Sunday, November 17, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE(46)

46


Jua la adhuhuri lilishachomoza na makali yake yalichoma mara mbili ya jua la utosi. Hali ya hewa ilikuwa ya joto kali lisilovumilika kusimama juani pasi ulazima. Muda huu wa saa tatu asubuhi Mzee Okello alikuwa na pilika pilika za kujiandaa kutoka nyumbani kwake kuelekea kaika mihangaiko yake.

Mkewe Rebecca alikuwa amesimama kando ya kitanda akiokota shati moja baada ya jingine na kuyatundika mkononi kwa minajili ya kuyarudisha kabatini alikoyatoa ili mumewe achague shati la kuvaa.

‘… Jerry haelekei kuikubali ndoa yake na Pamella’ akaongea huku akihangaika kuifunga tai yake mbele ya kioo kilichokuwa mbele yake.Mkewe akaachana na shughuli ya kuokota mashati na kumtazama mumewe kwa mshangao kidogo

‘haelekei kivipi?’ Rebecca akauliza akiitumbulia macho taswira ya mumewe iliyokuwa ikimtazama kupitia kioo.
‘hataki kumuona Pamella…’ Mzee Okello akajibu naye akimtazama mkewe kupitia kioo

Rebecca akahamanika kidogo kiasi cha kutaka kuangusha hata yale mashati yaliyokuwa mikononi mwake.
‘zungumza na Kristus….talk to Agapella…’ Rebecca akazitupia kitandani zile nguo ambazo ghafla zikuwa nzito mikononi mwake mithili ya kiroba cha simenti. Akachapua hatua za haraka na kumfuata Mumewe pale kwenye kioo. Macho yalikuwa yamemtoka kuonyesha ni kiasi gani taarifa ile ilimchanganya.

‘…hatuwezi kumlazimisha Jerry honey! this is for Pamella… sitaki aende kuishi maisha ya kuburuzwa kwa vile tu sisi tumeamua… na isitoshe ameniambia ana mtu moyoni mwake tayari’ Mzee Okello akamjibu mkewe akiwa tayari amemaliza kuifunga ile tai na kuhamia kwenye vishikizo vya mikono ya shati. Akamnyooshea mkewe mkono wa kuume ili amsaidie kufunga kile kishikizo. mkewe akaukamata mkono na asijue hata aufanye nini.

‘honey!...’ Mzee okello akamzindua mkewe akimshangaa pia
‘Ooh.. but… why…’ Rebecca akababaika kidogo akijitahidi kuiweka akili yake sawa na kufunga kile kishikizo
‘Patrick Mazimbwe ni msomi na kaka yake ni mtu anayejulikana pia nadhani…’ Mzee Okello akajaribu kumtoa wasiwasi mkewe na asijue ni kiasi gani alizidi kumvuruga. Akakatizwa!

‘Sikubaliani na uamuzi wa Pamella kuolewa na Patrick…. honey just do something… just… I mean…’ akababaika tena na maneno yakipotelea mbali na kinywa chake.
‘nini kinakupa wasiwasi kuhusu Patrick?’ mumewe akamhoji na kumfanya amkodolee macho kwanza, kichwani mwake akilijibu lile swali
‘you fool!...Patrick ni baba yake mdogo’ akajijibu mwenyewe kichwani hali akimtazama mumewe usoni.

‘Becca!... najua unataka lililo jema kwa pamella…me too… she is my only daughter… nisingekubali chaguo lake kama lingekuwa linanipa mashaka… I know Dennis… na namjua Patrick personally… he is…’ akajaribu tena kuonoa ile hali ya mashaka kwa Rebecca lakini akakatizwa na mkewe haraka sana

‘… you are gonna talk to Agapella…right!?... sidhani kama huyo Patrick ni mwanaume bora kuliko Jerry… lazima ipo namna ya kuwaleta hawa watu pamoja… ni marafiki… na wako karibu na wanaelewana…baby do something please!’ Rebecca akambembeleza mumewe uso ukionyesha ni namna gani alitaka analoliomba litimie. Mzee Okello akamtazama mkewe kwa upendo, akimhurumia pia kwa ile hali ya kuhamanika.

‘Okay!... if that makes you happy… fine!... nipe muda na wewe zungumza na Pamella basi’ mumewe akatoa wazo na angalau uso wa Rebecca ukajaa nuru tena na lile tabasamu mantashau likachomoza na kumfanya Mzee Okello amtandike mkewe busu la pajini.

Wakaagana na Mzee Okello akatoka na kuelekea kwenye shughuli zake. Rebecca akaufunga mlango wa chumbani kwake na kutembea kwa kusuasua kurejea kitandani. Hofu ikionekana wazi usoni pake na ile hali ya kuhamanika ikijijenga mara mbili zaidi. Macho yake yalipepesa kwa kasi na kuzunguka huku na kule pasi hata kuelewa kilichopita mbele yake!

Hakuwa na maelewano mazuri na Pamella, kukomaa kwa mahusiano ya Pamella na Patrick kulimuumiza kichwa mno. Kivuli alichokiunda miaka mingi iliyopita kilikuwa kimeanza kumuwinda mwenyewe. Alichachatika asijue kipi cha kuacha kipi cha kushika!
8888888888888888888888888

Pamella Okello alisimama mlangoni kwa Jerry kwa takribani dakika kumi sasa akigonga kwa juhudi zote pasipo kufunguliwa.
‘Hey! huyu mtu hajatoka kweli?’ akamuuliza Mlinzi aliyekuwa anamwagilia bustani
‘hapana dada… sijamuona akitoka tangu asubuhi’ mlinzi akajibu
‘loh!...’ Pamella akashangaa akitoka pale kwenye ngazi na kuzunguka nyuma ya nyumba. Dakika moja baadaye akarejea ena mbele na kusimama umbali mfupi aliposimama mlinzi.

‘si umpigie simu dada?’ mlinzi akampa wazo
‘nimepiga tangu niko njiani… inaita tu haipokelewi’ Pamella akajibu akiyajaza hewa mashavu yake na kuitoa ile hewa kwa mtindo wa kupuliza moto. Mlinzi akaguna na kutupia chini mpira wa maji na taratibu akaufuata mlango na kujaribu kugonga. Akagonga kwa juhudi zote bila kuitikiwa.

Pamella akalifuata gari lake na kufungua mlango, akainama na kuzama ndani nusu akipekua huku na kule kisha akatoka na simu, akaibonyeza bonyeza na kuipeleka sikioni. mkono mwingine ukifunga mlango wa gari kisha akauegemea. Sekunde mbili tatu simu aliyopiga ikapokelewa.
‘… Meddy uko wapi…. yaani ndio nimekuwahi hivi… niko hapa kwake…na mimi nimepiga mpaka basi… uko wapi?... poa basi’ akakata simu na kumtazama mlinzi aliyekuwa anakuja upande ule akitokea mlangoni

‘Kaka Meddy amesemaje?’ Mlinzi akauliza
‘Yuko karibu hapo anafika sasa hivi… kumbe naye kampigia tangu alfajiri’
‘Aisee!’ mlinzi akashangaa akigeuka na kuutazama mlango ule wa kuingilia ndani kana kwamba ungempatia majibu ya maswali yaliyokuwa yakikimbizana kichwani mwao dakika ile.

Dakika mbili tatu, honi ikasikika nje na mlinzi akkimbilia getini. Alipohakikisha ni Meddy akafungua geti kubwa na Meddy akaingia na gari lake. Akateremka haraka na kumfuata pamella pale alipokuwa amesimama
‘Vipi?’ akamhoji Pamella
‘Kama nilivyokwambia simu haipokelewi na mlango umefungwa kwa ndani… chumbani kwake taa inawaka…we zunguka uko nyuma uone’ Pamella akamueleza hali halisi akimalizia maelezo yake kwa kumtazama Meddy anavyokimbilia huko nyuma kuhakiki alichoambiwa.

Akarudi uso ukiwa umesawajika, taharuki mwenzake bumbuwazi! Meddy alisimama mbele ya Pamella akiwa amejishika kiuno. Mawazo mabaya yote yakipishana kichwani mwake kwa kasi ya ajabu mno. moyo ukimuenda mbio mwanaume wa watu.
‘jana uliongea naye?’ akamuuliza Pamella
‘mmh mmh’ akakataa akitikisa kichwa kulia na kushoto

‘Dah!’ akashusha pumzi kwa nguvu zote kifua kikinyanyuka na kushuka sambamba na pumzi. Mlinzi akiwa katikati yao akiwatazama kwa awamu.
‘huna ufunguo wa ziada kabisa?’ Meddy akamuuliza Pamella
‘hata kama ukiwepo kuna vitasa vingine vya ndani Meddy…’ Pamella akajibu ile hali ya subira ikianza kumtoka na wasiwasi kuupamba uso wake

‘Mungu wangu!’ Meddy akasema chinichini akifinya uso na kufikiria mara mbili
‘Tupige simu polisi… wanaweza kujua nini cha kufanya’ Pamella akatoa wazo
‘and what if tukikuta wala hayupo humo ndani?’ Meddy akauliza

‘yupo… jana nimemfungulia geti mwenyewe… na leo sijamuona akitoka’ Mlinzi akaingilia kati sasa

Jibu lile likawafanya Meddy na Pamella watazamane mithili ya watu wanaosomana mawazo kwa wakati mmoja.
‘ooh No! God forbid it!...’ Pamella akapiga ukunga wa woga akijua ni nini yeye na Meddy waliwaza. Hali ya kuchanganyikiwa sasa ilimtembelea waziwazi, akavua viatu na kusimama peku akimtazama Meddy ambaye alitoa simu n kujari bu kuipiga tena simu ya Jerry. Akasikiliza ikiita mpaka kukatika. Kiwewe kikamfanya ahisi vipepeo tumboni.

Akatoka mbio mpaka mlangoni na kuanza upya kuugonga, akaugonga kwa jazba mno akiliita jina la Jerry.
‘Mpigie simu Mzee Agapella…’ Pamella akatoa wazo lingine wakati akitembea kumfuata Meddy mlangoni
‘Atafia kwenye simu yule Mzee… wait!... wait!’ Meddy akaonekana kupata wazo lingine. akatoka mbio mpaka sehemu ilipo stoo ndogo karibu na alipooegesha gari lake. Akachukua ngazi ndefu na kumpa ishara mlinzi kumfuata.

Wakakimbizana kule nyuma kuisimamisha ngazi kwenye lile dirisha la chumba cha Jerry. Meddy akapanda na kuanza kuhangaika na lile dirisha. Akahangaika nalo kwa muda kiasi cha kuhitaji iki na kile ili kulifungua. Baada ya mahangaiko makubwa Meddy akavunja kioo na kubinua vyuma viliyokuwa dirishani hapo.  Akafanikiwa kupata upenyo wa kuingia.

‘Yupo?’ Pamella akapiga kelele
‘yeah!’ Meddy akajibu akianza kujipenyeza kuingia ndani.
Akatua kwa taabu na kukimbilia kitandani alikokuwa Jerry. Alikuwa amelala chali sehemu ya kichwa mpaka kiuno vikiwa kitandani na miguu ikiwa imening’inia chini. mdomo wake ulikuwa na mapovu kiasi. Akamkagua kwanza huku akijaribu kupima mapigo yake ya moyo.

Ghafla akawakumbuka akina Pamella, akatoka mbio mpaka sebuleni na kuhangaika na mlango. Alipoufungua tu Pamella akampita kwa kasi mpaka chumbani.

‘Jerry… Jerry’ akahamanika machozi yakiwa yameshamvamia, akamshika shika Jerry akijaribu kumuamsha, wakati akimruka na kwenda upande mwingine akakanyaga kitu mguuni.

taratibu akaachana na papara ya kumuamsha na kutazama kile alichokanyaga. Bastola! Akakodoa macho kwa juhudi zote akipiga yowe kubwa kumuita Meddy huku yeye akiruka kurudi upande aliokuwa.

Meddy akaingia akiwa na jagi la maji pamoja na kitambaa mkononi
‘Hey nini?’
‘ona hapo chini’ akamuonyesha mahali alipoikanyaga ile bastola. Meddy akasogea kwa tahadhari na kuinama kutazama kile alichoonyeshwa. Mwili ukamsisimka!

Haraka akatua lile jagi la maji chini, akitupia kile kitambaa begani na kuanza upya kumkagua Jerry.
‘naona hajaitumia’ akawatoa wasiwasi Pamella na Mlinzi aliyekuwa amesimama mbali kabisa

Wakaanza kazi ya kumhudumia, kumrejeshea fahamu, wakati wakihangaika huku na kule ndio wakagundua licha ya kunywa pombe kali, Jerry alikuwa amemeza vidonge vya usingizi vilivyokuwa vimetapakaa kitandani.
‘Mpigie dokta wao aje haraka…’ Meddy akatoa maagizo

saa moja baadaye Jerry alikuwa amelala kitandani, huku daktari akiwa amemaliza kumhudimia. Akawaomba watoke na kumuacha apumzike kwanza. Meddy na Pamella wakamfuata daktari sebuleni. Wakazungumza machache na kisha daktari akaondoka zake.

Pamella akalia kichinichini kiasi cha kumfanya Meddy amkumbatie na kumbembeleza
‘He’ll be fine…’ Meddy akamtuliza
‘But why?.... why Meddy?... pombe…dawa… bastola… kuna nini?... ana matatizo gani?’ Pamella akahoji akilitiririkwa na machozi. Meddy akameza funda la mate kwa juhudi kubwa akijaribu tu kujizuia kutomueleza ukweli Pamella. Ndani ya nafsi yake alijua ni Sindi Nalela ndiye aliyekuwa anammaliza rafiki yake.

Aliogopa mno! aliogopa si kitoto, yote aliyokuwa anamuonya rafiki yake kuwa angekuja kufanya kitu cha kijinga yalikuwa yanaanza kujitokeza. Akakumbatia Pamella kumfariji na kuifariji nafsi yake pia!
888888888888888888888888888

Sindi Nalela na Nadina walikuwa wameketi mbele ya mwanamke mwenzao mwenye umri ulikaribia miaka thelathini na ushee. Alikuwa kiongozi wa danguro lao. Alionekana mara chache sana katikati yao. Maneno ya chinichini yalidai alishastaafu kazi ya kujiuza na sasa alikuwa akimsaidia Adella kusafirisha madawa ya kulevya.

Mwanamke huyu mwenye sura ya upole na wajihi wa kuvutia aliwatazama mabinti hawa kwa awamu na kusikitika sana. Walimkumbusha mbali sana, walimkumbusha miaka mingi iliyopita alipoingizwa ndani ya jumba lile akiwa na miaka 16. Kumbukumbu zile zilimjia na kutoweka, akatabasamu na kumtazama Sindi kwa kina.

‘mabinti!... nimeongea mno na Adella kuhusu ninyi… nadhani ni wakati muafaka tuongee kitu kilicho mbele yenu na kilicho wazi… labda mnawaza mpambane mpaka mwisho na kama kufa ufe kishujaa… Adella hawezi kuwaua ni utajiua mwenyewe na dhambi ya kujiua ni yako… Adella hawezi kukuondoa hapa na akikuondoa ujue unapoelekea ni sehemu mbaya  zaidi…’ akatulia kidogo akisoma umakini wa hawa mabinti mbele yake. Walikuwa wanamsikiliza kwa makini kuliko alivyotarajia

‘…Adella hana roho tena ya imani, hana utu tena ni ili uelewane naye ni ufanye vile anavyotaka na ikiwa bahati yako utachukuliwa na mtu anayeeleweka na kuyakimbia haya maisha…. vinginevyo mateso utakayopitia I swear hutakaa uwe sawa kiakili maishani mwako!’ akawatisha

‘…tangu niingie hapa mpaka nianze kutoka hapa kwa safari za Adella na kurejea sijawahi kujua hapa ni wapi na nafikaje… umeshaingia mtegoni, umeshaingia jehanamu… kubali yaishe… vinginevyo kile mlichopitia jana ni kama salamu ya kuanzia siku…huwezi kutoroka ukafika mbali na hawezi kukuachia utoroke..’ yule dada aliongea kwa hatua na Sindi akashusha pumzi ndefu kuashiria kukata tama

‘Nina mimba!’ akajikuta akipayuka na kumfanya Nadina amtolee macho
‘Nini!?’ yule dada akauliza kwa mshangao
Sindi akaitikia kwa kutikisa kichwa juu chini mara kadhaa machozi yakivamia mboni zake
‘umeitoa wapi?...’ yule dada akauliza ule mshangao sasa ukipanda zaidi na kumfanya atoe macho yake kana kwamba sindi alikuwa akipungua kimo kila sekunde

Sindi akajiinamia na kulia kwanza kabla ya kujieleza, akitumia stori ile ya kubakwa na kutelekezwa. Akiuficha ukweli kuhusu Jerry Agapella. Taharuki ndogo iliyozuka pale ikatulia baada ya dakika kadhaa na yule dada akatumia busara zake kumjaza Sindi ujasiri.

‘…kuna wakati inakupasa kupitia mambo magumu sana maishani kwa ajili ya mtu Fulani… Adella akijua una mimba sasa hivi anaweza kuitoa kwa nguvu…cha msingi tulia na ufanye kilicho mbele yako mpaka pale utakapotimiza miezi sita… then nitabeba jukumu la kumwambia Adella kuhusu mimba yako… hataweza kuitoa kwa kipindi hicho na nitakupigania ujifungue salama…’ yule dada akaongea akiwa amishika mikono ya Sindi kwa nguvu zote. Alitaka amuelewe

‘unanisikia?.... unanielewa?... niahidi utatii sheria za hapa for the sake of your kid…sawa?... vinginevyo utampoteza na utabaki na uchungu usiosahaulika… Sindi!...unanielewa?’ akasisitiza kwa mtindo wa swali na Sindi akaitikia kwa kichwa
‘nakuahidi…. i promise… nitakusaidia kumuweka mtoto wako mikononi mwako ila tafadhali usijaribu kufanya chochote kitakchokuingiza katika mateso au kipigo…sawa?’ akauliza tena na Sindi akaitikia safari akionekana kuwa na nguvu

Nadina akatabasamu, tabasamu la uchungu, tabasamu la maumivu. Akamkumbatia Sindi aliyekuwa anatiririkwa na machozi. Yule dada akawatazama kwa huruma naye akajikuta akilengwa na machozi.
‘Naitwa Tima… wakati wowote ukinihitaji njoo chumba namba 25 kule karibu na lilipo jengo la mapokezi’ akawatoa katika ile hali ya kukumbatiana na kuzungumza nao. Wakamshukuru na yeye kuondoka.

Sindi Nalela akaligusa tumbo lake. Ilishatimia miezi miwili sasa. Mabadiliko kadhaa ndani ya mwili wake yalimjulisha uwepo wa kiumbe kile tumboni. Alimkumbuka Jerry mno. kitu kama majuto ya kumkimbia kilimjia kila siku.

Alitamani kuurudisha nyuma wakati na siku ile aliyomkwepa Jerry nyumbani kwa Dennis ijirudie naye amufungue mlango na kumkabilia. Ampe nafasi ya kujieleza, amwambie yeye ni nani hasa… lakini alikuwa amechelewa. Maamuzi yake ya hasira na pupa yalikuwa yamemuingiza katika mtihani mkubwa zaidi maishani mwake!
888888888888888888888888

Wiki kadhaa baada ya Fiona Agapella kuondoka nyumbani kwake na kwenda kuishi na rafiki yake Iloma. Kristus Agapella, mumewe Fiona hakujishughulisha kumtafuta wala kumuulizia popote.  Zaidi ya kuacha ujumbe kwa mlinzi kuwa Fiona akirejea asiruhusiwe kuingia ndani mpaka yeye awepo.

Fiona aliporejea na kupewa taarifa alichanganyikiwa na kukimbilia ofisini kwa Dennis Mazimbwe, mwanasheria wa Kristus Agapella. Bahati haikuwa yake, Dennis alikuwa hayupo nchini kwa kipindi hiki. Akalazimika kumsubiri mpaka arejee wakati huo akiishi na Iloma.

Jioni hii tulivu, Iloma alikuwa eneo eneo lake la kazi katika duka kubwa la dawa katikati ya jiji. Akiwa sehemu ya kulipia. Iloma alikuwa mbele ya kompyuta yake ya kazi akiiingiza baadhi ya vitu muhimu katika kompyuta huku bega lake la kushoto likiwa limebana simu iliyokuwa sikioni.

‘Fifi hebu tulia kwanza basi… kama Dennis hayupo basi msubiri mpaka aje si umeambiwa ndani ya wiki atarejea…. sasa tatizo liko wapi…. mumeo angekuwa ananifahamu ningeenda kuongea naye sasa mtu hanijui kabisa nikaanze kujitambulisha upya …. sidhani kama ndio amekuacha… hapana… mi sidhani bwana… una makosa ndio ya kuondoka bila kuaga unaenda wapi… Sikiliza dear…’ iloma akatulia kwanza kusikiliza upande wa Fiona ulivyokuwa ukilalamika

Ni dhahiri alikuwa amechanganyikiwa vibaya mno. Mlango wa duka la dawa ukafunguliwa na mwanaume mrefu, mtu mzima akiwa ameambatana na kijana wa makamo wakaingia. Uso wa iloma ukachanuka. Alikuwa Kristus Agapella!

Alitembea taratibu kumfuata Iloma pale alipokuwa na Iloma akajikuta akiharakisha maongezi
‘Hey hivi unasikiliza?’ Fiona akauliza kwa hasira
‘Dear ngoja nihudumie mteja’ iloma akakata simu na kujilazimisha kutabasamu
‘habari yako’ Kristus akamsabahi na iloma akaitikia akiwa amemtolea macho mzee wa watu. Kristus akamtulizia macho kwanza kisha akaeleza shida yake.

‘Oh… nenda upande ule wa mwisho… au ngoja’ Iloma akajiinua toka kitini na kumuongoza Kristus eneo lilipo dawa alizohitaji. Akamueleza hiki na kile kulingana na mahitaji yake kisha kumuonyesha mtu anayeweza kumsaidia zaidi.

Iloma akarejea eneo lake la kazi. Wakati akijiweka sawa simu ikaanza upya kuita na mpigaji akiwa Fiona. alipotaka kupokea akamuona Kristus Agapella akija upande ule aliokuwepo. Akaondoa sauti ya mlio wa simu na kuitupia kwenye droo. Mzee Kristus akaifikia meza ya Iloma na kuweka mezani dawa alizochukua.
Iloma akafanya kazi yake na wakati huo Kristus akimtazama usoni katika namna ya kuvutiwa na Iloma.
‘Unaitwa nani?’ sauti nzito ya Kristus ikamtoa Iloma kwenye kazi yake
‘Oh mimi?’ akauliza swali badala ya kujibu na kumfanya Kristus acheke
‘Yes wewe!’ akamkazia macho Iloma
‘Iloma..’ akajibu akibana midomo yake na kutawaliwa na aibu za kike
‘ wow!jina zuri…’ Kristus akalisifia jina lake huku akipokea mfuko wa dawa na kumpatia yule mlinzi wake.

Akatoa wallet yake na kulipia kisha akadondosha na noti mbili za elfu kumi juu ya chenji aliyokuwa amewekewa mbele yake, akamalizia na business card kwa juu.
‘ukipata muda utanipigia… na natumaini hutaniangusha’ Kristus akaongea akifunga wallet
‘oh no no no… asante tu’ Iloma akakataa kupokea zile pes na kadi lakini jicho la Kristus likamlainisha na akajikuta akiipokea kwa shingo upande
‘Sio lazima pia… kama you don’t feel comfortable kunipigia then it is okay… keep the money… tupa kadi’ akazungumza Mzee Agapella, akimuaga Iloma na kuondoka.

Iloma akaduwaa na zile pesa mkononi sambamba na ile kadi. Macho yalimtoka maradufu ya mwanzo. akaikumbuka ile simu kwenye droo. Alipotoa akakuta missed call 3 za Fiona mke wa Kristus Agapella. Kichwa kikamzunguka kama tiara!

ITAENDELA…..

1 comment:

  1. mtenda hutendwa!!! hya sasa mzee agapela kwa iloma!!! fiona atatoa mtu roho

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger