50
Alisimama mbele ya Sindi Nalela kama binadamu aliyevukwa na
fahamu, aliyekosa utashi na kupigwa bumbuwazi. Nadina akarudi kinyume nyume kwa
hatua hafifu zilizokosa uelekeo wa maana. Macho yako yalimwemweseka katika
namna ya kuzidiwa na ile hali ya bumbuwazi, midomo yake iliyokuwa wazi ilitulia
vile vile mithili ya mtoto asubiriaye tonge la ugali. Akarudi nyuma mpaka
alipogota ukutani, mikono ikiwa kifuani pake.
Akamtumbulia macho Sindi na asijue afanye nini. Akili
iliyokwenda matembezi ghafla ikamrejea, akajikuta tu akiutafuta mlango na
kutoka mbio pasi hata kuufunga itakiwavyo. Akakimbia kwa pupa na wahaka akiangaza
huku na kule kana kwamba msaada alioutaka ungetokea popote hewani.
Mbio zake zikamfikisha mapokezi ambako, wateja wachache
walikuwa katika utulivu mkubwa wakipitia albamu na wengine wakiongea kwa simu
na wawili watatu wakiwa meza ya mapokezi. Hakujishughulisha nao kwani kwa
haraka tu alijua wateja wale walikuwa wageni eneo lile. wazoefu hakupita
mapokezi!
Akamfuata msichana mwenzake aliyekuwa hapo mapokezi na
kumsogezea uso
‘Umemuona Da’ Tima?’ akamuulizia mwanadada aliyepata kuongea
nao siku za nyuma na kuwaasa kutulia. Akili yake ilimkumbuka na ndiye hasa
aliyeona angemsaidia kwa wakati ule.
Yule msichana akatikisa kichwa kulia na kushoto, naye uso
ukionekana kutaka kujua kulikoni kutokana na
taharuki iliyokuwa ikijionyesha usoni pa Nadina. Wanaume waliokuwa
mapokezi wakamtupia jicho Nadina kwa matamanio! Hakuwajali!
Akatoka mbio kuelekea nje ya jengo la mapokezi huku nyuma
wanaume watatu wakikimbizana mapokezi kuulizia oda ya yule binti, wakakatwa
maini na jibu la kuwatosha
‘Ameshalipiwa!’
Nadina katoka nje na kusimama kwa muda akili yake ikishindwa
kwenda sambamba na nguvu ya mwili wake. alitaka kukimbia huku na kule akimsaka
Tima lakini akili yake ilimfanya asimame kwanza kwani kukimbia tu bila kujua pa
kuanzia kukimbilia kungemchosha zaidi na kumpotezea muda.
Kama mtu aliyegutushwa na kitu kilichomjia ghafla kichwani
pake, akanyanyua miguu na kutoka tena mbio kulifuata jengo la Casino. Akaingia
kwenye Casino lile na kupishana na watu waliojazana humo. Akafanya kazi ya
ziada kupangua mikono ya wanaume waliomvutia huku na kule na kufanikiwa
kupanidsha ngazi zilizokuwa zikielekea vyumba vilivyo juu. Akalifikia lango
zito la kusukuma na kulipita. Kelele za Casino zikabaki nje na utulivu wa hali
ya juu ukatawala kwenye kordo ndefu iliyopita katikati ya vyumba
vilivyotazamana.
Akatembea kwa tahadhari akiangalia namba za vyumba zilizokuwa
zimebandikwa katika kila mlango. Hakukumbuka sawia namba aliyopewa na Tima
mwenyewe siku ile. Akapiga ishara ya msalaba, sasa akiukumbuka uwepo wa Mungu
katika hali kama hii. Sala ikamtoka na asijue alisalia kitu gani. Mawazo
yalikwenda kasi mno na kumuacha mtupu kichwani. Wakati akiukaribia mlango wa
mwisho kabisa, ghafla akasikia mlango ukifunguliwa na Tima akatoka ndani ya
chumba kimoja wapo. Akiwa bado anahangaika na funguo kwenye kitasa cha mlango.
Nadina alishageuka na kutabasamu, angalau katika maisha yake aliushuhudia
muujiza wa kujibiwa sala hapo kwa papo.
Akamfuata Tima kwa kasi ya ajabu na tima akajikuta akigeuka
kumtazama Nadina vile alivyokuwa akimjia kasi
‘Unafanya nini huku?’ Tima akauliza, mashaka yake yakishindwa
kujificha na akajikuta akiangaza kordoni kama kuna mtu alikuwa anawaona
‘Nahitaji msaada wako da’ Tima’ Nadina akasema kwa unyonge
‘Nani sijui… hebu sikiliza kwanza…’ Tima akamshika Nadina mkono
na wakati huo mkono wenye funguo ukirudi kwenye tundu la mlango na kuufungua
mlango kwa kasi. Akamuingiza Nadina ndani nay eye kuingia pia. Akaufunga mlango
na kumkodolea macho Nadina.
‘kuna nini?’ akauliza Tima
‘Sindi anaumwa sana…’ Nadina akajibu kwa wasiwasi
‘Nini?... umemwambia kiongozi wenu?’ Tima akauliza naye
wasiwasi ukimzidi, alimkumbuka Sindi na alikumbuka hali yake ya ujauzito.
Nadina akakataa kwa kutikisa kichwa tu
‘Ni kuhusu mimba?’ akauliza tena
‘Mmh mmh’ Nadina akakataa kwa kuguna na kutikisa kichwa huku
akihema kwa nguvu kiasi cha kufanya mabega yake yafanye kazi ya kupanda na
kushuka.
‘sasa kuna nini?’ sauti ya Tima alipaa kidogo na akajishtukia
ghafla na kujikuta akigeuka nyuma kana kwamba alihisi kuna alimsikia
‘Sijui lakini nahisi ni zaidi ya kuumwa kawaida… sijui…
anatoka damu puani na…na .. sijui amekuwaje… ni kama ametumia kitu… sielewi’
Nadina aaliongea akirusha rusha mikono na senyensi zake zikikosa mpangilio
unaoeleweka. Aliwayawaya!
Tima akatoa macho sasa, na taratibu akashusha pumzi kwa
nguvu. Akili yake ikifanya kazi mara mbili ya kawaida.
‘Okay…twende tukamuone tujue cha kufanya but… next time
usijaribu kuingia huku bila ruhusa binti!.... umenielewa?’ akamuuliza Nadina
wakati akiufuata mlango na Nadina akaitikia tu asijali sana lile onyo kwani
kama si kumtafuta Tima wala asingewaza kuingia eneo lile. Wakatoka kwa
tahadhari na kulifuata lile lango zito. Wakatokezea kwenye Casino na kuwapita
watu wakielekea nje.
Wakakimbizana huku na kutokea kule mpaka chumbani kwa Sindi
na kumkuta akiwa amelala vile vile, damu iliyokuwa imemtoka puani alishaacha
hata hivyo ilikuwa imechuruzika vya kutosha mpaka shingoni.
Tima alisisimkwa na ile hali, almanusura apige yowe la hofu.
Akameza mate kwa juhudi kubwa kabla ya kujikaza na kumsogelea Sindi, huku
akitetemeka akaushika mkono wa Sindi uliokuwa umelala hewani ukining’inia na
kupima mapigi ya moyo. Aliyahisi kwa mbali.
‘naomba simu yako mara moja’ akamuomba Nadina simu
‘Haturuhusiwi kuwa na simu’ Nadina akajibu na akajikuta
akikumbuka alikosea mno kumuomba Nadina simu. Akajipekua kwenye suruali yake ya
jeans na kutoa simu yake, haraka akazitafuta namba za mtu aliyehitaji msaada
wake na kuongea naye.
Dakika 15 baadaye, Mwanaume mmoja mtu mzima alikuwa
akimhudumia Sindi kwenye chumba kingine. Yule Mwanaume mtu mzima alimaliza kazi
yake na kumfunika vizuri Sindi kisha akasimama na kuwageukia Tima na Nadina.
Akashusha pumzi kidogo na kuvua miwani yake ya macho.
‘amejioverdose dawa za kulevya…’ akatoa jibu la awali
‘Dawa za kulevya!!?’ Tima na Nadina wakauliza kwa mshangao,
kwa pamoja kana kwamba waliambizana waulize kwa pamoja.
‘Yes!... sijajua ni dawa gani mpaka niithibitishe maabara…
ila kwa hii huduma ya kwanza she will be okay… apate tu muda wa kupumzika zaidi
na kutuliza akili… she will be fine na atahitaji kuwa chini ya uangalizi
vinginevyo kuna hatari kubwa sana ya kumpoteza yeye na kiumbe aliyenaye
tumboni…’ Dokta akaongea kwa msisitizo akiwaacha tima na Nadina katika mshangao
mzito.
Vichwa vyao viwaza kwa pamoja… Sindi alikuwa ametoa wapi madawa?... alianza
lini?...hii ni mara yake ya kwanza?... kwanini akatumia dawa hizi ilhali
alionekana kuwa msichana mwerevu mno. mawazo yale yaliyojaa maswali vichwani
mwao yaliwafanya wamtumbulie dokta macho kana kwamba majibu ya maswali yalisomeka
usoni pa tabibu yule. Nje ya mlango wa chumba kile msichana mmoja aliyekuwa
akiwasikiliza kwa kuibia!
888888888888888888
Watoto wa Daniella na Dennis walikuwa sebuleni wakitazama
luninga, ghafla tu wakaanza kunyang’anyana
rimoti kila mmoja akitaka kutazama sehemu aliyotaka yeye na si mwenzake.
Purukushani zile zikawafanya wakimbizane kiasi cha kumkera mama yake aliyekuwa
akiandaa chakula cha baba yao mezani.
‘Hey!... imetosha sasa! weka hiyo rimoti chini na muende
vyumbani mwenu sasa hivi’
‘Mama..’ pacha mkubwa aliyeshika rimoti akataka kulalamika na
mama yake akamkata jicho kali lililomfanya ateremshe rimoti mezani na kuanza
kujongea taratibu kutoka eneo lile la sebule.
Watoto walipotokomea vyumbani, Daniella akasikia mlango
ukifunguliwa na Dennis akaingia akitokea kazini. Daniella akatabasamu na
kumfuata mumewe, akamsabahi, akampokea akimbusu mumewe shavuni. Dennis akahisi
anaota wakati akiiachia briefcase yake ichukuliwe na Daniella. Akamtazama mkewe
kwa mshangao wa waziwazi wakati akielekea chumbani na yeye kumfuata nyuma.
Kule chumbani, Daniella aliitua briefcase ya Dennis na
kumgeukia mumewe
‘ukishaoga… chakula kiko tayari mezani… niko jikoni’
akatabasamu na kutoka mule chumbani akimuacha mumewe na ile hali ya kushangaa
zaidi.
Dennis akaoga na kurudi sebuleni kwenye meza ya chakula.
Akamkuta mkewe hapo akimsubiri. Uchangamfu aliokuwa nao Daniella ulimfanya
Dennis naye achangamke kidogo ingawa alionekana kutatizika mno. Daniella
akampakulia chakula na kumpatia
‘You look beautiful Ella’ Dennis akamsifia mkewe, kwa mara ya
kwanza tangu waanza migogoro Daniella alikuwa amejipamba, alikuwa amevaa mavazi
ya kuvutia na si nguo pana pana zilizomfanya aonekane mtu mzima kuliko umri
wake.
Alikuwa amejipura usoni na kutengeneza nyusi zake, uso wake
ulitulia vizuri na nywele zake zilikuw zimetengenezwa na kuvutia mno. Alikuwa
Daniella halisi aliyemuona miaka mingi iliyopita na kuvutiw anaye! Dennis
alimtazma mkewe kama mtu asiye amini huyu aliyekuwa mbele yake alikuwa
Daniella.
‘’Thanks’ Daniella alijibu akitabasamu na aibu ya kike
ikimpitia na kuzidi kumfanya Dennis ahisi anaota. Hakukumbuka mara ya mwisho
kuiona hali ile ilikuwa lini hasa. Daniella akampatia sahani mumewe nay eye
kujipakulia. Wakala kwa furaha, wakicheka na kuongea mambo mengi ya kufurahisha.
Wakati Daniella akinyanyuka kwa ajili ya kuondoa vyombo,
Dennis akasimama na kumzuia mkewe. Wakatazamana machoni kwa sekunde za kutosha,
mboni za macho yao zikicheza kulia na kushoto… mkono wake wa kushoto uliushika
mkono wa kulia wa Daniella wakati mkono wa kulia ukiinuka na kuteleza taratibu
usoni pa mkewe akianzia mwanzo wa nywele, akaserereka na kuligusa shavu kabla
ya kukishika kidevu na kukisogeza usawa na midomo yake. Wakaumana, macho
yakikosa nguvu na kufumba, wakabusiana kimahaba na kila mmoja sasa akimshika
mwenzake na kumpapasa kwa nguvu zote. mahaba mahabani!
Daniella akajitoa maungoni mwa mumewe ghafla wakati Dennis
akionekana kuzidi kumuhitaji kupitiliza. akatembea taratibu kuondoka eneo la
kulia chakula na kuyafuata makochi. Akaketi na kumngoja Dennis amfikie na
kuketi kando yake.
Dennis akataka kumvamia tena mkewe lakini safari hii Daniella
akamzuia
‘Nahitaji kukwambia kitu Dennis’ Daniella akasema kwa sauti
ya upole tu na Dennis akatulia na kumsikiliza mkewe, alitamani Daniella aendelee
kubaki katika hali ile ile ya utulivu, abaki na lile tabasamu, abaki na ule
uzuri aliokuwa nao muda ule.
‘…tumepita misukosuko mingi sana Dennis… mimi na wewe
tumelala njaa pamoja… tumetafuta watoto kwa bidii zote pamoja… hata ulipotaka kunirudisha
kwetu kwa vile tu uliona maisha ninayoishi siyastahili… sikukubali… nilitaka
kupita na wewe hatua zote kwa vile nilikupenda na ninakupenda Dennis’ Daniella
akaongea taratibu, akimtazama Dennis machoni na kukishikilia kiganja cha mkono
wa Dennis kwa upendo..
Dennis akakosa la kusema, akatabasamu akijua wazi
aliyoyaongea Daniella yalikuwa zaidi ya ukweli.
‘… nakupenda pia Daniella’ akajitutumua kujibu.
‘…but Dennis… I think it is time to let you go!’ Daniella akapoteza
lile tabasamu sasa
‘Ella…why?... how?’ mshtuko mwanzo wa taharuki, Dennis
alimtolea macho mkewe kana kwamba alitaka ukubwa wa macho yake uwakilishe
mshtuko wake
‘Dennis!’ Daniella akamuita kumtuliza
‘…nilipogundua una uhusiano na Rebecca… nilitaka uwe uongo…uwe
uvumi tu… na ulipokataa katakata nikafarijika… lakini nilipokushika na Rebecca
ukakiri kuwa mna uhusiano… niliumia sana… sana…sana Den’ Daniella akatulia na
Dennis akajiinamia
‘…ukaomba msamaha na ukaahidi usingerudia… it took me six
months to forgive you na kurudi katika maisha ya ndoa… it was not that easy…
lakini bado Dennis… kumbe haukuachana na
Rebecca mpaka nilipokushika tena…’ Daniella sasa kawa analengwa na machozi na
Dennis alikuwa amejiinamia vile vile akisigina magego yake. Ukweli ulimuuma!
‘….nikaamua kupambana na Rebecca… unajua yoooote yaliyotokea
baada ya vita yangu na Rebecca… nilikubali kushindwa…nikaondoka na watoto… kwa
ajili ya kuwa nao karibu na kwa ajili ya kukuumiza!’ Daniella akatabasamu kwa
uchungu wakati Dennis akiinua uso na kumtazama mkewe. Alitamani kumnyamazisha!
‘… nikaendelea kukutishia kuwa ningekutaliki na usingewaona
watoto tena… I’m sorry I used our own kids kukutisha, kuendelea kukuweka karibu
nami…it was so selfish’
‘Daniella Please!’ akalalama Dennis
‘…nimesali sana Mungu anirejeshee mume wangu… airejeshe
familia yangu… sikutaka kusikiliza ushauri wa mtu kuhusu wewe… nilitaka urudi,
ukiri makosa na tuanze moja… ila naona hilo halitotokea kamwe… Rebecca
anapendwa zaidi yangu na siwezi kupambana naye tena sababu yako!... this time ameshinda
pia…I surrender!’ Daniella akauma midomo na kukusanya nguvu kisha akahitimisha
‘… now… leo hii… hapa mbele yako!... nakupa uhuru wa
kunitaliki au mimi nianze kukutaliki na ubaki na watoto endapo watataka kubaki
na wewe… sitaki kupelekana mahakamani wala kuwa na migogoro isiyoisha… nakubali
kupoteza haki zangu zote na kukuachia amani… niko tayari kuanza upya maisha
bila kujali nguvu niliyowekeza nyuma…’ Daniella akatulia akipepesa macho kuzuia
machozi yasimdondoke
‘Sitaki kukutaliki Ella’ Dennis akamudu kutamka sentensi hii
‘Una chaguzi mbili tu!... umuache Rebecca Okello kimoja na
urudi kwangu au uniache niondoke kwa amani na ubaki na Rebecca… na endapo
utachagua kubaki na mimi na ukaendelea kucheat na Rebecca na nikaujua ukweli
baadaye… adhabu pekee kwako itakuwa ni kuondoka na watoto wote wawili and never
come back again wala kutuona tena!’
Dennis akakodoa macho, masharti yale yalipita kama shoti ya umeme
mwilini. Daniella akasimama na kumbusu mumewe mdomoni.
‘You have two days to think about this honey!...’ Daniella
akagongea msumari kuhusua uamuzi wake,kisha akajiondoa taratibu na kuishia zake
akimuacha Dennis kwenye hali ya kutokujielewa. Akakumbuka barabara kauli ya
Rebecca asubuhi ya siku hiyo juu ya kujiua kama ataachwa. Akaifikiria kauli ya
mkewe ambaye ameshamuumiza mno, akawaza kutowaona watoto wake tena. Kwa sekunde
mbili tatu alizowaza haya yote alihisi mwili na roho vikiachana na kurudiana ndani
ya sekunde! Alichachatika!
8888888888888888888
Mchana wa siku iliyofuata, Ndani ya duka kubwa la mavazi ya
harusi la Marino, huyu Marino ndio yule aliyempokea Sindi na kumremba
alipoletwa na Adella kule saluni, Pamella alikuwa chumba cha kujaribishia nguo,
huku mama yake akiwa na Marino mwenyewe wakiongea na kumsubiri Pamella
ajitokeze.
Alipotokezea Marino na Rebecca wakaguna kuonyesha
kutopendezwa na lile gauni
‘No darling… this doesn’t suit you… you can do better… here
we go…’ Marino akaongea akinyanyua gauni lingine na kumpatia Pamella
‘... mama hili gauni la sita sasa unalikataa… hivi hatuwezi
kuchagua kitu simple tu jamani’ Pamella akalalamika akilikusanya lile gauni
alilovaa na kujiburuza nalo kurudi kule ndani
‘it is your specila day Pam… you have to look special dear…’
Marino akamjibia Pamella aliyebaki kucheka cheka mwenyewe. Marino aliyempelekea gauni Pamella akarudi
kwa Rebecca na kumsogelea kimbeya
‘Nasikia it is Jerry Agapella’ Marino akauliza kishambenga,
muonekano wake wa ki’gay’ ukinogesha pozi zake
Rebecca akaitikia kwa kichwa, akaitikia kifahari zaidi, jina
la Agapella halikuwa jina dogo mjini.
‘aaaaw!... Bingo!... I don’t have to miss darling…’
akashadadia Marino akitupa tupa mikono yake kike
‘No way out Marino… huwezi kukosekana the super stylist in
town’ Rebecca akampamba na wakajikuta wakigongesha mikono na vicheko juu
‘Mama… hili linabana sana tumbo.. zipu haifungi’ Pamella
akalalamika kule ndani na Marino akageuka haraka kumuwahi mteja ‘ sweet nakuja’
Marino akampoza.
Rebecca akabaki mwenyewe akiangaza angaza mpaka Marino na
Pamella walipotoka mule kwenye chumba cha kujaribia. Kwa sekunde tatu Rebecca
alimtazama mtoto wake kwa mshangao. Gauni lilikuwa limemkaa vizuri mno!
akatikisa kichwa kuitikia kuwa lile ndilo gauni lililokuwa chaguo lake.
‘this is it Pam!... ndio gauni la kuvunjia siku na kuacha
historia baby… you look amazing’ akamsifia binti yake akimfuata pale alipokuwa
amesimama akijitazama kwenye kioo cha pembeni. Wakati anamfikia mlango wa duka
ukafunguliwa na Annie, dada yake Rebecca akaingia!
‘Wow! Ma’ mkubwa Annie’ Pamella akapiga ukelele akiweweseka
kwa furaha na kumkimbilia mama yake mkubwa. Wakakumbatiana kisha Annie
akauchukua mkono wa Pamella wenye pete na kukitazama kito
‘Don’t tell me ni Tanzanite’ Annie akauliza kiushabiki
akiitazama pete ya uchumba ya Pamella
‘Yeaaah!...’ akaitikia kifahari na kukumbatiana tena kwa
furaha kisha akawafuata Marino na Rebecca na kuwasalimia kwa kuwakumbatia
‘Nimemuona mumeo kwenye picha… mzuriii..mzuri
mnooo…utamuweza? maana mjini hapa atawindwa mpaka basi au ndio mwanzo wa
ugonjwa wa moyo mwanangu’ Annie akaweka mkono wake kwenye moyo wa Pamella,
akifanya watu wacheke sasa
‘Umeingia na ndege ya saa ngapi?’ Rebecca akamuuliza
‘Niko town tangu jana mbona…. I wanted to surprise you guys…
naona sughuli imeanza’ annie akazungumza akilitazama duka juu juu
‘Na ndio tulikuwa tunakungoja wewe tujue what is next…’
Rebecca akajibu kwa shauku
‘Ni binti pekee wa Okello… hii inabidi iende kiitifaki
haswaaa… lazima tuache historia kidogo midomoni mwa watu… au sio honey?’
akamuuliza Pamella naye akaitikia kishabiki kwa furaha
‘Kabisaaaa!’
‘haya umeandaa nini?’ Rebecca akuliza naye kwa shauku
‘…tunaanza na singo party… bi harusi wetu atachuliwa na
vikorombwezo toka mombasaaaa… kisha inakuja kibao kata kuna msondo huo unatoka
lamu…’ Annie akaelezea akitamba na wenzake wakacheka
‘….enheeee!’ wakaitikia wasikilizaji
‘Then tuna kitchen party… hapa kuna mfundaji sijui mshamsikia
anaitwa Laura Pettie wenyewe tunamuita LP a.k.a msema lolote popote…’ akauliza
kwanza
‘hahahahahaa LP?... mamaaaa aunt jamani kweli?… nishamsikia
huyu dada… mambo yake super hasaaa’ Pamella akashadadia
‘LP nilimuona kwenye kitchen party ya yule mtoto wa mbunge…
nilimpenda bure kwa kweli ila nikasikia kumpata sasa shughuli…’ Rebecca
akaingilia
‘basi ndio umempata sasa… yaani niliposikia harusi tu pah!
nikasema huyu dada asikose hii shughuli kabisaaa… tutamalizia na sendoff yetu
kama kawa… usiwe na hofu mwanangu… mama zako asili yetu mombasa na shughuli
zetu unazijua… kitu classic… unakwenda
kwa mume kwa heshima zote…unaagwa kwa shughuli zote mjini… uko kwa mume wajue
hawajakuokota mtini… wala hawajakutoa ndani kama kontena bandarini… na tuwahakikishie
kwenu hujafukuzwa wala hujachokwa…ila umeagwaaa’ Annie huyu akatamba mwenyewe.
Lile dera lake la kisasa, na ule mkoba wa gharama changanya na viatu mchuchumio
wa haja… uongeze na manukato ya bei mbaya na lemba la kinaija. Picha ya nje tu
ilitosha kukwambia Annie alikuwa mama shughuli!
Vicheko vikatawala kwanza
‘Mashangazi zake wanakuja lini?’ Annie akauliza akivunja
vicheko
‘Siku moja kabla ya sendoff… watakuja na ndege kwa pamoja,
wanasubiriana Nairobi kwa baba yake mkubw Pamella’ Rebecca akajibu
‘Watakuta tushafanya yetu!’ Annie akajibu akimgeuza Pamella
kwenye kioo ili walione gauni vizuri lile gauni alilokuwa amevaa
Shughuli ya harusi ilikuwa imepamba moto mno. Na
washughulikaji ndio hawa walikuwa shughulini kuandaa shughuli.
Wakati Pamella akihangaikia gauni lake, kule kwa Jerry. Fundi
alikuwa na kazi yake.
‘… koti lifike hapa?’ fundi aliyekuja kumpima suti Jerry
aliuliza akiwa na tepu ya kupimia.
‘ shuka chini kidogo’
Jerry akajibu akiangalia vema hapo alipotaka koti la suti yake liishie.
Meddy aliyekuwa na kinywaji mkononi, akiwa amekunja nne kwenye sofa mbele ya
Jerry na fundi aliguna kuonyesha kutoridhishwa na urefu wa koti
‘hili litakuwa koti au kanzu sasa… liweke juu kidogo bwana’
akashauri na Fundi akapandisha kidogo na kuuliza ‘hapa?’
‘Eeh hapo hapo…’ Meddy akajibu na Jerry akatazama hapo
aliposhauri Meddy.
‘Okay! fanya hapo basi’ akakubali
‘… hivi mkeo ameshafanya shopping ya nguo yake?’ Meddy
akauliza
‘Sijui kwa kweli’ Jerry akajibu akigeuka kufuatiza maelekezo
ya fundi na kazi yake ya kumpima na kuandika daftarini.
‘Hapo ndipo ninapokushangaa aisee..’ Meddy akanogesha soga
‘Kwanini?’ Jerry akabweua wakati akiuliza
‘Ni harusi yako lakini wala hauna ile hali ya mshawasha kuwa
unaoa…’ Meddy akadadisi kijanja
‘Sasa ulitaka nivae bango usoni au niweke tangazo hapo getini
kuwa sasa naoa and i’m so excited?’ Jerry akauliza na kufanya fundi acheke
kichinichini na Meddy acheke kwa sauti, yeye akiweka akiba kicheko chake.
‘ ile hali inakuja automatically bwana… kwako siioni hata
kidogo’ Meddy akapingana naye
‘Kwani mtu aliye excited anakuwaje?’ Jerry akauliza akitanua
mikono hewanikupima urefu wa mikono ya suti
‘tumuulize fundi… yeye ameshapima watu wanaotarajia kuoa…
hivi kusema kweli unavyomuona huyu jamaa ni mtu anayengoja harusi yake kwa
hamu?’ Meddy akamchonoa fundi mtu mzima aliyebaki kucheka tu
‘Fundi mwenyewe amecheka tu… vile ameona huna ile furaha
inayojulikana’ Meddy akachochea mawazo yake na kumfanya Jerry atikise kichwa
tu.
Fundi akamaliza kazi yake na kuongea na mteja wake hili na
lile kisha wakaagana. Jerry akajitupa kwenye sofa na kutikisa kichwa
‘Nimechoka aisee!... yaani hapa robo tatu ya shughuli zote
zinafuatiliwa na watu lakini bado hii robo iliyobaki imenichosha mno’
akalalamika
‘… bado wiki mbili sijui… utapumzika na mamaa Pamella…
sometime siamini you guys are getting married…’ Meddy akatabasamu alipoyasema
haya akimtazama Jerry
‘Me too…’ Jerry naye akaitikia bila tabasamu bali hali ya
kuchoka zaidi
‘but be honest Jerry… hujamuwaza Sindi kabisa tangu umchumbie
Pamella?’ Meddy akajikuta akishindwa kuvumilia na kuhoji
Meddy akageuka kichovu na kumtazama rafiki yake.
‘Sio kumuwaza… I dream about her almost every single night’
akajibu akitikisa kichwa juu chini
‘Nini??!... come on
Jerry… what?!’ Meddy akaiona ile glasi ina uzani wa kilo kumi, akaitua kwenye
meza ndogo pale sebuleni na kumtazama Jerry kwa mshangao wa kutoamini
alichosikia na Jerry wala hakujishughulisha naye, ndio kwanza alishusha pumzi,
na uso wake ulioonyesha kukosa furaha ukielekea mbele ya luninga.
Meddy alikuwa akihisi alichokuwa akikiwaza kichwani mwake
kilikuwa sahihi ila kwa kukisikia toka kwa Jerry mwenyewe alipata zaidi ya
uhakika na akaona wazi uamuzi wa Jerry kumuoa Pamella ulikuwa sawa na
kulifunika bomu linalohesabu dakika kwa mikono yake mwenyewe.
88888888888888888888888
Sindi Nalela alizinduka toka kwenye usingizi mzito na kufumbua
macho yake kwa taabu. Kwa macho malegevu yalijaribu kuangalia usawa ule
alioamkia na kumuona Nadina akiwa amelala kwenye kiti kilichokuw akando yake.
Akatabasamu kivivu na taratibu lile tabasamu likatoweka, na
wakati huo akili yake ikianza kufanya kazi na kuyatambua mazingira aliyokuwemo
hayakuwa mazingira aliyoyazoea. akajilazimisha kuangalia huku na kule lakini
bado hakupatambua kwa namna yoyote.
Akataka kumuita Nadina, lakini sauti yake ikakwamia kooni na
akajikuta akimwemwesa midomo yake pasi kutoa neno. akainua mikono yake kwa
taabu na kugundua kulikuwa na drip iliyokuwa ikiingiza maji mwilini mwake.
Akashtuka zaidi na kutaka kujiinua lakini maumivu ya kichwa yakamrejesha chini
haraka sana, akitumia ule mkono mwingine kukishikwa kichwa chake. ukelele mdogo
wa kuvumilia maumivu ya kichwa ulimshtua Nadina toka usingizini.
‘Oh.. Sindi umeamka/… unajisikiaje?... sindi… Sindi’ Nadina
akamhoji Sindi akiwa ameshamfikia Sindi pale kitandani. Akataka kumporomoshea
maswali mengi kwa wakati mmoja lakini akakumbuka ushauri wa daktari kuwa
alipaswa kumuacha apumzike kwanza.
‘Kiu…maji…maji’ kwa sauti ya kukwaruza Sindi akaomba maji na
Nadina akaifuata chupa ya maji iliyokuwa kwenye mfuko kando ya kitanda na
kuitoa. Akamrudia Sindi na kujaribu kumuinusha ili aketi wima angalau,
alipomuweka sawa kidogo hukua akiwa bado amemshikilia akafungua chupa ya maji
na kuanza kumnywesha
‘
mlango ukafunguliwa kwa nguvu na Adella akaingia mule
chumbani, moja kwa moja mpaka alipo sindi, akampokonya Nadina ile chupa ya maji
na kuirushia mbali, akaushika mkono wa sindi uliokuwa na drip na kuichomoa drip
bila kujali maumivu wala utalaamu uliohitajika kuchomoa ile drip akausukumia
mbali ule mlingoti uliotengenezwa kushikilia drip. Sindi akapiga yowe la
maumivu. Wakati Adella akimsukuma Nadina kando na kummuangushia chini Sindi.
midomo ya Adella iliachia kila aina ya tusi lililomjia akilinia
Ni wakati huo ndio Tima naye aliingia kwa kasi pale na kukuta
uharibifu wa Adella huku Sindi akiwa sakafuni kama mzigo
‘Angalau mara moja katka maisha yako Adella…fanya ubinadamu!’
Tima akasema kwa uchungu wakati Adella akimtazama Sindi pale chini
‘…ubinadamu?... nimewahi kuonyeshwa ubinadamu hadi nijue
kuwaonyesha wengine?... huyu Malaya asitake kucheza na mimi kabisa…. nitakuua
we’ binti… usiniletee umajinuni kwenye biashara zangu… pesa nilizotoa kukuleta
hapa sikuzitoa uje kujiuguza sijui kudeka deka kusiko na kichwa wala miguu… you
do drugs it your problem… your damn problem!...not mine… not my business… amka
toka toka hapo chini na urejee kazini sasa hivi’ Adella akaamrisha akihema kwa
hasira
‘Anaumwa’ Nadina akamtetea na Adella akageuka na kumtazama
Nadina
‘mara moja katika maisha yako…jifunze kutokuingilia mambo
yasiyokuhusu… na alaaniwe mwanamke aliyekuzaa wewe.. kafie mbele uko’ akamuonyesha
mlango na nadina kwa woga akajitoa na kutoka nje.
Adella akamtazama Sindi pale chini
‘Simama’ akamuamrisha
Sindi akajitahidi kusimama lakini mwili haukuwa na nguvu
‘Unaleta kiburi sio?’ akamuuliza akimuamrisha tena kusimama.
Sindi akajitutumua kwa nguvu zote lakini nguvu ile aikuweza hata kumpigisha
magoti sembuse kumuinua na kumsimamamisha
Adella akamvaa Sindi na kuanza kumtandika ngumi na mateke.
Tima akampigia kelele za kumuomba amuachie lakini hakuthubutu kumgusa Adella.
Alipoona Sindi anaelemewa na kipigo cha Adella akaropoka!
‘ni mjamzito!... she is pergnant’ Tima akasema akitetemeka,
akilengwa na machozi na wakati huo huo akigeuka kumtazama Nadina aliyekuwa
nalia mlangoni.
Adella akasimama ghafla na kumtazama Tima kwa mshangao, akamkodolea macho Tima na kwa mara ya kwanza
naye akakosa la kusema kwa sekunde kadhaa. Alimtazama Tima na kukimbiza macho
kumtazama Sindi pale chini alipokuwa anatweta
‘Ana nini?’ akauliza kwa sauti kali mno, macho yakizidi
kumtoka
‘Ana mimba’ Tima akajibu kwa sauti ya chini, sauti ya kusihi
huruma, sauti ya kurai huruma, sauti ya kukata tamaa.
‘Mimba??... mimba ya nani?’ Adella bado alikuwa hajaelewa
hata moja!
‘Sijui… lakini ameingia hapa akiwa na mimba tayari’ Tima
akazidi kuweka wazi, moyo ukimuuma mno, hakutarajia angekuwa wa kwanza
kuifichua siri ile hata kidogo lakini hakuwa na jinsi.
‘Siwaelewi… it seems kuna mambo yanaendelea humu ndani wakati
bosi nikiwa sina habari… Tima… Timaa… Timaaa’ Adella akaita kwa hasira akipasa
sauti zaidi kwa kila neno alilotamka
‘Please!... angalau huyu kuwa na huruma naye… nilipoteza
mimba yangu nikiwa na miaka 16 tu… please!... muache azae… muache amshike mtoto
wake mikononi mwake… angalau tulichokosa mimi na wewe yeye akipate… najua
unajua ni kiasi gani inauma kupoteza mtoto’ Tima akaanguka chini na kupiga
magoti mbele ya Adella. Akimuombea Sindi nafasi ya kuilea mimba yake…
Adella akacheka, akacheka kicheko cha hasira, kicheko
kilichoanza kwa sauti na kuishia chini taratibu
‘…kama sikupata moyo wa kumtazama mtoto wangu usoni baada ya
kumzaa mwenyewe kwa mikono yangu… sidhani kama nina moyo wa kumuachia mwingine
apate kile nilichokosa mimi… call the doctor nowr… ana wiki moja ya kuuguza
majeraha ya abortion na atarejea kazini akiwa na nidhamu zaidi ya hii uliyonayo
wewe!’ Adella akampita Tima na kutoka nje. Akimuacha Tima akifumba macho na
kububujikwa na machozi. Nadina akimfuata Sindi kwa kasi na kulia pamoja naye.
yule yule msichana aliyekuwa akiwachungulia wakati walipokuwa wakiongea na
dokta na huyu huyu aliyekuwa akiwachungulia sasa wakiwa wanalia, umbeya wake
ulishafanya kazi!
888888888888888888888
Saa nne na vichapo kadhaa usiku, Jerry aliendesha gari
taratibu na kulisimamisha mbele ya nyumba ya Pamella. Pamella mwenyewe akiwa
garini.
‘Unatakiwa kukaa nyumbani kwa wazazi wako Pam… not all alone
like this mpaka ukichukuliwa rasmi’ Jerry aliongea akimtazama mchumba wake
Pamella ambaye alitabasamu tu na kumbusu
Jerry pajini
‘Leo nimejisikia kuwa mwenyewe… nitalala hapa kwa mara ya
mwisho then kesho nitahamia home kabisa… you are just like my dad… always
overprotective!.. I’ll be fine’ Pamella akajitetea
‘Sihofii usalama wako Pam… you have been living all alone kwa
muda mrefu… nazungumzia mila na desturi et al’ Jerry akampinga kimzaha
akimfanya Pamella acheke
‘… okay hubby to be!... nitafuata mila… kesho asubuhi
nitarudi nyumbani nitulie ndani’
Pamella akasema kimadeko akimtazmaa mchumba wake
‘,,,naaaa’ Pamella akalivuta hilo na kwa mbwembwe kisha
kuimung’unya midomo yake
‘Na nini?’ Jerry akauliza uso ukiwa na umakini
‘Na mila zinasema hutakiwi kuniona tena mpaka siku ya
sendoff’ Pamella akasema lake
‘aaah wapi.. come here’ Jerry akakataa akimvutia Pamella
kwake na kuanza kumbusu wakati huo huo Pamella akiringa na kukataa kupigwa
busu. Wakatekenyana kama watoto kisha wakatulia wenyewe.
‘… usiku mwema babe!’
Jerry akaaga na Pamella akajileta mwenyewe mbele ya Jerry na kuruhusu busu la
mdomo. Wakakumbatiana na Pamella akashuka garini
‘Thank you kwa dinner Jerry; akamshukuru akiwa anamchungulia
kwenye dirisha la mlango wa gari baada ya kushuka na kufunga mlango wa gari.
‘Mila na desturi zinasema… hupaswi kuniita Jerry tena… naitwa
mume mtarajiwa’ Jerry akamkosoa tena na Pamella akacheka kwa sauti huku
mwenzake akikosa hata tabasamu
‘Okay okay okay… asante kwa dinner mume wangu mtarajiwa…’
Pamella akashukuru tena
‘Asante kushukuru… hivi umepata gauni?’ akamuuliza akikumbuka
hiyo inshu kwani ni yeye ndiye mwenye jukumu la kulilipia
‘Yeah!... nitakupitisha dukani kwa Marino au nitakuja na
picha za gauni ulione’ Pamell akajieleza
‘Okay .. fine!... take care’ Jerry akamrushia Pamella busu la
mbali na kuwasha gari. lile tabasamu alilokuwa nalo likitoweka wakati akipangua
gia na kuingiza gari barabarani. akazama mawazoni!
Pamella akalifuata geti lake na kuingia ndani.
‘dada…’ mlinzia akamuita mara baada ya kumfungulia
‘Pumzika tu… tutaongea kesho’ akamjibu mlinzi, akilini akijua
mlinzi alitaka kuanza kumueleza shida zake ili aombepesa. alishamzoea kwa tabia
yake hii. Kwa usiku huu alihisi kuchoka mno, hakutaka kabisa kuketi pale nje kusikiliza
stori za mlinzi, akamjibu mkato akijua angempa pes hizo asubuhi bila kuhitaji
kusikia.
akatembea akitabasamu na kucheka mwenyewe baada ya kukumbuka
utani wa Jerry kuhusu mila.
Akakorokochoa mlango na kuingia ndani. akaufunga mlango na kuuondoa ufunguo
mlangoni. Kulikuwa na giza mno, mwanga wa mbalamwezi uliopita dirishani
kulikokuwa hakujazibwa na mapazia yaliyokuwa yameachwa wazi ulileta mwanga
kidogo wa kuweza kuona anakopita.
Akageuka na moyo wake ukapiga mkambi, ghafla tu alihisi
baridi mpaka kwenye mifupa, ule ufunguo aliokuwa nao mkononi ukidondoka
sambamba na pochi. aliona kiwiliwili cha mtu kwenye sofa. Moyo ulipiga mara
mbili ya kawaida na msisiko uliompitia mwilini ulimsisimua mpaka vinyweleo
kumsimama.
‘Oh Mungu wangu..’ akasema kwa hofu mkono wa kulia ukiwa
kifuani, na ule wa kushoto ukitetemeka mno na kupapasa ukutani upande huo wa kushoto ili kuifikia swichi.
Akawasha taa!
uso kwa uso na Patrick Mazimbwe!... msisimko mwingine ukapita
mwilini mwake kama shoti ya umeme.
likuwa ameketi kwenye sifa lililokuwa mbele ya Pamella,
mezani kukiwa na chupa ya pombe kali na mikononi akiwa na bastola ndogo
aliyokuwa anaitazama na kuigeuza geuza kama mtoto mdogo anayelichunguza toi
lake.
Pamella alitetemeka, lakini akatetemeka zaidi wakati Patrick
alipoinua uso wake na kumtazama usoni kwa macho makali mno huku machozi
yakimtoka. hata nguvu za kupiga yowe zilimuishia!
Jmn laura nakupenda bure ila plz ifanye jery na sind waonane kapitia mengi mno
ReplyDelete