Leo mgeni wangu ni Mhadhiri wa chuo kikuu cha St. Augustine
University of Tanzania, bwana Robert Mkosamali. Pasi kupoteza muda karibu
utiririke na mtiririko wa maswali toka
kwa Blogger wako Laura Pettie…. Karibu sana !
MHADHIRI WA SAUT
BW. ROBERT MKOSAMALI
Laura Pettie Blog: Kwa maneno
matatu tu, unamwelezeaje Robert Mkosamali?
Robert Mkosamali: Haahaaa! Ninaweza
kumwelezea Robert J. Mkosamali kama mtu simple, straight forward na
hardworking!
Laura Pettie Blog: Kitu gani kilikuvutia kujiunga na tasnia ya
habari? Is there any motivational story behind?
Robert Mkosamali: Kitu
kilichonivutia kuingia katika tasnia ya habari ni umaskini uliokithiri wa
watanzania hasa wale wanaoishi katika mikoa ya pembezoni. Mikoa hii mbali ya
kuwa katika hali ngumu ya maisha ilikosa waandishi wa habari ambao wangeweza
kuelezea matatizo ya watu walio ndani ya mikoa hiyo na hivyo kuifanya serikali
iweze kuchukua hatua.
Nakumbuka
miaka ya 1993 kulikuwa na mfumko wa wakimbizi mkoani Kigoma lakini kwa bahati
mbaya maisha ya watu wa Kigoma yalionekana kuwa duni kuliko hata yale ya
wakimbizi kutokana na mashirika mengi ya kimataifa ........
na ya ndani kuelekeza nguvu nyingi kuwasaidia wakimbizi ilhali wenyeji wakitumia rasilimali zao chache kuwahudumia wakimbizi hao kwa takribani miezi mitatu kabla ya kuingia kwa mashirika ya kimataifa.
na ya ndani kuelekeza nguvu nyingi kuwasaidia wakimbizi ilhali wenyeji wakitumia rasilimali zao chache kuwahudumia wakimbizi hao kwa takribani miezi mitatu kabla ya kuingia kwa mashirika ya kimataifa.
Kungekuwa na waandishi wa habari wakati huo nchi
ingefahamu ni kwa kiasi gani wenyeji wenye hali duni sana nao walihitaji msaada kama hao wakimbizi.
Hii ndio ilikuwa motivation yangu kuingia katika tasnia hii ya habari.
Laura Pettie Blog: Ni
kwa miaka mingapi umekuwa mhadhiri wa chuo cha SAUT na unafundisha kozi gani?
Robert Mkosamali: Nimekitumikia chuo
Kikuu cha Mtakatifu Augustino kwa miaka 14 sasa nikifundisha kozi mbalimbali kama vile news writing
and reporting, introduction to computers na kwa sasa ninashughulikia zaidi
masomo ya utangazaji kwa njia ya radio yaani radio broadcasting.
Laura Pettie Blog: Kama si
kuwa mhadhiri, unadhani ungekuwa unajishughulisha na nini sasa?
Robert Mkosamali: Kama si kuwa mhadhiri
nadhani ningejikita katika utabibu wa binadamu. Naona tasnia hii bado ina
mahitaji makubwa ya watumishi waliobobea na mahitaji ya watu ni makubwa sana . Watu wanapoteza
maisha kwa sababu ya kukosa huduma nzuri hasa vijijini. Hii ilikuwa ndoto yangu
tangu nikiwa nasoma o-level na ilikuwa ni moja ya mambo yaliyonifanya kufanya
vizuri katika masomo ya sayansi.
Laura Pettie Blog: Kuna madai ya wahadhiri wa kiume kudai rushwa ya ngono toka kwa
wanafunzi wa kike vyuoni. Unalizungumziaje hili suala?
Robert Mkosamali: Rushwa ya ngono
imekuwa si suala linaloongelewa tu katika vyuo vikuu lakini hata maeneo ya
ajira mpya wahitimu wa kike wanapata matatizo makubwa katika kupata ajira mpaka
pale wanapokubali kutoa rushwa ya ngono.
Suala la rushwa la ngono vyuoni
linadidimiza maadili ya taifa, linawafanya wanawake kuwa wanyonge na kuwaondolea
hali ya kujiamini……linashusha hadhi ya elimu nchini kwani linawafanya watu
wenye uwezo na kujiheshimu kuonekana hawana uwezo kielimu na kuwapa wale
wahitimu wa kike wenye kukubali suala la rushwa ya ngono lakini hawana uwezo
kimasomo waonekane kuwa wana uwezo wa kielimu lakini kiutendaji hawana uwezo
wowote.
Ni suala baya ambalo
linapaswa kupigwa vita mno…..Ni tatizo la kitaifa na litaendelea kulitafuna
taifa kama
hatua thabiti hazitachukuliwa kuliondoa tatizo hili.
Laura Pettie Blog: Hivi Karibuni kumekuwa na malalamiko/ dhihaka na shutuma dhidi
ya wanahabari mnaozalisha vyuoni. Wengi wanatuhumiwa kukosa maadili ya kazi/
upeo na weledi mkubwa kuhusiana na majukumu yao .
Unalizungumziaje hili tatizo na unadhani linaletwa na nini?
Robert Mkosamali: Tatizo la
kukosekana kwa maadili na weledi kwa wahitimu wengi wanaozalishwa na vyuo vingi
Tanzania unatokana na
sababu nyingi.
Pili, tasnia ya habari
imeingiliwa na watu wasiokuwa waandishi. Hivi sana
kumekuwa na majina mbalimbali mfano waandishi wa habari makanjanja nk. Wamiliki
wa taasisi za vyombo vya habari wanawaajiri watu wasiokuwa na sifa zinazotakiwa
na hivyo kuwaharibia wale wenye mafunzo ya uandishi wa habari. Inawezekana
wanaochafua maadili na weledi wa uandishi wa habari ni wale wasiokuwa na
mafunzo ya maadili uandishi wa habari.
Tatu, ni kukosekana kwa
waalimu waliobobea katika masuala ya uandishi wa habari na vifaa vya kujifunza
kwa vitendo uandishi wa habari. Vyuo vingi vinapata shida ya kuwa na wanafunzi
wengi wasioweza kuwahudumia kwani kuna uhaba wa walimu wa kufundisha masomo
husika. Pengine mwalimu anaweza kuwa mzuri kwa nadharia lakini mafunzo kwa
vitendo kwake ikawa ni shida hii inawasababishia wanafunzi kuwa na maandilizi
hafifu na wanapoingia sokoni wanaonekana hawawezi kitu.
Nne, kukosekana na ushirikiano
duni kati ya vyuo na taasisi za habari nchini. Ni wanafunzi wachache wanaoweza
kupata nafasi ya kupata mafunzo kwa vitendo katika taasisi za habari nchini.
Wakati mwingine wale wanaopata nafasi wanakosa 'mentors' ndani ya taasisi hizo
za habari na kuwafanya wanafunzi hao kupoteza muda wao kufanya yale
yasioyotegemewa.
Tano, tasnia ya habari kwa
sasa inakumbwa na mabadiliko makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya
technologia. Leo msukumo wa habari umekuwa katika "New media" na
inasikitisha kuwa ni vyuo vichache sana Tanzania
vinatia msukumo kuwafundisha watu kutumia "new media" au mitandao ya
kijamii nchini. Tuanhitaji mabadiliko katika tasnia ya habari kuwawezesha
vijana wetu kuwa na maadilili na weledi uliotukuka.
Sita, Tasnia ya habari
imekuwa si sehemu salama kwa waandishi. Mauaji na vitisho vimeongezeka kwa kasi
na kuwafanya waandishi makini toka vyuoni kukimbilia tasnia nyingine kwa ajili
ya hofu ya usalama wao. Wachache wasiokuwa na jinsi wanaonekana kubaki na
kuendelea kuitumikia tasnia hii.
Hizi ni baadhi tu ya sababu
zinazobabisha kukosekana kwa weledi na maadili kwa wahitimu walio wengi
wanaozalishwa na vyuo leo hii.
Laura Pettie Blog: Kiingereza kimekuwa
kikitiliwa mkazo zaidi katika masomo ya uandishi wa habari mf. kuwepo kwa somo
la communication skills. Ni kwanini hakuna somo la Kiswahili ili kuwajengea
wanahabari umahiri katika matumizi ya lugha ya taifa ya Kiswahili kwa ufasaha?
ikizingatiwa asilimia 80 ya vyombo vya habari nchini vinatumia lugha ya
Kiswahili kuwasilisha taarifa zao.
Robert Mkosamali: Lugha si kitu.
Ukiwa na weledi unaweza kufanyakazi kwa kutumia lugha yoyote! Mwandishi
anapaswa kujua lugha mbalimbali ili kumuwezesha 'audience wake kujua yanayojiri
duniani. Fikiria leo anakuja waziri mmoja wa ufaransa na mwandishi hajui
kifaransa atawezaje kumhoji waziri huyo ili kupata habari kwa ajili ya
'audience' yake.
Dunia
ya leo inatutaka tuwe "multilingua" ili kuweza ku"interact"
vizuri na watu na kupata habari toka vyombo vingine vya kigeni kwa lugha
mbalimbali ili tuweze kuwahudumia walaji wa habari zetu kwa weledi wa hali ya
juu. Kutumia kiswahili peke yake kutawafanya watanzania kuwa watu wanaoweza
kuhudumia soko la ndani na kushindwa kuajirika katika soko la dunia. Tunahitaji
kubadilisha mitazamo yetu ya ndani na kuwa na mawazo mapana zaidi yenye
kutufanya kuona mbali.
Laura Pettie Blog: Unaizungumziaje tasnia ya habari kwa ujumla nchini Tanzania . Je
inakidhi matwaka ya jamii kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni?
Robert Mkosamali: Kwa kiasi fulani
tasnia ya habari imeweza kukidhi matakwa ya jamii kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni. Tatizo kubwa linaloikumba tasnia hii Tanzania na Afrika kwa
ujumla ni aina ya mafunzo tuyatowayo kwa waandishi wetu. Leo mwandishi anajua
habari kubwa ni siasa pekee wakati kuna habari nyingi ambazo zinapendwa na watu
pia.
Tatizo
hili linatokana na kutokuwepo na specilized training in journalism vyuoni.
Tungependa kuona kuna watu waliobobea katika nyanja za kimataifa, nyanja za
uchumi, nyanja za utalii, nyanja za usalama, na hata nyanja za utamaduni. Waandishi
walio wengi ni wale "wanaoweza kuandika kila kitu" "Jack of all
trades but masters of none".
Tunapaswa
kurudi nyuma na kufikiri tunawezaje kuwaandaa vijana wetu as specialized
journalist kama ni mtu wa masuala ya Bunge basi anajua
taratibu za bunge na anaweza kuibua masuala yaliyofichika bungeni. Mtu kama
huyu atawezakuwa na "jicho la tatu" la kuona yale watu wengine
wasiokuwa wataalamu katika eneo lake kuweza kuyaona. Kwa
jinsi hiyo tutaweza kusema mahitaji ya watu yanatimizwa kwa kiwango kikubwa.
Lakini hili litawezekana
iwapo mfumo wa umiliki wa taasisi za habari na utawala ndani ya taasisi hizo
utaacha kuyapa kipaumbele maslahi ya watu binafsi na kujikita katika
kujatumikia maslahi mapana ya umma.
Laura Pettie Blog: Katika
jamii yoyote yapo makundi ya watu wenye mahitaji maalumu. Watu hawa kama
vipofu, walemavu wa ngozi, jamii ya viziwi na kadhalika ni watu wenye haki ya
kupata habari na elimu husika. Je unadhani vyombo vya habari nchini na taasisi
za elimu kama
vyuo vinakidhi mahitaji ya hawa watu kuanzia kupata elimu ya chuo inahusiana na
masuala ya habari hadi kupokea habari? Na katika miaka yako ya uhadhiri
umeshawahi kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu chuoni?
Robert Mkosamali: Kama ilivyo katika
jamii yetu watu wenye mahitaji maalumu wamekuwa hawapewi kipaumbele. Angalia
mifumo yetu ya kijamii, angalia vyombo vyetu vya usafiri nk, havitoi huduma
maalumu kwa watu kama hao. Hali kama hii pia ipo katika vyuo
vyetu. Tuna wanafunzi wasioona, wasiosikia, wenye ulemavu wa ngozi lakini
hakuna huduma maalumu zinazotolewa kwao hata kujenga uelewa wa jamii juu ya
uwepo wa watu hao na kutafuta namna bora ya kuweza kuwahudumia.
Hali hii inajitokeza pia
katika vyombo vya habari. Hakuna sheria, sera au mwongozo wowote unaozitaka
taasisi za habari hasa za runinga kuwaajiri watu wenye uwezo wa kutafsiri alama
kwa ajili ya watu wasiosikia. Au kuwepo magazeti yanayoandikwa kwa lugha ya
wasioona kuweza kuelewa taifa linakwendaje ili nao wawezekufanya maamuzi sahihi
kutokana na taarifa wanazozipata.
Katika miaka yangu kama
mhadhiri hapa chuo kikuu cha mtakatifu Augustino nimepata kuwafundisha vijana
wasiosikia na wenye ulemavu ya ngozi. Kitu kikubwa nilichogundua ni kuwa watu
hawa wana uwezo mkubwa wa akili hata zaidi ya watu wenye kusikia na kuona pale
ambapo tunawapa attention ya kutosha. Nilimfundisha mwanafuzi mmoja mwenye
tatizo la kusikia na nilishangazwa sana na
uwezo wake darasani. Nilipaswa kutumia multimedia approach kumfundisha
broadcasting na kwa jinsi hiyo aliweza kufanya vizuri.
Laura Pettie Blog: Wasomi wengi ikiwemo wahadhiri wameonyesha mwamko wa kujiingiza
katika chaguzi za kisiasa. Je wewe umewahi kufikiri kujiunga na siasa?...
Kwanini?
Robert Mkosamali: Kwa kweli sijawahi
kufikiria kujiunga na siasa na si mwanachama wa chama chochote cha siasa.
Sababu inayonifanya nisijiunge na siasa ni kuwa naona siasa za leo ni za ubabe
na zisizojali mahitaji ya watu wa chini. Tunasoma, kusikia na kuona ndani ya vyombo vya habari
kukosekana kwa dawa hospitalini na watoto wanakufa, maliasili ya Taifa inatoweka
na vijana wanangamia kwa dawa za kulevya. Ni kazi ya siasa safi kujenga maisha
yenye matumaini kwa watu.
Uchumi umekuwa neema kwa
wanasiasa na si kwa watu wa kawaida. Tunawezaje kuitumia siasa kuboresha maisha
ya watu? Tunahitaji viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuyabadili maisha ya
watu na si wale wenye nia ya kujineemesha wenyewe na familia zao.
Baadhi ya vyama sasa
vinataka umiliki wa uongozi wa nchi hii na kuufanya wa familia. kwa nini
turudishe utemi au uchifu katika siasa za kidemokrasia? Bado kuna changamoto
nyingi sana
katika siasa ambazo hazinipi hamu ya kuwa mwanasiasa! Kwa nini hakuna wagombea
binafsi? haya ni baadhi ya mambo yanayonifanya niwe mtazamaji katika siasa za Tanzania .
Laura Pettie Blog: Katika
muda wako wa ziada unapendelea kufanya nini?
Robert Mkosamali: Katika muda wangu
wa ziada ninapenda kujisome vitabu, kutazama TV hasa zenye habari na wanyama na
kuwahudumia ng'ombe wangu na kuwatembelea watu wa kawaida kujifunza maisha yao .
Laura Pettie Blog: Ukipewa nafasi ya kupata chakula cha usiku na watu watatu wa
kaliba yoyote toka popote duniani, ungependa watu hao wawe akina nani?
Robert Mkosamali: Nikipewa nafasi ya
kupata chakula ningependa kuwa na watu wa kawaida na wanaharakati
wanaowahudimia watu hao ili kuwaunganisha kuwawezesha kujua ni changamoto gani
watu hao wanazo na ni namna gani wangependa changamoto hizo zitatuliwe. Watu wa
kawaida watatoka vijijini zaidi.
Kwa mantiki hiyo kwa kuwa
siwezi kuwaalika wote hao watu watatu nitakaopenda kula nao ni Rais Mstaafu wa
Marekani Bill Clinton, Pope Francis na Rais Paul Kagame.
Laura Pettie Blog: Ni sehemu gani duniani
ambayo unatamani kutembelea, nab ado hujabahatika kutembelea sehemu hiyo.
Robert Mkosamali: Sehemu ambayo
ningependa kutembelea ni nyingi sana . Lakini ninaona
bado kuna sehemu nyingi vijijini nchini Tanzania ambazo sijapata
kuzitembelea na kujifunza tunu mbalimbali za makabila yetu Tanzania .
Hivi karibuni nimetembelea
Mbulu nikajifunza simulizi nzuri ya binti mmoja wa Kiiraq aitwaye Imbori
aliyehukumiwa kifo kwa kutoswa msituni kwa sababu ya kupata ujauzito kabla ya
kuolewa lakini akaokoka. Simulizi hii ilinifanya nitengeneze Documentary ili
kuwawezesha watanzania wengine ni aina gani ya maisha watu wa makabila mengine
waliyaishi katika kusimamia maadili ya makabila hayo.
Hivyo nikipata nafasi ya
kuyatembelea makabila hayo nitawezajifunza maisha mengine ambayo sikuyajua!
Kwa upande mwingine nilipata nafasi ya
kuishi katika baadhi ya nchi za ulaya kama Italy ,
Ufaransa na Belgium na
hivyo ninahisi ninahitaji kujifunza zaidi kutoka tunu za makabila yetu Tanzania .
Laura Pettie Blog: Kila binadamu anazaliwa na kipaji chake, na wengi wetu
tunajikuta tukikua na kuzeeka pasipo kugundua talanta tuliyobarikiwa. Kwa
upande wako unahisi una kipaji gani?
Robert Mkosamali: Mimi nadhani kipaji changu ni
ufundishaji. Hili linatokana na ukweli kuwa kwa muda mrefu nimekuwa nakimbia
kazi hii lakini Mungu siku zote amenirudisha kuifanya. Baadaye nimejikuta
naipenda na kuwafanya wanafunzi wapende yale ninayowafundisha.
Mwaka jana Mwnafunzi wangu
mmoja alipata zawadi ya kuwa mmoja wa washindi wa EJAT na mshangao mkubwa
Mwanafunzi wangu huyu bwana Noel Thomson alinitunuku (dedicated) zawadi hiyo
mimi. Hili tendo lilinigusa sana na
nilihisi machozi kunitoka. Nilimshukuru Mungu na Noel Thomson kwa tendo hilo .
Kijana huyu alilitangaza
tendo hili facebook hata bila kunishirikisha kuonyesha ni namna gani
nimemsaidia katika kuifikia hatua hii. Kijana huyu pia amefanikiwa kupata
zawadi nyingine mbili za EJAT mwaka huu. Mungu aendelee kumbariki.
Kuna wanafunzi wangu wengine
wanaofanya vizuri katika utangazaji katika taasisi za habari za Kimataifa kama BBC
na Radio France Internationale. Matunda haya yananifanya niamini kuwa kipaji
changu ni ufundishaji!
Bw. Mkosamali alipowatembelea wanafunzi aliowahi kuwafundisha ambao sasa ni watangazaji wa Radio France internationale (RFI)- Pichani akiwa na wanafunzi hao
Laura Pettie Blog: Unapendela muziki gani na
mwanamuziki gani chaguo lako namba moja?
Robert Mkosamali: Ninapenda Country
music na mwanamuziki chaguo langu namba moja ni Kenny Roggers. Lakini hata
hivyo nimekuwa na mapenzi makubwa na blues na kundi jingine la muziki kama Abba na Maddona
pia
Laura Pettie Blog: Kitabu gani cha simulizi ni chaguo lako namba moja?
Robert Mkosamali: Ninapenda kusoma
Gifted Hands cha Ben Carson japo nimevisoma pia vitabu kama Think Big and Big
picture na Take Risk. Kitabu nilichosoma cha zamani ni "Something for
Joey" ambacho kinazungumzia mtoto mmoja alikuwa mgonjwa wa Lukemi, Joey
aliyempenda kakake John Capalletti aliyekuwa maarufu katika American College
Football. Siku moja alipopata zawadi ya Kitaifa iliyotolewa na Makamu wa rais
wa marekani aliamua kumtunukia mdogo wake Joey kwa kuwa chanzo cha msukumo wa
mafanikio yake katika hali yake ya Ugonjwa.
Laura Pettie Blog: Ni nini Falsafa yako?
Robert Mkosamali: Falsafa yangu ni
katika ubongo kuna sehemu iliyolala ambayo inaweza kuwa chanzo cha mabadiliko
katika maisha ya kila mmoja. Tunapaswa kuyapa maisha mtazamo mpya! Kwa kuiamsha sehemu hii ya ubongo!
Laura Pettie Blog: Jina la ubini wako
linafanana na la mbunge wa Muhambwe bw. Felix Mkosamali. Je una undugu na Mbunge
huyu?
Robert Mkosamali: Yap ! Mbunge wa
Muhambwe bwana Felix Mkosamali ni mdogo wangu. Yeye ni mtoto wa baba yangu
mdogo ndugu Francis Mkosamali aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Kibondo wakati wa utawala wa Nyerere na baadaye wakati wa Mwinyi. Kwa sasa Mzee
wetu amestaafu siasa!
Laura Pettie Blog: Ni kitu gani watu wengi hawakifahamu kuhusu wewe?
Robert Mkosamali: Kitu
wasichokifahamu kuhusu mimi ni vigumu kukijua. Lakini nadhani wengi hawajui kama elimu yangu kwa
asilimia kubwa, ukitoa shule ya msingi nimesomea shule za misheni kwa msaada
mkubwa wa Mhashamu Askofu mkuu Paul Ruzoka, Fr. Hans Peters and Shirika la
wamisionari wa Afrika yaani the White Fathers na St. Augustine University of
Tanzania. Kwa kweli ninawashukuru sana kwa msaada wao huo.
Laura Pettie Blog: Swali la mwisho, una neno gani la ziada kwa jamii?
Robert Mkosamali: Neno la ziada
katika jamii ni kwamba mababu wana mchango mkubwa katika maisha ya wajukuu wao.
Naona jinsi nilivyo imetokana na ukaribu mkubwa na Marehemu babu yangu Late
Daud Mkosamali aliyenifanya kuwa rafikiake wa karibu na kuniwekea ndoto za
kupenda elimu mbali ya kwamba yeye hakusoma na alikufa huku hajui kusoma wala
kuandika.
NASHUKURU SANA BW.
ROBERT MKOSAMALI KWA KUUTOA MUDA WAKO KWA AJILI YA MAHOJIANO HAYA…..NASHUKURU SANA KWA
HILI!....NIWASHUKURU PIA WASOMAJI WA BLOG HII AMBAO KWA NAMNA MOJA AMA NYINGINE
MMENISUKUMA KUMTAFUTA BW. MKOSAMALI ILI
KUPATA MACHACHE TOKA KWAKE
NI TUMAINI LANGU UMEJIFUNZA KITU KWA NAMNA MOJA AMA NYINGINE
SHUKRANI KWA KUWA NASI!
big up pettie
ReplyDeleteNimeipenda sana hii interview. Hongera Laura you sound professional.... Ikuze talent yako kwa kufanya vipindi vya tv....
ReplyDeleteSafi sana Petty, nashauri pia ufikirie kuwa na Tv program.. Kupitia mawazo yako mbalimbali naona una mafanikio makubwa sana mbeleni. Salam na Big up nyingi kwa Mr.Mkosamali, amejibu maswali yote kisomi sana. We always proud of You Sir"
ReplyDeleteNDIVYO INAVOTAKIWA IWE.. UMEHAMIA LEVEL NYINGINE HONGERA SANA
ReplyDelete