Tumeshukuru Mungu!
Kwa mara nyingine tena
tunakutana hapa kusoma makala hii ya UREMBO na Laura. Ni jambo la
kipekee kwa kweli. Mwaka umekuwa mgumu sana huu!
Haya siku ya leo nakuletea tiba ya kuondoa makunyanzi usoni.
Kuna vijana, ni vijana tu wala uzee haupo karibu leo wala kesho lakini wana mikuno
usoni Ashakum si matusi utasema ngozi ya
goti!
kuna makunyanzi ya paji la uso, ya pembeni ya macho, chini ya macho, kwenye mistari ya tabasamu na hata kidevuni.
Makunyanzi, kuna umri unafika hayaepukiki, ndio vile umri
umeenda. Ulaya uko wanafanya mpaka upasuaji wa kunyoosha ngozi. Ila kwako wewe
kijana tu hapana!....narudia hapana huna haki ya kuwa na makunyanzi
kabisaaaaa!!
Makunyanzi yanaletwa na mambo mengi mno. Seli zilizochoka
usoni na hazijaondolewa, Mwili hauna maji ya kutosha, lishe yako ni duni, una
stress, na kuna makunyanzi mengine wanasema ni ya kigenetic tu au namna unavyoukunja uso wako… lakini hii haimaanishi
usipambane nayo. Mwenzangu uso mchovu mwisho ukooo mjini kila mtu softi tachi hahahahaa! sasa wewe wa wapi hapa mjini?
Tunaishi mara moja katika maisha haya ya duniani, kwanini
usijipende tu, ukajihudumia na ukajifurahia kujiona ukipendeza, ukiwa na ngozi
ya kuvutia tena kwa kutumia mambo ambayo hayana gharama kabisa.
Wakati mwingine
tunakosa umaridadi na mvuto si kwa kuwa hatuna pesa za kumudu gharama za
mahitaji ila hatujipendi au tunaendekeza uvivu tu wa kuandaa hiki na kile ili
kuuleta umaridadi. na wakati mwingine nyuso zinakosa mvuto kwa kuwa tunatumia vipodozi visivyo sahihi vyenye kemikali.
NJIA ZA KUONDOA MAKUNYANZI USONI
Zipo njia nyingi sana. Kuha mafuta, krimu, vidonge, upasuaji
na kadhalika. Ila mimi nitakupa njia moja ya kiasili ya kuondoa makunyanzi.
MAHITAJI….
1. TANGO
2. NYANYA
JINSI YA KUFANYA….
1. Osha yango lako, kata kipande likiwa na ganda lake. Usimenye!
2. Hicho kipande kitwange kwenye vile vinu vidogo ya jikoni
au saga
3. Osha nyanya yako na ukate nusu , yale maji maji ya ndani
ya nyanya yakamulie kwenye Tango ulilosaga AU wakati unatwanga tango au kusaga
tupia kipande cha nyanya, kidogo tu
4. Osha uso na kausha kwa taulo safi…nasisitiza sana kutumia
vitu visafi kukausha uso. Maana kuna wakati rashes zako zinatokana na taulo tu
unalotumia. Labda limepigwa sana vumbi hapo unapolining’iniza au hujalifua siku
mbili tatu. Taulo la uso ni kitu cha muhimu sana kufuliwa mara kwa mara jamani.
Ukishaosha. Paka mchanganyiko wako kuzunguka uso mzima
5. Kaa kwa nusu saa hadi saa nzima. Ukipata sehemu yenye
upepo itakauka haraka sana
6. Ikishakauka, wakati wa kuondoa. Chovya vidole kwenye maji
na usugue ule mkauko polepole. Nasisitiza polepole jamani…. Hasa sehemu zile
zenye mikunjo.
7. osha uso wako na maji safi, na sabuni unayotumia kisha
kausha uso na uuache upigwe na upepo kidogo kabla hujapaka chochote
Fanya hivi kadiri unavyoweza iwe kila siku, iwe mara mbili au tatu kwa wiki. Ni wewe tu na juhudi
zako ila lazima makunyanzi yataondoka ama kupungua saaaaana. Utapata ngozi f’lani ng’aavu maana
nyanya inang’arisha uso.
TUKUTANE TENA PANAPO MAJAALIWA….