Sunday, October 27, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (44)

44
Pamoja na usiku huu kuwa wenye mvua na upepo wa kuleta usingizi mnono, kwa Sindi Nalela, usiku huu ulikuwa kama kitanzi shingoni. Matone ya mvua yaliyofanya michirizi kwenye dirisha la kioo lililokuwa limejengewa mita chache toka lilipo dari yalipita machoni mwa Sindi pasipo kutambulika akilini.


Alilala pale chini akiwa amejilaza kiubavu, akilitumbulia macho dirisha lile kule juu kana kwamba lingempatia faraja kwa kule kulitazama kwake. Akafumba macho yake taratibu na kuruhusu michirizi ya machozi iliteremke kwa ubapa. Alikuwa na majuto moyoni, alikuwa na maumivu mwilini, alikuwa na njaa tumboni. Vyote hivi kwa pamoja viliufanya usiku huu kuwa mrefu kupitiliza.

Alitaka kusali, lakini sala yake iliishia mdomoni, haikufika hata theluthi, kwikwi za kilio zilimkamata na kumfanya ajinyanyue na kujikunyata, akaikumbatia miguu yake kwa mikono yake huku akinesa kwenda mbele na kurudi nyuma. Alifanya hivi pasi kujitambua!

Njaa ilikuwa inamuuma mno, akajilaza tena kiubavu na kufumba macho kuisikilizia ile njaa. Haikuvumilika. Ilimkwangua mpaka utumbo. Ndani ya chumba kile kama stoo cha mita sita kwa sita hakukuwa na chochote zaidi ya ndoo moja aliyokisia ilikuwa mule kwa ajili ya kujisaidia. kukisia kwake kulitokana kusikia harufu ya mkojo aliyokuwa anaisikia tangu asukumiziwe mule ndani jioni ile baada ya kipigo!

Harufu ile ilimkereketa mno, litaka kutapika mara kadhaa akajikaza kupitiliza, akimuomba Mungu asiojiongezee sababu za kipigo. Mwili sasa ulianza kumtetemeka, akihisi pia kuishiwa nguvu. Sindi akalaani, akalaani moyoni, akamlaani Jerry akiuma meno na kusikiliza mkwanguo wa njaa uliompitia kwa mara nyingine. akajinyanyua tena, sasa akihisi midomo yake ikikauka sababu ya kumeza mate kwa juhudi zote ili kuituliza ile njaa. Kukauka kule kukaanza pia kumletea kiu ya maji.

‘Mungu wangu…’ akamudu kutamka kwa sauti hafifu, akishindwa kumueleza Mungu hitaji lake. mkono wake wa kuume ukanyanyuka na kuelekea kifuani pake. akajipapasa na kuitafuta rozari aliyokuwa ameivaa. Akaikamata kwa nguvu huku mkono ukimtetemeka na kufumba macho.

Akili yake ilisema na Mungu, wakati akiwa ameing’ang’ania ile rozari na mkono mwingine kulikumbatia tumbo lake. Machozi yalimtoka kwa fujo huku midomo ikimwemweseka katika namna ya kutaka kuongea, meno yake yaligongana kwa kasi mithili ya mtu aliyekuwa akisikia baridi. Akaserereka taratibu na kulala kiubavu sasa akilia kwa sauti ya kuomboleza. Sindi alikuwa katika maumivu ambayo ni yeye pekee angeliweza kuyasimulia!

imani yake kwa ile rozari ilimletea muujiza. Wakati akihamanika asijue la kufanya. mlango wa kile chumba ulifunguliwa na taratibu ukasukumwa kuelekea ndani kwa tahadhari kubwa. Nguvu ya kujiinusha tena hakuwa nayo. Aliukodolea mlango kwa huruma akiwa amelegea mno. Mfunguaji akanyata na kuingia ndani kisha taratibu akaurudishia na kuja mbio kumuinamia Sindi.
‘Sindi…Sindi..’ akamuita kwa sauti ya chini sana huku akimtikisa. Sindi hakuweza hata kuitikia ule mwito. Alishaanza kusikia kizunguzungu na hali ya fahamu kumtoka. Yule aliyekuwa amemuinamia alikuwa Nadina.

Kwa mikono inayotetemeka kuashiria kujawa na hofu, alimuinua Sindi na kujitahidi kumketisha kisha haraka akaingiza mkono kwenye mfuko wa sweta alilokuwa amevaa na kutoa chupa ndogo ya maji. Akaifungua kwa kasi na kujaribu kumnywesha mwenzake. Papara ya kuyaonja maji ilimfanya Sindi apaliwe na kuanza kukohoa. Nadina akamuwahi na kumfumba mdomo huku yeye akiutazama mlango kila sekunde na sala za kuomba kutokutwa pale zikimmiminika. Sindi akakohoa kwa dakika kadhaa akiwa ameushikilia mdomo wake sambamba na Nadina ili kuizuia sauti.

Alipotulia, Nadina akashusha pumzi na kujibweteka chini kama mzigo.
Wakatumbuliana macho kwa sekunde kadhaa. Nadina akimhurumia Sindi na Sindi akifarijika kumuona Nadina pale. Haraka kama mtu aliyekurupushwa akaingiza tena mkono mfukoni na kutoa kitambaa cha mkononi kilichokuwa kimefungwa kama kifurushi kidogo.

Akakifungua na kukianika mbele ya sindi. Kulikuwa na chakula ndani yake. Sindi akakivamia na kukila kwa fujo kubwa huku Nadina akitikisa kichwa kumhurumia. Ilikuwa kama mfungwa aliyeona chakula baada ya masaa kadhaa. Ndani ya dakika mbili alishakimaliza na kuokota mpaka punje za wali zilizodondoka chini.

Nadina akampatia tena maji na safari hii akayanywa vizuri bila pupa. Nguvu iliyoanza kumtoka ikaanza kurejea mwilini mwake.
‘Asante…’ akamwambia Nadina huku akimtazama usoni kama mwokozi wake
‘Shiiii’ Nadina akakiweka kidole chake cha shahada mdomo mwake akimtaka Sindi asiongee.

Akampa ishara ya kumjulisha kuwa alikuwa anaondoka na Sindi akatikisa kichwa juu chini akikubaliana naye. Nadina akachukua kile kitambaa na ile chupa ya maji na kuvirudisha kwenye mfuko wa sweta. Akamkumbatia Sindi, alipomuachia akamtazama usoni kwa sekunde kadhaa kabla ya kunyanyuka na kutoka tena kwa tahadhari.

Sindi akazungusha macho yake yalioanza tena kujaa machozi huku akipepesa kope zake kwa kasi. Angalau alitaka kutabasamu pengine kumshukuru Mungu kwa ule muujiza. mikono yake ikalikumbatia tumbo lake, akilipapasa na angalau akifarijika kuwa hakuwa peke yake katika madhila yale, alikuwa na kiumbe mwingine tumboni mwake!
888888888888888888

Asubuhi ya siku iliyofuata, danguro la Adella linaonekana kuwa busy na pilika pilika za hapa na pale, mabinti kadhaa wakiwa na mavazi ya kulalia ndani ya chumba kimoja wakisukana na wengine wakijipamba.
‘zungumza na mwenzio Nadina… hapa atakufa bure na maiti isionekane…’ mmojawapo aliyekuwa akimsuka mwenzake alimsemesha Nadina aliyekuwa ameketi kitandani akiwatazama wenzake walioitikia kila mmoja na stori yake.

‘…kuna mwingine alikuja na ubishi wa aina hii… kila akipigwa ndio kiburi juu… kila akilazwa njaa ndio jeuri juu…madam akamuunguza na pasi mapajani humu hadi huku’ akaacha kusuka na kuonyesha hizo sehemu ziliounguzwa ikiwemo sehemu za siri.

‘… umenikumbusha Samira… dah! yule dada sijui kama yu hai… alipelekeshana na madam mpakaaa… so we ongea na Sindi mwambie tu ndio ameshaingia jehanamu…’ mwingine akaitikia akizidi kumtisha Nadina

‘… atajiumiza tu kwa ubishi wa aina ile… jana ile tumekusaidia kumpelekea  chakula ni bahati tu… ungekutwa pale ungehudumia wateja kwa mwezi bila ndururu…’ huyu akaonya akikumbushia nay a jana yake.

‘cha msingi hapa unajitumaaa… siku ukipata mtu anayeeleweka unamsimulia mambo yako… anakusaidia kusepa’ ukatoka ushauri
‘kwanini hao wanaotoka wasitoe taarifa polisi?’ Nadina akauliza kwa jazba kidogo

‘Heheheee… wapi?... polisi?... weee!... hiyo kiu ya haki ingoje peponi… nenda kajieleze tu mwisho wa siku utarudi humu ndani kuanza moja ama ndio utauhama mji ndani ya saa 24…unamjua Adella wewe?...’ huyu akafafanua zaidi na mwingine akidakia

‘…hebu kwanza… jamani duniani kuna mambo kayaani jana mwenzenu niliyaona ya dunia yakanitosha nikatosh…’ akaanza mchapo akibadili mada na kuchangamsha mazungumzo
‘…kuliko ya Maria yale ya mwanaume kulia kama beberu?’ mwenzake akadakia na kufanya watu wacheke
‘Yale madogo wallah!.... bora angelia kama mbuzi ningemuelewa yule wa jana…Ashakum si matusi sijui alikuwa amefungasha nini pale kati khaaa!... yaani heheheheee mbona maumbile’ msimuliaji akacheka na kufanya wenzake nao wacheke kabla hata hajajieleza zaidi.

Ghafla wakanyamaza baada ya mlango kufunguliwa na Sindi kuzukumiziwa kati yao. Adella naye akafuatia nyuma na kusimama kwenye kizingiti cha mlango.
‘Mpeni maelezo kamili ya hapa ni wapi na mimi ni nani. sawa?’ akawauliza aliowakuta nao wakaitikia kwa kichwa. Akamtazama Sindi aliyekuwa ameangukia katikati ya chumba

‘Lady!... wewe ni kitu kidogo sana mbele ya pesa ninayoitafuta… tafaaadhali! usifanye daftari langu la dhambi mbinguni likajaa kabla ya wakati… hii iwe mara ya mwisho kusumbuana namna hii. umenielewa?’ Adella akamuuliza Sindi ambaye hakujibu wala hakumuangalia hata huyo msemaji.

Adella kfunga chumba na kutoka zake, akiwaacha wale mabinti wakisaidiana kumuondoa Sindi pale chini na kumlaza kitandani. Kila mmoja akisema lake la kuubadili msimamo wa Sindi.
888888888888888888888888

Dennis Mazimbwe alitembea kona moja mpaka nyingine, akizungumza kwa jazba kali na huyo aliyekuwa akizungumza naye kwenye simu
‘…kwanini nisiambiwe?... why?... pamoja na yote I’m still their dad… how come wanaenda vacation mbali hivyo na siambiwi lolote?’ Dennis alisimama sasa akitaka kulisikia vizuri jibu la mkewe daniella

‘sikuelewi Ella…sikuelewi… kama ni hivi we better file for  divorce Daniella… you cant do this to me… nisikilize… listen!... Ella!...Ella!...Shit!!’ akalaani baada ya kujua upande wa pili ulishakata simu kitambo. Akairusha simu kwenye kochi na kusimama pale sebuleni kama bwege.

Alikuwa amewakumbuka watoto wake na mkewe alikuwa akiwatumia kama silaha ya kumuadhibu. Alimzuia kuongea nao, aliwaweka mbali naye kwa gharama yoyote. Alishayachoka maisha yale kwa kiasi Fulani na alitaka yaishe na awe na uhakika wa kuwaona watoto kisheria kuliko maisha ya kuwa kama mke na mume huku akizuiwa kuwa karibu na watoto wake.

Akiwa bado na ile taharuki ya kugombana na mkewe, mlngo ukafunguliwa na Patrick akaingia akiwa ameongozana na Nanny. Akamsabahi lakini kinyume na alivyotarajia Dennis alimvaa mdogo wake kwa jazba.
‘and you moron stop messing around na binti wa Okello, unanisikia?’ akaongea kwa hasira  akimnyooshe amdogo wake kidole cha shahada akilikolozea lile onyo

‘hayo ni maisha yangu binafsi… kwanini unichagulie nani wa kuwa naye au kutokuwa naye?’ Patrick naye alianza kuja juu
‘nimesema uachane naye mara moja… hili sio ombi ni taarifa Pat’ Dennis sasa alikuwa akihema kwa hasira
‘hivi unaongea kama nani?’ Patrick naye akahoji, mshipa wa hasira ukipata nguvu ya kusimama
‘wewe ni mtu wa kuniuliza naongea kama nani?.... wewe ni mtu wa kuhoji mimi ni nani?’ Dennis sasa sauti yake ilipaa hewani, alianza kumfuata Patrick kwa kasi kubwa na Nanny alijua kilichofuata kingekuwa shambulio la mwili. akawahi haraka na kusimama mbele ya Patrick akimtazama Dennis usoni kwa mshangao

Una matatizo gani wewe?’ Nanny akamuhoji Dennis aliyekuwa anahema kwa nguvu sasa kiasi cha kunyanyua kifua chake juu chini
‘Next time kabla hujanijibu utumbo… make sure una kaka mwingine aliyekulea na kukufikisha hapo ulipo… toka nje!’ akamtimua mdogo wake ambaye alikuwa ameduwaa na asielewe zile jazba kali zililetwa na nani na nini.

Nanny akamgeukia Patrick na kumsihi kwa upole aondoke kuepusha shari zaidi. Kwa unyonge uliochanganyikana na mshangao Patrick akaondoka na alipoufunga tu mlango. Denni akageuza mgongo na kuanza kuondoka pale sebuleni ila Nanny akamuwahi kwa kumuita kwa sauti.

Alipogeuka alimtazama Nanny akiwa bado na ile hali ya hasira
‘hata kama anakosea kutoka  na huyo binti wa nani sijui…. huwezi kumkaripia mdogo wako kwa staili hii… huyu ni mtu mzima Dennis… Patrick sio mtoto tena’ Nanny alimlaumu na lawama zake zilimgusa Dennis akatazama pembeni, ulimi wake ukikimbilia kuligusa jino la mwisho la upande wa kushoto

‘Shughulikia hasira zako na matatizo yako na Daniella kwanza ndio uanze kuhofu kuhusu Patrick’ Nanny alimuongezea jiwe lingine
‘Najua ninachofanya Nanny…’ akajitetea akimkaribia Nanny, uso sasa ukionyesha hatia
‘kuhusu nini?... kumzuia Patrick kuwa na huyo binti kwa amri na vitisho bila kumpa sababu?’ Nanny alihoji akimtazama Dennis kama mtoto aliyekosea

‘Ni ngumu kumwambia kwa nini… nikisema tuanze kubembelezana hatanielewa…’ akajitetea zaidi
‘ila kwa mabavu ya hivi ndio atakuelewa eeh?’ nanny naye akambana zaidi na Dennis akakosa jibu la kumpa. Akajiinamia tu na asijue ajitetee vipi.

taratibu akainua uso wake na kumtazama Nanny kwa sekunde kadhaa
‘Nataka kumtaliki rasmi Daniella’ akavunja ukimya na kumshangaza Nanny aliyemtolea macho mithili ya mtu anayekabwa
‘talaka?!... Dennis…hebu njoo kwanza’ Nanny alihisi mwili ukimsisimka. akamshika mkono Dennis na kumuongoza kwenye kochi. Wakaketi wakielekeana. Uso uliojaa hofu na mshangao ulimtazama Dennis kwa huruma pia. zile mvi chache zilizoanza kuonekana kichwani pa Dennis hazikumfanya Nanny asimuone Dennis aliyemlea tangu akiwa na wazazi mpaka leo hii, tangu yeye Nanny akiwa kigoli mpaka leo hii na uzee huu uliokuwa nao.

Dennis alikuwa kama mtoto wake. Aliziona juhudi zote za Dennis kumlea Patrick wakiwa kwenye umaskini ulioletwa na ndugu waliochukua mali mpaka leo hii Dennis anaposimama kama mmoja wa wtu walio na maisha bora kabisa.
‘Kwanini?’ akamuuliza Dennis aliyekuwa  amjiinamia na Dennis akainua uso na kumtazama Nanny.

‘hanihitaji tena… amegoma kunisamehe… na sasa  ananitenga na watoto wangu kama adhabu ya kilichotokea kati yetu’ Dennis akajieleza kwa upole
‘sidhani Deni… sidhani… kama haya unayosema ni kweli hata simu yako asingepokea… umemuumiza mno Daniella… hata hii adhabu anayokupa haitoshi kutibu kidonda ulichompatia’ Nanny akaongea kwa hisia akiishika mikono yote miwili ya Dennis

‘… aliacha kila kitu kwao, amekuja hapa kuanza maisha na wewe… amevumilia dhiki ngapi na wewe… na wakati huo huo anahangaika kutafuta mtoto… baadha ya madhila yote haya anakuja kugundua wakati yeye akilala chini na wewe… akikosa usingizi kwa kutoshika mimba wewe ulikuwa na mahusiano na mtu mwingine na mbaya zaidi bado una uhusiano naye mpaka sasa… hivi hiki ulichomtendea ni haki?...’ Nanny akauliza akitikisa kichwa kwa huzuni

‘…lakini nilimtaka radhi’ akajitetea kipumbavu
‘na ukategemea kirahisi hivyo akusamehe na maisha yaendelee… umemkosesha wachumba wangapi wa maana ambao wangempa furaha maishani mwake… Dennis!... natumaini unapoidai talaka hii una uhakika na unachofanya na sio shinikizo la kuendeleza ulichokuwa unafanya na Rebecca… Mungu atakuadhibu!’ Nanny akanyanyuka na kutoka pale sebuleni akielekea jikoni na kumuacha Dennis peke yake.

Alishusha pumzi ndefu, Pamoja na mtihani wa kuwatenganisha mdogo wake na mtoto wake alikuwa na mtihani  mwingine wa kuamua kumuangukia Daniella na kumuacha jumla Rebecca. maneno ya Nanny yalikivuruga kichwa chake na kukiacha kama fuvu la mtu wa kale.
888888888888888888888888

Fiona Agapella alikuwa bustanini mchana huu akiwa anapata juisi baridi ya maembe. mkononi alikuwa na jarida moja la mitindo akilifunua kurasa baada ya kurasa, taratibu huku akinyanyua glasi ya juisi yake na kuipeleka mdomoni kisha kuirudisha mezani.

Mlio wa honi ya gari kule getini ndio uliofanya ageuze shingo yake na kutazama kule getini. Akamtazama mlinzi aliyekuwa akihangaika kufungua geti na kisha gari aina ya Toyota prado ikaingia na kwenda kuegeshwa sehemu iliyotengwa kwa maegesho.

Kama aliyelitambua lile gari, Fiona aligeuza kichwa chake na kuendelea kusoma jarida lake kana kwamba hakuona chochote cha kumshughulisha na lile gari. Mzee Agapella akateremka akisaidiwa na yule msaidizi wake, upande wa dereva akateremka Jerry Agapella na kufungua mlango wa nyuma. akatoa mifuko iliyokuwa na vitu vya baba yake kisha akafunga mlango na kuungana na msaidizi kuelekea ndani. Walipokaribia ngazi za kuelekea lango kuu la kuingilia ndani. Mzee Agapella akasita na kusimama akimtazama Fiona aliyekuwa hana hata habari nao.  kule kumtazama Fiona kukafanya Jerry Agapella na yule msaidizi nao wamtazame Fiona kule alikokuwa.

Akayaondosha macho yake kwa Fiona na kuyaleta kwenye ngazi, taratibu akianza kupandisha ngazi kuelekea ndani. Walipoingia ndani na kelele za jenifa kusikika akimlaki baba yake. Fiona akageuza kichwa chake na kutazama kule mlangoni waliokoingilia akina Jerry.

Alipatazama akiimung’unya midomo yake mithili ya mtu amung’unyaye pipi, alionyesha wazi kutofurahia shangwe aliyokuwa akiisikia mule ndani. Aliporudisha macho yake katika jarida mlango ukafunguliwa na Jerry Agapella akatoka peke yake. Akapiha hatua kadhaa kulifuata gari alilokuja nalo lakini  akahairisha na kuchukua uelekeo wa kule alikoketi Fiona.

alipomfikia, akasimama mbele yake na Fiona akaachana na jariba lake. Wakatazamana, wote wakitabasamu!
‘Long time no see’ Jerry akaanzisha mazungumzo
‘Yes son!... how have you been?’ Fiona akauliza kwa sauti ya kuvuta huku akimtazama Jerry usoni.

Jerry akatumbukiza mikono yake yote kwenye mifuko ya suruali. Akaangalia huku na kule kama mtu anayetafuta cha kuongea na hapo hapo uso wake ukionyesha hali ya tabasamu kisha akautoa mkono mmoja na kuuegemeza mezani huku yeye ajikunja kidogo na kumuelekea Fiona. Ni kama vile alitaka atakachoongea kisikike kwa Fiona tu!

‘I’m fine!... we are fine!...’ akatamka kwa majivuno
‘That is great…’ Fiona naye akajibu kwa kujiamini akisindikiza na tabasamu
‘of course… hasa kwa familia ya kikulacho ki nguoni mwako… it must be great!’ Jerry alilalaza lile neno lake la mwisho akiondoa tabasamu na kumtolea macho Fiona ambaye naye alivuta oumzi ndefu ya ndani kwa ndani na kunyanyuka.

‘Sijamfanyia lolote baya baba yako… nilifanya kila ninaloweza kumtembelea hospitali… si mlinizuia wenyewe’ Fiona aliongea kwa hasira lile tabasamu la uongo likitoka mbio na kuchanja mbuga kusikojulikana
‘ hatukukuhitaji ma’am… wanasema mchawi mpe mtoto wako akulelee… nimemrudisha mikononi mwako…’ Jerry akajibu na kugeuka, akianza kuondoka

Fiona akatoka haraka pale alipokuwa amesimama na kumfuata Jerry kwa kasi, akamfikia na kumpita kisha akasimama mbele yake
‘Stop haya mafumbo yako ya kikulacho sijui mchawi na vitu gani…. niambie usoni unalotaka kuniambia…’ akamvaa Jerry ambaye alisimama na kucheka huku akitikisha kichwa kulia na kushoto
‘nikwambie nini?... hicho unachohisi nakizungumzia ndicho ninachomaanisha… you are the devil himself’ Jerry akabwatukia na kumpita kwa kasi akilifuata gari lake. huku nyuma Fiona akawa anapayuka kwa hasira na machozi yakianza kumtoka. Jenifa ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoka na kuhoji kulikoni.

Fiona akaeleza matusi ya Jerry huku akilia kwa uchungu kama mtu aliyeumizwa mno na maneno ya Jerry. Jenifa akamuwahi kaka yake aliyekuwa anaingia garini na kuanza kuhoji uhalali wa kumtukana Fiona namna ile.

‘She is our mother Jerry… tunajaribu kurudisha amani wewe unaiondoa… una maana gani?’ Jenifa akahoji akikerwa na ile hali ya malumbano
‘Our mother?.... may be yours!...excuse me!’ akamrai jenifa asogee ili aufunge mlango wa gari. Akaliondoa gari lake na kuishia. Akimuacha Jenifa anambembeleza Fiona pale nje
888888888888888888888

Nadina na Sindi walikuwa wakinyata taratibu kwenye kordo za lile danguro, wakielekea nje. kila mara walilazimika kuchuchumaa kimya kwa sekunde kadhaa kila waposikia aina yoyote ya sauti waliyohisi ingetibua mpango wao.

Wakateremka mpaka sehemu waliyopanga kuitumia kupitia na kufanikiwa kutoka nje. nadina alitangulia mbele akihakikisha tahadhari kisha Sindi alimfuata nyuma akichechemea. Wakafika eneo waliloweka stuli na kuifunika kwa majani na takataka nyinginezo.

Nadina akamshika Sindi mikono.
‘ukisharuka usisimame… kimbia kwa kadiri unavyoweza Sindi’ Nadina aliongea kwa tahadhari lakini uso wake ulionyesha alichoongea aliaka Sindi akitimize kwa namna yoyote ile
‘Hatuwezi kwenda wote Nadi?’ Sindi aliuliza kwa huruma na Nadina akatikisa kichwa kulia na kushoto
‘Haiwezekani… nakubeba wewe ili uruke na mimi nitahitaji mtu ili niruke… please! ukisharuka kimbia Sindi… ni bora tukimuokoa huyo kiumbe tumboni kuliko wote tukifia hapa…’ Nadina aliongea kwa huruma akilishika tumbo la Sindi

Tangu Sindi Nalela alipomweleza kuhusu mimba yake. Nadina alikosa amani moyoni. Alimhurumia mno Sindi. Alitaka kumsaidia kwa kadiri alivyoweza.
‘Siwezi kukusahau Nadina…’ Sindi alisema akitokwa na machozi, wakakumbatiana!

Nadina akajitoa maungoni mwa Sindi na  kumtaka Sindi apande kwenye ile stuli. Sindi akasimama tu kama mlingoti akimtazama Nadina.
‘Sindi!’ Nadina akamtikisa akimtaka ajitoe kwenye ile hali ya simanzi na kufanya kilichowaleta pale. Sindi akajiinamia na kuendelea kulia

‘Sindi!... tutashikwa hapa…’  akamsihi tena Sindi huku akimvuta na kumuonyesha stuli. kwa unyonge akaipanda ile stuli na nadina akachuchumaa na kupitisha kichwa katikati ya miguu ya Sindi. Akajitutumua kunyanyuka huku akijishikilia kwenye ukuta uliokuwa mbele yake na kutaka kuipanda stuli.

Sindi naye alihangaika kuufikia ukingo wa ukuta na akaukamata. kujishikiza kule kwenye ukuta kukampa nguvu Nadina ya kupanda kwenye stuli na kumuwezesha Sindi kuparamia ukingo wa ukuta na hatimaye kuukalia. Sindi akageuka kumtazama Nadina huku machozi yakimtoka.

‘Ruka… ruka Sindi!’ Nadina akamuhimiza na Sindi akaruka. Kile kishindo kule nje kiliwashtua walinzi na Nadina akahisi wangekuja upande ule. akaiondoa stuli na kukimbia nayo upande uliokuwa na giza zaidi. Walinzi wale walikuja eneo lile na kuangaza huku na kule wakati Nadina akiwachungulia.

Mlinzi mmoja kaiokota rozari ya Sindi iliyokuwa imeanguka eneo lile. Nadina akafumba macho na kubana pumzi wakati akiwasikiliza wale walinzi waliokuwa wakiijadili ile rozari. Mlio wa honi kule getini ukawafanya walinzi warudi eneo la kazi na kumpa nafasi Nadina kurudi ndani.

Sindi Nalela alijiinusha taratibu akisikilizia maumivu ya mguu uliokuwa unamuuma kutokana na kule kukanyangwa na Adella wakati wa kipigo. alichechemea kwa shida  akiangaza huku na kule. Baridi ilikuwa kali mno na dalili za mvua kunyesha kama usiku uliopita zilionekana. Mwangaza wa taa uliokuwa ukiletwa na taa zilizokuwa juu ya kuta za nyumba, ulimfanya alitafute giza ili asionekane.

Akatembea kwa kuchechemea akilifuata giza na asijue aendako. Akaupeleka mkono kifuani akitarajia kuishika ile rozari lakini haikuwepo kifuani. Hamaki ikamvaa! akajipapasa kwa taharuki huku akigeuka kutazama kule alikotokea. Hakujua ameiangushia wapi!

Alitaka kurudi kuitafuta, alitaka pia kukimbia kabisa lakini mguu haukumruhusu. Akatembea kwa kujivuta zaidi huku akijikumbatia kupunguza baridi ya upepo. dakika tano mbele alifika kwenye giza la kutisha. hakuona njia wala mwanga wa kumuongoza. Manyunyu ya mvua nayo yalianza kudondoka. Akaitoa khanga aliyoifunga kiunoni na kujifunika kichwani na kuikusanya mikono yak echini ya kidevu.

Hakujua pa kuelekea. akarudi kinyume nyume mpaka alipojigonga kwenye mti na kugota hapo. Woga ukimfanya atamani kupiga yowe la kuomba msaada. Akaangaza tena akitafuta mwanga na asiuone. huku akitetemeshwa na ile mvua na baridi Sindi akaamua kuchukua uelekeo wa kulia na kutembea tu pasipo kujua aendako.

Baada ya mwendo mfupi akatokezea kwenye barabara ya changarawe na kusimama hapo akitetemeka. Mwanga wa gari uliotokea kwenye kona na kuingia barabarani ghaflani ulimfanya ayakinge macho yake kwa mkono wake wa kuume.

Gari lile aina ya Toyota Prado lilikuja usawa wake na kupunguza mwendo. Dirisha la upande wa dereva likashuka na Sindi akaonana uso kwa uso na Madam Adella!

NINI KITAFUATA!

2 comments:

  1. he jamani ee Mungu muokoe Sindi na huyu Shetani!

    ReplyDelete
  2. jamani sindiii!!!! amtafute tuu jerry amrudie tabu zote hzi za nini na alikua anaishi vizuri tuu jamani

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger