45
Sindi Nalela alikuwa sakafuni ndani ya chumba kile kile
alicholazwa usiku uliopita, uso wake uliovilia damu hapa na pale ulilalia shavu
la kushoto sababu ya kule kulala kiubavu huku mikono yake ikiwa imefungwa nyuma
kwa kamba. Miguu yake ilikuwa imeunganishwa kwa kamba nzito ambayo haikumruhusu
kutanua miguu yake hata kwa sentimeta moja. Alilala vile akimtazama Nadina
aliyekuwa amelala mbele yake!
Alimtazama kwa huzuni na uchungu, akimhurumia kwa ile hali
aliyokuwa nayo. Naye alikuwa amelala kiubavu akiwa amefungwa mikono kwa nyuma
pamoja na miguu yake. hakuonekana kuwa na fahamu kwa wakati ule. Uso wake
ulikuwa umejeruhiwa na mwili wake ulikuwa umevimba na kuvilia damu achilia
mbali sehemu zilizojaa michubuko ya kusisimua. Sindi alifumba macho na kuruhusu
machozi yamtiririke, aliyafumbua alimtazama Nadina na kujaribu kumuita kwa
sauti ya chini.
‘Nadina…Nadina… Nadina…’ aliita kwa sauti yenye kitetemeshi
akijaribu kujisotesha kumkaribia Nadina na ikamuwia vigumu mno kusogea. Midomo
ikamchezacheza wakati akiruhusu kijito kingine cha machozi kifanye njia usoni
pake. Akalia kwa kupepesa macho na uchungu ukamfanya agugumie kilio na hatimaye
kukitoa kwa kwikwi huku akifumba macho na taswira ya kilichotokea na
kuwafikisha ndani ya chumba kile ikipita kichwani mwake kama kipande cha
sinema.
Baada ya kuokotwa kule njiani, aliletwa kwenye chumba ambacho
aliishia kufungwa mikono kwenye kiti
huku miguu yake pia ikifungwa kwenye miguu ya kiti. akapokea suluba ya
kutosha na kutisha huku akilazimishwa kumtaja aliyemsaidia kutoroka. Kipigo
kilikuwa kimekolea mno wakati Adella alipohisi suluba alizokuwa anampatia
zilikuwa si mali kitu!
Jasho lilikuwa linamchuruzika, nywele zake zilizokuwa
zimefungwa kifagio nyuma zilikuwa hazikueleweka, alikuwa amelegea mno na
maumivu aliyokuwa anayapata yalimfanya sasa ahisi kama vile mwili ulikuwa unaelekea
kufa ganzi. Alitamani kufa tu na kupumzika ila ndio vile kifo nacho kilisimama
pembeni na kumsikitikia!
‘Niletee waya wa moto…’ Adella aliutupa chini mkanda aliokuwa
akitumia kumpigia Sindi na kuagiza silaha nyingine ya kumuadhibia. Sindi
akajitutumua kuinua uso na kumtazama Adella ambaye alitabasamu kana kwamba
alichoagiza kilikuwa kitu chenye kumletea faraja Sindi.
Yule mlinzi aliyekuwa nyuma ya Adella aliduwaa kwanza na
asiamini alichosikia akiagizwa
‘hujanisikia au?’ adella akageuka na kumuuliza
‘Lakini yawezekana alikuwa mwenyewe..’ Mlinzi akajaribu
kumtetea kwani hata yeye aliguswa na kile kipigo alichokuwa ameshapewa Sindi.
‘…nina uhakika na ninachokiamini… niletee waya… naona ana
moyo wa mshumaa kukubali kuungua kwa ajili ya kumulika wengine… tutaenda
sambamba tu…tuone mwisho wako bitch!’ lle tusi la mwisho likaenda sambamba na
kofi kali la shavuni lililomfanya Sindi akaribie kuanguka na kile kiti. Mlinzi
mwingine aliyekuwa nyuma ya Sindi alimpa mwenzake ishara ya kutii amri ya bosi
wao.
Kule kuduwaa hakukumpata mlinzi peke yake, bali pia baadhi ya
wasichana waliokuwa nje ya kile chumba wakisikiliza kilichokuwa kinaendelea
mule ndani. Nadina alirusha rusha miguu kama mtu aliyebanwa na haja ndogo huku
akikung’uta viganja vya mikono yake kwa kiwewe. Mlinzi alipotoka wale mabinti
walitazamana kwanza na Nadina akahisi
alipaswa kujitokeza kabla ya waya uliogizwa haujamfikia Adella. Akawatoka
wenzake na kuufuata mlango kwa kasi lakini wenzake wakamuwahi na kumshika
‘Nadina!... hivi unajua kitakachofuata?....’ Mwenzake
akamtisha kwa kumtahadharisha
‘lakini ni mimi ndio nilimsaidia’ Nadina akatetea uamuzi wake
na wakati akibishana na wenzake yule mlinzi akawapita akiwa na waya pamoja na
chetezo kilichokuwa na vipande vya mkaa wa moto. Nadina akaweweseka na ile hali
ya kushauriwa akaiona kama ilikuwa ikimuweka Sindi hatarini zaidi lakini ndio
vile wenzake walimshikilia kwa nguvu zote.
Mlinzi akazama ndani na kufanya wale wasichana watulie na
kusikilizia. hakukuwa na maongezi yoyote lakini dakika mbili mbele Sindi
alipiga yowe kali la maumivu akimuita mama yake… akimuita Mungu wake… yowe lile
lilibeba ujumbe wa maumivu makali yasiyovumilika na Nadina ambaye sasa alikuwa
akilengwa na machozi aliwaponyoka wenzake na kuuvamia ule mlango wa kile
chumba. Akaingia kwa pupa na kumkuta Adella akiinua tena ule waya uliobadilika
rangi na kuwa mwekundu akiufuata mgongo wa Sindi.
Nadina akamvamia Adella na kumuangukia miguuni, akilia kwa
uchungu na kiwewe.
‘Ni mimi… ni mimi…’ akakitegua kitendawili cha Adella ambaye
aliurudisha ule waya kwenye chetezo na kumtazama Nadina kwa ghahabu kubwa!
‘Pumbavu!’ akaachia tusi lililokwenda sambamba na makofi
mfululizo kwa Nadina. Akaokota ule mkanda na kumcharaza nao Nadina kwa hasira
zote huku Nadina akiwa ameushikilia mguu wa Adella akimuomba msamaha.
Akanyanyua ule mguu uliokuwa umeng’ang’aniwa na Nadina na kumsukuma katika
mtindo wa kumpiga teke. Nadina akaangukia miguuni pa Sindi na kujitutumua
kuketi, haraka akasotesha matako kinyumenyume akimkimbia adella aliyekuwa anamfuata.
Maumivu yalimtembelea mwilini kama jeshi la siafu!
Masikini akagotea kwenye ukuta na kujikunyata, Adella ambaye
alishamfikia alinyanyua mguu wake wa kulia uliokuwa na kiatu kirefu kiasi na
kumkanyaga Nadina shavuni, akambana kwenye ukuta na ule mguu wake mpaka
alipohisi kutosheka. Akauteremsha mguu na kuchuchumaa mbele ya Nadina aliyekuwa
anatetemeka kupitiliza. Alitarajia kipigo baada ya kujitokeza ila si kipigo
kama kile!
mkong’oto aliompa ulikuwa wa haraka na wa uhakika. Ndani ya
dakika zile alikuwa amemchakaza mno Nadina ambaye maumivu yalimfanya asielewe
hata kile alichokuwa akiambiwa na Adella. Alichachatika nusu akili zikimruka!
‘Sikuwaleta hapa kucheza kombolela na mimi… na nyie sio wa
kwanza kuja hapa na hamtakuwa wa mwisho… ukiwa mstaarabu nakuwa mstaarabu ukiwa
mshenzi nakuwa mshenzi mara mbili… hapa sijakupiga binti… nimekupapasa kwa
upendo sana…’ Adella aliongea taratibu lakini kwa sauti iliyojaa hasira ndani
yake
Akanyanyuka na kuachana na Nadina na kurejea kwa Sindi
aliyekuwa amelegea pale kwenye kiti. Akakishika kidevu chake na kukitumia
kuinua kichwa cha Sindi. Wakatazamana!
‘Hatujamalizana bado… nataka ili liwe funzo la kwanza na la
mwisho kwako’ akakiachia kichwa cha sindi na kukifuata chetezo. Kitendo kile
kikamfanya Nadina ajue Adella alitaka kuendelea kumchoma Sindi na ule waya wa
moto.
Akajikuta tu akinyanyuka kidogo na kutembelea magoti kumfuata
Adella, akimuomba msamaha na kuahidi kila alichoona kingewaokoa toka katika
kile chumba. Adella akageuka na kumuamrisha yule mlinzi aliyekuwa nyuma ya
Sindi kumtandika Nadina. Kilio cha Nadina kilimfanya hata Sindi aliyekuwa hana
nguvu naye ajitutumue kuomba msamaha ili tu Adella asiendelee kumuadhibu Nadina.
Mlinzi akampiga Nadina kiasi cha kupoteza fahamu pale
sakafuni huku yeye Adella akitabasamu. Aliporidhika akamuamrisha yule mlinzi
kusimamisha kipigo. Akaagiza wawekwe kwenye kile chumba alichokiita kuzimu na
kuishia zake. Sindi akalia akimtazama Nadina aliyekuwa anavuja damu puani na
sehemu mbalimbali za mwili. akajivuta kwa nguvu na kusababisha aanguke na kile
kiti na kulala kando ya Nadina.
Akalia, akalia mno na alilia kwa mengi lakini hakuwa na jinsi
na hata baada ya kuingizwa ndani ya chumba kile bado Nadina alikuwa hana fahamu
na ndio alikuwa akimtazama kwa uchungu, akitamani yote yale yanayotokea katika
maisha yake yawe ndoto! Ulikuwa usiku mwingine mrefu kupindukia!
8888888888888888888888888
Ala ya muziki wa taratibu ilisikika toka katika redio
iliyokuwa mita chache toka kilipo kitanda chake. Jerry Agapella aliisikiliza ala
ile ya forever in love ya Kenny G, ala itumiwayo katika kipindi cha chombeza
time cha redio moja nchini. Ala ya muziki aliyopenda kuiskiliza kila alipohisi
upweke, ala ile ilimkumbusha mbali mno, ilimkumbusha mtu aliyezunguka kichwani
mwake karibu ila robo tatu ya siku yake iendayo kwa Mungu. Alimkumbuka Sindi
Nalela!
Glasi ya mvinyo iliyokuwa mkononi mwake iliganda mkononi
pasipo kuelekea kinywani wala kutua chini. Aliitazama ile glasi wakati akili
yake ikipotelea mbali na upeo wa macho yake. Ilimjia kichwani siku ile ambayo
Sindi alikuwa akigombana na Peter mdogo wake na yeye kuwa katikati yao …
akaikumbuka siku aliyomtembelea Sindi kule kwenye lile darasa alilokuwa
akifundisha na kusababisha watoto kupoteza umakini na kumtazama yeye Jerry
wakati akimchungulia Sindi… akatabasamu zaidi wakati alipoikumbuka siku ile
aliyomletea Sindi zawadi ya khanga iliyoandikwa ‘nikikosa nirekebishe’,
akalikumbuka tabasamu la binti huyu, kicheko chake na zaidi uzuri wake!
Tabasamu la Jerry likatoweka taratibu kichwa chake kilipoamua
kuirejesha siku ile ya mwisho aliyokuwa na Sindi….‘Wewe ni naniiii?.... wewe
sio Jerry John….wewe ni nani?....unataka nini kwangu?’ sauti ya sindi na
taswira yake akiwa amehamanika vibaya mno vilimjia moja kwa moja na kumfanya
afumbe macho na kuweweseka.
Akaiweka ile glasi ya mvinyo kwenye kabati dogo lililokuwa
kando ya kitanda na kukikamata kichwa chake kwa nguvu kana kwamba kuna mtu
alitaka kuking’oa.
‘Oh God please!..’ akarai huku akiligeukia lile kabati dogo
na kuitazam chupa ya mvinyo iliyokuwa kando ya glasi. Akaivamia na kuipeleka
mdomoni, akipiga funda kadhaa kwa pupa na kuitua ikiwa tupu.
Mwili ukamsisimka, wakati akikiinua kichwa na kuitazama picha
ya kuchora iliyoandikwa maneno matamu kuhusu Sindi, picha ile ilikuwa imebandikwa mbele yake. Akaitazama kwa
huruma mno wakati midomo yake ikimchezacheza na asijue la kutamka.
Haya ndio yalikuwa maisha yake, upande wa pili wa maisha yake
ambao ni Meddy tu ndio aliyeujua kwa undani. alijitahidi mno kuwa sawa mbele za
watu lakini kila usiku uliopita akiwa peke yake Jerry aliuweka uanaume kando na
kulia peke yake, akasononeka na kujiliwaza kwa pombe kali kutuliza mawazo na
maumivu.
Ala ile iliyokuwa imechachamaa sasa na vyombo kusikika
vikiomboleza katika namna ya kuvuta hisia ilizidi kumtia wehu Jerry. Akainuka
na kusimama kando ya kitanda akipepesuka
kidogo na kujitahidi kupiga hatua kuelekea kabatini. Akalifungua kabati
na kutulia kwanza akiwa ameshikilia milango ya kabati kwa pamoja. kisha taratibu
mkono wake wa kulia ukakiachia kitasa na kuzama ndani ya kabati. Akatoa bastola
ndogo na kuishikilia mkononi. Taratibu akatoka kabatini na kurudi kuketi
kitandani. Akiendelea kuitazama ile bastola huku machozi yakimtiririka…
88888888888888888888888888
Usiku huu haukuwa mgumu kwa Jerry peke yake bali pia Fiona
Agapella. wakiwa wameketi kitandani kwa Iloma. Fiona alikuwa anamtazama iloma
na kutikisa kichwa kulia na kushoto kuonyesha hali ya kukata tama
‘he won’t call… nimeondoka muda mrefu sana Iloma… alitakiwa
awe amepanic na kuanza kunitafuta… ona…’ akanyooshea saa iliyokuwa ukutani
‘Saa saba kasoro… na hajapiga simu yangu wala yako… hii
inamaanisha nini sasa?’ Fiona aliongea akitaka kushuka toka kitandani na Iloma
akamuwahi.
‘Wakati unaondoka alikuona?’ Iloma akamuuliza haraka na hivyo
kumfanya Iloma asitishe uamuzi wa kutoka kitandani pale
‘aliniona sana… hata wakati naweka nguo sandukuni he was
there..’ Fiona alijibu kwa hamaki kidogo
‘hakusema kitu?’ Iloma akauliza tena na Fiona akatikisa
kichwa kulia na kushoto mara kadhaa
‘okay Fifi…listen…’ Ilom akamkaribia rafiki yake na kumshika
mikono akitafuta maneno ya kumfanya pengine atulie na kulala japo kwa masaa
machache yaliyobaki.
‘ni masaa machache tu yamepita tangu uondoke… subiri kesho
asipokutafuta ndio tujue cha kufanya…’ Iloma akamshauri huku moyoni akimlaumu
rafiki yake huyu kwa kutikisa kiberiti kipindi kama hiki.
Fiona akatazama pembeni akiashiria kutokuukubali uamuzi ule
ila ndio vile hakuwa na jinsi
‘What is asiponitafuta si ndio nitakuwa nimeachika?’ Fiona
akauliza akionyesha dalili zote za maumivu ya moyo
‘atakutafuta Fiona!...trust me! na asipofanya hivyo tutajua
cha kufanya… come on Fiona where is the iron lady I used to know!...’ Iloma
alijaribu kumuweka Fiona sawa pamoja na kujua ukweli kuwa mwenzake alikuwa
katika hamaniko kubwa mno!
ukimya ukapita kati yao wakitazama chini kama watu
wanaofikiria kisha Iloma akainua uso na kumtupia Fiona swali.
‘dada yako Adella yuko wapi?’
Fiona akainua uso na kujitutumua kutabasamu lakini tabasamu
lile halikudumu usoni pake. machozi yalimlengalenga na akajikuta akiyawahi
kabla ya kuteremka mashavuni
‘Sijui kama yu hai au mfu… sijui… I just don’t know na sitaki
hata kujua’ Fiona akajibu akilazimisha tena lile tabasamu
‘Why?...’ Iloma akadadisi kwa shauku mno akijisogeza karibu
na Fiona. Kuna mengi mno alikuwa hayafahamu kuhusu huyu rafiki yake.
‘…ni long story but nilipotoroka kwa mjomba nilimuacha
akitumikishwa kama mkewe… miaka miwili baadaye nilimtafuta na nikamkuta
mjamzito…’ Fiona akasita kwanza akivuta kamasi nyepesi
‘… nikamtorosha na kwenda kuishi naye… alikuw kama mwehu…
nadhani sababu ya mateso na kubakwa… akajifungua mtoto wa kike na siku
aliyojifungua sikuwepo… akamtelekeza mtoto kwangu na kutokomea… sikumuona tena…
sikumuona tena adella… sikumuona tena dada yangu’ Fiona alitiririkwa na machozi
na kujiinamia.
Iloma akamsugua sugua mgongoni kumtuliza mpaka Fiona
alipoinua kichwa na kujaribu kufuta machozi.
‘sasa mtoto aliyemzaa yuko wapi?’ iloma akajikuta tu akiuliza
‘…Nilimuita Nadina… niliishi naye kwa kinyongo sana sababu alikuwa
damu ya mjomba… sikuwahi kumjali wala kumpenda… aliishi akijua mimi ni mama
yake na siku zote alishangaa namna nilivyokuwa nikimchukia… usiku mmoja
alipoteza pesa ya chakula… sikuwa hata na senti iliyobaki… nikampiga mno…
nikamuadhibu vibaya mno na kumfukuza… Nadina akaondoka… ni miaka mingi
sijamuona… sijui alipo… sijui’ Fiona aliongea taratibu safari hii akilitazama
shuka na kutiririkwa na machozi.
Iloma naye akafuta machozi na kutikisa kichwa kwa huzuni.
‘…nimeishi maisha yote mabaya duniani… then I met Sophia
Agapella… akanitoa mitaani na kunipa makazi na kazi, akanifanya ndugu yake wa
pekee kwa vile alikuwa yatima aliyelelewa katika kituo… akaniamini mno and see
what I did to her… nikamuua… nikamuua Sophy…’ akashindwa kuendelea na kulia
zaidi sasa kwa sauti kubwa ya kuombolez na Iloma akafanya kazi ya ziada
kumbembeleza.
ITAENDELEA….
kuna mengi nyuma ya pazia kuhusiana na fiona!!! good story laura!!!!
ReplyDeletemwisho wa ubaya aibu!!! fiona mwisho wake umefika
ReplyDelete