40
Pale alipokuwa amesimama, Sindi alinesa nesa mwili mzima,
ilikuwa zaidi ya kutetemeka, zaidi ya hofu na kuchanganyikiwa
kulikochanganyikana na hali ya kutoamini alichokiona. Mlango ulipogongwa mara
ya pili, Sindi alifumba macho kwa nguvu zote na kujaribu kujikakamaza asianguke
ila mwili uligoma kutulia, uligoma kutii amri ya kukakamaa na kinyume chake
kila sehemu ya mwili ilimcheza mpaka utumbo!
Jerry hakuielewa ile hali ya ukimya mule ndani hali taa
zilikuwa zinawaka. Akaachana na kugonga kwa mlango na kuamua kubonyeza kengele
iliyokuwa sentimeta chache tu mbele yake. Kengele ile ilitoa mlio uliomfanya
Sindi ababaike zaidi na kurudi kinyumenyume mpaka alipogota kwenye kochi.
Jasho lilikuwa linamtoka, alichoka kutetemeka na sasa machozi
yalikuwa yakimnyemelea. Nguvu alizokuwa nazo hazikutosha hata kumpigisha hatua
moja mbele sembuse kumuondoa pale na kumkimbiza ndani. Kengele ikalia tena na
Sindi sasa akahamanika na kutoa ukelele mdogo wa hofu, akiziba masikio
asiusikie ule mlio wa kengele. Haikusaidia!
Jerry akasimama pale mlangoni akikosa uamuzi wa haraka.
Akageukia kule alikokuwa mlinzi na kutaka kumuuliza kama kulikuwa na mtu ndani
lakini akasita. Akatembea taratibu na kulifuata gari lake. Akauegemea mlango wa
dereva kwa kuulalia kwa mgongo huku mkono wake wa kushoto ukizama mfukoni na
ule wa kulia ukipeleka simu sikioni.
Akazama kwenye maongezi! kutoweka kwake pale mlangoni
kukaleta ukimya kule ndani. Ukimya uliompa nguvu Sindi. Akajikusanya hali
akiweweseka na kunyata kulifuata dirisha lile lile alilotumia kuchungulia nje.
Akajikwaa kwenye stuli iliyokuwa na ile sahani yenye chungwa alilokuwa anamenya
kabla ya ujio wa Jerry. Stuli ikayumba na kuibwaga chini sahani iliyotua kwenye
tiles kwa kelele huku chungwa likiserereka na kuingia chini ya meza.
Ukelele ule ukamfanya Jerry ainue uso na kutazama lile
dirisha lililokuwa karibu na mlango wakati Sindi aliuma midomo yake kwa nguvu
zote akiwa amefumba macho na kujichuchumisha chini kwa hofu. Kwa sekunde tano
alisali sala zote zilizomjia akilini.
Jerry akaendelea na maongezi yake kwenye simu na Sindi
akajinyanyua na kulifuata dirisha. Kwa tahadhari kubwa akalifunua tena pazia na
sasa akamuona Jerry vizuri zaidi. alisimama kwenye mwanga wa taa uliommulika
barabara. Alikuwa Jerry yule yule ila mwenye tofauti kubwa katika mavazi yake.
Alionekana kuwa kijana mwenye maisha ya juu zaidi alivyowahi hata kufikiria. Lile
wazo la Jerry kuwa mpelelezi lilipata nguvu zaidi. Moyo wake uligonga kwa kasi
mno na mawazo ya ajabu ajabu yakipita kichwani mwake!
Jerry akasimama wima akimalizia kuongea kwenye simu na kuikata.
Akampa ishara mlinzi afungue geti huku yeye akifungua mlango wa gari na
kujitoma ndani, akawasha gari lake la kisasa na kuliondoa taratibu eneo lile.
Jerry akaishia!
Sindi akashusha pumzi sasa na akili yake ikikimbizana na
maswali ambayo kwa wakati ule yalikosa majibu na uhakika pekee aliojipa ni kuwa
Jerry anamtafuta na pengine ameshajua yuko mule ndani. Akaogopa zaidi,
akababaika kupitiliza. Kwa mwendo wa kusuasua akajipeleka kwenye kochi na
kujiachia kama mzigo.
Akawaza alichoondoka nacho kwa Jerry kiasi cha kumsaka vile.
Akalishika tumbo lake dogo, tumbo lililokuwa na mimba changa ya Jerry! Moyo
wake uliokuwa ukigonga kwa nguvu nao ulipata kimuhemuhe pia, pamoja na hofu
yote iliyomtembelea dakika chache zilizopita bado alitamani Jerry arejee pale
tena, akatamani arejee na yeye ajitokeze na kumvaa kwa maswali na misuto,
akatamani tu arejee tena na amchungulie tena na tena.
88888888888888888888888
Eneo la Mgahawa wa Samaki Samaki uliopo eneo la Mlimani City
lilikuwa limechangamka mno. Muda huo wa saa mbili usiku. Watu wa mataifa
mbalimbali walionekana wakifurahia maisha huku mabinti warembo walioingia na
kutoka wakiongeza nakshi katika eneo hili. Dennis Mazimbwe alikuwa mmoja wa
watu waliokuwa kwenye mgahawa huo akiongea na kucheka na baadhi ya marafiki
zake aliokuwa nao.
Simu yake ilipoita, akajitoa kando na kuipokea huku akitembea
taratibu na kuliacha mbali eneo la mgahawa. Alikuwa akiongea na Jerry Agapella
wakati ule alipokuwa ameegemea gari. Waliongea kwa kirefu na wakamalizana
kuhusu mambo yao, alipotaka kurejea akapata wazo la kuelekea ATM ya CRDB
iliyokuwa ndani ya jengo la Mlimani City.
Akakumbana na foleni ndogo iliyomfanya ageuze na kusimama nje
akiwaza cha kufanya, apange foleni au aende eneo lingine lenye ATM za benki
hiyo. Wakati akiwaza hayo, akamuona mtu aliyetokea ndani akiwa na mifuko ya
shoprite mingi. Hakutarajia kumuona mtu yule eneo lile na muda kama ule.
Akakaza macho yake kujipa uhakika zaidi na akapata! Alikuwa Rebecca Okello.
Alimtazama alivyotembea upesi upesi kuelekea eneo la maegesho
na akajikuta akimfuata nyuma. Sehemu aliyoegesha kulikuwa na kijigiza kidogo.
Rebecca alilifikia gari lake na kufungua mlango wa abiria akatua vitu vyote
alivyokuwa navyo na wakati akitaka kuufunga mlango. Simu yake iliyokuwa mkononi
sambamba na ufunguo wa gari ikaita. Akakitazama kioo cha simu na alipolisoma
jina la mpigaji akaikata na kuendelea kuweka sawa ile mifuko aliyoitua katika
kiti cha abiria. Simu ikaanza upya kuita na alipoliona jina la mpigaji likiwa
ni lile lile akatikisa kichwa chake kulia na kushoton akionesha kukereka na ile
simu. Akaiacha iite kwa sekunde tatu kisha akaikata.
akaufunga mlango wa gari na kuzunguka kuelekea upande wa
dereva. Akasimama ghafla, akichia sauti ya mshtuko huku mikono yake ikikimbilia
kukishika kifua chake kana kwamba kilitaka kumponyoka ghafla. Akahema kwa nguvu
huku akimtazama Dennis aliyekuwa amesimama karibu na ule mlango wa kuingilia
kiti cha dereva.
‘Rebecca!... why?’ Dennis akaongea polepole asijali sana ule
mshtuko aliomletea mwenzake kwa kusimama pale kama kizuka.
‘umenishtua mno… what are you doing here?’ Rebecca aliuliza
akiwa bado na ile hali ya mshtuko
‘nataka kuongea na wewe… hupokei simu zangu…hujibu text…
why?’ Dennis aliuliza taratibu akimakazia macho Rebecca ambaye aliangaza huku
na kule kama vile hakutaka kuonekana na mtu yoyote akiongea na Dennis eneo lile
Wakatazamana! Rebecca akashisndwa kuhimili kutazamana kule na
aukayashusha macho katika namna ya kubabaika kidogo huku akimfuata kwa kasi
Dennis na kujaribu kumuondoa pale aliposimama ili aufungue mlango wa gari.
alifanya kosa!
Dennis Mazimbwe alikwanyua ule ufunguo wa gari toka mikononi
mwa Rebecca na kurudi nyuma hatua moja. Rebecca akajaribu kuuchukua ufunguo
wake kimabavu na kuzua hali ya kugombea ufunguo kama watoto.
‘this is not funny Dennis… nipe ufunguo wangu niondoke eneo
hili’ Rebecca akakemea na Dennis akacheka.
‘Huendi popote usipokubali kuwekana sawa na mimi…. hivi
unajua ni kwa kiasi gani umeniathiri wiki hii nzima?... sijafanya lolote la
maana…’ Dennis akaongea akimtazama Rebecca usoni
‘Sijali… una maisha yako nami nina yangu… usipofanya mambo
yako ya maana … hainisumbui… wewe ni nani kwangu nijali unachofanya au
usichofanya… hebu nipe ufunguo wangu niondoke’ Rebecca alijibu kwa sauti ya
kufoka akiwa amekunjua uso. akamkaribia tena Dennis na likawa kosa lingine.
Dennis alimshika ghafla na kumuegemeza kwenye gari lake,
akiuwahi mdomo wake na kuumiliki. akambana barabara kwa sekunde mbili tu na
kumuachia huku tayari akiwa ameshatimiza azma yake. kumbusu!
Rebecca alifurukuta na hata alipoachiwa naye aliachia kofi
kali lililotua barabara shavuni mwa Dennis.
‘Stupid!... usijaribu kunigusa tena Dennis…’ akakaribia
akitaka kuuchukua ufunguo uliokuwa mkononi mwa Dennis ambaye aliukwatua mkono
wake uliokuwa na funguo hali akisuguasugua shavu lililonaswa kibao.
‘Fine!... sitakugusa tena…’ Dennis akaongea polepole kisha
taratibu akageuka na kuanza kuondoka eneo lile.
Rebecca akanyong’onyea. Alihitaji ufunguo wake. Akamtazama Dennis
alivyokuwa akizidi kupiga hatua kuelekea eneo lingine la maogesho akahisi
alitaka kuondoka.
akajikuta tu akimfuata kule alikokuwa anaelekea na mpaka
anamfikia, Dennis alishalifikia gari lake na kusimama kando akimtazama Rebecca
‘Dennis Please!... nachelewa kwangu…’ Rebecca akabembeleza
‘Si mimi ninayekuchelewesha…. we need to talk Rebecca…
hatuwezi kukimbiana hivi siku zote… it kills me Becca cause I love you and I
can’t take it anymore… please naomba uni…’ akakatishwa na Rebecca
aliyemnyooshea kiganja cha mkono mithili ya tafriki anayesimamisha gari.
alimtaka anyamaze.
‘Unajua sisis sio sio watoto wala teenagers… niliona kwa
macho yangu kilichotokea kati yako na Fiona… na uliutarajia niifurahie hali
ile?...’ Rebecca alianza kuja juu
‘Na ndiyo nahitaji nafasi nijieleze Babe… ulichokiona sio
hali halisi unayowaza’ Dennis alijitetea
‘Kwa hiyo yale yalikuwa mazingaombwe si ndio?’ Akauliza kwa
sauti ya dhihaka akikusanya mikono yake na kuipishanisha chini ya matiti yake
kwa mtindo wa nibebe nikubebe.
Dennis akamtazama Rebecca kwa kituo kwanza.
‘Unanichelewesha jamani… nipe ufunguo wangu haya mazingaombwe
yako utanielelza siku nyingine… nahitaji kumuwahi mume wangu’ Rebecca
akanyoosha mkono wake wa kushoto akisubiri kupewa huo ufunguo.
Dennis hakumjibu wala hakupepepesa hata macho, aliendelea
kumtazama Rebecca na safari hii akiumizwa kidogo nay ale mashauzi ya Rebecca ya
kumtaja mume wake. Haikuwahi kutokea!
‘So unamtaja mume wako ili uniumize zaidi au ni nini?’ Dennis
aliongea kwa sauti ya kunung’unika
‘Kukuuumiza?... ni mume wangu wa ndoa… kipenzi changu… kumtaja mbele yako ni haku yangu… iwe
unapenda kusikia au hupendi kumsikia that is up to you… nipe ufunguo!’ Rebecca
alizifisha nyodo sasa na aliyaona maumivu ya Dennis waziwazi
‘Rebecca unaniambia mimi hivi?’ Dennis alihisi kuumia zaidi
‘Khaa! kwani naongea na haya magari hapa…’ akamuonyesha
magari yaliyokuwa eneo la maegesho ‘…naongea na wewe ndio!’ akahitimisha jibu
lake akimsonta Dennis kwa kidole cha shahada cha mkono wa kushoto
Dennis akainamisha kichwa chini kwa muda kisha taratibu
akainua kichwa na kumtazama Rebecca
‘Sijawahi kuwa na uhusiano na Fiona… I swear… ‘ akatikisa
kichwa na kuvua miwani yake ya macho. Rebecca akazungusha macho yake kijeuri na
kutazama pembeni akiimung’unya midomo yake
‘Nakupenda Rebecca… na unajua hilo na unajua mapenzi yangu
kwako yalivyoigharimu ndoa yangu… you know it ni kiasi gani tumemuumiza
Daniella… nikaubeba msalaba wote ili kuitunza ndoa yako… is it fair kuongea
unachoongea hapa?’ Dennis aliongea kwa unyonge mno na kwa hisia kali
‘Unanipigia kelele Dennis… nini kilichokuumiza?.... kumtaja
mume wangu?... yeaaah! Okello is my husband and I love him mno… na ndio ananimiliki
kihalali…unipe ufunguo nimuwahi mume wangu…’ akairudia kauli yake kwa nyodo
zaidi akijua ni kiasi gani alimuumiza mwenzake. alikuwa analipa kisasi cha
maumivu aliyoyasikia yeye alipowakuta na Fiona Agapella.
‘Rebecca!... umekuwaje?....’ Dennis hakuamini
‘hebu nipe ufunguo’ akaamrisha
‘Wait… Do you love me?’ Dennis akauliza akiwa amehamanika
‘No!... nikupende kama nani?... wewe ni nani kwangu
nikupende?...’
‘Kweli?... Rebecca aunaongea hivi?... sababu tu umemkuta
Fiona ofisini akanibusu shavuni?....
like seriously?...’ Dennis aliweweseka
‘Busu?... you guys mlikuwa meshikana… na pengine nisingetokea
mngefanya unayoyafanya ofisini mule na mimi…and it means sio mimi peke yangu
ninayevuliwa mule ndani… I caught you red-handed’ Rebecca alikuja juu zaidi
‘Becca!... hivi unanichukuliaje?’ akahoji
‘Malaya!’ akajibiwa haraka tu
‘What!...ookay…fine…fine… fine’ akachachatika, akitikisa
kichwa juu chini na tabasamu lisiloeleweka likimvamia. Akashusha pumzi na kuvaa
miwani yake. Akaunyoosha mkono uliokuwa na funguo na kuuning’iniza mbele ya
Rebecca, aliyeukwanyua haraka kana kwamba alihofia ungerudi ulikokuwa.
Dennis akafungua mlango wa gari lake na kujitoma ndani.
akaufunga mlango na kuwasha gari. taratibu akampita Rebecca na kuishia zake
akimuacha mwanamama huyu akiwa na hali ya maumivu kuliko hata aliyokuwa nayo
kabla ya kuongea na Dennis. alijihisi hatia ghafla kwa vile alivyomjibu Dennis
Mazimbwe.
Pamoja na yote yaliyotokea, hakustahili kumjibu Dennis vile!
Maumivu aliyoyahisi baada ya Dennis kuondoka yalikuwa maradufu, badala ya
kujisikia fahari kwa kulipa kisasi alihisi alikuwa amejiongezea jitimai kwa
kuvuruga zaidi uhusiano wake na mwanaume aliyekuwa anampenda kupitiliza!
888888888888888888888888888
Asubuhi na mapema, jua la Karima lilishachomoza na kuleta
mwanga juu ya anga la Karima. Fiona Agapella alikuwa sebuleni kwa rafiki yake
Iloma akiongea na mtu kwenye simu. Jazba alizokuwa nazo zilitosha kabisa
kumfanya Iloma amtazame kwa mshangao na kumfuatisha kwa macho zile nenda rudi
nenda rudi alizokuwa akifanya pale mbele yake.
‘Kimeshindikana nini?... wapi?... kuna ulinzi gani mpaka
mshindwe kutumia hata sindano ya sumu… siwaelewi… kwahiyo… kitu gani?... sio
papara… sielewi nini kinachukua muda huu kutimiza kazi niliyowatuma… aaargh…
hebu fanyeni kazi acheni upumbavu’ akakata simu na kumtumbulia macho Iloma
‘…wameshindwa tena?’ Iloma akamuuliza
‘Wapumbavu hawa sijui wanaenda na mabango ya matangazo hapo
hospitali… eti ulinzi mkali sijui takataka gani… the guys are not serious…
yaani sijui nipate wapi vijana wa kazi wanaojua kazi zao… haya magumashi ndio
yamesababisha Jerry bado anaisumbua akili yangu…’ Fiona alifoka akimfuata Iloma
pale kwenye kochi na kuketi kando yake. akiirusha simu yake sofa la pili
lililokuwa kando.
‘ukute ni kweli kuhusu ulinzi…’ Iloma alitetea
‘Aaah wapi… waoga tu wale… this time wakishindwa naenda
mwenyewe’ akasema kwa kujiamini.
‘Fiona!... hebu tulia kwanza, ya Dennis umefikia wapi?’ iloma
akataka kubadili uelekeo wa mada
‘Dennis ni smart… hawezi ingia mtegoni kijinga jinga tu…
naweka sawa mitambo yangu ikimnasa kwenye kumi na nane zangu atafanya kila
ninalotaka na zaidi…’ akaongeza kujiamini
‘ Usije tu ukamblackmail mwanasheria wa watu kwa inshu za mke
wa Okello’ Iloma akaonya akigeuka na kuchuka gazeti aliloliweka kando kabla ya
ujio wa Fiona pale. Fiona akamtazama shoga yake na kucheka
‘Kwanza nimeshawatibu nadhani… all in all Dennis is hot… na
umri ule kwa muonekanano wake mwanamke yoyote lazima uvute pumzi kwanza… zaidi
ya kumtumia namtaka pia…’ Fiona akatamka kwa majidai na kumfanya Iloma aliweke
tena gazeti kando na kucheka kwa sauti
‘Nini?... you can’t be serious Fifi… unamataka Dennis?’ iloma
akakaa kiumbeya zaidi akinaba bana kicheko chake
‘Siku nyingi tu… usiniambie hujawahi kumtazama Dennis
ukamuwazia tofauti… changanya na kuolewa na zee hili yaani akibusu shavu
akaandika cheque ya pesa amemaliza… a woman needs more than that’ Fiona
alitetea tama yake
‘Hukuliona hilo kabla kumuondoa mwenzio?’ iloma akamshushua
na kumfanya Fiona amtie singi na kunyanyuka. Alitaka kuelekea ndani na simu
yake ikaita tena. Akaichukua na kuipokea.
‘Enhee… kweli?... sawa mwanangu… sawa mama… haya’ akakata
simu na kumtazama Iloma
‘Nani?’ akauliza Iloma akikunja uso
‘Mwendawazimu wangu Jenifa… hakuna linalompita asiniambie…
ananichosha tu na yeye mama mama… ingekuwa amri yangu nacho ningeshakifukuzia
mbali kule… hivi ndio vinavyomaliza sehemu ya urithi tu… akafie uko aniachie
nafasi’ akasonya zake na kuishia ndani akimuacha iloma anacheka pale kochini na
hapo hapo akisikitika pia.
8888888888888888888888
Meddy alikuwa akisoma baadhi ya vitini vilivyokuwa juu ya
meza ya kazi ya Jerry wakati akimsubiri Jerry.
akamalizana na vitini na kuchukua gazeti ambalo alilipitia juu juu kabla
ya kugeuka na kuangalia mlangoni alikoingia Jerry na sekretari wake.
Jerry akakifuata kiti chake na kuketi, akavuta droo na kutoa
faili moja kubwa aliloanza kulipekua huku akiongea na sekretari wake aliyekuwa
anaandika mambo muhimu kwenye notebook iliyokuwa mkononi mwake
‘…umesema kikao na Mr. Otoyo kiwe juma ngapi?’ sekretari
akauliza
‘Jumatano saa sita mchana’ akajibu Jerry akiwa amezamisha
macho yake kwenye faili. Akaongeza na maelezo mengine huku akinyofoa karatasi
kadhaa toka katika lile faili na kumpatia yule sekretari
‘Iwe tayari kabla ya saa kumi jioni… uitume kwa fax na risiti
zote… hakikisha idara ya fedha ina nakala husika..right?’ akampa maelezo yule
binti naye akaitikia na kuzipokea zile karatasi. Akaondoka.
‘Naomi is beautiful…’ Meddy akamsifia yule sekretari
‘Nimezungukwa na wanawake wazuri Meddy kiasi kwamba nimeanza
kusahau uzuri ni nini… Enhee! umefanikisha inshu yako bandarini’ Jerry akabadili mada hali akionekana kuwa
busy na kompyuta iliyokuwa kando yake.
‘Tuyaache yote a weka kila kitu kando… just talk to me
Jerry…najua unajaribu kumeza hisia za maumivu but kupretend kila kitu kiko poa
huku unaumia… ni hatari zaidi’ Meddy akaongea kwa sauti iliyojaa umakini na
Jerry akaacha kila kitu na kumtazama Meddy kwa kituo
‘Nifanye nini?... nilie kila tunapokutana… you told me to be
a man and that is what I’m doing right now…’ Jerry akajitetea
‘while drinking 24 hours…. hivi unadhani sijanotice uwepo wa
chupa ya pombe kali hapo chini… au unadhani manukato uliyopata yanadrive away
harufu ya pombe kinywani mwako…. Jerry!...’ Meddy alimuita rafiki yake kwa
huruma na ule uso wa Jerry uliokuwa na hali ya kujiamini ukatoweka. huzuni
ikautawala uso wake na hali halisi iliyopo moyoni mwake ikajitokeza usoni pake.
akajiinamia kwanza!
‘… najua inauma lakini utaumia zaidi ukipretend uko sawa
wakati moyoni hauko sawa’ Meddy akamsemesha
‘Nampenda Sindi… sijui nisemeje… but ni kama ameondoka na
sehemu Fulani ya mwili wangu… I love her kwa moyo wangu wote na kukubali kuwa
amenikimbia ni kitu ambacho sijui namna ya kupambana nacho… anakuja kichwani
kila dakika kila… sekunde… I’m trying…najaribu…’ Jerry akaongea kwa kusitasita
taya zake zikisigana na kuonyesha ni namna gani alipambana kiume asiangue kilio
tu.
Meddy akashusha pumzi na kupunguza ukubwa wa macho yake
kidogo, wakati huo huo akimtamza Jerry katika namna ya kumuhurumia.
alishaipitia hali ya kuachwa solemba na mwanamke aliyempenda kupitiliza lakini
kwa tukio la Jerry alihisi alichokipitia yeye kilikuwa theluthi tu ya
anachopitia rafiki yake.
Jerry akajiinamia tena kisha akanyanyua uso na kujitahidi
kutabasamu ili kuipoteza ile hali ya huzuni iliyopita kati yao
‘kaa karibu na Pamella, she will heal you baada ya muda ila
uwepo wake utasaidia kucontrol huu unywaji unaoelekea kubaya’ Meddy akatoa wazo
na Jerry akacheka kwa sauti na kujilaza kwenye kiti chake akijizungusha
taratibu kulia na kushoto
‘Nahisi ipo siku atachapana makofi na Clarita’ akasema
akicheka tena
‘na Clarita anakupenda aisee… baada ya kwenda na kurudi bado
yupo available for you… wengine mliogeshwa na mitishamba gani mlipozaliwa …
watu tunafukuzia watoto wakali kwa mitego wewe wanajileta wanajitega…’ Meddy
akatania na Jerry akacheka zaidi
‘Kismati tu… ila funga kazi ni Sindi Nalela… pamoja na yote
yeye ameweza kuniweka kando akaishia zake just like that… kwamba sikuwahi
kuingia moyoni mwake… na mimba yangu sijui ameitoa sijui ataitunza…aaah Sindi… yaani
akijitokeza leo akasema Jerry nenda kariakoo pale ukamhubirie kila mtu namna
unavyonipenda aisee niko radhi kuhubiri mapenzi yangu kwake wiki nzima’ Jerry
akalalamika na Meddy akamcheka kwelikweli
Wakachangamka sasa na kupiga stori zao mbalimbali
8888888888888888888888
Wakati Jerry na Meddy wakimzungumzia Sindi asubuhi hii.
Nyumbani kwa Dennis nako Nanny na Dennis walikuwa wakimzungumzia Sindi Nalela
pia.
‘Umegundua saa ngapi kuwa hayupo?’ Dennis aliuliza katika
hali ya kuchanganyikiwa
‘Nilipofika tu!... nilienda kumuangalia chumbani ili nimsabahi
ndio nikakuta hicho kikaratai kikisema ameondoka na tusimtafute…. cha
kushangaza akaondoka bila nguo zake… nahisi aliogopa kuulizwa na mlinzi’ Nanny akaelezea alichojua
na Dennis akachoka zaidi
‘umeongea na mlinzi?’ akauliza Dennis
‘amesema alitoka usiku…sijui kuna mgeni alikuja alipoondoka
yule mgeni naye akatoka akidai anaenda kununua soda na ndio hakumuona tena’
Nanny akazidi kumchanganya Dennis ambaye sass alikumbuka wakati alipoingia
Mlinzi alitaka kuongea naye ila hakumsikiliza. Alikuwa na jakamoyo lake
alilotoka nalo kule mlimani city alikozinguana na Rebecca. Pengine
angemsikiliza Mlinzi usiku ule labda saa
hizi wangekuwa wanajua pa kuanzia.
Dennis akamtazama Nanny kama mtu aliyechoka akili kupitiliza.
Akalegeza hata tai aliyokuwa ameikaza barabara.
Sindi Nalela alikuwa alikuwa ameondoka nyumbani kwa Dennis
Mazimbwe, akimkimbia Jerry Agapella kwa hofu kuwa angerejea kumtafuta. Laiti tu
angeliujua ukweli wa mambo ulivyo!
…. ITAENDELEA….
No comments:
Post a Comment