Haya wadau wangu, Mungu katujaalia uzima mpaka muda huu wengine tunaandika wengine mnasoma....hili pekee ni jambo la kumshukuru Mungu, maana kwa maisha sasa kuliona jua la kesho ni majaaliwa.
.......Nisizunguke sana, niende moja kwa moja kwa ninalotaka kulisema barazani hapa!
Kauli ni mali...hasa kama kali hiyo ni njema yenye kuburudisha, kuelimisha na kuleta kila aina ya raha. Kama ilivyo mali, kauli pia ina thamani yake, Mali ukiichezea utakula za uso sawasawa na kauli ukijichanganya utakula za uso.
..... kuna binadamu wenzetu wakifumbua mdomo kumjibu mtu utatamani umtandike kibao cha uso papo hapo. yaani utasema amesukutulia maji ya mtaro. Kama hakukujibu atakupindishia mdomo kama utasema indiketa ya gari.
Ewe mja juu ya uso wa dunia unapungukiwa nini ukimjibu vizuri binadamu mwenzako?..... unapungukiwa nini ukitumia dakika zako mbili tu ukamsikiliza na kumjibu mtu vema tena unakuta mtu unayemjua vizuri kabisa! Mungu naye akikuwekeka nyodo unazomnyodolea mwenzio itakuwaje?
...... Hii tabia wanayo sana wale wenzetu wa maofisi achilia mbali uswahili kwetu kule......umeajiriwa hapo na si kwamba umewekwa ukae hapo milele na unalipwa chenji hizo ili uwajibu watu wanaokuja kukuuliza hapo wasipokuja utakuwa na kazi tena hapo? Hebu staarabikeni jamani!
. Leo unayemjibu ovyo si ajabu kesho ukamgongea ofisini kwake kuhitaji msaada. Kama kitu hakikugharimu hata senti jamani kinakushinda nini kutoa kauli njema kwa wenzio. Bora na wanaume, sisi wanawake ndio kabisa nyodo zimetutuna kichwani utadhani ukimjibu mtu vizuri umemuongezea visenti kwenye akaunti ya pesa. Poh! hebu rekebisheni midomo hiyo kha!
Maisha duara, maisha ni ngazi unayempita hapa si ajabu ukamkuta mbele ya safari kabla hujafika uendako. Hapo ulipo hebu jiulize ni mara ngapi umewajibu watu nyodo kwa kuwahukumu kwa mavazi yao ama kipato chao am chochote tu kilichopelekea umjibu ovyo....kisha ichukue nafasi ya yule mtu na umuweke ndugu yako umpendaye au hata mzazi wako kama unaye halafu jiulize ungejisikiaje....mtu huyo kujibiwa kama wewe unavyomjibu huyo mtu asikuhusu!
Wengine mngepigana mpaka Sungusungu waje!.......kumbe inauma eeh!.....
Heshima na Kauli havitangamani, heshima ikitangulia ni lazima kauli mali itafuata! jaribu leo kumuwekea tabasamu binadamu mwenzio kwa kumjibu vizuri, kuzungumza naye vizuri.....thawabu kwa Mungu sio kukusanya gunia la pesa kuwapelekea yatima.....wakati mtu mmoja tu umeshindwa kumfanya naye ajihisi yu na thamani! utatosa gunia la sukari baharini!
Yangu machache hayo!....Kauli ni mali na ukweli kwamba hakuna aliyebora mbele za Mwenyezi Mungu ndio kabisa unapaswa kujiuliza unajibu ovyo kwa manufaa gani na kwa lipi hasa?
Alamsiki!
No comments:
Post a Comment