Monday, November 18, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE(47)

47


Ni sauti za vijiko kugonga sahani ndiyo hasa iliyokuwa inasikika katikati ya mlo huu wa usiku. Jerry alitua kijiko chini na kunyanyua glasi ya maji iliyokuwa kando ya sahani. Akapiga funda moja la kutosha na kurudisha glasi mezani.


Akamtazama pamella aliyekuwa ameketi mbele yake, akionekana kuzama mawazoni na kuchezea chakula chake kwa kijiko, alikichota taratibu na kukirudisha kwenye sahani, akaucheza mchezo huo mara kadhaa pasipo kujitambua. Ni dhahiri akili yake haikuwa pale kabisa.

Jerry akamtazama Pamella kiudadisi, akaunyoosha mkono wake wa kushoto akiufuata mkono wake Pamella wa kulia uliokuwa umeshika kijiko. Akaugusa na kumshtua Pamella aliyeinua uso wake na kujaribu kutabasamu.
‘umeshiba?’ akauliza kwa sauti ya upole hali lile tabasamu likionekana kudumu usoni pake

‘Talk to me Pam… kuna tatizo gani?’ Jerry hakutaka kupotezea ile hali
‘No!... usijali…’ akajibu akishusha pumzi na kujiinusha toka kwenye kiti.
‘This is not fair Pamella…’ Jerry akalalamika katika mtindo wa kubembeleza akilaza kichwa nyuma kidogo na kuinua uso juu ili aweze kuutazama uso wa Pamella  aliyekuwa amesimama

Pamella akamtazama Jerry kwa sekunde kadhaa kama mtu anayejishauri cha kumwambia, kisha akaghairi na kuanza kuondoa vyombo mezani.
‘Ni kuhusu Patrick?’ Jerry akajaribu kuotea na akamfanya Pamella asimame kwenye kizingiti cha kuingilia jikoni akiwa amempa mgongo Jerry. Taratibu akageuka na kumtazama tena Jerry katika mtindo ule ule wa ‘sijui nikujibu nini’.

‘Nimekusikia ukigombana na mama yako kuhusu Patrick…’ Jerry akaona aweke wazi anachojua
‘Sijisikii kuzungumzia hayo muda huu’ akajibu kwa upole na kuelekea jikoni akimuacha Jerry amejiinamia.
Akajiinusha toka pale kwenye kiti na kuelekea chumbani kwake. Wakati anaingia hakugundua mabadiliko yaliyotokea mule chumbani mpaka alipotuliza akili na kuona baadhi ya vitu vilikuwa vimehamishiwa upande mwingine huku vitu vikiwa vimepangwa kiustadi. Akatabasamu akionyesha wazi kuufurahia mpangilio mpya alioukuta chumbani kwake.

Akakifuata kitanda na kujitupa chali, sekunde moja tu ilitosha kumfanya ukunje ndita kadhaa usoni na kutikisa kichwa kuashiria kutoridhishwa na kitu. Picha iliyokuwa inamhusu Sindi, picha iliyokuwa inakaa mbele ya ukuta unaotazamana na kitanda chake ilikuwa imeondolewa na kurudishwa picha ya Pamella iliyokuwepo Mwanzo kabla ya kuiondoa na kuiweka ile inayomhusu Sindi.

Akatoka kitandani kwa kukurupuka na kwenda kusimama karibu na ule ukuta, akiwa kama haamini ile hali ya mabadiliko. Akaufuata mlango kwa kasi na kutoka nje akimfuata Pamella jikoni.
‘Picha umeipeleka wapi?’ akamvaa Pamella aliyekuwa naosha vyombo kwenye sinki
‘Picha?... Picha gani?’ Pamella akahoji akiiacha kazi yake na kufuta futa mikono kwa kitambaa kilichokuwa begani kwake.

‘Picha iliyokuwa ukutani chumbani kwangu’ Jerry aliongea kwa sauti ya kufoka akinyoosha mkono kuonyesha uelekeo wa chumbani kwake.
‘Nimeiondoa for good Jerry… You need a break… you…’ hakumalizia nasaha zake Jerry alimuwahi

‘…Wewe ni nani wa kunipa break mimi…Picha umeiweka wapi?’ akahoji kwa ghadhabu sasa na kumfanya Pamella amtolee macho ya kutoamini alichosikia
‘nimeiweka stoo… I thought niko hapa kukupa utulivu wa akili kumbe unaniona sina msaada wowote’ Pamella naye alianza kuja juu

‘did I ask you to be here… nilikupigia magoti ukae hapa?... sijui stoo sijui wapi please Pamella don’t mess with my house… it is my house lady… Nahitaji hiyo pich irudi humu ndani sasa hivi’ akaamrisha mwanaume, akafoka na kuongea kimamlaka kiasi cha kumfanya Pamella aduwae kwanza.
‘Fine!’ Pamella akajibu kwa sauti kali lakini iliyomezwa na maumivu. Akaitupa chini kile kitambaa alichokuwa anafutia mikono na kuufuata mlango wa kutokea nje. Akatumia dakika mbili na ushee kisha akarejea na picha aliyokuwa anadaiwa.

Akamfuata Jerry chumbani kwake na kumkuta ameketi kitandani akiwa amejiinamia. Akamtupia miguuni ile picha na kumfanya Jerry ainue uso na kumtazama Pamella ambaye alivuta stuli na kuipanda akihangaika kuindoa picha yake iliyokuwa ukutani. Akaiegesha chini na moja kwa moja akalifuata kabati na kutoa sanduku lake.

Zipu ya sanduku ikalia shwaaaaa… upande wa juu wa sanduku ukatupwa kule na Pamella akaanza kukusanya vitu vyake na kuvitupia kwenye sanduku. ile jazba aliyokuwa nayo Jerry, ikashuka sasa, na akatambua alikuwa ameongea maneno makali sana kwa Pamella ambaye kwa wiki kadhaa alikuwa amejitoa kuishi naye mule ndani akimpikia na kumfanyia kila kitu kama mkewe. Faraja aliyokuwa amempatia na msaada wa kumtuliza kiakili Pamella hakustahili kujibiwa vile sembuse kumkoromea kwa kitu kama kuondolewa kwa picha.

Alitumia dakika tano tu kuhakikisha alikuwa amekusanya kila kitu chake. Wakati akauacha mlango na kuelekea sebuleni na sanduku mkononi. Jerry akanyanyuka na kumfuata nyuma akimuita kwa sauti ya kujutia alichosema.

Pale sebuleni, Jerry akamuwahi na kumshika mkono uliokuwa na Sanduku. Akamnyang’anya Sanduku kwanza na kuliweka kando
‘I’m sorry’ akatamka kwa sauti ya upole mkono wa kulia ukiwa umeushika mkono wa Pamella na wa kushoto ukiwa kifuani pake, akimtazama Pamella aliyekuwa anatazama mbele na kutikisa kichwa kuashiria kutokukubaliana naye.

‘Enough is enough Jerry!’ akaongea kwa hasira akigeuka na kumtazama Jerry usoni
‘…of course hukuniita, hukuniomba msaada wowote,…ni kweli hii ni nyumba yako na hainihusu… niwie radhi nimekutibulia nyumba… nimekuvamia na misaada isiyohitajika… please!’ akarai akiutazama mkono wa Jerry uliokuwa umemshika, akaukwatua taratibu na kutaka kulinyanyua sanduku lake lililokuwa kando ya Jerry.

hakulifikia! Jerry alimzuia na kujaribu kumgusa lakini Pamella alipangua mikono yake tayari machozi yakimlengalenga.

‘Achana na mimi Jerry… uliponusurika kufa kule porini nani alikufuata?... nani alikusitiri kama sio mimi… juzi umenusurika kufa hapa… for three weeks nimekaa na wewe hapa nikimdanganya Patrick wa watu sababu yako… yuko wapi huyo Sindi?... wakati ulipohitaji mtu wa kukuinua ulipokuwa unamuuguza mama yako…. ulipofiwa na mama yako… Sindi alikuwa wapi?.... alikusaidia nini?... hata kama hunipendi Jerry… hata kama huna hisia na mimi… Nastahili heshima Jerry… sio majibu kama yale’ Pamella aliongea utadhani mghani mshairi… akitamba kwa uchungu na machozi yakimtiririka. Kebehi za Jerry zilimuumiza!

Maneno yale yalimchoma mno Jerry. Akapigania kumzuia Pamella asiondoke pamoja na mwenyewe kushikilia msimamo wa kuondoka usiku ule. Wakagombana mno na mwisho Pamella akasimama mbele ya Jerry akilia kwa kwikwi na kumtazama Jerry asimuelewe.
‘I love you… I love you Pamella’ Jerry akakiri, akakiri kwa upole na hisia zote akimfuata Pamella na kumuangukia miguuni

Zile sentensi mbili zilimsisimua mno Pamella. Zilipita kama waya wa umeme uliokatikia kwenye mwili uliotota maji. Hakukumbuka ni lini mara ya mwisho alimsikia Jerry akimtamkia maneno yale tangu Sindi Nalela alipokuja maishani mwao. Akafumba macho na kuruhusu machozi zaidi wakati Jerry akiwa amemkumbatia kiunoni na kichwa chake kukilaza usawa wa tumbo la Pamella.

Ukapita ukimya kidogo ukiwa umeambana na  vijikwikwi toka kwa Pamella. taratibu Jerry akainua uso na kumtazama Pamella usoni.
‘Pamella Okello...my best friend!… ‘ Jerry akatamka kwa sauti nzito iliyojaa umakini wa kile alichotaka kuongea. Pamella akatabasamu katikati ya machozi
‘Will you marry me?’ kauli ile ikavuma kwenye masikio ya Pamella kama mwangi wa radi. Akaachama mdomo na kupepesa macho yaliyojaa machozi na asimini anachosikia toka kwa Jerry.

‘Will you?’ Jerry akauliza tena naye sasa akijitahidi kutabasamu
‘Oh my God…’ Pamella akahisi yu ndotoni sasa, machozi yakazidi kumporomoka wakati Jerry alipoinuka na kusimama usawa wake
‘no more Sindi drama kati yetu… no more fights juu ya Sindi… will you marry me?’ Jerry akajieleza na Pamella akaitikia kwa kichwa sasa akitaka kucheka na kulia kwa wakati mmoja

‘Yes…Yes..’ Pamella akaitikia kwa sauti na kuzidi kutikisa kichwa. Wakakumbatiana wapendanao hawa. wakakumbatiana kwa nguvu zote. lakini wakati uso wa Pamella ukiwa umejaa machozi ya furaha, hali ya amani, matumaini ya mema yajayo, uso wa Jerry ulikuwa mtulivu mno ukionyesha wazi kuwa moyo wake ulikuwa umebeba zaidi ya msalaba! Ni kwamba hajamaanisha alichosema ama bado alikuwa haamini kama ameweza kukata shauri moja juu ya kumsahau Sindi Nalela.
88888888888888888888888

‘ you are not serious Jerry… you popped the question huh?!’ Meddy aliyekuwa ameketi kwenye kiti mbele ya meza ya kazi ya Jerry aliuliza huku akigeuka kumfuatiza Jerry aliyekuwa naelekea kwenye kabati kutunza faili la kazi. Jerry akacheka kidogo na kurejea kwenye kiti chake, akimpa kibarua Meddy cha kugeuka tena na kutazama na Jerry pale mezani.

‘Yes Sir!’ Jerry akajibu na kumfanya Meddy acheke kwa sauti sasa
‘eti?... so unamuona Pamella Okello?.... like seriously… ghafla tu umesahau mwanamke uliyemlilia kwa miezi miwili mfululizo… damn! this is what we call a nightmare’ Meddy akatania na kumfanya Jerry acheke huku akimuonyesha ishara ya kutaka kumtwanga ngumi.

Wakajadiliana hili na lile lakini bado Meddy aliona kama hakikuwa kitu sahihi.
‘Bado siamini kama uamuzi umetoka moyoni au ni ile hali ya kukata tama ya kutomuona tena Sindi…’ Meddy alielezea wasiwasi wake
‘Kwanini unadhani simpendi Pamella?’ Jerry akahoji
‘unajua ndoa sio kitu cha majaribio au bora liende tu… unapompenda mtu kwa dhati utamvumilia kwa kila hali… pengine nikuulize baada ya kumuona Pamella kisha Sindi akajitokeza… moyo wako utakuwa tayari kumuignore Sindi kabisaaaa’ Meddy akauliza swali lililoonekana kuwa gumu kwa Jerry

‘…sasa ina maana sitaoa maishani kwa vile Sindi amenikimbia?’ Jerry akapangua swali bila kulijibu.
‘Kuoa sio tatizo… kunja tofauti ya kumuoa Pamella na kumuoa mwanamke mwingine tu uko… she is your best friend kumbuka hilo kwanza… pili anamjua Sindi na anajua hisia zako kwa Sindi… ulichomuahidi kuwa suala la Sindi halitaibuka tena maishani mwenu ni uongo Jerry… nina uhakika kwa vile nakujua best…’ Meddy akatetea mawazo yake

‘watu wanabadilika Meddy… nimeamua kumove on…’ Jerry akataka tu mazungumzo yaishe kijuu juu
‘Kumove on sio tatizo… nimekupa tahadhari tu… ila pengine nikuulize huna mpango na Sindi kabisa hata akijitokeza leo hii?’ Meddy akauliza akicheka pia
‘Sina!... nimeamka asubuhi ya leo nikiwa nimefuta kumbukumbu zote za kuanzia nilipomuona mpaka alipoondoka… it is just me and Pamella baaaasi… akijitokeza ukaamua kumchukua…no problem!’ Jerry akajibu akinyanyuka na kuondoa koti lake alilokuwa amelitundika kwenye kiti na kuanza kulivaa.

Meddy akamtazama kwanza kisha akacheka kwelikweli
‘Saw bwana!.... good luck!’ Meddy akakubali yaishe lakini moyoni alihisi rafiki yake alikuwa hamaanishi anachoongeam ila tu hakutaka kubishana naye zaidi. Akamtakia kila la kheri!

Wakati wakijiandaa kutoka Meddy akasimama kwanza kama mtu aliyekumbuka kitu
‘Kuna binti nataka umuone aisee’ akajieleza
‘Mmh!... hatimaye umeslimu amri eeh hahahahaaa… I hope Madam Adella atasikitika kupoteza mteja wake mwaminifu’ Jerry akatania

‘Ni binti mwenyewe yupo ndani mule… nadhani ni binti mpya… yuko tofauti kabisa… na anaonekana mgeni kwenye mambo haya’ Meddy akafafanua na kumfanya Jerry amkodolee macho ya kumsuta kidogo

‘… Malaya ni malaya Meddy! hakuna Malaya mwenye utofauti… na sitarajii uje kuniambia unataka kuwa kwenye uhusiano serious na binti toka kwenye danguro...’ Jerry akampinga akikifuata kitasa cha mlango
‘Come on!... unajua nimeshamuona mara mbili hivi… moyo wangu…kichwa changu vimegoma kumtoa akilini kabisa… I wish umuone tu kisha uniambie lolote’ Meddy akaonekana kutekwa na huyo binti wa kwenye danguro

‘Yaani uniburuze toka hapa mpaka kwenye madanguro uko kumuangalia msichana?... Meddy acha huu upumbavu kaka… kuna mabinti wangapi wanaojiheshimu kitaa mpaka ukazoe malaya wa uko… aisee bora nikuazime hata Clarita sio takataka za madanguroni’ Jerry akabeza kabisa

‘Poa! ila angalau mara moja tu twende umuone’ akasihi na Jerry akamtazama rafiki yake kwanza kwa kituo
‘Next time utataka nikusindikize kununua bangi pia maana nahisi tayari umeshaanza kuivuta….shame on you… tutakwenda kesho’ akakubali baada ya kumnanga mwenzake aliyeishia kucheka tu
8888888888888888888888888
Nyumbani kwa Dennis Mzimbwe, Patrick alikuwa sebuleni akizungumza na watoto wa kaka yake. Walionekana kufurahi mno kumuona baba yao mdogo. Nanny aliyekuwa jikoni akawaletea juisi kwenye glasi zilizokuwa zimebebwa kwenye chano kilichosukwa kwa ukili. Wakazipokea glasi kwa bashasha huku pia wakimtania Nanny hapa na pale.
‘Bibi kule kuna baridi mpaka barafu zinadondoka…’ Pacha mmoja alimsemesha Nanny akimsimulia hali ya uko walikotoka na Nanny akionekana kufurahia simulizi zile.

Wakati watoto wakifurahia kurejea nyumbani kwa baba yao, chumbani kwa Dennis, mkewe Daniella alikuwa akiondoa nguo kwenye sanduku na kuzipanga kabatini wakati Dennis alikuwa amesimama umbali mfupi toka pale alipokuwepo mkewe. Anachapua hatua kadhaa na kumfuta mkewe. Akataka kumkumbatia kwa nyuma na Daniella akajitoa maungoni mwa mumewe na kusimama mbali kidogo

‘Niliposema nimerudi kwa ajili ya watoto…nilimaanisha ninachoongea’  akarudia msimamo wake
‘kwa muda gani Daniella?... mpaka lini?... you are my wife’ Dennis akatetea alichoona ni sahihi, taratibu akimfuata mkewe na mkewe akirudi nyuma kumkwepa

‘Your wife?... Den!... kama ulijua hilo nini kilikufanya ukasaliti kiapo cha ndoa nje?’ Daniella akauliza kwa sauti  ya msisitizo. 
‘Shit!’ akalaani Dennis alishachoka kusikia kauli ile kila mara toka kwa mkewe
‘Come one Ella… niliomba radhi…nikaomba radhi…nimeomba radhi na hata sasa nakuomba radhi… hivi lini utasamehe bila kunisimanga?’ akalalamika masikini akihisi kero zaidi

‘…Sijui!...’ Daniella akajibu akimpita mumewe na kulifuata dirisha akasimama hapo akitazama nje
‘Shida zangu nikatimize wapi sasa?’ mumewe akamuuliza swali zito lililomfanya akagune kwa dharau kwanza kisha akageuka na kumtazama mumewe
‘uko uko ulikokuwa unazitimiza kabla sijaondoka na kabla sijarejea’ akajibu kwa ukali akilifuata sanduku la nguo na kuendelea na kazi yake

‘Na tutaishi hivi mpaka lini sasa…I’m a man… na wewe ni mke wangu… kweli chumba kimoja…kitanda kimoja…nakuangalia tu’ Dennis akahisi utata

‘nani amekwambia nitalala humu ndani?’ mkewe akamuuliza
‘Na utaleta picha gani kwa watoto kwa kulala nje ya chumba hiki?’ Dennis naye akaja juu. Mkewe akamtazama tu pasipo kumjibu kisha akaendelea na shughuli zake. Dennis akaona kuendelea kukaa pale kungefanya wajibizane zaidi. Akatoka kwa jazba na kuwapita wanawe pale sebuleni kwa kasi ya ajabu. akatoka na kuubamiza mlango.

Nanny na Patrick wakatazamana tu, walijua uko ndani alikotoka hakukuwa na usalama.
88888888888888888888888888

Ndani ya mgahawa mmoja katikati ya jiji. Fiona na iloma walikuwa wakipata chakula pamoja. Baada ya kulipia na sahani kuondolewa wakabaki na vinywaji vyao. Fiona akamtulizia iloma macho kwanza kabla ya kumrushia kombora lililomfanya akaribie kupaliwa.
‘Kazungumze na Agapella  Iloma… nahisi kumpoteza mume wangu’ Fiona aliongea kwa huruma na iloma almanusura apaliwe
‘…. ukijitambulisha atakusikiliza tu’ akaendelea kubembeleza

‘Fifi… unadhani ni rahisi tu… kwanini usimfuate tena Dennis… anaweza kuwa amerejea kazini sasa…’ iloma akakwepa majukumu
‘kwa Dennis matokeo ni asilimia kumi tu…. mimi na Dennis hatuivi na inshu kama hii ndio atapalilia talaka yangu kabla sijafanya mambo yangu’ akakazana kumshinikiza Iloma amtimize shida yake.

