Katika safu yetu ya leo ya barazani… ninayo machache tu ya
kusema na wewe ndugu msomaji…
Yawezekana wewe ni mwanamke…. una kazi nzuri yenye
kukuingizia kipato… una afya njema tu inayokupa nafasi ya kuzunguka huku na kule….
una marafiki wanaoifanya siku yako iishe katika namna ya kupendeza…. lakini
huna mume pengine huna hata boyfriend ama unaye lakini maumivu anayokupatia
katika uhusiano uliopo unajihisi kama mtu mpweke sana .
Pengine unavyo vyote hivi lakini huna mtoto na unaona kama
dunia inakuonea, Mungu amekutupa!
Yawezekana wewe ni mwanaume… kazi uliyonayo si sawa na elimu
uliyoisotea… pengine maisha yako ni ya chini sana
kulinganisha na maisha ya rafiki zako… unafanya hiki na kile katika kuongeza
kipato lakini bado maisha yako hayako katika hali unayoitaka… matatizo ya
kimaisha yanakuandama kila uchao… unajihisi mpweke hujui hata ufanye nini
kuboresha hali yako… mwanamke umpendaye anaelekea kushindwa kukuvumilia…
heshima yako kama mwanaume inatetereka kwa vile maisha yako ni duni… unahisi
kuonewa, Mungu amekutupa!
Huna furaha ya kweli ndani ya moyo wako…. unasema I’m blessed
huku ndani ya moyo wako unajua unaudanganya ulimwengu kwa vile unachokitamka si
kile unachokihisi… unasema nina furaha huku uso wako umekosa nuru ya kweli
Rafiki unapaswa kushukuru kwa dhati!
Wakati ukijiona mwenye bahati mbaya na mikosi…. wakati
ukishindwa kufurahia kile kidogo ulichobarikiwa kama afya njema kumbuka kuwa
kuna watu wako kitandani kwa miaka kadhaa wakiugulia maumivu yasiyopoa… wako
hospitalini kwa miaka kadhaa kwa kukosa kiasi Fulani cha fedha kurejesha afya
zao…. kumbuka kuna watu wenye ulemavu wa maisha unaowazuia hata kuifikia elimu
uliyonao, hata kuzunguka huku na kule unakozunguka wewe… hata kuwa na marafiki
wanaoipendezesha siku yao…. hata kuwa na kazi hiyo hiyo ndogo unayoona haikufai…
Kwanini usimshukuru Mungu kwa yale aliyokubarikia?....
kwanini usiwe na furaha ya kweli kwa yale uliyonayo?... kwanini uudanganye
ulimwengu uko sawa wakati moyo wako umejaa Simanzi?... kwanini ulitunze
sononeko moyoni wakati una kila sababu ya kuamka kila asubuhi na kumshukuru
Mungu kwa hali uliyonayo!
Mungu wetu ni Mungu wa rehema… Anasikia, anasikiliza na
anajibu sawasawa na mapenzi yake! Mshukuru kwa yale aliyokupatia kwanza,
furahia yale uliyobarikiwa kwanza, utavuta hali chanya katika maisha yako.
Mungu atakupatia mengine mengi zaidi. Lakini unaponung’unika moyoni ukidhani
binadamu hawatokusikia jua Mungu anakusikia, unaposhindwa kuyafurahia maisha
yenye unafuu aliyokupatia sasa kwa jambo moja dogo tu katika maisha yako…
UNAKUFURU!
kuna watu waliopata kubarikiwa kila unalotamani na
wakavipoteza ndani ya muda mfupi tu!... Jifunze sasa kushukuru kwa dhati toka
moyoni na si kumpatia Mungu sifa ya
uongo mbele za watu kuwa amekubariki huku ndani ya moyo wako una fundo moja
kubwa la huzuni kuhusu maisha yako!
USIACHE KUMUOMBA MUNGU NA USIACHE KUMSHUKURU PIA!
Wasalaam, Laura Pettie!!
thnx sis
ReplyDeletesafi sana na asante kwa kunikumbusha hilo.
ReplyDelete