Haya jamani mpo wana kona ya urembo na Laura?
Kama umepata nafasi ya kujumuika nasi hapa, ukaisoma makala
hii, basi tuna kila sababu ya kumshukuru
Mwenyezi Mungu!
Leo nataka kuongea na akina dada weusi… weusi tiiii kama mimi
ambao bado hawajajikwangua au ndio wanafikiria kujikwangua. Anti wewe ni mzuri
tu, …..na weusi wako huo ulionao…..unaweza kuendelea kuwa mzuri hivyo hivyo
ulivyo!
Kuna watu wanadhani kuwa mweupe ndio kuwa mzuri, ndio kuwa
mrembo, ndio kuwa mlimbwende! HAPANA!!.... si kweli! Hata ukiwa na weusi wako
huo huo ulionao bado unaweza kuamua kujiweka katika namna ya kuvutia na
ukavutia. Siku zote vile utakavyosimama mbele za watu ndivyo watu
watakavyokuchukulia…. Ukijiamini watu nao
watakuamini pia!!
Nimepaka wanja na Lip Balm tu!....
usoni hata poda ya kawaida haijapita
Katika pitapita zangu mitandaoni, hivi karibuni nimegundua
kumekuwa na ongezeko la bidhaa za kujichubua. Tena wauzaji wakisifia kabisa
kuwa unakuwa mweupee, unatakata, unakuwa na rangi f’lani amazing n.k kana
kwamba kuwa mweusi ni laana au uchafu!
Huwa nasikitika sana ninapoona feedback ya bidhaa hizi
kwenye picha ambapo mtu aliyekuwa na
weusi wake mzuri tu amekuwa mweupe na ndio anasifiwa kuwa amependeza na amekuwa
mzuri.
Uzuri ni vile unavyowaza wewe na unavyojichukulia! Miaka fulani nikiwa mtoto mdogo nilikuwa na rafiki yangu aliyekuwa
mweupe sana……. Namna alivyojipenda na kujisifia kila mara kuhusu rangi yake alikaribia kunifanya niamini
mimi sikuwa na rangi nzuri hata kidogo hata hivyo kila nilipojitazama
niliipenda rangi yangu pia.
Ni mweusi lakini mzuri tu!!
Nilitaka kuanza kuamini weupe ni uzuri mpaka siku moja
tukiwa wawili mbele ya watu fulani, mtu mmoja akasema kwa sauti…Laura usije
ukajichubua baadaye baki hivyo hivyo una rangi nzuri sana! Rangi adimu! Mweusi
anaweza kuwa mweupe lakini mweupe hawezi kuwa mweusi!
Kumsikia mtu akiisifia ngozi yangu kulinipa kujiamini sana,
na sasa ndio nikagundua watu wengi wanasikia watu wakisifia weupe wanadhani
weupe ndio uzuri (kama mimi nilivyokuwa
nasikia rafiki yangu akijisifia sana)…..kwa kuwa ni nadra kwao kusikia mtu
akiwasifia kwa ngozi zao nyeusi (kama mimi nilivyosifiwa)….
Wakati naingia usichana,
mama yangu aliniambia kila mara usije ukajichubua baki hivyo hivyo huoni mimi
nilivyo mzuri tu (mama yangu ni mweusi pia)… kumsikia mama akisema hivi kulinijaza
ujasiri zaidi na leo naweza kumwambia mtu yoyote mweusi BAKI HIVYO HIVYO ULIVYO
HUONI MIMI NILIVYO MZURI TU HAHAHAHAAAAA!!
Ni mweusi Ti! na bado ni mzuri tu
na anajikubali mpaka weupe tumemkubali!
Yaani unakuta mtu kajichubua ana sugu balaaa, mwingine
mashavu yameungua….mwingine mpaka ndevu zimemtoka… mkorogo umembabua miguu
yaani unamtazama unamhurumia maana badala ya kuwa mrembo anakuwa kituko
kwelikweli…. Mwingine mweupe kama karatasi yaani mpaka unajiuliza yote haya juu
ya nini jamani?
