11
Pazia jepesi lililojaa matundu yaliyotosha kuigeuza pazia ile
kuwa kama nyavu ya kuvulia samaki, ilipepea dirishani na kuruhusu hewa safi
iliyosukumwa na upepo ipenye kwa mapana na kumfikia Sindi Nalela pale kitandani
alipokuwa amejilaza chali, akili yake ikiwa imekimbilia kusikojulikana na
kukiacha kichwa chake wazi mithili ya mtungi uliotoboka.
Macho yake yaliitazama
dari huku yakifumba na kufumbuka taratibu mithili ya mtu aliyekuwa
akinyemelewa na usingizi. Alikuwa ametopea mawazoni kiasi cha kutojielewa
sawasawa kwa wakati ule.