini leo…’ yule bibi alijibu akitabasamu
‘Hivi ana nini leo… kwanini hajaenda kazini?’ Patrick
akauliza akianza kutumbukiza mguu garini
‘Mi hata sikujua kama yupo… atakuwa na yake tu… kaka yako
anahitaji kumrudisha Daniella na watoto haa nyumbani… haya mambo ya mke yuko
amerika mume yuko Afrika tabu tupu vijana… mimi nazeeka na babu yenu Magomeni
pale… tunaona nyumba za makuti zinageuka maghorofa pamoja…tunashangaa pamoja…
tunakwepa vifusi pamoja…’ bibi aliongea kwa vitendo kidogo na kufanya Patrick
acheke kwa sauti na hata mlinzi aliyekuwa akijiandaa kufungua geti alicheka
pake yake kule getini.
Patrick akaingia garini na kuwasha gari akimpungia mkono yule
bibi na kuondoka eneo lile. Kichwani akiwaza na kuwazua sababu za Dennis
kumuuliza ghafla habari za Pamella Okello. aliguna mara kadhaa na maswali yake
yalikosa majibu ya kuridhisha!
88888888888888888888888888
Alitembea kivivu kwa kuyumba yumba wakati akiufuata mlango
uliokuwa ukigongwa kwa fujo kidogo. Pale sebuleni aliitazama saa yake na
ukutani na mshale mdogo ulikuwa unaikaribia namba 11 huku ule mrefu ukiwa
kwenye namba 10. Alipiga mwayo mrefu aliojaribu kuuzuia kwa kiganja cha mkono.
kisha akajvuta na kufungua makomeo kadhaa kabla ya kuhangaika na mlango wa
chuma uliotangulia uko nje.
Jenifa akaingia kwa jazba kidogo akimpita Jerry ambaye
aliurudishia mlango na kumgeukia mdogo wake, mwayo mwingine mrefu ukifuatia
‘Hiki nini sasa…’ Jenifa akashangaa chupa za pombe zilizokuwa
juu ya meza
Jerry hakujibu wala hakuonekana kutaka kulijibu lile swali,
alijivuta na kujitupa kwenye kochi, akajiegemeza kizembe na kumtazama mdogo
wake.
‘Nimegonga jamani….nimegonga nusu ya kuota sugu kha!... ndio
kulala au kufa?’ Jenifa akauliza kwa dhihaka akiruka chupa kadhaa za pombe
zilizokuwa chini na kuketi sofani.
Jerry hakujibu aliendelea kumtazama Jenifa kana kwamba
alikuwa akimletea burudani kwa wakati ule
‘una matatizo gani Jerry… mama analalamika umemkataza
asimuone baba hospitali… una matatizo gani eeh’ Jenifa alihoji kimamlaka wala
simpe kaka yake nafasi ya kujieleza
‘wale ni watu wazima wanajuana wao…. wewe unapowaingilia na
kuanza kuwafarakanisha… unakuwa na lengo gani hasa…. baba sasa hivi ana…’
Jenifa aliongea kwa jazba na Jerry akamkatisha kwanza kwa kupunga mkono hewani
akimaanisha hakutaka kusikia zaidi ya kile alichosikia
‘Mama?... hivi bado tuna mama dunia hii?... mama?...
Jenifa!... yule mwanamke anakufadhili kwa lipi hasa mpaka unamtetemekea?...’
Jerry alikuja juu sasa
‘Sio kumtetemekea… amenipokea pale kwake na amenirudisha
chuo… wewe si ulikuwa unamtegemea Pamella… wewe unavyomtetemekea Pamella
kakufadhili kwa lipi?...’ Jenifa alirudisha mashambulizi yaliyomfanya Jerry
amtolee macho kwa mshangao.
‘Umesema?’ akauliza kwa kutaka uhakika alichosikia
‘You heard!’ Jenifa akamjibu kwa kiburi
Jerry akajirudisha nyuma na kujilaza kizembe tena, akifumba
macho na kutulia vile vile
‘Nimekuja kukwambia tu kuwa acha kuingilia ugomvi wa wazazi
Jerry….utaleta matarizo maugbwa zaidi’ Jenifa alikata ukimya akimtazama kaka
yake
‘Pumbavu!...nyanyua ngoko zako utoke humu ndani upesi’ Jerry
alifoka akinyanyuka na kumuonyesha mlango Jenifa
‘unanifukuza?!’ Jenifa alisimama akiuliza na kushangaa lakini
akiwa na ule mshangao Jerry aliukwanyua mkono wake na kumburuza kuelekea
mlangoni. Pochi ya Jenifa ikadondoka lakini Jerry hakujali alimkokota mdogo
wake mpaka mlangoni. akaufungua mlango na kumsukumia nje, akafunga mlango!
‘Jerry pochi
yangu….Jerry…Jerry’ Jenifa alipiga piga mlango akimgongea Jerry ambaye
aliiokota ile pochi na kufungua mlango. Akairushia mbali ile pochi na Jenifa
akaambulia kuitazama ikipita pale mlangoni na kupepea kuelekea kwenye ngazi.
Jerry akafunga mlango na kumuacha Jenifa ameduwaa mlangoni.
Jazba za Jerry hazikuwa za kawaida. Alishagombana sana na
kaka yake lakini haikuwahi kutokea kashikashi ya kutupwa nje namna hii.
Aliweweseka pale mlangoni kwa sekunde kadhaa kabla ya kutoka taratibu na
kuifuata pochi yake ambayo ilipotua chini ilifunguka na kutawanyia mbali baadhi
ya vitu vilivyokuwemo ndani. Aliinama na kuviokota taratibu, mara kadhaa
akiutazama mlango aliotokea na asimiani kama ni yeye ndio alisukumiwa nje vile.
kule ndani Jerry alirejea kochini na kujibwaga tena pale,
akionekana kuelemewa na ulevi aliotandika usiku uliopita sambamba na mawazo juu
ya Sindi Nalela.
888888888888888888888
Saa Nane mchana, Sindi Nalela alikuwa ameketi kitandani
akimalizia kupata chakula. tabasamu lake dogo na tulivu liliupamba uso wake
mara tu alipomuona Dokta Kashindye akiingia pale wodini.
‘naona umepata nafuu haraka sana… una maumivu yoyote?’ Dokta
alimuuliza huku akitabasamu na Sindi akatikisa kichwa kukataa
‘Sasa..’ dokta akaongea kwa kuivuta hiyo sasa akiuma midomo
yake kwanza kama mtu anayepangilia sentensi yake vizuri
‘Okay… aliyekuleta hapa…atafika muda wowote ule naaa…’
akavuta tena lile neno na huku akikunja uso kidogo kisha akahairisha kuzungumza
alichotaka kuzungumza
‘Subiri kidogo..’ akaomba udhuru na kutoka akimuacha Sindi na
maswali kichwani. Alikumbuka vema kilichotokea, lakini hakukumbuka alifikaje
pale. alikuwa na maumivu kidogo mguuni na hata alipoligfusa tumbo lake alihisi
lilikuwa kama lilivyokuwa. alijikagua hapa na pale na kuona michubuko midogo
mkononi, plasta ndogo kwenye kiwiko na michubuko kwenye mguu ule uliochotwa na
gari.
Alimshukuru Mungu kwa kumuokoa lakini moyo wake ulikosa
utulivu. alitaka kumuona huyo aliyemgonga na kumuokoa. kuna kitu alijiuliza
sana tangu ile alfajiri aliyopata fahamu. litaka kuficha kila kitu kuhusu yeye
lakini pia roho ilisita. Hakumuamini mtu mjini hapa tena hasa baada ya maisha
yake na Jerry Agapella. Mambo mengi yalipita kwa kasi kichwani mwake na akakosa
uamuzi wa maana. Bado alikuwa anaweweseka na tukio la kutengana na Jerry!
Mawazo yake yakakatwa na ujio wa Dokta Kashindye akiwa
ameongozana a mwanaume mrefu, mtu wa makamo, mwenye mvi chache za kutosha,
mwembamba kiasi mwenye mwili mkakamavu. Miwani ya macho iliyokuwa usoni pa
mwanaume yule ilimkumbusha mtu aliyemuona akimuinamia dakika chache kabla ya
kupoteza fahamu. Akahisi ndiye aliyekuwa akimngojea!
Dennis Mazimbwe alimfuata Sindi kitandani na kumsabahi,
akimpa pole nyingi na kuketi kwenye kingo ya kitanda. mguu mmoja ukifika chini
na mwingine ukielea hewani.
‘Unajisikiaje sasa?’ akamuuliza Sindi huku akimtazama kwa
umakini mkubwa. alikuwa binti mzuri mno na zile aibu za kike alizokuwa nazo kwa
mwanaume yoyote rijali wa umri wowote lazima angelimtukuza Mungu kwa uumbaji
wake. Dennis alimkodolea macho Sindi na kukosa la kuongea kwa sekunde kadhaa
mpaka pale Dokta Kashindye alipoamua kuokoa jahazi.
‘Anaweza kutoka hata sasa…’ akatoa ruhusa na Dennis akaitikia
akimtazama Sindi na kisha kumgeukia Dokta, akikosa kabisa neno la kuongeza.
Dakika tano zlitosha Sindi kujiondoa pale kitandani na kusaidiwa na Dennis kuondoka
wodini.
Ukimya mkubwa ulitawala garini wakati wakielekea nyumbani kwa
Dennis Mazimbwe. Mpaka wanafika na kupokelewa na Bibi, Dennis hakuwa amemuuliza
hata jina lake la kwanza tu. Bibi akampokea kwa bashasha kwa vile alishaelezwa
kuhusu ujio wake.
‘Akamsaidia kutembea kwa kumshikilia mpaka ndani ambako
alimpitisha mpaka kwenye chumba alichokuwa ameandaliwa.