Anyway, unawezaje kutunza
ngozi yako nyeusi na ikavutia?
MAMBO 10 YA KUZINGATIA
1. KUNYWA MAJI MENGI…. Kunywa maji kadiri uwezavyo, Uvivu wa
kunywa maji unachakaza ngozi na badala ya kuitibu watu hukimbilia makemikali
kuing’arisha kinguvu wakati kumbe maji ni dawa nzuri sana!.... najitahidi lita
1 hadi mbili kila siku! ukiona hayana ladha weka vionjo kama limao kwa mbali au ndimu.
2. Safisha ngozi yako kwa vitu visivyo na kemikali, pendelea
vitu natural hata kama ni vya kizungu ila vyenye ingredients natural…. Mfano usoni
napenda sabuni ya Liwa, zile natural kabisa au zile zinazofungwa kwenye cover
ya kahawia zimeandikwa sandwool soap bee and flower!
3. Tumia vipodozi vinavyoendana na ngozi yako…. Poda,
foundation etc viwe vya ngozi yako vitakupa muonekano mzuri sana.
4. Kula chakula bora hususani matunda na mbogamboga
usisubiri uandikiwe na daktari
5. Fanya mazoezi- mazoezi mepesi tu ambayo yatakutoa jasho
kidogo. Ukiwa mvivu wa mazoezi kama mimi, weka hata muziki wa bolingo ucheze
mpaka jasho likutoke. Jasho linapokutoka unapunguza uchafu mwili na ufungua
vitundu vya kwenye ngozi hivyo ngozi hupumua
6. Kuwa na furaha…. Stress kuleta makunyanzi! Haijalishi una
msukosuko kiasi gani katika maisha, Jifunze kujipa nafasi ya kutabasamu na
kushukuru japo hata kwa uhai ulionao. Usiweke vitu moyoni au kichwani kiasi cha
kukunyima furaha kwa muda mrefu. Unapokosa amani ya moyo unakosa usingizi ambao ni chanzo cha ngozi kuharibika
7. Jipende, Jithamini, Jiamini…. Jifanyie mambo ya
kupendeza, jisikie wewe ni wa kipekee, jizawadie, jipambe, jitunze, jiheshimu. Usikubali mtu akuaminishe wewe ni mbaya kwa kuwa ni mweusi.... unapojipenda utagundua staili ya nywele inayokufaa...staili ya wanja inayokufaa... rangi ya lipstick inayokupendeza...yote haya utayagundua ukijipenda kwanza!
8. Ielewe ngozi yako- Je una ngozi kavu, una ngozi ya mafuta
sana au ya kawaida. Ukiijulia ngozi yako itakusaidia uepuke vipodozi vyenye
mafuta ambavyo vinaweza kukuletea chunusi… au kutumia vipodozi vikavu huku
ngozi yako ni kavu
9. Usibadili badili vipodozi kufuata mkumbo- kwa kuwa
umesikia kipodozi fulani kinatangazwa sana basi unakitafuta na kujaribu…
vipodozi au vifaa vya kusafishia ngozi unavyotumia vikikukubali tulia navyo tu
usihangaike kubadilibadili vitu.
10. Jifanyie Scrub za asili, massage, steaming nk kuondoa cell
zilizokufa kwenye ngozi na kuipa uhai zaidi. Scub husaidia sana kuondoa cell zilizokufa na vijimakovu na alama nyeusi.
Wewe dada uliye mweusi tulia na weusi wako!
Usirubunike kuchubua ngozi yako ukiamini ndio utaupata
urembo
Hivyo hivyo ulivyo unaweza kuamua kuwa mrembo
Najivunia kuwa mweusi kwa kuwa sasa naweza pita mahali
nikajikuta ni mweusi peke yangu na nikaonekana na mvuto kuliko hata hao weupe
hihihiiii
ADIOS!!!
No comments:
Post a Comment