Sunday, November 1, 2015

IJUE HALLOWEEN NI NINI NA IMETOKA WAPI....


Chimbuko la Haloween na Laura Pettie.
Kwanza niwatakie heri ya mwezi mpya wa Novemba! nimerudi kublogua kwa kudonyoa donyoa tu. Tuendelee!!

Ni sherehe inayofanyika usiku wa Oktoba 31 kila mwaka! Unapoitafuta maana halisi ya sherehe hii utakutana na maana nyingi zikiwa na mrengo tofauti tofauti.

Kubwa ni  kuwa chimbuko la Halloween ni sherehe ya kipagani iliyokuwa ikifanywa na watu waitwao wacelts miaka 2000 iliyopita. Wacelts kwa miaka ya leo wanatajwa kuwa ni watu wa Ireland, Scotland, Brittany, Wales na kadhalika kwa kuwa chimbuko la lugha ya celts iko ndani ya mataifa haya.


 Wacelts walikuwa na sherehe inayoitwa Samhain inatamkwa ‘Sawin’. Sherehe iliyokuwa inahitimisha kipindi cha mavuno na kuanza kwa majira ya baridi, kuanza kwa mwaka mpya. Kipindi hicho cha baridi kilikuwa kinaitwa  ‘Darker Half of the year’  yaani kipindi cha mwaka kisicho na nuru kulingana na kalenda ya wacelts, walipoanza majira hayo walikuwa wanaanza mwaka mpya kwao.

Wacelts walikuwa wanaamini kwamba wafu wanaweza kutembea katikati ya watu walio hai. Na wakati huu walipokuwa wanamalizia mavuno na kujiandaa na majira ya baridi ya mwaka mpya, wacelts waliamini usiku huo kabla ya mwaka mpya mpaka unaowatenganisha walio hai na wafu huwa unatoweka hivyo mizimu ya wafu huja duniani tena.

Na wanaporejea husababisha majanga mengi ikiwemo kuharibu mavuno yao. Lakini pia waliamini mizimu hii inapokuja duniani tena huwasaidia watabiri kutabiri mambo yao katika mwaka huo wa baridi na giza. Waliamini wanapofanya kafara na kuacha vyakula nje ya nyumba zao au kutoa vyakula na wanyama kwa ajili ya kafara. Mizimu yenye roho nzuri itawasaidia kukivuka kipindi cha badiri salama.

Pia wacelts walitembelea makaburi ya ndugu zao, wakafanya ibada na matambiko yao wakiamini wafu wangeweza kuwatabiria yajayo. Kwa kipindi hicho watababiri walikuwa watu muhimu mno na walioaminiwa na kutumainiwa kutoa mwongozo wa mambo yajayo.

Katika kuadhimisha hii siku, watabiri hao walitengeneza moto mkubwa. Wenzetu wanaita Bonfire. Ambapo watu walijumuika kuchoma mazao na wanyama kama matambiko kwa miungu ya Wacelts.

Walipokuwa wakifanya hivi, walivaa mavazi rasmi ya kutambikia miungu… vichwa vya wanyama, ngozi za wanyama. Wengine walivaa mavazi ya kutisha ili kuwachanganya mizimu wadhani na wao ni mizimu wenzao hivyo wasiwadhuru kwa namna yoyote ile wanapokuwa nje usiku wa samhain. Wengine waliwapa hii mizimu pipi na vitu vitamu ili kuituliza isiwadhuru.


Hii ndio Bonfire

Mwaka 43 A.D ….Ngome ya Rumi  ilifanikiwa kuiweka Celtic chini ya utawala wake kwa miaka 400 (mia nne) dadeeeki!.... hivyo sherehe mbili zenye asili ya rumi ziliunganishwa na sherehe ya Samhain ya waceltic.

Sherehe ya kwanza iliyoitwa Feralia ambayo ilisherehekewa  na warumi siku za mwisho za mwezi Oktoba ambapo warumi waliadhimisha siku ya kukumbuka waliotangulia (wafu).  Na sherehe ya pili  ilikuwa ni sherehe ya heshima ya muungu wa matunda na miti aitwaye Pomona.

Alama ya Pomona ni Apple na sasa ukijumlisha hizi sherehe mbili na Samhain ya waceltic  unapata kwanini Kwenye Halloween kuna mchezo wa Bobbing apple!... huu mchezo huchezwa wakati wa Halloween hususani na watoto ambapo maji hujazwa kwenye beseni au bakuli…. Apples hutumbukizwa kwenye maji na yanapoelea kwenye maji. Unatakiwa uokote apple kwa mdomo na sio kwa mikono. Tena wengine mikono hufungwa nyuma kabisa ili usifanye udanganyifu.
Mchezo wa Bobbing Apple


Umeanza kuelewa eeh!!
On May 13 609 A.D Papa Boniface IV aliligeuza jumba la miungu ya kirumi kuwa la kikatoliki kwa heshima ya mashahidi wa imani ya kikatoliki. Inasemekana hili ndilo jumba la kwanza la kipagani kubadilishwa kuwa Kanisa la kikristo.  Aliyeunda mchoro wa jengo hili  anaitwa Marcus Agrippa aliliunda kwa heshima ya miungu wote wa kirumi.


Jengo la Rome Pantheon  ambalo mpaka leo lipo kabisaaa
Na mbele lina chapa ya Marcus Agrippa iliyowekwa na Hadrian aliyelimalizia
Mwaka 125 CE wakati wa utawala wake.

Hii feast ya wakatoliki ya All Martyrs day ilikuja kuanzishwa rasmi na Papa Gregory III (731-741) na baadaye ikahusisha pia watakatifu pamoja na mashahidi/ mashujaa  wa imani na ikaondolewa toka May 13 na kuwa Nov 1.

Kufikia karne ya 19, ukristo ulishaenea zaidi kwenye jamii ya waceltic na kufanya waceltic waunganishe baadhi ya mila zao na mila ngeni kwao za ukristo.
Inasemekana Kanisa lilikuwa linajaribu kuiua  Samhain ya kipagani kwa kuireplace na maadhimisho yenye mrengo wa kitakatifu  kwa mfano  Souls day sijui nitafsirije uwiiii…ilisherehekewa kimfanano na Samhain. Watu walivaa kama watakatifu, malaika wakawasha bonfire pia. 

Na Siku ya watakatifu ilikuwa inaitwa all hallows au all hallowsmas  ikiwa na maana All Saints!!...sasa ule utamaduni wa usiku wa Samhain katika eneo la waceltic nao  ukaanza kuitwa All-hallow Eve na hatimaye likaja neno Halloween!!... utamaduni wa Samhain uligoma kuisha pamoja na Ukristo kuingia katika jamii ya Waceltic. Walijitahidi kuukubali ukristo hapa na pale lakini walishindwa kuacha imani zao za kipagani na hivyo wakaamua kuzichanganya changanya na ukristo kukidhi mahitaji yao!! Na ndio Samhain yao ilivyogeuka Halloween!!

Umepata jibu kwanini Halloween inahusishwa na ukristo??.... ni vile tu watu hatuelewi historia ya Halloween! Hivyo wapagani walioletewa ukristo walilichukua neno all hallows lenye  maana ya watakatifu…neno ambalo lilitumika siku ya watakatifu ya wakatoliki …. wakaliweka katika sikukuu yao ya kipagani na hatimaye wakapata jina lao la Halloween!!



Wahamiaji toka maeneo ya Waceltic walipohamia bara la Amerika, waliingiza utamaduni wa Halloween pia. Ndio hivi leo hata wamarekani wanaadhimisha Halloween.

Ilipoingia Amerika, Halloween ilibadilika taratibu. Safari hii maadhimisho yaliongezewa manjonjo kama michezo, na sherehe ya mavuno ambapo majirani walikutana na kushea hadithi za wafu na hadithi za kutisha. Wakitembelea watabiri kusikiliza maajaliwa yao, waliburudika kwa kuimba na kucheza.
Kipindi cha karne ya 19, Amerika ilipata wahamiaji wengi zaidi. Wahamiaji hawa ambao wengi walitoka Ireland ambao walikuwa wanakimbia janga la ukame mwaka 1846, walisaidia kuongeza umaarufu wa Halloween kwa kuwa ni watu waliotoka katika jamii ya waceltic.
Waamerika nao wakaanza kuvaa mavazi ya Halloween wakipita nyumba hadi nyumba kuomba chakula na pesa kama sehemu ya kusherehekea Halloween. Kumbuka utaratibu huu ulitoka kwa waceltic ambao walipita nyumba hadi nyumba wakiomba mazao na wanyama ili wakatoe kafara zao kipindi kileee mwanzo.
Utaratibu huu ndio ukaja kuwa Trick and treat ya leo inayofanyika Halloween. Trick and treat ni kwamba watoto wanapita nyumba hadi nyumba wakikusanya pipi, biskuti wengine wanatoa pesa. Trick ni kitisho tu kuwa usipotoa watakufanyia mazingaombwe. Treat ndiyo hiyo unawapa ili wasikufanyie mazingaombwe hahahahaaa!!


utamaduni wa Trick and treat ambapo watoto hupita kukusanya vitu
Miaka ya 1800 mwishoni, Halloween ilianza kubadilika zaidi. Ikajumuisha jamii kwa ujumla ambapo ikawa kama get together party…yaani party ya pamoja zaidi kuliko mambo ya kusimuliana mambo ya wafu na mizimu au uchawi. Michezo mingine ikabuniwa. Vyakula vikaletwa pamoja, na vyombo vya habari vikaomba wazazi wapunguze mavazi ya kutisha  au michezo ya kutisha sana ili kutoshtua watoto.
Maonyo kama haya yakachangia sana kuifanya Halloween ipoteze ile sifa kubwa ya kuihusisha na uchawi na wafu.
Miaka ya 1920 – 1950 Halloween ilianza kuingia hadi mashuleni. Siku ya Halloween watoto walivaa mavazi ya ajabu ajabu, wengine wakiigiza watu maarufu, wengine wakivaa kama wanyama na kadhalika  Na ndio wakati huo trick and treat ile ndio ikapamba moto. Na hapa sasa Halloween ikawa utamaduni mpya wa waamerika mpaka leo hii!!
Leo hii Waamerika ndio wanaongoza kwa kusherehekea Halloween. Wakiipamba kwa matangazo na mbwembwe zingine nyingi za kibiashara zaidi kuliko imani maana mavazi ya Halloween yanakuwa ya kuiga watu maarufu badala ya mizimu...wengine huvaa character za wahusika katika filamu kama spiderman au Batman.
Mwaka huu nimeona wapo waliovaa kama Michelle na Obama!wengine kama Papa ili mradi vituko vitupu.
Mwaka jana... North wa Kim Kardashian alivaa kama rabbit
Na Blue Ivy wa Beyonce alivaa kama Michael Jackson

Huyu amevaa kama Batman

Ya mwaka huu.... Mtoto alivaa kama Papa LOL!!
hapo akipokea treat toka kwa rais Obama!!
Je Mkristo anapaswa kushereheka hii Halloween!...Kwa mtazama wangu binafsi jibu ni sijui! kwa kuwa binafsi siwezi lakini pia sitaki kumhukumu mtu kwa kuwa dhana nzima ya kusherehekea hii kitu imebadilika mno pamoja na  kuvaa mavazi ya kutisha hivyo sijui dhamira halisi ya mtu na hivyo nashindwa kuhukumu!... Zipo sherehe nyingi ambazo nashiriki kuziadhimisha kwa maneno na vitendo  ingawa sijui maana yake na chimbuko lake kama ni chukizo kwa Mungu ninayemuabudu. 
YAPO BADO MAELEZO MENGI SANA SANA KUHUSU HALLOWEEN INAVYOSHEREHEKEWA LEO CHANZO CHAKE na  Kuhusu kutumika kwa maboga yaliyowashataa ndani yake na kadhalika
NILITAKA TU UJUE KWANZA HALLOWEEN ILITOKA WAPI.
Natumaini kuna kitu umeambulia!!
Wasalaam
Laura Pettie!!
SOURCE: Mitandao mbalimbali na vitabu


1 comment:



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger