Wednesday, June 1, 2011

WARAKA WA MWISHO....3 Na Laura Pettie

Tuliongozana kuelekea garini. Dakika kumi na tano baadaye tulikuwa sinza kwa Remmy nilikokuwa naishi na mchumba wangu Sakina.

Tulimkuta mdogo wangu Edna akiandaa chakula mezani hivyo muda mfupi baadae tulijiunga mezani na kupata chakula cha mchana pamoja na Bonny hali maongezi yakizidi kupamba moto.

“Maisha bwana kitendawili! Hivi ulitegemea kuwa siku moja utakuja kuwa mtu wa kuishi mwenyewe ndani mwako bila sapoti ya washikaji” bonny aliniuliza huku akijimiminia maji ya kunywa katika glasi yake na kugugumia mafunda kadhaa.

“aah! Wapi bwana lakini ndio hali halisi hivi Martin Totoz yuko wapi?” Nilimtupia swali Bonny wakati tukiiacha meza na kurejea sebuleni. Bonny aliachia tabasamu na kumtazama Sakina aliyekuwa hana habari na mazungumzo yetu kisha taratibu akanikonyeza.

Nilimuelewa hakutaka kuzungumzia habari za huyo Martin Totoz tukiwa pale na Sakina karibu. Tuliongea mengi na kukumbushana hili na lile. Mwishowe Bonny aliaga na kushukuru kwa mapokezi tuliyompa. Nilimuomba Sakina aniruhusu nimsindikize Bonny kwa vile usiku ulishaingia naye bila hiyana aliniruhusu.

Sakina, kama kuna siku ambayo nailaani basi ni siku hii uliyonipa ruhusa hii ya kumsindikiza Bonny. Ni huko ndiko kulikotokea chimbuko la mimi na wewe kutengana hivi, naogopa hata kumsingizia shetani kuwa ndiye aliyenipitia .

Tukiwa njiani kuelekea nyumbani kwa Bonny maeneo ya mbezi beach Nilimkumbushia tena Bonny juu ya wapi aliko Martin Totoz ambaye tulimpachika jina la Totoz kutokana na tabia yake ya kupenda wanawake bila kubagua rangi. Umri wala maumbile. Bonny aliachia tena tabasamu na kuniambia

“tunaishi karibu kabisa, yaani kwangu na kwake pua na mdomo”
“wacha bwana!” nilistaajabu
“ tena tupite kwake atakuwa yupo tu, siku hizi katulia kidogo” alisema Bonny
“Martin katulia! Aah! Wapi kwani ameoa?” nilimuuliza hali nikiyahamisha macho yangu toka mbele na kumtazama Bonny kwa mshangao

“Ana kifaa hicho bwana si mchezo! Yaani ni new model ya kisasa automatic baba!” tuliangua kicheko kwa kauli hiyo ya utani na ni wakati huo Bonny alikatiza kicheko na kunionyesha kona moja fupi ilibeba njia iliyoishia katika geti moja jeusi lililokumbatia ukuta wa kadri uliosujudia nyumba ya ghorofa moja.

“Martin anaishi hapa!”Bonny alitamka hayo huku akilikaribia geti la nyumba ile ya vigae na kupiga honi. Punde kijana mmoja alifungua geti na kuja mbio mpaka upande ule alioketi Bonny.
“shikamoo Mzee” alimsabahi kwa heshima kubwa na akionekana wazi kumfahamu Bonny
“Marhaba, mzee yupo?”

“Hapana ametoka kidogo lakini alinipa maagizo kuwa kama mtu akija kumtafuta amngoje”

“sawa kijana!” Bonny aliitikia na kuanza kulielekeza gari kuelekea ndani ya nyumba ile nikajikuta natabasamu baada ya kuona mtu kama Bonny kijana wa miaka thelathini na ushee akiitwa mzee.

Ilikuwa nyumba ya kisasa mno. Bustani kadhaa za maua na miti ya matunda ilileta mandhari tulivu yenye harufu ya kipekee. Kwa vyovyote ungepata jibu la kuwa wanaoishi hapa walikuwa na neema ya maisha haswa! Magari mawili ya kisasa yalikuwa yamepaki upenuni mwa nyumba.

Tuliteremka garini na moja kwa moja Bonny kama mtu aliyepazoea pale alinielekeza mlangoni na sote tukajitoma na kuivamia sebule kubwa iliyotapakaa mapambo ya kila namna. Makochi aghali, zulia la hariri na vitu kadha wa kadha vilivyonifanya nitunduwae tu!

Mwanzo ndio huoooo ITAENDELEA....

No comments:

Post a Comment



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger