Saturday, June 29, 2013

SINDI....NA LAURA PETTIE (23)

23

kwa uso uliojaa mashaka vile vile, Pamella aliukorokochoa mlango wa chuma na kuufungua huku akiusukumia mbele kule alikosimama Fiona. Sasa wakatazamana uso kwa uso, paji kwa paji hali Fiona akijaribu kujenga tabasamu ambalo hata hivyo halikudumu usoni pake.



Pamella aliyekuwa bado akimtazama kwa jicho la kuuliza kulikoni, hakukumbuka hata kumkaribisha mgeni yule ndani.
‘tunaweza kuzungumzia ndani’ Fiona akamshtua  Pamella

‘Yeah…karibu…karibu ndani’ Pamella akamkaribisha, na Fiona alipoupita mlango  wa mbao na kuingia ndani.
Pamella aliuvuta ule mlango wa chuma na kuufunga hali uso ukisinyaa na kukunja ndita kadhaa, macho yakikimbizana huku na kule kama mtu aliyetafuta majibu ya maswali ambayo pengine hata hakuyakumbuka. Alichachatika ghafla!

Akashusha pumzi na kuufunga ule mlango wa mbao kisha kumgeukia mgeni wake ambaye alikuwa amesimama wima wima akitembeza macho yake sebuleni pale.
‘Nice house!’ Fiona akamsifia Pamella ambaye alijitahidi kutabasamu
‘Asante…karibu uketi’ Pamella alijibu na hapo hapo akikumbuka alikuwa amesahau hata kumkaribisha mgeni wake sofani.

Fiona akaketi na Pamella akalifata kochi lingine na kuketi. Uso wake ukitanuka kidogo wakati akimtazama Fiona ambaye alishusha pumzi ndefu kidogo na kumtazama Pamella kwa kituo.
‘Long time no see Pam…. umetususa sana’ Fiona alimuongelesha lakini alichoongea si kile Pamella alichotaka kukisikia. Alitamani kumshurutisha Fiona aseme haraka lililomleta asubuhi ile kama mvuzi wa dagaa ziwani.

Pamella akatabasamu tena na nidhahiri tabasamu lake halikutoka moyoni, liliufanya uso wake uonekane kama mtu anayejiandaa kusafisha meno yake ya mbele na kisha kufumba kinywa ghafla. Alijikakamua mno!

Fiona naye akawa kama mtu anayetafuta pa kuanzia na asijue
‘Unaishi mwenyewe?’ Fiona akamtupia swali ambalo lilimfikishia ujumbe Pamella kuwa Fiona alikuwa akizungusha maongezi bila mpango. Akakereka lakini hakutaka kukurupuka!
‘yeah..’ akajibu kiufupi akiunda tena lile tabasamu lake feki na kulikata mara moja
‘Okay!... umepanga au ulinunua nyumba?’ Fiona akatupa tena swali lake na Pamella uvumilivu ukafikia kikomo.

‘What do you want Madam!’ akamtandika swali na uso wa Pamella ukionyesha kutotaka kuendeleza masikhara ya mahojiano ya  kama karani wa sensa. Fiona akamtulizia macho Pamella usoni kama mtu aliyekuwa naisoma akili ya Pamella. Kwa hili alimbabaisha Pamella kidogo na akaonekana kubabaika

‘Jerry yuko wapi?’ Fiona akamsukumia Pamella swali lenye uzito wa kutosha kumfanya aachame mdomo wake na kutoa macho kama mtu aliyetandikwa kibao cha ghafla na mtu asiyemuona
‘una maana gani?’ Pamella akajikuta akilijibu swali kwa kuuliza swali na akili yake ikifanya kazi kwa kasi ya ajabu.

‘Jerry ameonekana mahali akiwa na gari lako’ Fiona akazidi kumuwehusha Pamella ambaye hamaniko lililosomeka usoni pa Pamella lilimfanya Fiona ahisi alilotaka kulijua alikaribia kulijua kwa marefu na mapana.

‘Come on Pam…. unajua alipo si ndio?’ akambana zaidi Pamella ambaye alinyanyuka na kutembea hatua kadhaa akionekana kuduwaa lakini pia kichwa chake kikifanya kazi ya kumkumbusha ni siku gani Jerry alilirudisha gari lake alilokuwa analitumia. Akalipata jibu na likamtuliza nafsi haraka sana! Akamgeukia Fiona akiwa ameukunja uso wake vile vile.

‘Jerry??’ akamuuliza Fiona na sasa akipata nguvu ya kumshangaa Fiona. Mara ya mwisho Jerry kuliendesha gari lake ilikuwa ni wiki moja na siku kadhaa zilizopita, ilikuwa inaelkea wiki ya pili sasa. Kama ni kweli Fiona alimuona wiki mbili zilizopita ni kwanini hakumfuata siku ile ile. Akapata jibu Fiona alikuwa ameletewa taarifa na mtu!

‘Yes! Jerry ndio na alikuwa akiendesha gari lako’ Fiona akajibu kwa kujiamini naye akisimama wima. Wanawake hawa wakatazamana kwanza kila mmoja akitabasamu na akiwaza lake kichwani.

Pamella akacheka kwanza, akacheka kicheko cha dharau kilichochanganyikana na waiswasi
‘I wonder….Jerry ameonekana akiendesha gari langu….  kutafutwa kwake kulihusisha polisi pia….sasa Madam how come uko hapa all alone unanipa taarifa za kunisakama… nilidhani ungeongozana na mumeo na polisi?’ Pamella akamuuliza Fiona ambaye alionyesha kuhamanika na kule kubanwa na Pamella

‘He is my son!’ Fiona akafoka akitetemeka kwa hasira
‘tangu lini?....lini?... tangu lini Jerry is your son…come on may be wewe ndio unayejua nini kilimkuta Jerry na labda wewe ndio unayejua yuko wapi…. kabla hujatupachikia kesi wengine kwanini kesi isianzie kwako?’ Pamella sasa akaongea kwa kujiamini akimfuata Fiona kwa ukaribu zaidi.

Hali ya kubabaika kwa Fiona ilimfanya Pamella acheke tena
‘Nenda kachange karata zako tena…. and make sure Mr. Agapela knows where is his son …right?…now with due respect…get out of my house!’ Pamella akamtwanga Fiona mkwara uliomfanya amung’unye midomo yake tu pasipo kupata neno la haraka.

Fiona akaikwanyua pochi yake na kutoka pale sebuleni pasipo kumuaga mwenyeji wake wala kumtazama Pamella. alipotoka na kulifuata gari lake nje ya geti la nyumba ya Pamella. Huku ndani Pamella alilipoteza lile tabasamu alilokuwa nalo na hofu iliyochanganyikana na tahamaki ilimvaa na kumfanya atumbue macho kwa bidii huku akizunguka pale sebuleni.
‘hizi sio dalili njema kabisa…’ aliongea mwenyewe akigosha gosha vizole vyake

Kule nje, Fiona alikuwa garini akionekna kuwa na hamaki ya kumtosha kushuka na kutembea kwa miguu na kulisahau hata gari lake.
‘Damn!,,,shit…No…no…’ akalaani akipiga na mayowe ya hasira huku akiubamiza usukani kwa ghadhabu. Alikuwa akihema kwa hasira, wasiwasi na mashaka ya  siri yake kubumburuka.

Tangu Jenifa alipomweleza kuwa alimuona Jerry wiki iliyopita akiwa na gari la Pamella, Fiona hakulala, alihisi kuandamwa na kivuli cha Jerry ambaye alishajua yum fu siku nyingi. Kuonekana kwake hakukuwa dalili njema hata kidogo.
888888888888888888888888

Kulishakucha vizuri na jua kuchomoza, Sindi alikuwa amejifunika gubigubi kitandani wakati Jerry alipokuwa akivaa nguo zake baada ya kutoka kuoga. Moyoni alihisi kusutwa na kile alichokifanya lakini kwa upande mwingine alijisikia raha mno. alijisikia mwanaume haswa kwa kitendo alichofanya alfajiri ya siku hiyo. Aliyatazama mashuka aliyoyatoa kitandani na kuyatupia katika tenga  la nguo chafu akatamani kuyabeba na kumpelekea Meddy kama ushuhuda.

Alipomaliza kuchomekea shati lake alimfuata Sindi kitandani na kumgusa lakini Sindi alimtandika kipepsi kikali akikataa kule kuguswa. Hali ile ilimfanya Jerry atabasamu zaidi. Ni aliifirahia ile hali ya Sindi na hapo hapo akimuone huruma pia. Akamuacha, akiweka pesa za matumizi hapo kitandani na kuondoka.

Sindi aliposikia mlango ukifungwa alifunua shula lake na kulala chali. Alfajiri ikipita kichwani mwake na kukumbuka kilichotokea, Jerry alivyomdhibiti kisawasawa na kutimiza azma yake.

 Alitaka kumlaumu Jerry lakini akakumbuka Jerry aliiomba ruhusa yake nay eye akaikubali bila kufikiria mara mbili. Akafumba macho na kusikilizia maumivu ya hapa na pale, kisha taratibu akajiinusha na kujiburuza kidogo kuufuata ukingo wa kitanda, akateremsha miguu chini.

Alitaka kusali lakini moyo wake ukawa mzito mno, akaachana na sala kwanza, akashuka kitandani na kutembea kwa shida kidogo kuufuata mlango. Wakati akilivuka kochi kuufuata mlango akaiona simu ya Jerry kwenye sofa ikiita. Akaitazama na kutaka kuachana nayo lakini akakumbuka Jerry alishaondoka hivyo si ajabu alikuwa akipiga kuhakikisha kama simu ilibaki nyumbani.

Akaichukua ile simu na kutazama jina la mpigaji
‘Pam?’ akajiuliza mara baada ya kusoma jina la mpigaji. Akatulia kidogo na kuamua kuipokea
‘Hallow’ akaipokea na kusikiliza kwa makini.

Pamela aliyekuwa naipiga ile simu aliduwaa kuiskia sauti ya mwanamke kupitia simu ya Jerry. Haikuwahi kutokea. Moyo wake ukapiga mara mbili zaidi, wivu ukimtembelea maradufu na akajikuta akiikata ile simu pasipo kuongea lolote.

Sindi akashangaa na kuguna kisha akairudisha simu sofani na kuelekea nje alikokuwa anaelekea.  Mpaka anawasili kwa Meddy na kubadili nguo na kuwa Jerry halisi. Bado alikuwa hajagundua kuwa simu yake ilikuwa imebaki nyumbani.

Meddy aliyekuwa akiandaa kifungua kinywa jikoni kwa kukaanga mayai, aligeuka na kumtazama Jerry aliyeingia pale jikoni
‘Bado sijaamini…’ Meddy alongea akicheka
‘Aisee….hebu cheki kwanza…’ Jerry alitanua shingo ya t shirt yake na kumwonyesha alama ya kung’atwa na meno aliyoiacha Sindi begani mwake. Meddy akacheka zaidi baada ya Jerry kumwonyesha alama za kuparuzwa na kucha na kufinywa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Wakati wakiongea hili na lile, kengele ikasikika ikilia na Meddy akamuomba Jerry amshikie ile kazi aliyokuwa anafanya ili akaisikilize ile kengele.
Dakika moja baadaye Jerry alimsikia Meddy akibishana na mtu sebuleni.

Akasogea kidogo na kusikiliza! akaitambua ile sauti haraka sana… Alikuwa Pamella
‘Utaua mtu??? Meddy alishangaa na maneno yake yalimfanya Jerry akaribie kuangusha kikaangio
‘I love Jerry….I love him Meddy…Please help me het him back to me…please’

‘Sikuelewi Pam’ Meddy akaonyesha kushangaa ile hali ya Pamella kuwa kama aliyechanganyikiwa

‘I love Jerry jamani….i want him back..’ Pamella sasa alikuwa analia na Jerry akaduwaa huku ndani na kikaangio kimtoka mkononi na mlio wa kikaangio kudondoka ukawafanya Meddy na Pamella watazame kule mlio ulikotokea….


.....USIKOSE TOLEO LIJALO....UNA MAONI GANI MSOMAJI.....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger