48
Casino la Madam Adella lilikuwa na utulivu ulioambatana na
muziki wa taratibu uliokuwa ukiporomoshwa na Dj aliyekuwa zamu, taa za rangi ya
bluu na nyekundu zilimulika ndani ya Casino hilo na kuleta mchanganyiko wa
rangi uliohamasisha mahaba. Watu wengi walionekana kutulia sehemu zao huku
wahudumu waliovalia nguo fupi za kuacha sehemu kubwa ya miili yao wakihudumia
kwa kupita pita huku na kule kwa madaha.
Katikati ya casino hiyo kulikuwa na meza ya duara iliyojengewa juu kidogo, Katikati ya meza kulikuwa na mlingoti ambao
binti aliyevalia nguo maridadi za ndani alikuwa akijinyonga nyonga na kuchezea
mlingoti ule huku akifuatiza ule muziki wa taratibu, alionekana kuchota akili
za wengi mule ndani walioonekana kufurahia uchezake wake.
Pamoja na burudani ile, bado Jerry Agapella alikosa utulivu
wa nafsi. Akili yake iligoma kuona hali chanya mule ndani, akajikuta tu
akitikisa kichwa katika namna ya kusikitika na kumgeukia Meddy aliyekuwa
amezamisha akili yake kwa yule binti kule mlingotini.
‘Aisee, I’ve to go…’ akanena akimtazama Meddy ambaye
hakumsikiliza wala kumsikia.
‘Meddy!’ akaita tena kwa msisitizo wa kubweka na Meddy
akamgeukia akitabasamu, pengine kwa kudhani mwenzake alikuwa pamoja naye katika
kuburudika. Akakumbana na uso uliojaa ndita kadhaa usoni, akashangaa!
‘Vipi?!’ akauliza akishangaa na hapo hapo akitupa jicho kule
mlingotini na kisha kurudisha macho kwa Jerry. Ni kama vile hakutaka kupitwa na
miondoko ya yule binti.
‘Come on Meddy… hebu nisikilize kwanza’ Jerry aliiona ile
hali ya kupaparika kwa Meddy. Akahisi asingeeleweka bila kuulazimisha umakini
wa Meddy uhamie kwake na akafanikiwa. Meddy akajigeuza mzima mzima na kumtazama
Jerry.
‘Sioni cha kuniweka hapa… mi si shabiki wa kuangalia tupu za
wanawake maeneo kama haya Meddy…’ Jerry akaongea kwa msisitizo
‘Just a minute na binti atakuwa hapa… unakimbilia wapi?’
Meddy akamtuliza
‘Sio kukimbia, sifurahii haya mazingira… mimi sio mtu wa
makasino Meddy’ Jerry sasa aliongea kwa ghadhabu kidogo
‘Okay!... nipe dakika 15 na binti atakuwa hapa… ukishamuona
tu nitakupa funguo uondoke na gari’ akamatuliza kwa unyonge uliochanganyikana
na hali ya kutokukubaliana na Meddy akalazimika kutazama pembeni tu akikwepa
kuizamisha akili yake katika mazingira yale.
Sekunde chache tu tangu marafiki hawa wabishane, Nadina
akatokezea kwenye lango la kuingilia na kutembea kwa madaha kuifuata meza ya
akina Meddy. Robo tatu ya wanaume waliokuwa mule ndani waligeuza shingo zao
kumtazama Nadina aliyetembea taratibu, akimwagika kama mpunga unapopembuliwa, akikwatua
hatua kwa hesabu za kukokotoa, akijumlisha hatua zake kwa tabasamu mantashau.
Akakatiza meza kadhaa, akikwatua mikono ya wanaume wakware
waliokimbiza mikono yako japo kukigusa hata kiganja chake. Akawafikia akina
Meddy na kuwasabahi. Jerry akajilazimisha kutabasamu na waakti huo huo macho
yake yakionekana kumezwa na urembo wa Nadina. Alikuwa na mwanya! mwanya mdogo
uliotenganisha safu ya meno yake kiustadi kiasi cha kutamanisha aendelee
kuuweka wazi kila sekunde iendayo kwa Maulana.
‘Umelipia?’ akauliza kwa sauti laini iliyomtekenya Meddy
mpaka kwenye nyongo.
‘Yeah!... usiwe na hofu’ Meddy akajibu akitoa risiti yake na
kumpatia Nadina ambaye aliipokea a kuitazama kisha kumrudishia Meddy huku
akitabasamu tena na kuzidi kumuua mwanaume wa watu.
‘Jerry!... kutana na Nadina hapa’ Meddy akatoa utambulisho na
Jerry akatabasamu tu huku Nadina akiinamisha kichwa chake chini na kukinyanyua
kama ishara ya heshima na kuukuali utambulisho ule.
‘Mmmh!... Huyu ni rafiki yangu kipenzi anaitwa Jerry’ Meddy
akamtambulisha Jerry na Nadina akatabasamu zaidi
‘Nashukuru kukufahamu’ akatamka kwa bashasha akitanguliza
mkono wake wa kulia mbele ya Jerry ambaye naye akajikuta akiutoa mkono wake na
wakasabahiana kwa kutikisa ile mikono yao.
Maongezi ya hapa na pale yakapamba moto. Nadina alikuwa
mcheshi, mchangamfu mwenye stori za kufurahisha. Wakati wakiendelea na
mazungumzo yaliyoonekana hata kumchota Jerry. Nadina akafuatwa na mmoja wa
wahudumu na kunong’onezwa kitu sikioni. Nadina akageuka ghafla na kutazama kule
alikokuwa Dj na wakati huo mhudumu akiondoka zake. Akatabasamu na kumgeukia
Meddy
‘Nataka kuimba!’ akazungumza akiwa anajiandaa kutoka kitini.
Meddy na Jerry wakatazamana na kisha kugeuka kumtazama Nadina aliyekuwa ameshaa
nza kulifuata jukwaa tulivu lililokuwa na pazia lililomulikwa na taa kali ya
blue. Akasimama katikati ya lile jukwaa dogo akiwa na kipaza sauti kilichokuwa
kimesimamishwa katika kifaa chake. Mwanga ule ulimpendezesha zaidi.
Mara moja tu akamtupia Meddy jicho kisha akamtazama Dj
aliyekuwa kwa juu kidogo na kuitikia, ikiwa ni ishara ya kumruhusu aachie ala
za wimbo aliotaka kuuimba. Ikasikia Ala tulivu lakini iliyorindima katika
mahadhi ya muziki wa zouk. ala ile ilipaa hewani na kuvuta hisia za wengi
walioacha kila kilichokuwa mbele yao na kumtazama Nadina.
Hata Sindi Nalela aliyekuwa chumbani, aliisikia ala ile na
kufunga jarida lake kwanza, akatega sikio
‘Nadina’ akaita kwa upole akijua ni Nadina ndiye aliyetaka
kuimba. Kwa wiki nzima alikuwa akiufanyia mazoezi wimbo huo akishirikiana na
yule Dj wa casino na tayari alishauimba mara mbili kwenye casino hilo.
Akashusha pumzi na kusikilizia zaidi
Kule Jukwaani Nadina alipasua anga ghafla kwa kuanza kuimba
‘Moyo wangu… roho yangu…nafsi yangu vina maumivuuu… najaribu
najaribu kukusahau lakini maumivu yamegoma kunitoka… Eeh mungu wangu Mungu
wangu naumia japo nacheka usoni na tabasamu mdomoni…’ akaimba akivuta sauti,
akiipandisha na kuishusha kisha taratibu akasikilizia muziki ukichanganya na
kukifikia kiitikio kilichoonekana kuanza kukaririwa na baadhi ya watu waliopata
kuusikia siku mbili tatu nyuma alipouimba hapo Casino.
‘….juu ya yote ….Nenda nenda nenda na wala usiangalie
nyuma…na wala usinitafute tena na wala usinikumbuke… nimekubali kwa moyo mmoja
tuuu… kuwa sitokuwa nawe …mileleee… nenda nenda nenda na wala usiangalie
nyuma…’ akakirudia kiitikio kile kwa madaha, akiimba kwa hisia
Jerry aliyekuwa anamtazama na kumsikiliza kwa makini alihisi
kulengwa na machozi. Ilikuwa ni kama wimbo ule ulikuwa mahsusi kwake.
Alimkumbuka Sindi. Akashusha pumzi na kunyanyuka, akimgusa Meddy begani na
Meddy akageuka na kumtazama
‘usiku mwema!’ akajibu akichukua ufunguo wa gari uliokuwa
mezani na kuondoka taratibu, akimuacha Meddy anamatazama tu. Jerry akatoka
mpaka kwenye maegesho na kusimama hapo, akafumba macho na kusikitika.
‘Sindi uko wapi mama?’ akaongea mwenyewe akionekana wazi
kuumia moyoni.
Kule ndani ya Casino, Madam Adella aliyekuwa ofisini kwake
pia, alitanua pazia na kutazama kule kwenye Casino, akiona moja kwa moja pale
jukwaani. Wimbo ule ulimgusa sana, alionekana kuumia pia.
‘Binti yangu… kweli nimeenda na sikuangalia nyuma…’ akaongea
mwenyewe akifunika pazia na kurudi kitini. uso wake ukiwa na simanzi nzito. Ni
dhahiri pamoja na kumkimbia binti yake miaka mingi iliyopita lakini kama
mwanamke na mzazi, moyo wake ulikuwa na kovu la majuto na hasira dhidi ya nafsi
yake.
Kule chumbani kwa Sindi, Sindi alikuwa katika dimbwi la
machozi, alifuta machozi na kuimba sambamba na Nadina kwenye kile kiitikio
ambacho kilihitimisha wimbo na ala tu kubaki hewani.
‘Ooh Jerry…Jerry jamani…’ akaomboleza kimya kimya masikini,
maneno yale yalikuwa kama alikuwa akitamkia Jerry. Alilia akilishika tumbo
lake, akikisha kiumbe chake toka kwa Jerry Agapella. Tumaini la kumuona tena
likiwa limezimika na kupotea kabisa.
Nadina akashuka jukwaani, akipigiwa makofi na kupongezwa.
Akamfikia Meddy aliyenyanyuka na kumlaki kwa kumkumbatia. Akijisikia fahari
zaidi kuwa binti aliyepasua anga muda mfupi uliopita alikuwa wake, katika meza
yake na hilo aliliona wazi kwa namna watu walivyomkodolea macho Nadina.
‘Sipati maneno ya kutosha kuelezea ulivyo na kipaji’ Meddy
akaongea akiwa ameishika mikono yote miwili ya Nadina ambaye alibaki akicheka
kwa furaha.
Wakaongea kimahaba, wakifurahia kuwa pamoja. Wakati
wakiendelea na furaha yao, Adella akawafikia kwenye meza ile na kusimama
pembeni yao.
‘Long time no see Meddy’ akamsemesha Meddy
‘Ooh No! mbona nipo almost kila wiki…’ Meddy akajitetea
‘Umemlipia mrembo wangu?’ akauliza uso ukikosa hata tabasamu
la uongo
‘najua kila kitu kilicho hapa kinapatikana kwa cash… usijali
she is mine usiku mzima na get a bonus too…’ Meddy akajibu akilala ubavu na
kuchomoa wallet. Akatoa noti kadhaa na kuziweka mezani, akazisukuma mpaka ule
upande wa Adella na kuziacha hapo.
Adella akabinua nyusi zake juu, akionekana kushangazwa na ule
ukarimu wa Meddy. Akamung’unya midomo yake wakati akizichukua zile pesa. Wakati
akiziesabu, simu ya Meddy ikaita na akawataka radhi akinyanyuka na kwenda
kuongelea pembeni.
Adella akamtazama Nadina kwa jicho kali kidogo, kisha
akamsogelea na kumuinamia, akiweka mdomo wake usawa wa sikio, akaachia maneno
yake
‘Usije ukachanganya kazi na hisia zako binafsi… ni marufuku
na zaidi ya yote Meddy is mine...’ Akajiinua akimuacha Nadina akipoteza nuru
usoni mwake huku yeye Adella akitabasamu sasa na kumtazama Meddy aliyekuwa
anarejea pale. Akamuinamia Meddy na kumbusu shavuni, na pasipo kujua dhamira ya
Adella kufanya vile Meddy akachekelea busu lile na asijue ni kiasi gani alikua
anamsaidia Adella kudhihirisha maneno yake.
88888888888888888888888888
Usiku ule chumbani kwa Rebecca Okello, mama yake Pamella.
kulikuwa na hali ya kutokuelewana kati ya Okello na mkewe Rebecca. Walishalala
na kuzima taa lakini ugomvi wao ulifanya Mzee Okello awashe taa na kuketi kitandani akimtazama
mkewe aliyekuwa amelala kwa kumpa mgongo.
Nimekukuta unalia… nakuuliza tatizo husemi… nakugusa hutaki…
nikueleweje sasa?’ Okello alimuuliza mkewe ambaye wala hakujitikisa sembuse
kujisumbua hata kumtazama mumewe
‘Becca!’ mumewe akamuita kwa kubembeleza lakini pia
hakuitikiwa.
‘kama inshu ya Pamella na Jerry…. mtoto amekuja leo akasema
amekubali kuolewa na Jerry na ndio kitu kilichokuwa kinakuumiza… now what
Becca!.. una nini?’ Okello alikomaliza kujua tatizo la mkewe na akamfanya atupe
shuka na kujiinusha akimgeukia mumewe
‘Niache…sawa?... nina matatizo yangu’ akajitetea, macho
yakionekana kuvimba na kuvilia wekundu wa kulia
‘matatizo yapi ambayo huwezi kunishirikisha mimi mumeo?...
kama ni mamabo yenu ya upatu mmedhulumiana uko si useme upewe pesa’ Mume
akajaribu kuotea hata shida ya mkewe ili tu amuweke sawa kipenzi chake lakini
ikawa kazi bure tu
‘Zima taa tutale… Nimechoka!’ akajibu kwa ufupi akirejea
kulala alivyokuwa amelala. Okello akazima taa na kujiweka kitandani.
Wakigeuziana migongo na kuacha nafasi ya kutosha kuweka gunia kubwa la mkaa
kati ya mgongo na mgongo.
kule alikogeukia Pamella hakulala, alikuwa ameutumbulia ukuta
macho akiwaza yake.
‘That handsome man… caring… devoted husband of your age is
my husband…my husband…husband not a boyfriend!... with due respect now take
care your old man please because I’m back…. see you around!’ maneno ya
Daniella kule supermarket yalipita kichwani pake vema akiikumbuka waziwazi
dhihaka ya Daniella kwake. Akafumba macho na machozi ya hasira yakamtiririka
‘She is my wife Becca… na nahitaji kuwaona watoto wangu’ akayakumbuka
maneno ya Dennis kwake mara tu alipolalamika kuhusu Daniella. Sasa akalia kwa
kwikwi zilizoshindwa kujificha na Okello akajikuta akijiinusha na kuwasha taa
tena. Akaketi kitako
‘Becca… talk to me honey!’ akaongea akijitahidi kumgeuza
mkewe ambaye aligeuka akili na kukubali kuweka ubavuni pa mumewe aliyejitahidi
kumtuliza. Masikini bila kujua mkewe alikuwa akimlilia mwanaume mwingine
kabisa.
Rebbeca aliumia kuona wakati akijitahidi kutatua tatizo la
Pamella na Patrick ili abaki na Dennis kwa amani, tatizo lingine kubwa
limeibuka na lile la kwanza kujizima. Akaumia zaidi kuona Dennis alikuwa
anagemea upande wa Daniella sasa huku akisahau nay eye ni mke wa mtu.
888888888888888888888888
Hekaheka za usiku hii zinaishia nyumbani kwa Dennis
anayeingia kwake akiwa amelewa kiasi cha kuyumba kidogo. Anapoingia chumbani
anakuta chumba chake kitupu. Anaduwaa na kuangaza mpaka maliwatoni ambako haoni
hata kivuli cha mtu aliyetarajia kumuona. Anatoka na kukifuata chumba cha
wageni, pasipo kugonga anajaribu kufungua na kukuta mlango umefungwa kwa ndani.
Anaugonga kwa jazba, akimsihi huyu aliyendani aufungue
haraka. anapotumia nguvu zaidi kugonga na kunyonga kitasa. Daniella anafungua
na Dennis akaingia chumbani humo kwa kasi
‘what are you trying to do Ella?’ akamuuliza mkewe aliyekuwa ndani ya gauni la kulalia
‘we are no longer husband and wife… nikafanye nini chu…’
akajitetea na Dennis akamuwahi
‘Sijakutaliki Daniella… hiyo excuse yako siielewi’ Dennis
akampandishia
‘Niko hapa kwa ajili ya watoto tu… usinilazimishe mengine
nisiyotaka’ Daniella naye akaja juu
‘Watoto?... na unawajengea picha gani unapolala nje ya chumba
chako cha kulala… unawapa ujumbe gani sasa… kama upo hapa kwa ajili yao huu ni
ujumbe gani unawapa?’ Dennis hakujali tena kwamba ule ulikuwa ni usiku
usiohitaji kelele zile
‘Nimeingia humu baada ya wao kulala Dennis…ni wewe ndio
unayeleta picha isiyoeleweka… tabia zako zimenishinda…nimekuchoka Dennis…
imagine unaingia hapa ndani muda kama huu… wewe ni baba wa aina gani sasa?’
Daniella akajitetea tena na akigomba kwa sauti na ugomvi wao ukawaamsha watoto
wao waliotoka chumbani na kuja kusimama mlangoni wakati wazazi wao
wakijibishana
‘Are you guys fighting?’ mtoto mmoja akauliza na kufanya
wanandoa hawa wakatize majibizano na kuduwaa wakati wakiwatazama watoto wao
‘No!..No honey… twende mkalale…’ Daniella akajitahidi
kutabasamu akiwafuata watotot wake na kuwaongoza kurudi chumbani. Akatumia
dakika kadhaa kisha akatoka na kufunga mlango polepole.
Dennis alikuwa amesimama kwenye kizingiti cha ule mlango wa
chumba alichokuwemo Daniella. Alikuwa amejiegesha hapo akimsubiri mkewe.
Daniella naye akasimama kwenye kizingiti cha mlango aliofunga na kumtazama
Denis usoni.
‘Please Ella…’ Dennis akabembeleza na Daniella akamtazama tu
bila kujibu kitu, ni kama vile alikuwa na hasira naye ila alijikaza kutoilipua
tena muda ule. Akaingia chumbani mule alikokuwa na kutoa mto wa kulalia,
akatoka na kuelekea chumba chao cha kulala huku Dennis akimfuata nyuma.
Chumbani mule Daniella alilifuata kochi kubwa na kuweka mto
pale, kisha taratibu akalifuata shuka kitandani.
‘hapana Ella… lala tu kitandani mimi nitalala kwenye kochi’
akamsemesha mkewe aliyekubaliana na ombi lake akarejesha mto kitandani na
kupanda kitandani. Dennis akashusha pumzi za kusikitika kisha taratibu akaaanza
kutatua vifungo vya shati lake na kulivua. Mwili wake uliojengeka kiume ukawa
wazi na Daniella akamchungulia kwa kuibia, akamtazama mumewe huyu kwa upendo na
matamanio wakati akielekea bafuni. Akatabasamu hata yeye hakujua kwanini
alitabasamu!
8888888888888888888888888
Siku chache baadaye, Pamella Okello alifikia tamati y
mahusiano yake na Patrick kwa kumwambia ukweli kuwa uhusiano wao ulikuwa
umefikia mwisho. Patrick hakukubali, alitaka sababu na Pamella hakuwa tayari
kusema alikuwa mbion kuolewa na Jerry. Akamlazimisha tu kukubali kuwa uhusiano
wao umefikia kikomo.
‘Sikuelewi Pam… ghafla hivi… why?... nimekufanyia nini mpaka
unafikia uamuzi kama huu?... why?’ Patrick alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa
wakati akiongea na Pamella kwenye simu siku moja tu baada ya Pamella kumueleza
ukweli wenye kuumiza.
Pamella aliyekuwa nashuka kwenye gari nyumbani kwao, alifunga
mlango wa gari kwa mguu baada ya kuelemewa na simu sikioni, mkono mmoja ukiwa
na mifuko ya shopping. Akatembea hatua mbili tatu na kusimama kwanza
‘Patrick… nimejitahidi kuwa mkweli na muwazi… it is over…
najua inauma but nimeona ni bora kuwa mkweli kuliko kukufanyia visa bure’
akajitetea na asijue mwenzake alikuwa amechanganyikiwa kiasi gani. Patrick
akaongea mfululizo akijitetea kwa kosa ambalo hata hakulijua, Pamella akamkatia
simu na kuizima. Patrick alipoijaribu tena na kukuta imezimwa akainama kwa
uchungu, akisigina magego yake na kupambana na maumivu ya moyo kiume. Aliumia
kupita neno lenyewe maumivu!
Wakati Pamella akizozana na Patrick uku nje, kule ndani mama
yake alikuwa akigombana na Dennis kwenye simu.
‘huwezi kuniamrisha nisikupigie simu au nisikutumie meseji
Dennis… Daniella ni nani akupangie wakati wa kuwasiliana… sikuelewi…
nitatuliaje wakati naona wazi unavyoegemea kwa Daniella… sikuelewi Dennis… jana
hukupokea simu yangu… missed call 4 na ushindwe kutuma hata meseji…. usinitajie
jina la Daniella sitaki kulisikia…. so what?.... hata mimi nina mume Dennis… Dennis!...Dennis!...Dennis!’ akaita mara
kadhaa kabla ya kugundua simu ilikatwa kitambo.
Akahisi msumari wa moyo ukititia moyoni. Akaketi kwenye kochi
akiwa ameushikilia moyo wake kana kwamba ulikuwa mbioni kuchomoka na kutimua
mbio. Dennis alikuwa amemuumiza mno. akajikaza mtoto wa kike asilie, asipige
mayowe, akajikaza hasa mpaka mishipa ya shingo ikamsimama dede. Wakati huo huo
binti yake akafungua mlango na kuingia kwa furaha.
Akamfuata mama yake kwa mbwembwe pale kwenye sofa na kuketi
kando yake akitua ile mifuko kwenye meza ndogo mbele yao
‘Pale saluni kwa Marino wamefungua massage centre… mama it is
amaziiiing’ Pamella alimsemesha mama yake akitanua mfuko mmoja na kutoa
kujipeperushi kilichokuwa na maelezo kuhusu hiyo huduma, alipogeuka kumpatia
mama yake akagundua akili y mama yake haikuwa pale
‘Mama!... kuna tatizo?’ akamuuliza mama yake akimgusa pajani
kumshtua na mama yake akamgeukia taratibu na kumtazama binti yake usoni.
Alionekana wazi kuwa na maumivu ya moyo, mawazo na huzuni.
‘Mama… huzuni ya nini na nimekubali kuolewa na Jerry
uliyekuwa unamtaka!... nini tena sasa?’ akamuuliza mama yake ambaye hakumjibu
kitu. Alinyanyuka taratibu na kuanza kuchapua hatua kuelekea ndani.
Pamella akasimama wima na kumtazama mama yake kwa huruma ya
kumsikitikia
‘Ni kuhusu Dennis?’ akaotea na kupatia.
mama yake akasimama pasipo kugeuka, akafumba macho na
kusikilizia ukweli ule ukimchoma vizuri. kameza mate na kufumbua macho
kilegevu, alishaanza kulengwa na machozi sasa. akageuza kichwa tu na kumtazama
binti yake. akautanua mdomo wake apate la kunena na akakosa, akajikuta tu akikirudisha kichwa chake mbele
na kuchapua hatua za kivivu kuelekea mbele
‘Mom, this is not fair… not fair at all… baba akijua sidhani
kama…’ Pamella akaongea kwa sauti akimfuata mama yake nyuma na mama yake
akamgeukia haraka sana kabla ya kumalizia sentensi yake
‘Pamella Please…stay out of this… please’ machozi yakashuka
wakati kope zake zikimwemweseka na kuruhusu machozi, akageuka haraka na kukaza
mwendo akimuacha pamella amemtolea macho ndi!. Aliumia kwa kushindwa
kujiongoza. Nafsi ilimsuta, alikuwa mama wa aina gani wa Pamella lakini hisia
zake kwa Dennis hazikuangalia alikuwa nani kwa nani. Akahitimisha ya wahenga
mapenzi hayana umri!
8888888888888888888888
‘Baba bwana… mimi sijapanga harusi kubwa hivyo… iwe ndogo ya
kisasa inatosha’ Jerry Agapella aliongea na baba yake wakati akijiandaa
kuondoka hapo kwao alikofika kumsabahi baba yake
baba yake akacheka kwanza akitikisa kichwa
‘Aah wapi… balozi mstaafu hawezi kuruhusu harusi ya kijana
wake pekee iwe kama sherehe ya ubatizo… come on Jerry!’ akampiga piga kijana
wake begani na wote wakatembea hatua moja kuufuata mlango.
Wakati wakiukaribia, mlango ukafunguliwa na mlinzi akaingia
na kuutanua zaidi mlango akiashiria alitaka mtu aliyekuwa nyuma yake aingie.
Mzee Agapella akatabasamu zaidi akionekana kumjua aliyetarajia kuingia.
Iloma akaingia mule ndani na kusimama mbele ya mtu na baba
yake, huku mlinzi akirudi kazini kwake na kufunga mlango.
‘You look beautifu Iloma’ akamsifia na Iloma akatabasamu kwa
aibu na kuinamisha kichwa chini, ile asante yake ikimezwa na lile tabasamu.
‘Oh.. Jerry kutana na iloma… my friend’ Mzee agapella
akatambulisha ile ‘my friend’ ikisindikizwa na tabasamu kali na Jerry
akiitafsiri alivyojua na kuitikia kwa kichwa
wakapeana mikono, na Mzee agapella akamtambulisha Jerry kama
kijana wake mkubwa. Wakamtaka radhi Iloma na kutoka nje wakimuacha anashangaa
ukubwa wa lile hekalu, mapambo na vitu vya thamani vyenye kuvutia pale
sebuleni.
‘Fiona ndio alikuwa naishi hapa…duh!’ akashangaa zaidi
akiumiza shingo kwa kubinua uso juu kushangaa kila lililopita machoni pake.
Pale mlangoni, Jerry alimtazama baba yake kwa jicho la msuto
‘Hujamtaliki Fiona bado…’ akamkumbusha
‘Mara moja katika maisha Jerry… jaribu kufurahia maisha bila
kuingiza lakini this lakini that… unamuonaje?’ Mzee agapella akaweka uzee kando
kwanza
‘She is the booomb dad… just make sure she doesn’t explode in
there’ akamtania baba yake na kumfanya acheke sana wakati yeye akiteremsha
ngazi chache mbele ya lango lao na kulifuata gari lake. Wakapungiana mikono na
Agapella akarudi ndani.
Alipoingia tu, akatumbukiza mkono kwenye mfuko wa suruali
yake na kutoa kidani cha almasi. Akamfuata Iloma aliyekuwa amesimama mbele ya
kabati la kioo lililokuwa na samaki wadogo wadogo waliokuwa wakifungwa hapo.
‘mnawalisha nini?’ Iloma akauliza akishangaa zaidi
‘Vipo vyakula maalumu…’ Agapella akajibu akizungusha mikono
yake shingoni mwa Iloma na kukilaza kile kidani.
‘aaawww… asanteee’ Iloma akajibu akikipapasa kile kidani kwa
mkono mmoja na ule mwingine ukinyanyua nywele zake kwa nyuma ili Agapella
akifunge kile kidani. Alipomaliza Iloma akamgeukia na kumtazama Agapella usoni
kisha akajiinamia kukitazama kile kidani.. Kiliwaka na kuvutia mno.
‘It is Diamond!’ Agapella akamtajia aina ya madini ya kidani
na kile na Iloma akamtazama kwanza kabla ya shukrani kummiminika.
Akamuongoza nje kwenye bustani kulikokuwa na meza pamoja na
viti. Wakaketi hapo wakiongea hili na lile na Iloma akishindwa kabisa kuibua
inshu ya Fiona kama walivyokubaliana na Fiona. Alimpigia simu Agapella na kudai
alikuwa amekubali mwaliko wake na hapo hapo akimdanganya Fiona kuwa alikuwa
amempigia Agapella na kujitambulisha kama rafiki wa Fiona. Fiona akamsaidia
kumuelekeza na kumpa maneno ya kuongea ili kumtetea lakini nafasi ya kuanzisha
mada ya Fiona au tu kujitambulisha kama rafiki wa Fiona, ilikosekana,
ilishindikana na mkutano wao ukaisha bila Fiona kuzungumziwa!
88888888888888888888888888888
Jioni hii baada ya pilika pilika za kazi na mambo chungu
nzima. Dennis Mazimbwe akaingia kwake akiwa na uchovu wa kutosha. Watoto wake
wakamlaki na kuongea naye hili na lile naye akiwaahidi wikendi atawapeleka dar
es salaam zoo.
akaingia chumbani kwake na kumkuta Daniella akishona kifungo
cha shati kwa sindano ya mkono. Wakasabahiana na Dennis aipomfuata mkewe ili
ambusu shavuni, Daniella akakwepa. Dennis akaachana naye na kwenda kuweka vitu
vyake kwenye meza anayoweka vitabu vyake na kisha kuingia bafuni.
Simu ya Dennis ikatoa mlio wa kuita, Daniella akaitazama tu,
ikatoa mlio wa kuingia meseji na Daniella akanyanyuka na kuifuata ile simu.
Akaifungua
‘Dennis babe plz call me’ akausoma ule ujumbe ulitoka kwa
Rebecca aliyeseviwa kwa jina lake. Daniella katikisa kichwa kulia na kushoto.
Mwanamke aliyempa onyo siku chache zilizopita alikuwa hajaonyeka!
Dennis akatoka bafuni akifuta kichwa kwa taulo, akashangaa
kuona mkewe ameketi kitandani na simu yake mkononi.
‘Rebecca again!... she wont leave me alone… why are you guys
doing this to me?... why Dennis… nimeacha vyote kwetu… kila kitu nikaambata
nawe ukiwa huna kitu… nimekupa watoto dennis… nimevumilia tabu zote mpaka hapa…
Kwanini unanifanyia hivi?’ Daniella akaongea kwa hasira akilia kwa kwikwi,
akiomboleza kwa hasira
Dennis akajaribu kuingilia kati na kumbembeleza lakini ikawa kazi
bure kabisa. Alikataa kuguswa na mumewe, alikataa kumsikiliza.
‘It is time Mr. Okello ajue mkewe ananivunjia ndoa yangu…’
akaongea kwa hasira akitoka mule chumbani na Dennis akiharakia kuvaa ili
amuwahi mkewe. Daniella alitoka mbio mpaka sebuleni na kukumbana na Nanny
aliyempokea na kumuweka kifuani, akimbembeleza na kujaribu kumtuliza Daniella.
Dennis akatokea pale sebuleni wakati Nanny akiwaondoa watoto na kuwataka waende
nje kwanza.
Wanawake hawa wawili wakamtazama Dennis kwa ghadhabu.
Daniella alikuwa akijaribu kuzuia machozi huku akigombana na mumewe aliyemtaka
wazungumzie lile sula kwanza kabla ya kumfuata Okello. Mlango ukafunguliwa na
Patrick akaingia kwa jazba.
Aliingia moja kwa moja na kumfuata Dennis kaka yake,
akamtandika ngumi moja kali iliyompepesusha na kukaribia kumbwaga kochini.
Akiwa bado na ile hali ya kushangaa Patrick akamvaa ili amkung’ute kisawasawa
lakini Nanny akamuachia Daniella na kukimbilia kuamulia ugomvi wa mtu na ndugu
yake.
‘Heeeeey!’ Nany akapiga ukelele wa nguvu na kuwaachanisha
hawa ndugu kwanza. Wote wakihema kwa hasira
‘hongera!... hatimaye Pamella ameniacha… it was you… you
bastard!’ Patrick amatusi kaka yake na kutaka kumvaa tena lakini Nanny
akawazuia na Daniella sasa alikuwa amemshikilia Patrick.
‘Nimefanya nini?.... nimeongea na Pamella lini?....’ Dennis
alihoji kwa mshangao na hasira juu
‘Sio wewe uliyenitishia niachane na Pamella… hukuwa wewe?...
na Nanny ni shahidi yangu hapa… haukuwa wewe?.... nijibu… she is no longer
mine… happy now?...’ Patrick aliongea
kwa hasira akiweweseka na machozi kumtoka kwa hasira. Mwanaume uvumilivu
ulifika kikomo
‘so… mama na binti yake wanatoka na mtu na kaka yake… wow!...
unamtishia Patrick aachane na Pamella Okello wakati wewe umeshindwa kuachana na
Rebecca Okello?... Oh Mungu wangu’ Daniella akajiinamia na taratibu akalifuata
kochi na kuketi huku akilia.
Patrick sasa akabaki mdomo wazi, akiwa haamini alichosikia.
Akarudi kinyume nyume na kuufikia mlango, akaufungua na kutoka. wakati Daniella
akisimama na kuufuata mlango pia, akatoka na kuubamiza. Dennis aliyebaki kama
mlevi akasimama na kumtazama Nanny kichovu, jasho likimtoka.
‘umefanya nini hiki sasa?’ Nanny akamuuliza kwa huruma
‘… angalau ungejitoa kafara kwa kumuacha Rebecca ili Patrick
awe na mwanamke anayempenda… hukuifikiria hata furaha ya mdogo wako?’ Nannya
akamuuliza kwa sauti ya upole ila yenye kusuta
‘Sio hivyo!’ Dennis akajibu akiweweseka
‘Ni nini sasa?’ Nanny akamuuliza akimsogelea Dennis na
kumketisha chini kwenye sofa. akakaa kando yake na kumtazama Dennis aliyekuwa
amejiinamia.
‘Dennis!’ Nanny alisisitizia kujibiwa
‘Pamella ni binti yangu wa damu… my real daughter’ akapasua
ukweli kwa sauti kuvuta, sauti ya kujuta, sauti ya kutetemeka. Nannya akakuza
macho yake saizi ya ndimu changa. Aliyakodoa hasa almanusura yamchomoke!
Daniella ameenda wapi?....Patrick atachukuliaje?... nini
kitafuata?... jiunge nami hapahapa USIKOSE!
ITAENDELEA…. NIPE MAONI YAKO KUHUSIANA NA SIMULIZIA HII NDUGU MSOMAJI
sasa utamu ndio umeanza jamani iloma naye kwa mzee Agapella je Fiona akijua itakuwa nini
ReplyDeleterebecca ndoa itamshinda cku c nyingi
ReplyDeleteSawa, Fiona akijua sijui patatosha? Yani utamu hadi masikioni lahaulah
ReplyDelete