Iloma akaonyesha wazi kuelemewa na lile ombi
‘mpe muda kidogo… atakutafuta’ akakwepa tena
‘Hawezi… ni wiki kadhaa zimepita …. hata simu…hata meseji… no way out may be kuna mwanamke mwingine ameshamteka ila nakuhakikishia… atakayemsogelea Kristus wangu nitakufa naye… yaani atakufa vibaya mno kuliko alivyokufa Sophy… na sitaki hata kuwaza kuwa kuna mtu maana nitafanya vitu vya ajabu mno’ Fiona akaongea kwa jazba akimuacha mwenzake anamtazama kwa uso wa mashaka. Akilini akiikumbuka sura ya Mzee Kristus Agapella wakati alipoonana naye pale kazini.

‘Hey!’ Fiona akamzindua baada ya kuanza kujimwagia kinywaji bila kujua. Alihisi kusisimka mpaka kwenye mifupa!
8888888888888888888888888888

Siku mbili tatu baada ya kuingia jijini, Daniella akaingia supermarket kufanya shopping ya vyakula. Akazunguka na toroli lake taratibu huku akizungumza na simu yake ya mkononi. Akasimama na kuibana kwa bega wakati akitazama baadhi ya bidhaa na kuziweka kwenye toroli lake. akaikamata simu kwa mkono mmoja na mwingine kusukuma toroli mpaka sehemu nyingine.

Alipokata simu na kutaka kusukuma tena toroli akamuona mtu anayemfahamu akiwa mbele yake upande wa kulia akisoma maelezo kwenye bidhaa aliyokuwa nayo mkononi. Akatabasamu na kumfuata yule mtu.

Rebecca Okello akageukia kule alikosikia salamu ikitokea, macho yakamtoka alipokumbana uso kwa uso na Daniella, mke wa Dennis Mazimbwe.
‘Long time no see!’ Daniella akaanziasha mazungumzo akitabasamu

Kama mtu asiyeamini alichoona, akachungulia yuma ya Daniella akitarajia pengine kumuona Dennis. Kulikuwa na wateja wengine tu waliokuwa busy na ununuzi wa bidhaa.
‘I’m back!’ Daniella akaongea tena pengine kumsaidia Rebecca atoke kwenye lile bumbuwazi
‘Karibu!’ Rebecca akajibu na kujaribu kuendelea na mambo yake ila Daniella akamuwahi

‘That handsome man… caring… devoted husband of your age is my husband…my husband…husband not a boyfriend!... with due respect now take care your old man please because I’m back…. see you around!’ Daniella akaongea kwa kubana meno, kwa msisitizo na tabasamu juu kiasi kwamba kwa aliyekuwa umbali mfupi angelisema wanawake hawa walikuwa wakiongea jambo la kheri.

Daniella akaendesha toroli lake na kutokomea akimuacha Rebecca ameduwaa na kuweweseka mwenyewe. Hata hamu ya kufanya shopping ikamuisha. Akatoka mbio kuliwahi gari lake. Akili ilikaribia kumruka. Hakutarajia kumuona Daniella pale na wakati kama ule.

Akaendesha gari moja kwa moja mpaka ofisini kwa Dennis. Alipoingia ofisini mule na kumkuta Dennis na mteja. Rebecca hakujali kitu
‘Why…why Dennis why… why” akauliza kwa jazba na kumfanya Dennis amtake radhi mteja wake na kumuomba awapishe kidogo. Baada ya kuufunga mlango akamgeukia Rebecca akimshangaa

‘huwezi ingia ofisini kwangu kama unaingia chumbani kwako… hii ni ofisi Becca!’ alikerwa na ile hali ya kuparamiwa na Rebecca
‘I don’t care!... Kwanini hukuniambia unamfuata Daniella?... ulisema ni safari ya kikazi tu… daniella ametoka wapi… why amerudi… amekuja kufanya nini sasa?’ Rebecca akahoji kwa kupanic mno. Akimtazama Dennis kana kwamba alitaka Dennis ambishie kuwa aliyeonana naye si Daniella.

‘She is my wife Becca… na nahitaji kuwaona watoto wangu’ Dennis akajitetea
‘Kwanini usingewachukua watoto peke yake… mimi nimeshindwa kukupa nini hadi umrejeshe Daniella?’ wivu ulimsumbua mno Rebecca
‘huwezi kuelewa situation ilivyo’ Dennis akajitetea tena na Rebecca ahakumuelewa
‘So mnalala chumba kimoja?... real?... Dennis?... sitaki kuamini hili…no!...no Dennis… it is either tuvunje huu uhusiano au umuondoe Daniella… and I cant stand losing you… muondoe Daniella as soon as possible please!’ akaotoa amri yake iliyokuja kwa mtindo wa ombi na kuishia zake akimuacha Dennis anahisi maumivu ya kichwa.
88888888888888888888888

usiku wa saa nne na vichapo kadhaa, Meddy anaegesha gari ndani ya himaya ya Adella akiwa na Jerry.  Anaenda ndani kisha baada ya muda anarudi na kumuomba Jerry amafuate. Kwa roho nzito Jerry anamfuata Meddy nyuma na wanaingia kwenye sehemu iliyo kama Casino tulivu. Wanachagua meza na kuketi huku Jerry akishangaa ,abinti wanaocheza kwenye meza maalumu za kuonyeshea shoo.

Mabinti kadhaa wakiwa wamevaliza nusu uchi wakipita na kusambaza vinywaji.
‘Khaa! ndio ukaokota mwanamke humu?’ Jerry akashangaa na kumfanya Meddy acheke tu
‘Anakuja…vuta subira kidogo’ Meddy akamuomba uvumilivu.
‘Nakupa dakika 10 tu…hizi sehemu za kishetani hapana aisee….naweza kujikuta nakuwa mtumwa wa hawa wadudu wakati ni mume mtarajiwa’ Jerry akajinasibu na kumfanya Meddy acheke sana.

Kule chumbani kwa Nadina na Sindi, Nadina alikuwa akimalizia kujiangalia kwenye kioo namna alivyokuwa anavutia wakati Sindi akiwa amejitupa kitandani akisoma jarida.
‘twende bwana ukamuone…’ Nadina akamgeukia Sindi ambaye alimtazama na kuguna
‘… basi umchungulie tu kwa mbaaali.. ni mzuri sana’ Nadina akasifia

‘Nitaenda kuwaona wangapi… kila siku mteja mpya’ Sindi akatania
‘Huyu nadhani atakuwa wa kila mara… nahisi nampenda… nahisi kamaaa’ Nadina akjizungusha wakati akizungumza na Sindi akacheka
‘Sijakutana na mteja ninayehisi kumpenda… mungu wangu kuna wakati natamani kuwatemea mate… kuna yule babu wa kihindi... ananivutia kwa vile huwa haitaji ngono… shida yake umchezee nachi basi…’ Sindi akaongea akijiinusha na kuketi kitako

‘Twende basi…yupo kule kwenye casino’ Nadina akampigia magoti Sindi
‘Ha-pa-na!’ akakataa na Nadina akakata tamaa wakati mwenzake akijirudisha kitandani na kuendelea kusoma jarida lake


ITAENDELEA….

5 comments:

  1. maskini sindi angejua wakati wake wa ukombozi ndio huu angeenda tuu!!!

    ReplyDelete
  2. Laura story nzur ila unatuacha njia panda tumalizie bas

    ReplyDelete
  3. daah!Pet you're talented and gifted mumy!

    ReplyDelete
  4. laura unatukwanza jamanii wiki ya pili hii hadithi haendelei jamani basi uw unaweka mbili mbili jamanii au unalipia

    ReplyDelete
  5. ASANTENI SANA WASOMAJI WANGU....Anony wa mwisho...pole sana mpenzi...pole mno kwa kungoja sana.... mambo yanakuwa mengi na yanaingiliana. Trust me natamani kupost hata kila siku mpendwa. Nivumilie tu my dear

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger