Monday, June 16, 2014

UREMBO NA LAURA:...KANUNI ZANGU 10 ZA KUWEKA USO WA MWANAMKE KATIKA HALI YA KUVUTIA

Uso ni moja ya sehemu ya mwili yenye ngozi ‘sensitive’ sana, n kiwa na maana si sehemu nzuri kufanyia majaribio yoyote kwa vile ni rahisi kuungua, kutoa vipele, kuwasha nk mara tu mambo yanapoenda sivyo ndivyo.
Uso ni utambulisho wa mtu na kwa sisi wanawake uso ni sehemu inayotuumiza kichwa sana inapotokea kuwa katika hali isiyovutia. Kwa kutambua hili Blog ya LauraPettie inakujia na makala mbali mbali za urembo zenye nia ya kukuweka fresh usoni na sehemu zingine za mwili.
Kwa kuanzia leo naomba nikupe KANUNI 10 ambazo mimi binafsi nazifuata  kama njia ya kuuweka uso wangu safi. Tunaanza na hizi njia kumi kisha matoleo yajayo  ndio nitaweka aina za vitu na njia za kusafisha ngozi ya uso na kukupatia muonekano maridadi kabisaaaa tena kwa gharama nafuu!!!

1. USISHIKESHIKE USO KILA MARA:

Uso wangu ukiwa bila kipodozi chochote tayari kwa kufanya scrub ya unga wa liwa

…. Kuna watu wana mazoea ya kushika uso kila mara, iwe kwa kufuta jasho au kutumbua tumbua vipele. Mikono yetu inashika vitu vingi vyenye bakteria. Mf. Pesa, sehemu zenye vumbi nk. Unapopeleka mkono usoni kila mara unahamisha bakteria wa mikononi kwenda usoni na kama nilivyosema ngozi ya uso ni kitu sensitive ni rahisi kuleta harara usoni. Jijengee mazoea na kutogusa uso mara kwa mara na ikiwezekana tumia kitambaa au tishu safi kufuta uso pale inapokulazimu. Ondoa mazoea ya kugusa gusa uso utaona mabadiliko!


2. USIKAMUE VIPELE VIGUMU:

…. Mara kadhaa tunaweza kujikuta na vipele au chunusi ngumu usoni ambazo hazijaiva kiasi cha kuhitaji kutumbuliwa. Ondoa mazoea ya kutumbua vipele kwani kwanza huleta maumivu makali ya kichwa na  pili huzalisha makovu usoni. Acha kipele kiive na tumia tissue safi kukikamua taratibu ili kuondoa kile kiini cha ndani cheupe… osha uso wako kwa sabuni yako unayotumia kila siku. Endapo kinachukua muda mrefu kuisha fanya Scrub (nitakuletea aina za scrub za asili ambazo zitakusaidia kupoteza vipele hivyo)

3. USIPAKE VITU TOFAUTI TOFAUTI USONI:

… kuwa na aina moja ya kipodozi unachotumia kwa muda mrefu. Epuka kupaka poda au losheni tofauti tofauti usoni. Tumia ile iliyokuzoea na unapoamua kubadili kitu hakikisha unaelewa hicho kitu unachotaka kujaribisha kina mchanganyiko wa vitu gani… ukiuelewa uso wako utajua kipi cha kupaka na kipi cha kuepuka.  Unaposafiri au kwenda mahali beba vipodozi vyako mf. Poda ili kuepuka kupaka chochote utakachokikuta ugenini. usijaribishe vipodozi kwa vile tu vimeikubali ngozi ya rafiki yako.

4. TUMIA TAULO SAFI MAALUMU KWA USO:

…. Jaribu kuwa na taulo dogo  maalumu la kufutia uso unapotoka kuoga. Fikiria taulo unalokaushia miguuni lipite tena usoni. Hakikisha Taulo hilo linafuliwa mara kwa mara na itakuwa rahisi kwa kuwa ni dogo…. Hakikisha linakaa sehemu ambayo halipati  vumbi kirahisi. Unapotundika kitaulo hicho karibu na dirisha unalijaza vumbi linalopita dirishani kisha baada ya kuosha uso unalipitisha tena usoni, huku ni kupaka uchafu usoni. 

5. BADILI PILLOW CASE COVER MARA KWA MARA:

… unalala na cover ya pillow wiki nzima khaaa!... ondoa ondoa ondoa kila baada ya siku tatu…mbona chupi hurudii?.... jaribu kuzingatia hili pia utaona mabadiliko makubwa kama huwezi kubadili mpaka wiki iishie basi baada ya siku tatu tandika khanga safi juu ya pillow na uitumie kwa siku zinazobaki kisha ondoa vyote na ufue…. Acha uvivu!

6. SAFISHA USO ASUBUHI NA USIKU:

…. Hii iwe kama sheria!...ninaposema kusafisha namaanisha kufanya cleansing. Hapa na kuna aina tofauti tofauti za product kwa ajili ya kusafisha uso. Kwa watu wa kipato cha kawaida zipo ESKINOL za tango, papai, limao, tikiti nk.  Kwa bei ya elfu 3 tu unapata moja ambayo utakuwa unaitumia asb na usiku. Unainyunyuzia kwenye pamba kidogo na kusugua usoni mpaka shingoni. Kadri unavyotumia asubuhi kabla ya kupaka chochote na usiku kabla ya kulala utagundua tofauti Fulani usoni. Kikubwa zingatia kusafisha uso kila siku kwa njia hii, usilale na kipodozi chochote usoni…. Mazoea hujenga tabia, anza leo na ujiwekee lengo la kusafisha uso kila siku kwa mwezi mzima

7. FANYIA STEAMING USO WAKO MARA MOJA KWA MWEZI: 


… zipo aina nyingi za steaming ya uso. Moja wapo iliyorahisi ni ya kutumia maji ya moto. Chemsha maji na ujifukize uso kwa mvuke wa yale maji. Kwa dakika 15 tu. Njia hii husaidia kufungua vipele vidogo vidogo vilivyoko usoni… fanya hivi mara moja kwa mwezi na hutoona vipele vidogo usoni mwako.

8. TENGENEZA USO WAKO KWA VITU VYA ASILI

…. Kwanza ni gharama nafuu sana, pili vinapatikana kwa urahisi mno. Watu wengi hukwepa kutumia vitu vya asili kwa sababu vinahitaji kuandaliwa mf. Kuchanganya unga wa dengu na kiini cha yai... au kuchukua muda kuleta matokeo…. Ila nakuhakikishia vitu vya asili ni bora zaidi na nafuu zaidi na vinapoleta matokeo hudumu kwa muda mrefu sana… na faida kubwa zaidi ni kutokuwa na matokeo hasi kama kubabuka au kuwashwa usoni.  Tutaendelea kufahamishana ni vitu gani vya kutumia kadiri tunavyoblogua. Si kwamba hupaswi kutumia vitu vya viwandani la hasha vipo vitu vyenye ubora lakini vingi hupatikana kwa bei kubwa ambayo wengi wetu hatuimudu kila mara. Na sasa vitu vya asili pia vimeboreshwa na kujazwa katika makopo tayari kwa kutumiwa.!


9. TUMIA MEDICATED SOAP

…. Tafuta sabuni iliyo Anti-Bacterial ni nzuri kuliko kutumia sabuni yoyote ile usoni hasa za urembo au sabuni ya kipande ya kufulia. Dettol hiyo elfu na mia tano tu!


10. KUNYWA MAJI MENGI

…. Unaweza kuanza na nusu lita kila siku kwa kunywa kidogo kidogo na hatimaye kumaliza lita moja kwa siku. Njia ngumu kidogo kwa vile wengi wetu hatuna mazoea ya kunywa maji mengi mara kwa mara lakini ni vema kuanza mazoea haya kwani sit u itakuletea ngozi safi usoni na mwalini lakini pia itakuepusha na maginjwa mengine ya njia ya mkojo au yatokanayo na ukosefu wa maji mwilini.

NB. HIZI NI KANUNI ZANGU BINAFSI NINAZOZIFUATA NA ZIMENILETEA MATOKEO CHANYA
TUKUTANE TENA PANAPO MAJAALIWA!

2 comments:

  1. asante mamangu, yani umenikoshaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa........ulijuajeee?

    ReplyDelete
  2. Nilitumia Hiyo detol kunawia uso kwanza iliniunguza uso ukaniwasha sana vipele vidogo vidogo na uso uka kakamaa nikaitupa kabisa 😭😭

    ReplyDelete



Snowfall Widget for Blogger


Snowfall Widget for Blogger