41
‘yaani hatutalewana humu ndani leo… kamtoe umrudishe uko uko
ulikomtoa’ sauti ya mwanamke mtu mzima ilimfikia vema Sindi Nalela pale
sebuleni alikokuwa ameketi. Sauti ilitokea chumba cha pili alichohisi kilikuwa
chumba cha kulala.
‘Mke wangu huyu binti ni sawa na tu na mwanetu Zamzam kwanini
usikae naye ukamsikiliza basi… ana matatizo makubwa sana na hapo alipo hana
makazi’ Mzee aliyemleta Sindi pale kwake aliongea kwa upole akijitahidi
kuzishusha jazba za mkewe.
‘sasa kama hana makazi sisi ndio shirika la kupokea
wakimbizi?... nenda kamtoe na kama huwezi niambie nikamng’oe mwenyewe’ sauti ya
yule mama ilijaa shari zilizomfanya Sindi atamani kumuita yule Mzee kwa sauti
ili amuage tu na kwenda kutafuta msaada mbele ya safari.
‘Una roho gani mke wangu?... binti huyu una mashaka yapi naye
hali hujasikiliza tulichoongea mpaka mimi kumleta hapa’ Mzee akazidi kujieleza
‘Sijali mliongea ama mliimba… miaka hii si miaka ya nyuma
kwamba utakaribisha usiyemjua na upokee mitume… miaka hii utakaribisha usowajua
na upokee mashetani… binadamu tumewashinda wanyama kwa unyama… fanya fanya
fanya baba kaniondolee mzigo wako huo sebuleni… wewe mwenye roho safi katafute
pa kumuweka’ Yule mama alitamka kwa sauti na akitaka sasa Sindi amsikie vizuri
‘… mwanamke mwenzio sawa na mwanao kabisaa!’ Yule Mzee
alishangaa
‘Mradi ni mtu mzima aliye sawa na mwanao anaweza pia kuwa mke
mwenzio…. nenda kamuondoe’ akakazia mama mwenye nyumba na yule mzee akaachana
na mkewe na kurudi pale sebuleni. Akampa ishara ya kumuomba Sindi amfuate kule
nje na Sindi akanyanyuka na kumfuata. Wakatoka pale varandani na yule Mzee
akasimama kama anayewaza kitu.
Alikuwa Mlinzi katika moja ya maduka yaliyokuwa karibu na
kule nyumbani kwa Dennis. Sindi Nalela alipotoka nyumbani kwa Dennis alizurura
na asijue pa kwenda. Pesa aliyokuwa nayo aliogopa hata kuipangia chumba kwa
ajili ya kulala usiku mmoja kwani hakujua ya kesho yangeendaje na mbali ya
yote, hakujua afanye nini na aende wapi.
Aliumia kuwa katika hali ile, alijuta na zaidi alihisi
kuchanganyikiwa. Akajikuta tu akitafuta mahali na kuketi huku akilia. Sala iliyokuwa
ikimtoka kimoyomoyo ilisikiwa na Mungu na akamleta Mzee Rajabu mlinzi wa eneo
alilokuwa ameketi Sindi akilia.
Mzee yule alimhurumia, akamsikiliza na kumtia moyo huku
akimpa hifadhi usiku huo. Asubuhi yake ndio hivi akamchukua na kumleta kwake
kigogo Luhanga ila mkewe hakukubaliana na wazo la kumhifadhi Sindi siku mbili
tatu.
Pale Varandani alipokuwa amesimama alikuwa akiwaza pa
kumpeleka Sindi. Hakutaka tu kumwambia aende zake. Alimhurumia kama binti yake
na kibinadamu tu aliguswa na madhila yake. Akapata wazo!
‘Twende mama’ akamsemesha Sindi aliyekuwa amesimama nyuma
yake akiwa amepakata kimfuko kidogo kilichokuwa na nguo moja na pochi yenye
pesa zake basi.
‘Unampeleka wapi sasa?’ mkewe akamuuliza wakati wakiiacha
varanda na kuingia barabarani. Mumewe hakumjibu wala hakugeuka hata kumtizama
mkewe. Akachapa mwendo na Sindi akimfuata nyuma. Wakavuka barabara na kupita
kando kando ya maduka yaliyokuwa pembezoni mwa njia. Wakanyoosha tu huku Mzee
Rajabu akisabahiana na watu kadha wa kadha waliomjulia hali au yeye kuwajulia
hali. Alionekana kufahamika eneo lile.
Wakachepuka katika kichochoro kimoja na kukaza mwendo.
wakatokezea barabara kubwa ya vumbi iliyokuwa na pilika pilika nyingi mithili
ya soko lisilo rasmi. Sindi akalazimika sasa kufanya kazi ya ziada ya kupangua
mikono ya wanaume iliyokuwa ikimgusa katika namna ya kumchokoza.
Wakanyoosha na njia ile mpaka kwenye kona iliyoungana na
barabara kubwa ya lami. Kulikuwa na baa hapo, wakaingia na yule Mzee akamtaka
Sindi aketi katika moja ya viti viliyokuwa hapo baa na amsubiri. Sindi
akatulizana kwenye kiti huku akishangaa hiki na kile kwa kuzungusha macho hapa
na pale.
Mzee Rajabu akatokomea upande ulionekana kuwa jikoni,
akapotelea uko kwa dakika kadhaa kabla ya kurudi pale alipoketi Sindi akiwa na
mwanamke nyuma yake. Sindi akasimama na kumsabahi yule mwanamke huku akimpigia
lile goti la heshima.
Alikuwa kipande cha mwanamke, mrefu, mweupe kama karatasi,
kidevu chake kikiwa na ndevu chache za mkorogo, kichwani akiwa na nywele
zilizoparazwa na dawa ya relaxer na kuzifanya ziwe kama manyoya yaliyonyeshewa.
Alikuwa na mwili tipwa uliosheheni nyama kila kona.
‘Marhaba mwanangu…za kwako?’ akaijibu salamu ya Sindi huku
akimgeukia Mzee Rajabu
‘Ndio huyu binti mwenyewe?’ akamuuliza Mzee rajabu
‘Ndio huyu!...’ Mzee akaitikia akimuonyeshea kidole Sindi
‘Mmh sasa mkeo naye kile kichwa kimejaa vumbi la mkaa wallah…
kwa akili gani ukamletee mke mwenza ndani kwa staili hii…’ yule mama akashangaa
akisonya msonyo mkali kidogo na
kumgeukia Sindi
‘Una njaa?’ akamuuliza Sindi naye akatikisa kichwa kukataa
ilhali tumbo lilikuwa likimsakama kupitiliza. Yule mama aliuona ule uongo
waziwazi na akatabasamu
‘Kachirii…we kachiri…’ akapaza sauti akiwa amegeukia kule
jikoni alikotokea na Mzee Rajabu
‘Sinasudi hebu niitie kachiri uko jikoni…’ akaagiza na
kuwageukia wageni wake.
‘Kaeni sasa mpate kifungua kinywa kwanza ndio tujue yapi ya
alifu yapi ya ujiti’ akatoa angalizo lake naye akikifuata kiti meza ya pembeni
ili kuongezea kiti pale walipokuwa wamesimama.
Wakaketi na huyo Kachiri akaja mbio mbio kuchukua oda ya
staftaha. Maongezi yakaendelea sasa. Yule mama akimhoji Sindi hiki na kile
kujiridhisha na alichoambiwa na Mzee Rajabu.
‘sasa mama… mimi msaada wangu ni kukutafutia kazi za ndani au
ndio nikufanyie mpango uuze baa hapa… kaa chini ufikirie leo, kesho unipe jibu…
nijue tunaanzia wapi… umenielewa?’ yule mama akataka uhakika kama aliyoongea
yalieleweka
Sindi akaitikia kwa kichwa akiona haya pia. Wakaletewa oda
zao na kuanza kukishambulia chakula. Moyoni Sindi akiyaona haya yote kama ndoto
tu. Alikuwa akitoka hapa na kuingia pale kama miujiza. Angalau alipata tumaini
la wapi pa kuanzia kesho yake! lakini upande mwingine wa moyo wake ulijaa mzigo
wa siri.
Alikuwa ameficha kuhusu mimba yake na alikuwa ameficha ukweli
kuhusu Jerry Agapella. Stori yake ilikuwa ni kuletwa mjini kufanya kazi na
aliyemleta amemfukuza. Akashusha pumzi akiyatupilia mbali mawazo yale na
kukishambulia chakula chake. alishaamua liwalo na liwe.
888888888888888888888888
Mzee Agapella alikuwa amechangamka asubuhi hii, akionekana
kuwa na nafuu kubwa pale kitandani alipokuwa ameketi. Daktari aliyekuwa
anamhudumia alifunga faili lake na kuhitimisha matibabu yake huku akitabasamu
‘unaweza kutoka leo au kesho asubuhi… ila uko imara kabisa
sasa…’ Dokta aliongea akimtazama Mzee Agapella
‘kuna dawa zozote ataendelea kutumia nyumbani?’ Jerry
akamuuliza daktari
‘yeah.. yeah.. zipo na baada ya wiki mbili tatu atahitajika
kufanya uchunguzi mdogo mdogo tu na kuhakiki afya yake’ dokta akajibu huku
akiaga pia na kuwaacha mtu na baba yake wenyewe.
‘umeshaongea na Pamella?’ baba yake akamtupia swali mara tu
baada ya dokta kufunga mlango
‘Baba!’ Jerry akashangaa mshangao uliotoka kwa sauti ya
kukereka
‘nalizungumza hili suala kwa mara ya ngapi Jerry?...’
‘inshu sio kwa mara ya ngapi… siko tayari kuoa sasa hivi nina
mengi baba na akili yangu ina vurugu nyingi sana…’ akajitetea
‘Mengi kama yapi Jerry?... ‘ baba yake akambana na Jerry
akamtumbulia macho baba yake akitamani kumweleza kuhusu Sindi lakini stori
ingekuwa ndefu na maswali toka kwa baba yake yangefanya siku yake iishe vibaya
mno. Akameza mate akimezea na kinachomtatiza
‘Unaona!... sioni kipingamizi chochote na zaidi mimi ndio
ninayekufanyia harusi Jerry… humpendi Pamella?’ akamuuliza swali lililougusa
moyo wake na almanusura alijibu pale pale. Akajizuia tena na kuendelea
kumtumbulia macho baba yake katika namna ya kupotea mbali kimawazo.
‘Hey!’ baba yake akamshtua
‘…Nahitaji muda zaidi baba’ Jerry akajaribu kukwepa majukumu
‘One week…’ baba yake akampa ‘deadline’ na Jerry akashusha
pumzi zake ndefu angalau akishukuru kuhitimisha maongezi yale.
‘Tukutoe leo au kesho?’ akamuuliza baba yake akibadili mada
haraka sana
‘Utakavyoona’ baba yake akamjibu akimkazia macho usoni na
Jerry akatazama pembeni, alihisi baba yake alikuwa akijaribu kuisoma akili yake
kwa wakati ule. Hakutaka kuendelea kukaa pale hata dakika moja zaidi alihisi
angebanwa zaidi kuhusu suala la kumuoa Pamella. Akaaga na kuondoka!
88888888888888888888888
Mlango wa chumba cha kulala ulifunguliwa na Pamella akaingia chumbani kwake huku mama yake
akimfuata nyuma. Pamella akaenda mpaka ilipo meza ya kujirembea na kusimama
hapo akiwa amegeuka na kumtazama mama yake kama mtu asiyeamini alichokisikia.
‘Mtapangaje vitu bila kunishirikisha?... mnajua mipango ya
Jerry?... mnajua mipango yangu?’ Pamella aliuliza akija juu
‘It is for good darling!... na Jerry ni rafiki yako wa muda
mrefu’ mama yake alijaribu kumuelewesha akimfuata mpaka pale aliposimama na
kujaribu kumshika. Pamella akapangua mikono ya mama yake na kumpita akienda
kusimama kule alikokuwa amesimama mama yake kabla ya kumfuata.
‘… I can’t believe mpaka leo hii kuna wazazi mnaamini katika
kuunganisha watu bila idhini zao…’ Pamella alilalamika
‘unataka kuniambia humpendi Jerry?’ mama yake akamuuliz
‘I love him… I love him dearly mama but niko katika mahusiano
na Patrick Mazimbwe’ Pamella akatamka kwa msisitizo na asijue nia kiasi gani
aliupasua moyo wa mama yake.
‘What!... Pam!... wait…’ mama yake alikatakata maneno na
asijue alichotaka kuongea kwa dakika zile. alifumba macho kama mtu
anayesikilizia hali Fulani ya uchungu kisha akafumbua macho na kushusha pumzi.
Akamkodolea binti yake macho ya mshangao, akiwa ameyatoa kwa upana wa kutosha.
‘darling! unaolewa na Jerry… hili sio ombi tena binti yangu…
ni taarifa tu’ Rebecca aliongea kwa msisitizo akiaanza kuchapua hatua na
kumpita binti yake ambaye naye bumbuwazi lililompata lilimfanya ageuke na
kumfuata mama yake nyuma pasipo kuongea kitu. Wakatoka wakifuatana mpaka
sebuleni ambako mama yake alichukua funguo za gari zilizokuwa juu ya meza na
kuufuata mlango wa kutokea.
‘why are you doing this to me mama?’ akamuuliza mama yake kwa
sauti ya kulalamika
‘kwasababu najua ninachoafanya!’ Rebecca akamjibu binti yake
kwa sauti iliyoonyesha dhahiri kuwa hakuwa akitania.
‘nampenda Jerry ndio but niko na Patrick na nina hakika Jerry
ana mtu anayempenda sasa…’ Pamella aliongea kwa uchungu wakati mama yake
akigusa kitasa cha mlango.
Ukimya ukapita kati yao. Pamella akimtazama mama yake na mama
yake akiitazama kitasa cha mlango kama mtu anayewaza kitu.
Taratibu akakizungusha na kuufungua mlango, akatoka pasipo
kugeuka kumtazama binti yake. Rebecca aliingia kwenye moja ya magari yaliyokuwa
yameegeshwa hapo nje ya nyumba yao na kuliingiza barabarani. Alikuwa anaelekea
ofisini kwa Dennis Mazimbwe.
Alipoingia kwenye eneo la maegesho, Rebecca alitulia garini
kwa dakika kadhaa akiwa ameulalia usukani. Alikusanya nguvu za kwenda kuongea
na Dennis. Hata alipoteremka, alishuka kinyongea mno akitembea kwa hatua za
taratibu mpaka mapokezi ambako alisabahiana na mtu wa mapokezi na kuifuata
kordo iliyokuwa inaelekea ofisini kwa Dennis. akaufikia mlango na kusimama tena
pale kwa sekunde kadhaa. Akishusha pumzi mara kadhaa kabla ya kugonga.
‘Karibu!’ sauti ya Dennis iliitikia kwa ndani mara tu
alipogonga. Akashusha tena pumzi na kukishika kitasa cha mlango. akakinyonga na
kukisukumia mbele na mlango ukatii amri na kufunguka. Akajitoma ndani!
Dennis Mazimbwe alikuwa busy na shughuli zake kwenye kompyuta
iliyokuwa mbele yake, aliinua uso wake na kumtazama Rebecca mara moja tu kisha
akazama tena kwenye kazi zake. Rebecca alitembea taratibu na kuifikia meza ya
kazi ya Dennis ambaye bado aliendelea kujikita katika ile kazi aliyokuwa
akiichapa kwenye kompyuta yake.
‘Habari yako!’ Rebecca akamsabahi na Dennis akanyoosha mkono
wake wa kushoto akimuonyesha kiti cha kuketi pasipo hata kumtazama, akaendelea
na kazi yake. Rebecca hakuketi! Dennis naye hakuacha ile kazi yake. ikakatika
nusu dakika nzima kukiwa na ukimya kati yao.
Rebecca akatikisa kichwa kuonyesha kuumizwa na ile dharaua
aliyofanyiwa na Dennis.
‘We need to talk Dennis’ akaongea taratibu akimtazama Dennis
kwa upole
‘Nimekuonyesha kiti uketi’ akajibu Dennis pasipo kumtazama
wala kuiacha kazi yake. Rebecca akashusha pumzi kwa sauti kidogo na kuketi.
Akangoja tena dakika mbili nzima na ndipo Dennis akaachana na
kazi yake na kumgeukia Rebecca.
‘Nakusikiliza’ akamsemesha Rebecca akimtazama usoni
‘Ni kuhusu Patrick…’ akaanza Rebecca na Dennis akabweua kwa
sauti ya kero akimtazama Rebecca kwa mshangao.
‘It is always about Patrick… you know what Mrs. Okello…’
Dennis aliongea kwa hasira kidogo akichukua simu yake na kuhangaika nayo,
akavuta karatasi dogo na kuandika namba kwenye karatasi hiyo kisha akaisukumia
mbele alipoketi Rebecca
‘Hizo hapo ni namba zake… talk to him!’ akaongea kwa jazba
‘Kwamba aachane na binti wa kaka yake… si ndio?’ Rebecca naye
akaja juu
‘Whatever!’ akajibu Dennis akimkodolea Rebecca macho ya
hasira
‘una uhakika?’ Rebecca naye akauliza akimtolea macho Dennis
‘ otherwise nisingetoa namba!...’ Dennis alijiamini
‘Na uko tayari Patrick amwambie Pamella ukweli kuhusu baba
yake?’ Rebecca sasa aliongea kwa unyonge kidogo
Dennis hakujibu, alifumba macho na kuinamisha kichwa chini.
Rebecca akaiokota ile karatasi na kuikunja vizuri, akaishika mkononi na kisha
taratibu akajiinua toka kitini. Wakati alipotaka kukiacha kiti Dennis akainua
kichwa na kumtazama Rebecca. alijizuia kuongea alichotaka kuongea lakini
hakuweza kujizuia kutonyanyuka toka pale kitini na kumfuata Rebecca aliyekuwa
anachapua hatua kuufuata mlango.
akamtia mikononi mwake na kumkumbatia kwa nyuma. Rebecca
akafumba macho sambamba na Dennis. Hisia zao ziliongea kwenye miili yao
iliyoshikamana. taratibu Rebecca akageuka na kumtazama Dennis usoni, wakipapasana
na kuanza kutandikana mabusu kimya kimya. Rebecca akalishika shati la Dennis na
kutenganisha vifungo na tundu lake hali mikono ya Dennis akihangaika na blauzi
ya Rebecca
‘I love you Dennis…’ sauti uliyochoka na kukatika katika kwa
mihemko ilitoka mdomoni mwa Rebecca wakati Dennis alipoitoa blauzi yake mwilini
mwake. Mchezo waliousitisha miaka michache iliyopita walikuwa wameurudisha bila
kujali hatari iliyokuwa mbele yao
888888888888888888888888888
Kwenye ile wodi aliyolazwa Mzee Agapella. Mtu aliyevalia kama
daktari anatembea kwa wasiwasi akiangalia huku na kule. Anaikatiza kordo na
kuufikia mlango wa chumba kile. Anasimama na kutoa simu yake ambayo anaipiga na
kusikiliza
‘Hakuna mlinzi yoyote leo…poa’ akataka simu na kuingia ndani
ya wodi kwa tahadhari. Moja kwa moja anakifuata kitanda cha mgonjwa na kutoa
sindano ya sumu anaichoma kwenye chupa ya drip. Sindano ile inaachia sumu
ichanganyikane na maji ya dawa yaliyokuwa katika chupa ile.
Anaitimiza kazi yake na kuharakia kutoka pasipo kuonwa na mtu
yoyote. Anatoka na kuishia zake kwenye lifti. anavua mavazi ya bandia ya udokta
na kubaki na nguo zake. anatoka na kuyafiata maegesho ambako analikuta gari
linalomgonja.
Anaingia garini na dereva ni Fiona Agapella.
‘Done?’ anamuuliza kwa shauku
‘Done!’ anaitikia kwa furaha na Fiona akapiga ukunga wa
furaha akicheka kwa sauti bila kikomo. Furaha aliyokuwa nayo muda ile
sisngewezekana kuisimulia
Alichotaka kukitimiza kilikuwa kimetimia!
.... TUKUTANE HAPAHAPA....
No comments:
Post a Comment