‘Aah aah… achana na sanduku mwanangu…au kuna dhahabu umo?’
bibi alimtania Sindi wakati Sindi alipotaka kupokea sanduku lake toka kwa
Dennis
‘Ngoja nikuandalie kitu unywe kwanza… tulia upumzike
kwanza…sawa?’ bibi alitoa maelekezo na Sindi akatabasamu kiuoga kidogo na
kuitikia kwa kichwa akiwa ameshapandishwa kitandani. Dennis akatabasamu na
kutikisa kichwa wakati bibi akiongea na Sindi. Kisha wakatoka na kumuacha Sindi
mwenyewe akishangaa kupitiliza, akiangaza macho huku na kule mdomo ukiwa wazi,
akistaajabu ukubwa wa chumba, mapambo, na kila lililokuwemo mule ndani.
Kule nje ya chumba Bibi alimtazama Dennis kwa macho ya
kumsuta
‘Ulitaka kuua malaika wa watu huyu kwa mawazo gani
sasa?....anaitwa nani?’ bibi akauliza akimtoa Dennis mlangoni pale na kuanza
kuelekea naye sebuleni
‘Sijamuuliza kitu kuhusu yeye… zungumza naye?’ Dennis
akamrushia majukumu yule bibi aliyempapasa mgongoni na kutabasamu
‘hilo sio kazi… sema lingine…’ bibi akajibu na kufanya Dennis
acheke chinichini
‘ni mzuri..’ Dennis akasema akitabasamu na akimtazama yule
bibi katika namna Fulani ya kungojea jibu la kufurahisha
‘Dennis!!...’ Bibi aksitisha kutembea na kumtazama Dennis usoni
kwa umakini lakini Dennis aliendelea kitabasamu
‘una mke na watoto… huyu ni binti yako kabisaaaaa’ bibi
akaonya
‘Sijafika uko Nannny…’ Dennis akajitetea akizidi kutabasamu
‘Kwani huwa mnafikaje uko?... nikusikie tena!...’ akaonya
Bibi akimuachia mkono Dennis na kupiga hatua chache kuelekea mbele
‘Nataka kwenda mlimani city mara moja… kama nitachelewa
tafadhali mwambie huyu binti asitoke wala asiwe na wasiwasi…. kesho uwahi
kidogo kuja ili asijisikie mpweke sana’ Dennis akaongea na yule bibi ambaye
aliitikia maelezo yake na kuridhia.
Dennis akaondoka, na bibi alipomaliza shughuli zake, akamuaga
Sindi na kumpatia maelezo kadha wa kadha huku akilitambua jina la Sindi nay eye
akijitambulisha kama Nanny. Akamuacha Sindi mwenyewe mule ndani.
Saa mbili kasoro usiku, Sindi alitoka chumbani akichechemea
mara baada ya kusikia kengele ikilia mno. taa zilikuwa zinawaka sebuleni hivyo
alipotoka alipepesa macho kuangaza kama kulikuwa na mwenyeji yoyote lakini
hakuona mtu. Kengele ilizidi kulia na Sindi akajikuta akilazimika kuufuata
mlango huku akichechemea.
Akahangaika kuufungua na alipoweza aliutanua mlango taratibu
na kuuweka wazi. kijana jamali mwenye aliyefanana mno na yule baba wa makamo
aliyemtoa hospitali alikuwa mbele yake. Walitazama tu pasipo kuongea lolote!
‘Wow!...’ Patrick alipiga ukunga akimtazama Sindi usoni,
akili ikimpotea ghafla na mshangao wake ukipitiliza na kumduwaza. Alimtazama
Sindi kuanzia chini mpaka juu na kumtulizia macho, tabasamu la Sindi
likiuchachafya ubongo wake na kumfanya zezeta kwa sekunde kadhaa.
‘Karibu!’ sauti ya Sindi ilipiga masikio yake na kuyatia
uziwi wa muda, wakati ubongo wake ukipokea mawimbi ya sauti ya Sindi.
Hakuwahi kumuona msichana yoyote maishani mwake aliyempitisha
katika mshtuko wa aina ile. Ndani ya moyo wake alikiri msichana huyu alikuwa
mzuri, alikuwa na mvuto wa aina yake, alikuwa na nguvu ya asili, nguvu ya
kuvuta na kunasa. Patrick akamtumbulia macho Sindi Nalela asiweze kuitikia ile
karibu wala kupiga hata hatua moja ya kizembe kuingia ndani. alimkodolea macho
tu mithili ya mtu aliyepigwa na shoti ya umeme ghafla!
Sindi akazidi kutabasamu asijue ni kiasi gani alizidi
kuuharibu mfumo wa fahamu wa Patrick Mazimbwe na jenereta lake lililokuwa
miguuni pake.
…..USIKOSE KUJUA NINI KITAJIRI…. NIPE MAONI YAKO….
No comments:
Post a Comment